Sunday, August 13

Magufuli afuta shamba jingine la Sumaye


Waziri Mkuu wa mstaafu, Frederick Sumaye ameingia matatani tena baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kumpokonya shamba lake lenye ukubwa wa ekari 326 kwa madai ya kutoendelezwa huku ikisema Rais John Magufuli ameridhia hatua hiyo.
Hili ni shamba la pili Sumaye kunyang’anywa baada ya ekari 33 zilizopo eneo la Mabwepande kuchukuliwa Novemba mwaka jana huku Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi akisema Serikali ilifikia uamuzi huo baada ya kiongozi huyo mstaafu kushindwa kuliendeleza kama notisi ya siku 90 ilivyoeleza.
“Oktoba 28, mwaka huu, Rais John Magufuli alibatilisha hati ya kumiliki ardhi ya shamba namba 3,074 lililopo Mabwepande. Shamba hilo lilikuwa na hati namba 53086. Jina la mmiliki lililoandikwa katika hati ni Frankline Sumaye,” alisema Hapi.
Jana, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mvomero, Frolent Kyombo alisema Rais Magufuli amekubali kufutwa kwa umiliki wa shamba hilo kupitia ilani ya ubatilisho ya Mei mwaka huu.
Kabla ya kupokonywa shamba hilo, Kyombo alisema Sumaye alipewa notisi ya siku 30 iliyomtaka kueleza sababu za kutoendeleza matumizi ya shamba hilo kwa shughuli za kilimo kama lilivyosajiliwa lakini hakutoa sababu zilizoweza kushawishi kutofanyika kwa mabadiliko hayo.
“Hatua ya pili, tukatoa ilani ya ubatilisho wa shamba hilo, kuna maelezo alitoa lakini tuliona hayakuwa na uzito, tukayatupilia mbali, shamba hilo alikuwa anaendesha shughuli za kilimo pamoja na ufugaji. Alikuwa anatumia asilimia 15 hadi 20 tu ya shamba lote,” alisema Kyombo.
Alisema mbali na kutumia sehemu ndogo huku nyingine ikiwa haitumiki, Mwenyekiti huyo wa Chadema Kanda ya Pwani alikuwa amekiuka Sheria ya Mipango Miji, namba 8 ya mwaka 2007 pamoja na Sheria ya Ardhi namba 4 ya 1999.
“(Sumaye) alitakiwa kutumia shamba hilo kwa ajili ya kilimo tu na siyo kwa shughuli nyingine za ufugaji, hilo ni kosa kwa mujibu wa sheria hizo. Kwa hiyo mchakato umeashaanza wa kuligawa shamba hilo kwa wananchi na tunategemea miezi minne ijayo tutakuwa tumemaliza taratibu zote,” alisema.
Desemba 15, 2015, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alitangaza kiama kwa watu wanaomiliki mashamba bila kuyaendeleza huku wakiyatumia kama dhamana ya kukopea fedha benki.
Akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya kuteuliwa na Rais Magufuli, alisema kuna watu wamehodhi mashamba makubwa lakini hawayaendelezi, hawayalipii kodi na mbaya zaidi, wanayatumia kukopa fedha benki.
Kabla ya DED huyo kulithibitishia Mwananchi habari hizo, mapema asubuhi ya jana, taarifa iliyoelezwa kuwa imeandikwa na Sumaye, ilisambaa kwenye mitandao ya jamii ikieleza hatua kwamba Rais Magufuli amechukua shamba jingine la kiongozi huyo.
“Mtakumbuka baada tu ya kuingia Serikali hiyo madarakani, ilitishia muda mrefu kuchukua mashamba yangu bila sababu za msingi, hata wakati wa kampeni baadhi ya viongozi wa CCM walitamka hadharani kuwa huyu dawa yake ni kumnyang’anya mashamba yake,” taarifa hiyo inamnukuu Sumaye.
Hata hivyo, akizungumza hatua za upokonyaji wa mashamba yasiyoendelezwa katika Halmashauri ya Mvomero, Kyombo alisema katika awamu ya kwanza mwaka 2014, iliorodhesha mashamba makubwa 63 na saba kati ya hayo, Rais Magufuli aliyafuta.
“Awamu ya pili nikiwa tayari DED wa Mvomero, tuliwasilisha mapendekezo ya ubatilisho kwa mashamba matatu na yote Rais Magufuli aliyafuta, yalikuwa na ukubwa tofauti. Kwa sasa tumepeleka mapendekezo ya ubatilisho wa mashamba mengine manne kwa Rais, lakini bado hayajajibiwa,” alisema Kyombo.
Kwa mujibu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendelezo ya Makazi, utaratibu wa ilani ya ubatilishaji umeanza kufanyika baada ya Serikali kuagiza halmashauri zote nchini kukagua mashamba na kuwasilisha taarifa zake wizarani kwa hatua stahiki ili kama kutakuwa na ambayo hayajaendelezwa, wakurugenzi husika watume ilani hizo kwa wamiliki.
Baada ya siku 90 kumalizika, halmashauri hizo zitatakiwa kuwasilisha mapendekezo ya ubatilisho wizarani.
Akizungumzia ubatilishwaji huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Jonas Zeeland alisema walipewa taarifa hiyo katika baraza la madiwani lililokutana Ijumaa Agosti 11.
“Ni kweli umiliki wa shamba hili umebatilishwa kutoka kwa Sumaye na taarifa tulipewa jana (juzi) kwenye kikao cha baraza,” alisema Zeeland.
Mwenyekiti huyo alimpongeza Rais kwa kuridhia kubatilisha umiliki wa shamba hilo akisema kwa muda mrefu walikuwa wakiomba warejeshewe.
Alisema bado kuna mashamba mengi katika halmashauri hiyo ambayo hayajaendelezwa hivyo amemuaomba Rais kuharakisha ubatilishaji wake ili waweze kuyapangia matumizi mengine.
Hata hivyo, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Mashariki, Juliana Pilla alisema mashamba waliyoombea kubatilishwa ni zaidi ya ekari 30,000.
“Kuna wamiliki wamesharejea na kuanza kuendeleza mashamba yao baada ya kutoa notisi, kama Mvomero waliombea mashamba 26 lakini hadi sasa wamiliki 17 wamesharudi na wanaendeleza mashamba yao,” alisema kamishna huyo.
Alisema ameziagiza Halmashauri zote kufanya uhakiki kwa mara ya mwisho ili mashamba hayo yabatilishwe huku akizitaja wilaya za Mvomero, Morogoro na Kilosa kuwa ndizo zenye mashamba mengi yasiyoendelezwa.
Alipotafutwa jana kuzungumzia suala hilo, Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miaka 10 mfululizo kuanzia Novemba 27, 1995 mpaka Desemba 28, 2005, alisema hawezi kuzungumza suala hilo mpaka atakapowasiliana na mawakili wake.

No comments:

Post a Comment