Na Mwandishi Maalumu, Lufilyo
Jana, Jumamosi tarehe 22 Julai 2017 ilikuwa siku ya kipekee familia ya Profesa Mwark Mwandosyak kwani Wananchi wa Busokelo walifanya tafrija pale Lwangwa, Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo, ya kumuaga rasmi kama Mbunge wao kwa vipindi vitatu kuanzia mwaka 2000 mpaka mwaka 2015.
Akiwa amehemewa na tukio hilo, Profesa Mwandosya alisema hiyo ni heshima iliyoje kwake, Mke wake Lucy Akiiki, watoto wao; Max Mwandosya, Sekela Mwandosya, Emmanuel Mwandosya, na wajukuu Tusekile, Lusekelo, na Queen Maria, Mkwe Digna Mwandosya, na ndugu na marafiki wa karibu.
Katika risala iliyosomwa kwa niaba yao na Mwalimu Juma Mwakikuti, Mwalimu Mkuu wa Seminari ya Manow, Wananchi wa Busokelo, au Rungwe Mashariki kama Jimbo lilivyojulikana kabla ya kuwa Halmashauri kamili, walishukuru kwa kile walichoona kama mchango mkubwa alioutoa katika maendeleo ya Busokelo, Rungwe, Mbeya na Tanzania kwa ujumla, katika kipindi ambacho Profesa Mark Mwandosya alikuwa Mbunge wao.
Waliorodhesha mambo mengi ikiwa ni pamoja na: elimu; afya; mawasiliano; miundombinu; utamaduni; utawala (kuanzishwa kwa Halmashauri); maji safi karibu kila kijiji; umeme kila kata kuanzia mwaka 2002; mshikamano wa Jimbo; michezo; Kituo cha Utamaduni, Mila, Historia, na Desturi za Wanyakyusa; Benki ya NMB; Ujenzi kupitia Shirika la Nyumba la Taifa; na kadhalika. Kipekee walimshukuru Mama Lucy Mwandosya kwa kulea watoto yatima na kuwasomesha kuanzia chekechea mpaka vyuo vikuu, na kujenga kituo cha ufundi cha watoto hao ambacho amekikabidhi kwa Serikali na sasa kimekuwa Chuo cha Ufundi cha VETA.
Pia walishukuru kwa kuunganishwa na Dunia kwa kupata wageni wengi kutoka nchi mbali mbali, ikitimia ahadi ambayo Profesa Mwandosya aliitoa mwaka 2000 kwamba si lazima Busokelo iifuate Dunia, bali Dunia itaifuata Busokelo.
Wananchi wa Busokelo waliikabidhi familia ya Profesa Mwandosya zawadi mbali mbali ikiwa ni ishara ya shukrani na kwa ajili ya kumbukumbu.
Akijibu risala hiyo, Profesa Mwandosya, kwa niaba ya familia yake iliyowakilishwa na Mama Lucy Mwandosya, Emmanuel Mwandosya, Wazee wake, na Malifumu wake, aliwashukuru sana wananchi wa Busokelo kwa heshima kubwa waliyompa kuwatumikia kwa muda wa miaka 15 mfululizo, na kumchagua, bila kupingwa, vipindi vyote vitatu kuanzia mwaka 2000.
Alisisitiza kwamba hastahili hata kidogo kupewa heshima na shukrani bali yeye ndiye angewashukuru Wananchi na angelikuwa na uwezo angeliwaandalia hafla Wananchi wote wa Rungwe Mashariki ili kuwashukuru! Aliuliza, kati yake na Wananchi, nani hasa apewe shukrani? Jibu lake ni Wananchi. Bila wao kumkubali,alisema, asingeweza kufanya lolote. Yeye alikuwa ni chachu tu ya maendeleo.
Pili aliwasihi waendeleze elimu kwa kila hali na kila hatua kwani bila elimu maendeleo ya binadamu ni duni. Amewaomba wasiridhike na idadi na ukubwa wa shule zilizopo kwani idani ya wananchi inaongezeka kwa kasi, kiasi cha kwamba miaka 15 ijayo tatizo la mwaka 2000 litajitokeza tena.
Amewaomba viongozi kusimamia ujenzi wa vituo vya mafunzo ya wakulima ili kilimo kiwa cha kisasa na sio cha ujima. Aliwakumbusha kwamba Katika Mkoa wa Kilimanjaro barabara za lami zimefika kila Tarafa. Hivyo basi wasicheleweshe ujenzi wa barabara ya lami ya Katumba-Lwangwa- Tukuyu kwa kuipeleka Serikali Mahakamani kwa madai ya kulipwa fidia kwanza, hasa pale ambapo tayari uthamini umefanywa, akisisitia kwamba fedha za Serikali ni chache. Zinagombaniwa. Zinaenda pale zinapohitajika zaidi.
Aliwakumbusha na kuwashukuru kwamba walikubali ushawishi wake wa kutotaka fidia ili umeme usambazwe kila kata hata kabla ya Mradi wa Umeme Vijijini.
Aliwaomba viongozi wa Halmashauri na Dayosisi ya Konde KKKT kuhakikisha kwamba ujenzi wa Chuo Kikuu Kishiriki, Manow unakamilika, licha ya changamoto zilizojitokeza.
Tatu alikiri kwamba alisononeshwa sana na baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Rungwe kuchoma kwa kutumia matairi barabara kuu ya kutoka Uyole kwenda Kasumulu na Malawi kutokana na tofauti za kisiasa mwaka 2015, akisema kuwa barabara hiyo ni mshipa wa damu katika maendeleo ya Wilaya, Mkoa na Taifa. Aliwaahidi yeye, familia yake, na marafiki zake wataendelea kushirikiana na Wananchi wa Busokelo katika kusukuma maendeleo, na kusisitiza wasiridhike kabisa na hali waliyonayo, akisisitiza elimu, elimu, elimu, elimu.
Sherehe hiyo ilihudhuriwa pia na Mheshimiwa Njobelo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo; Mheshimiwa Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo; Mheshimiwa Cynthia Hilda Ngoye, Mkuu wa Wilaya na Mbunge Mstaafu (Viti Maalum Mkoa wa Mbeya); Ndugu Meckson Mwakipunga, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo; Walimu Wakuu; Viongozi wa Dini, na wawakilishi kutoka kila kata.
Globu ya jamii pia inachukua nafasi hii ya kumpongeza Profesa Mark Mwandosya, mmoja wa watu wa kwanza kabisa kututia moyo na kutupa msaada mkubwa wa mawazo na kubwa kuliko yote ni kuonesha waziwazi kuamini kwamba tufanyalo ni sahihi na daima alisisitiza tusichoke na tuendelee kuendesha Michuzi Blog kiweledi huku tukifuata misingi yote ya taaluma, |
No comments:
Post a Comment