Wednesday, August 2

Bei ya mafuta yashuka


 Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetoa bei kikomo ya bidhaa za mafuta aina ya petroli kwa Agosti , ambazo zimeendelea kushuka kwa miezi minne mfululizo kuanzia Aprili.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Godwin Samwel, bei zitakazoanza kutumika kesho zimeshukwa kwa Sh36 na Sh44 kwa lita ya petrol na dizeli mtawalio.
Taarifa hiyo inasema kwamba tofauti ni katika mafuta ya taa ambapo bei yake imeongezeka kwa Sh24 kwa lita, hali iliyosababishwa na kuongezeka kwa gharama ya usafirishaji wa bidha katika mfumo wa Uagizwaji wa Mafuta kwa Pamoja (BPS).
Wastani wa matumizi ya mafuta kwa siku ni lita milioni tano, milioni tatu na 100,000 kwa dizeli, petrol na mafuta ya taa, sawia.
Kutokana na bei hizo mpya, kuanzia kesho lita moja ya petrol katika jiji la Dar es Salaam itauzwa kwa Sh1,978 kutoka ilivyokua mwezi uliopita ya Sh2,014, wakati lita ya dizeli sasa itauzwa Sh1,830 kutoka Sh1,874 na mafuta ya taa yatapanda mpaka Sh1,830 kutoka Sh1,806 kwa lita kwa mwezi uliopita.
Mhandisi Samweli amesema kwa Mkoa wa Tanga, hakutakuwa na mabadiliko kwa petroli na dizeli kwa sababu hakuna mzigo uliopokelewa kupitia bandari ya Tanga kwa mwezi wa saba 2017. Hii itafanya bei za bidhaa hizo kwa mkoa huo kubaki kama zilivyokua kwa mwezi wa saba 2017.
“Pia, kwa kuwa hakuna bidhaa mpya ya mafuta ya taa iliyoingizwa kupitia bandari ya Tanga, wafanyabiashara wanashauriwa kuchukua bidhaa hiyo kutoka mkoa wa Dar es Salaam na pia, bei ya mafuta ya taa kwa mkoa wa Tanga zitategemea na gharama za mafuta ya taa yaliyopokelewa kupitia bandari ya Dar es Salaam na gharama za usafirishaji kutoka Dar es Salaam hadi Tanga”, amesema.
Kwa upande wa waendesha magari ambao wangependa kupata bei za mafuta, wanaweza kupata bei kikomo kwa kutumia simu ya mkononi kwa kupiga *152*00 na kisha kufuata maelekezo.
Taarifa ya Ewura inasema puia kuwa kampuni za kuuza mafuta ziko huru kuuza bidhaa zao katika bei ya ushindani yenye faida, isipokuwa wazingatie kuwa bei hizo hazizidi bei elekezi.

No comments:

Post a Comment