Thursday, August 17

BARABARA YA KIMARA BARUTI-CHUO KIKUU JIJINI DAR ES SALAAM YATAKIWA KUKAMILIKA NDANI YA SIKU 60

Serikali imetoa siku 60 kwa mkandarasi wa Kampuni ya Hari Singh & Sons kumaliza ujenzi wa kipande cha barabara cha kilomita 1.5 kilichobaki kwa kiwango cha lami katika barabara ya Kimara Baruti-Msewe-Chuo Kikuu yenye jumla ya urefu wa kilomita 2.6.
Akitoa agizo hilo jijini Dar es salaam, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, amemtaka mkandarasi huyo kuhakikisha kuwa anamaliza mradi huo haraka na kwa viwango vilivyo kwenye mkataba ili idumu kwa muda mrefu.
"Ikifika mwezi Oktoba nataka unikabidhi barabara hii ikiwa imekamilika kwa kiwango cha lami na vigezo vinavyokubalika, amesisitiza Eng. Ngonyani.

Aidha, Naibu Waziri Ngonyani amefafanua kuwa mkandarasi huyo hatoruhusiwa kutekeleza mradi mwingine wa barabara nchini endapo atashindwa kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa wakati.
Kwa upande wake Mhandisi Mradi kutoka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Ngusa Julius, amesema kuwa TANROADS tayari imeshatoa notisi kwa mkandarasi huyo kuwa kama hatakamilisha kazi ya ujenzi ndani ya muda wa mkataba hatua za kudai fidia kulingana na mkataba zitafuata na baadae kukatisha mkataba.
Ameongeza kuwa mradi wa ujenzi wa barabara hiyo unasimamiwa na TANROADS kupitia kitengo chake cha wahadisi washauri wazalendo (TECU) na unagharimu shilingi Bilioni 5.7 ikiwa ni fedha za Serikali kwa asilimia mia moja.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Eng. Ngonyani amekagua daraja la Mlalakuwa lenye urefu wa mita 15 kila upande, lililopo barabara ya Mwai Kibaki jijini Dar es salaam na kusisitiza kwa mkandarasi Milembe & Kika JV kuhakikisha anamaliza ujenzi wa daraja hilo kwa wakati.
Ujenzi wa Daraja la Mlalakuwa unagharimu shilingi Bilioni 4.8 na unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwakani.
 Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, akitoa maelekezo kwa mkandarasi wa kampuni ya Hari Singh & Sons, Jaspal Singh (kushoto), wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Kimara Baruti – Msewe – Chuo Kikuu yenye urefu wa KM 2.6 kwa kiwango cha lami, jijini Dar es Salaam.
 Mkurugenzi wa kampuni ya Hari Singh & Sons, Jaspal Signh, akitoa ufafanuzi kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, kuhusu maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Kimara Baruti – Msewe – Chuo Kikuu yenye urefu wa KM 2.6 kwa kiwango cha lami, jijini Dar es Salaam.
 Muonekano wa sehemu ya barabara ya Kimara Baruti – Msewe – Chuo Kikuu yenye urefu wa KM 2.6 inayojengwa kwa kiwango cha lami, ambapo ujenzi wake umefika asilimia 57.
 Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, akitoa maelekezo kwa Mkandarasi wa Kampuni ya Milembe & Kika JV anayejenga Daraja la Mlalakuwa lenye urefu wa mita 15 kila upande, lililoko barabara ya Mwai Kibaki, wakati akikagua ujenzi wake, jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa sehemu ya chini ya ujenzi wa Daraja la Mlalakuwa lenye urefu wa mita 15 kila upande, lililoko barabara ya Mwai Kibaki, jijini Dar es Salaam. Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano,

Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS)

No comments:

Post a Comment