Thursday, July 20

Upangaji safu 2020 chanzo Dk Nagu kufikishwa Polisi



Mbunge Dk Mary Nagu
Mbunge Dk Mary Nagu 
Hanang’. Imebainika kuwa chanzo cha vurugu katika kikao cha kamati ya siasa ya (CCM) wilayani Hanang, ambazo zilisababisha kufikishwa polisi kwa mbunge Dk Mary Nagu ni upangaji wa safu za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Kutokana na vurugu hizo zilizoibuka juzi, Dk Nagu, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, George Bajuta ambaye pia ni katibu wa uenezi wa CCM wilayani humo na Katibu wa chama hicho wa wilaya, Othman Dunga walifikishwa polisi baada ya Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Sara Msafiri aliyekuwapo katika kikao hicho kuagiza askari wafike katika eneo hilo.
Akizungumzia suala hilo jana, Dunga alisema mkuu wa polisi wa wilaya alifika na kuwanong’oneza akiwataka wakutane nje ya ukumbi na baada ya kutoka walitakiwa kufika kituoni.
Baada ya kufika kituoni, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Francis Masawe alisema viongozi hao walitoa maelezo na kuruhusiwa kuondoka.
Hii ni mara ya pili kuibuka kwa mgogoro ndani ya wilaya hiyo, wa kwanza ukiwa katika uchaguzi wa mjumbe wa NEC uliowakutanisha Dk Nagu na Waziri Mkuu mstaafu, ambaye baadaye alihamia Chadema, Frederick Sumaye.
Katika uchaguzi huo wa mwaka 2012, licha ya Dk Nagu (pichani)kushinda, viongozi wa CCM wilayani humo waligawanyika kutokana na kundi lililokuwa linamuunga mkono Sumaye ambaye ndiye aliyemwachia Dk Nagu jimbo la Hanang kuona kama alidhalilishwa.
Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Michael Bayo alisema uundaji safu kwa ajili ya kugombea ubunge wa jimbo hilo mwaka 2020 ndicho chanzo cha vurugu zilizotokea.
Kikao cha kamati ya siasa kiliandaliwa kupitisha majina ya wagombea uenyekiti, ukatibu, ukatibu mwenezi na wajumbe wa kata.
Kwa mujibu wa mabadiliko ya kanuni ndani ya CCM, wagombea ubunge hawatapigiwa kura na wanachama wote, bali mkutano mkuu wa wilaya ambao baadhi ya wajumbe wake ni viongozi wa kata.
Dunga ni mmoja wa wanaotuhumiwa kuhusika katika upangaji wa safu kwa ajili ya uchaguzi mkuu ikiwa ni pamoja na kuharibu taswira ya chama hicho kwa kuwadanganya wananchi kuwa atawapatia matrekta. Pia alituhumiwa kwa ubadhirifu.
Hata hivyo, Dunga alikanusha madai hayo akisema ni upotoshaji na hayahusiani na kikao cha chama hicho kilicholenga kuwajadili walioomba nafasi za uongozi ili majina yao yapelekwe ngazi ya mkoa.
“Hili suala hata hivyo, limekuzwa na mkuu wa wilaya ambaye ni mjumbe wa kamati ya siasa ya wilaya kwa kuwa angeweza kukemea vurugu lakini badala yake aliita polisi waliotuchukua mimi, mbunge na mwenyekiti wa halmashauri,” alisema Dunga.
Alimtuhumu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya na wajumbe wengine wanne kwamba wanapanga njama za kumchafua ili aonekane hafai kuwapo Hanang’ lakini Bajuta alisema hajatangaza nia na hatagombea ubunge wa jimbo mwaka 2020.
Hata hivyo, Dk Nagu alipoulizwa alisema hawezi kuzungumza na waandishi wa habari mambo yaliyotokea kwenye vikao vya chama hicho. “Kanuni haziruhusu mimi kuzungumza yaliyotokea kwenye vikao vyetu, kwa hiyo siwezi kuzungumza lolote juu ya hayo,” alisema Dk Nagu.
Mkuu wa wilaya hiyo, Msafiri juzi usiku alisema kwamba aliagiza kukamatwa kwa viongozi hao, lakini naye hakuwa tayari kueleza kwa undani kwa maelezo kuwa alikuwa bado kwenye kikao.

No comments:

Post a Comment