Saturday, August 12

DKT.SHEIN AKUTANA NA UJUMBE WA KATIBU MKUU WA JUMUIYA YA MADOLA




Na  Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
JUMUIYA ya Madola imeahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo kama ilivyo kwa wanachama wengine wote 52 wa Jumiya hiyo.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Baroness Patricia Scotland aliyasema hayo leo wakati alipofanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein Ikulu mjini Zanzibar.
Katika maelezo yake Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa Jumuiya ya Madola inaendelea kutekeleza mipango na mikakati kabambe ambayo imeiweka kwa wanancha wake ikiwemo Tanzania ambapo Zanzibar pia, ni miongoni mwao.

Baroness  Scotland alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa juhudi kubwa anazozichukua katika kuhakikisha Zanzibar inakuza uchumi na kuimarisha amani na utulivu na kusisitiza kuwa Jumuiya anayoiongoza haitokuwa nyuma kumuunga mkono.
Aidha, Bi Scotland alimueleza Dk. Shein miongoni mwa mipango ya Jumuiya hiyo kwa nchi wanachama wake wote 52 ikiwa ni pamoja na kuongeza fursa katika sekta ya biashara nan uchumi, kuwasaidia wanawake, vijana, upatikanaji ajira kwa vijana, elimu, kutunza mazingira, uwezeshaji na mengineyo.
Aliongeza kuwa uchumi kwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo umekuwa ukiimarika kwa kiasi kikubwa kwa zile nchi za Bara la Afrika na hata nchi za Bara la Asia uchumi wake umeimarika kwa asilimia 5 hadi asilimia 8.

Katika mazungumzo hayo, Bi Scotland alimueleza Dk. Shein kuwa miongoni mwa maeneo yaliopewa kipaumbele na Jumuiya hiyo ni katika kuhakikisha nchi zake wanachama zinaimarika kiuchumi ni pamoja na miundombinu na nishati.
Akieleza juu ya Jumuiya hiyo ilivyoweka mikakati katika kusaidia katika kupambana na changamoto ya hali ya mabadiliko ya tabia nchi hasa kwa nchi za Visiwa, Bi Scotland alitoa mfano wa nchi yake ya kisiwa cha Jamhuri ya Dominica jinsi ilivyopata athari zilizotokana na hali hiyo.

Nae Rais Dk. Shein kwa upande wake alitoa pongezi kwa kiongozi huyo kwa ujio wake hapa Zanzibar sambamba na juhudi kubwa zinazochukuliwa na Jumuiya hiyo katika kuendelea kuiounga mkono Zanzibar.

Dk. Shein kwa upande wake alimueleza kiongozi huyo kuwa Zanzibar iko salama na usalama wake unatokana na kuwepo kwa amani na utulivu mkubwa hatua ambayo inapelekea hata uchumi wake kuzidi kuimarika siku hadi siku.
Aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweza kupata mafanikio makubwa katika kuimarisha uchumi wake kutokana na sekta ya utalii, sekta ambayo bila ya kuwepo kwa amani na utulivu ni vigumu kuimarika.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar jinsi inavyochukua hatua katika kuimarisha sekta za maendeleo na kueleza azma ya ujenzi wa bandari mpya ya Mpiga Duri pamoja na kuuimarisha uwanja wake wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume kwa kujenga jengo jipya la abiria.
Aidha, Dk. Shein alieleza mafaniki yaliopatikana katika kuimarisha demokrasia na utawala bora hapa nchini huku akimueleza juhudi zilizochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutunga sheria ya maadili kwta viongozi  wa umma.
Dk. Shein, pia, alitumia fursa hiyo kumueleza Katibu Mkuu huyo hatua zinazochukuliwa na Serikali anayoiongoza katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa akina mama na watoto sambamba na juhudi za Serikali za kuanzisha Pencheni Jamii kwa wazee kuanzia miaka 70, jambo ambalo Bi Scotland alilipongeza.
Pia, alimueleza hali ya mabadiliko ya tabia nchi jinsi inavyoathiri mazingira ya Zanzibar hasa katika kasiwa cha Pemba na sehemu nyenginezo na kueleza hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali pamoja na Jumuiya za Kimataifa katika kupambana na hali hiyo huku akitolea mfano mkutano wa nchi zinazoendelea za visiwa (SIDS) uliofanyika mwaka 2014 huko Samoa na maazimio yake juu ya hali hiyo.
Akijibu masuali ya waandishi wa habari baada ya mazungumzo hayo, Bi Scotland aliwataka wapinzani kushirikiana na Serikali anayoiongoza Dk. Shein kwa lengo la kuwaletea maendeleo endelevu wananchi wa Zanzibar na kusisitiza kuwa Zanzibar inafaidika na misaada ya Jumuiya hiyo kupitia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Jumuiya ya Madola  ilianzishwa karne ya 20 kwa lengo la kuikutanisha Uingereza na yaliyokuwa makoloni yake duniani kwa jukumu la kuhakikisha wanachama wake wanajikwamua katika Nyanja mbali mbali za kimaendeleo ikiwemo kisiasa, kiuchumi, kijamii, michezo na burudani huku Malkia wa Uingereza akiwa ndiye Kiongozi Mkuu wa Jumuiya hiyo.
  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kushoto) akisalimiana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola  Bibi Patrica  Baroness Scotland alipofika Ikulu Mjini Unguja leo akiwa katika ziara ya siku moja na ujumbe aliofuatana nao.
  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) alipokuwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na  Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola  Bibi Patrica  Baroness Scotland alipofika Ikulu Mjini Unguja leo akiwa na ujumbe aliofuatana nao katika ziara ya siku moja. 
/Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akiagana na mgeni wake mara baada ya kumaliza mazungumza na  Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola  Bibi Patrica  Baroness Scotland alipofika Ikulu Mjini Unguja leo. 
Picha na Ikulu

No comments:

Post a Comment