Rais Paul Kagame wa Rwanda ameapishwa kuongoza taifa hilo kwa miaka mingine saba na akakemea mataifa ya magharibi yanayokosoa Afrika na kuilazimisha kufuata mitindo na mifumo ya utawala wa kimagharibi.
Amewaasa viongozi wa afrika kupigania kujiwezesha kwa mataifa yao kama linavyofanya taifa lake.
Hayo ameyasema katika sherehe za kumuapisha kuiongoza nchi hiyo kwa muhula wa tatu madarakani, baada ya kushinda uchaguzi wiki mbili zilizopita.
Sherehe za kula kiapo zimefanyika mjini Kigali na kuhudhuriwa na marais kutoka nchi 19 za Afrika.
Uchaguzi huo ulikosolewa na baadhi ya mataifa kama Marekani ambayo ilisema hali ya siasa nchini Rwanda inatoa fursa tu kwa mtu mmoja pekee kwendelea kuiongoza nchi hiyo.
Rais Kagame amesema miaka 23 baada ya Rwanda kukumbwa na mauaji ya kimbari wananchi wake sasa waliamua kujenga taifa linalojiwezesha.
Amekemea bila kutaja majina, mataifa yanayozitaka nchi za afrika kuiga mifumo ya utawala ya kimagharibi:
"Tulilazimika kupambana ili kulinda haki zetu na kufanya kile ambacho ni kizuri kwetu na tutaendelea kufanya hivyo. Lakini Rwanda haiwezi kuwa mfano pekee lazima kila mwananchi wa Afrika, kila taifa lipiganie kuishi bila kuetegemea wengine au bila kujali wengine wanavyotaka. Wanataka mifumo inayofanya kazi vizuri kwetu tuibadilishe na mifumo yao ambayo wananchi wao wameanza kupoteza imani nayo."
Mara tu baada ya uchaguzi kufanyika Marekani ambaye ni mshirika wa karibu wa Rwanda licha ya kupongeza wananchi wa Rwanda kwa uchaguzi nchi hiyo ilisema kulikuwa na dosari zilizojitokeza kabla na wakati wa uchaguzi.
Isitoshe nchi hiyo ilipokea shingo upande mabadiliko ya katiba yaliyompa fursa rais Kagame kugombea muhula wa tatu madarakani.
Katika uchaguzi huo rais Kagame alishinda kwa asilimia 98 ya kura.
Wapinzani wake ambao ni Philippe Mpayimana na Frank Habineza wa chama cha Green walijumlisha asilimia 1 tu ya kura.
Rais Kagame hakutaja ajenda yake ya miaka 7 ijayo, lakini baadhi ya wananchi wameeleza kufurahishwa na mafanikio ya utawala wake.
Miongoni mwa marais na wakuu wa serikali za mataifa ya Afrika waliohudhuria sherehe hiyo, alikuwepo rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.
Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo ilimtuma spika wa bunge Obe Minaku nayo Tanzania ikawakilishwa na rais mstaafu Benjamin Mkapa.
Burundi haikuwakilishwa lakini alikuwepo rais wa zamani Pierre Buyoya aliyealikwa miongoni mwa marais wastaafu.
No comments:
Post a Comment