Kumbukumbu hiyo imefanyika leo ikiwa ni Siku ya Mashujaa ambayo huadhimishwa Julai 25 ya kila mwaka ikilenga kuwakumbuka na kuwaenzi wanajeshi waliopoteza maisha wakiwa kwenye majukumu ya kupigania uhuru wa nchi katika nchi za Afrika.
Akizungumza wakati wa kufanya usafi, SSGT Kennedy Laizer aliyemwakilisha Mkuu wa kikosi hicho, Kapteni M.J. Shomari amesema pia wamefanya kazi hiyo kwa ajili ya kuboresha uhusiano kati yao na wananchi.
Laizer amesema wamepokea changamoto kutoka kwa wananchi ya ukosefu wa uzio na jengo la wodi ya wagonjwa, akiahidi kusaidia kuitatua kwa kadri watakavyoweza.
Akizungumzia changamoto za kituo hicho cha afya, Mganga Mfawidhi, Aziza Saidi amesema wamekuwa wakipatwa na matatizo mengi kutokana na ukosefu wa uzio, ikiwemo kuvamiwa na wanyama na mifugo.
“Tumejaribu kupanda miti katika eneo la kituo lakini mifugo iliiharibu. Usiku tunafanya kazi kwa wasiwasi wa kuvamiwa hata na majambazi maana hakuna uzio lakini pia nyumba za wahudumu ni shida, wengi wanatoka mbali hadi wanachelewa kazini,” amesema.
Saidi ameiomba Serikali kuwajengea jengo la wodi kwa kuwa moja lililopo limegawanywa na linatumika kwa ajili ya wanawake na wanaume.
Diwani wa Oldonyosambu, Raymond Lairumbe amesema kituo hicho walikijenga kutokana na wananchi kuteseka na huduma za tiba, hivyo kwa walipofikia wanaiomba Serikali kuwasaidia sehemu iliyobaki.
No comments:
Post a Comment