Kutokana na changamoto hiyo, Hospitali ya Aga Khan imeanzisha mpango wa kuwahimiza wanawake kuwanyonyesha watoto wao kwa muda unaotakiwa kwa manufaa yao wenyewe na watoto.
Hospitali hiyo imeanzisha kundi la akinamama wanaonyonyesha kwenye Whatsapp ambalo litakuwa na wanawake 50 pamoja na wauguzi wa Aga Khan.
Akizungumza na vyombo vya habari leo, daktari bingwa wa magonjwa ya watoto na mtaalamu wa unyonyeshaji, Dk Mariam Nooran amesema mama anayenyonyesha vizuri anapata faida nyingi ikiwa ni pamoja na kupunguza hatari ya kupata saratani ya matiti.
Nooran amesema mtoto pia anapata kinga ya magonjwa kutoka kwenye maziwa na kwamba, ambaye hanyonyeshwi anaweza kupata magonjwa mbalimbali ikiwamo homa ya mapafu na kuharisha.
"Changamoto kubwa tulizoziona kwenye unyonyeshaji ni kwamba mama wengi hawana elimu ya kutosha kuhusu namna bora ya kunyonyesha. Pia, wengi wanatumia maziwa ya kopo hata kama hawana tatizo lolote," amesema Dk Nooran.
Mtaalamu wa Lishe wa Aga Khan, Asna Yusuph amesema lengo la kundi hilo ni kutoa elimu kwa wanawake hao ili nao wawe walimu kwa wanawake wengine kwenye suala la unyonyeshaji watoto.
No comments:
Post a Comment