MAHAKAMA YA AFRIKA KUHAMASISHA WADAU NCHINI GUINEA BISSAU KUHUSU UWEPO NA KAZI ZA MAHAKAMA HIYO
Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) yenye makao yake makuu Jijini Arusha inafanya Ziara ya kikazi nchini Guinea Bissau ili kukutana na kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali kwa lengo la kuitangaza Mahakama hiyo.
Katika ziara hiyo ya siku mbili inayoanza Jumatatu August 14 hadi 15 mwaka huu,Wajumbe wake ambao ni pamoja na Majaji watatu wa Mahakama hiyo na baadhi ya Maafisa wa Ofisi ya Msajili wa Mahakama watakutana na Rais wa Guinea Bissau,Waziri wa Mambo ya Nje,Waziri wa Sheria na Spika wa Bunge la nchi hiyo.
Rais wa AfCHPR, Mheshimiwa Jaji Sylvain Ore’ amesema ili kufanikisha malengo ya AfCHPR na pia kuimarisha mfumo wa Haki za Binadamu Barani Afrika,Nchi nyingi za Umoja wa Afrika hazina budi kuridhia itifaki iliyounda Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kwa Mujibu wa kifungu cha 34(6) na kutoa tamko rasmi la kutambua na kukubali Mamlaka ya Mahakama hiyo kuweza kupokea kesi za watu binafsi na Mashirika yasiyo ya kiserikali(NGO’s).
Kwa mujibu wa Jaji Ore’,Uelewa wa wadau hao kuhusu uwepo wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu pia utaleta hamasa kwa Nchi nyingi zaidi za umoja wa Afrika kuridhia itifaki iliyoanzisha Mahakama hiyo.
Hadi sasa ni Nchi 30 kati ya Nchi 55 wanachama wa umoja wa Afrika ndiyo zimeridhia itifaki na kati ya hizo,Ni nchi 8 tu ndio zimekwisha toa tamko rasmi la kutambua Mamlaka ya Mahakama hiyo na kuruhusu Watu binafsi na Mashirika yasiyo ya kiserikali kupeleka kesi katika Mahakama hiyo.
Guinea Bissau imetia saini mkataba ulioanzisha AfCHPR mwezi June,1998 lakini haijaridhia na wala kutoa tamko la kuruhusu watu binafsi na Ngo’s kupeleka kesi Mahakamani hapo.
“Tangu mwaka 2010,AfCHPR imefanikiwa kuendesha programu mbalimbali zinazolenga kuhamasisha na kutoa elimu juu ya uwepo wa Mahakama hiyo na shughuli zake ambapo imefanya ziara katika baadhi ya Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kuendesha Semina na Mikutano katika ngazi ya Kitaifa na Kikanda kwa lengo la kukuza uelewa wa wadau juu ya uwepo wa Mahakama.”Alisema Jaji Ore’.
Mwezi April mwaka huu,Mahakama hiyo iliendesha semina kama hiyo ya uhamasishaji Nchini Misri na Tunisia na tayari Tunisia imetoa tamko la kuruhusu watu binafsi na NGo’s katika nchi hiyo kupeleka kesi zao moja kwa moja katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu,huku Misri ikieleza kuridishwa kwake na utekelezaji wa shughuli za Mahakama katika kipindi cha Miaka 10 iliyopita na kuahidi kuwa itaridhia itifaki husika.
Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ilianzishwa kwa mujibu wa kifungu namba 1 cha itifaki ya mkataba ulioanzisha Mahakama hiyo ambapo Itifaki hiyo ilikubaliwa juni 09,1998 nchini Burkina Faso na ikaanza kutumika Januari 25,2004 na ilianza shughuli zake rasmi Novemba 2006.
No comments:
Post a Comment