Friday, July 14

WATUMISHI WA MAHAKAMA WAASWA KUSHUGHULIKIA VITENDO VYA RUSHWA.


WAZIRI wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amewaasa watumishi wa mahakama kushughulikia vitendo vya rushwa kwani vinaipatia mahakama taswira hasi na kuzitaka tume za  mahakama na maadili kuchunguza vitendo vya ukiukwaji wa maadili na kuchukua hatua stahiki.

Waziri Kabudi, amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na watumishi wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani juu ya mustakabali wa taasisi hiyo, ikiwa ni mara yake ya  kwanza kufanya ziara tangu alipoteuliwa kuwa Waziri.

Amesema, majaji na mahakimu mara nyingi, wamekuwa wakihusishwa na vitendo vya rushwa hivyo, na kuchangia kuwepo kwa kutokuwa na imani kwa wananchi wanaokuwa na shida ,mbali mbali katika taasisi hizo, hasa wale wenye kesi.

 ‘’Pamoja na mabadiliko makubwa katika mahakama bado kumekuwa na changamoto ya uadilifu hususan vitendo vya rushwa na uwajibikaji ambavyo vimeleta taswira hasi kwa wananchi wanaotafuta haki na kusababisha ushiriki mdogo,’’alisema Profesa Kabudi.

Ameongeza, watendaji wanapaswa kubuni mbinu mbali mbali za kuweza kubadili taswira hiyo kwa kuwachukulia hatua za kinidhamu wanaokiuka maadili na kusogeza huduma kwa wananchi.Kwa mujibu wa Profesa Kabudi, mahakama inanafasi kubwa ya kuchangia maendeleo ya nchi na kwamba jambo wanalopaswa kufanya ni kuimarisha utendaji kazi na kutokomeza rushwa.

Kwa upande wake, Kaimu Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma alisema kuwa wataendelea kutumia sheria kwa ajili ya kuwainua wananchi wengi kwa lengo la kukuza uchumi.

Profesa Juma alisema majaji na mahakimu ni sehemu ya jamii ambao wanapaswa kushiriki kustawisha wanaqnchi ili kutokomeza umasikini.
Akiwasilisha ripoti kuhusu mahakama, Mtendaji Mkuu wa mahakama, Hussein Katanga alisema kuwa idadi ya majaji imeshuka kutoka 100 hadi 80 huku uhitaji wake ukiwa ni kati ya 100 hadi 120.

Katanga alisema majaji 20 wameacha kazi kwa sababu mbalimbali ikiwemo kustaafu na kwamba uhitaji huo unachangia kasi ya kuongezeka kwa ufunguaji mashauri. 

No comments:

Post a Comment