Viongozi hao walikamatwa Julai 7 mwaka huu, baada ya polisi kuvamia kikao chao cha ndani kilichokuwa kinafanyika katika ukumbi wa Manzagata ulioko Kata ya Muganza wilayani Chato.
Baada ya kukamatwa, walifikishwa mahakamani Julai 10, kwa kosa la kusanyiko lisilo halali na kunyimwa dhamana baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha hati ya kiapo iliyosainiwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) ya Chato, Alex Mkama kupinga dhamana.
Hata hivyo, Julai 26 Mahakama mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Chato, Jovith Kato ilitupilia mbali ombi la zuio la dhamana baada ya kukubaliana na hoja za wakili wa utetezi, Siwale Yisambi kuwa Kifungu cha 148 (5) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kilichotumiwa na upande wa mashtaka kuwasilisha zuio la dhamana hakiendani na ombi hilo.
“Pamoja na kukubaliana na pingamizi za upande wa utetezi, Mahakama hii inaruhusu washtakiwa kuachiwa kwa dhamana kwa sababu sheria inaelekeza kwamba ni marufuku mtu anayeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mwenye kosa hilo hadi pale itakapodhihirika pasipo shaka kuwa ana hatia,” alisema Hakimu Kato katika uamuzi wake.
Licha ya kuachiwa kwa dhamana, viongozi na wanachama hao wa Chadema wameendelea kusota mahabusu kwa kile kinachoelezwa kuwa Jeshi la Polisi lenye dhamana ya kuwaleta mahakamani, limekosa usafiri wa kuwatoa Biharamulo hadi mahakamani Chato ili kukamilisha utaratibu wa kuachiwa kwa dhamana.
Hadi jana, Hakimu Kato alikuwa amekamilisha kupitia barua 102 za wadhamini wa washtakiwa hao ambao kila mmoja alitakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini hati ya dhamana ya Sh500,000 kila mmoja.
Akizungumzia kwa simu juzi, Hakimu Kato alisema Mahakama imetimiza wajibu kwa kutoa dhamana kwa washtakiwa kwa kupitia na kujiridhisha juu ya usahihi wa barua za wadhamini, kazi ya kuwafikisha mahakamani washtakiwa imebaki mikononi mwa Jeshi la Polisi.
Akijibu malalamiko ya viongozi wa Chadema kuhusu washtakiwa kuendelea kusota mahabusu licha ya kutimiza masharti ya dhamana, hakimu huyo alisema suala hilo uulizwe uongozi wa Jeshi la Polisi kwani ndiyo wenye majibu ya kwa nini hauwafikishi washtakiwa hao mahakamani kulingana na hati za kuwatoa gerezani zinazotolewa na mahakama kila shauri linaposikilizwa.
“Kwa mara zote nne shauri hili liliposikilizwa, Mahakama imetoa hati za kuwatoa mahabusu na kuwafikisha mahakamani washtakiwa; lakini hawajaletwa kwa kile polisi wanachoeleza ni kukosekana kwa usafiri. Jukumu la kuwafikisha washtakiwa mahakamani ni la polisi kwa wale ambao wako mahabusu,” alisema Kato.
Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo ili azungumzie suala hilo ziligonga mwamba baada ya mwandishi kujaribu kumtafuta kwa simu bila ya mafanikio na baadaye kufika ofisini kwake ambako alielezwa kwamba alikuwa katika kazi za nje.
Alielekezwa aonane na Ofisa Mnadhimu wa Mkoa, Stanley Kalyamo ambaye hata hivyo, alikataa kuzungumza kwa maelezo kwamba Kamanda Mwabulambo yupo ndani ya mkoa hivyo aendelee kutafutwa.
Akizungumzia suala hilo, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Ziwa Victoria, Ansbert Ngurumo alisema chama hicho kinaamini polisi wanafanya makusudi kutowafikisha mahakamani washtakiwa hao ili waendelee kusota mahabusu kinyume cha sheria kwa sababu wametimiza masharti ya dhamana.
Alihoji sababu ya polisi kuwapeleka washtakiwa hao mahabusu ya Wilaya ya Biharamulo katika Mkoa wa Kagera, umbali wa zaidi ya kilomita 100, badala ya Geita ambako ni karibu na kunafikika kirahisi.
No comments:
Post a Comment