Sunday, July 9

STAMICO SASA KUMEKUCHA NA MAKAA YA MAWE


· Yaanza kuuza makaa hayo kwa kasi
· Yakiri kuwa na akiba ya makaa ya mawe ardhini ya kuchimba kwa zaidi ya miaka mia moja. 

Na Koleta Njelekela-STAMICO

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeanza rasmi kuuza makaa ya mawe yanayozalishwa katika Mgodi wake wa Kabulo ili kukidhi mahitaji ya watumiaji wakiwemo viwanda vya saruji na nguo na hivyo kukuza Pato la Taifa.

STAMICO ilianza uzalishaji wa majaribio wa makaa ya mawe katika mgodi wa Kabulo uliopo Kijiji cha Kapeta, Wilaya ya Ileje Mkoa wa Songwe mnamo tarehe 30 Aprili 2017 na mpaka sasa imeweza kuzalisha tani 6,197.

Akihojiwa na Mwandishi wa Habari hii, mara baada ya zoezi la uuzaji makaa ya mawe kuanza rasmi huko Kabulo jana (6 Julai 2017), Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Bwana Hamis Komba, amesema Shirika kupitia mradi wake wa makaa ya mawe wa Kabulo, sasa linaweza kukidhi mahitaji ya watumiaji wote wa makaa ya mawe nchini, katika kipindi cha miaka mia mfululizo kutokana na kuwepo kwa mashapo ya kutosha (mineral resources) na nyenye ubora wa juu katika mgodi huo.

Bwana Komba amesema matarajio ya Shirika ni kuongeza kiwango cha uchimbaji makaa ya mawe kutoka tani 600 hadi tani 1000 kwa siku, hatua ambayo itaiwezesha STAMICO kuzalisha zaidi ya tani 300,000 kwa mwaka. 

“Nchi yetu ina rasilimali nyingi za madini yakiwemo makaa ya mawe, hivyo tunapenda kuwahikishia wenye viwanda vinavyotumia makaa hayo hususani viwanda vya Saruji (Cement), kwamba nchi ina makaa ya kutosha hivyo Serikali haitoshindwa kutosheleza mahitaji na makaa yam awe huku ikitekeleza kwa vitendo azma yake kujenga Tanzania yenye viwanda, ili kukuza uchumi wa Taifa" Alifafanua Bwana Komba.

Amewataka wenye viwanda nchini, kuwasilisha maombi ya kununua malighafi ya makaa ya mawe, ili STAMICO iweze kuwauzia makaa hayo, ambayo yana viwango vya ubora vinavyofaa katika uzalishaji wa nishati ya umeme viwandani. 

Aidha Kiongozi Mtendaji Mkuu wa STAMICO amesema hivi sasa Shirika linaendelea kuimarisha mradi huo wa Kabulo, kwa kuboresha miundombinu, maabara ya kudhibiti ubora wa makaa na kununua mashine mpya (Crusher) kwa ajili ya kuponda makaa, kulingana na mahitaji mahususi ya vipimo vinavyhitajiwa na wateja katika soko.

“changamoto zilizopo katika utekelezaji wa mradi huu ni pamoja na mtaji mdogo, mabadiliko ya hali ya hewa hasa nyakati za mvua na ubovu wa kipande cha barabara yenye urefu wa zaidi ya kilomita 15 kutoka katika eneo la mgodi, mpaka eneo la mauzo, ambapo barabara hiyo haiwezi kumudu malori ya zaidi ya uzito wa tani 15 kupita”. alibainisha Bwana Komba.

Awali Mratibu wa Mradi wa Makaa ya Mawe wa Kabulo-Kiwira Bwana Alex Rutagwelela, amesema amefurahishwa na matokeo chanya ya mradi huo ya kufikia hatua ya uuzaji makaa ya mawe, kwani ni fursa nzuri kwa Shirika, baada ya Serikali kuweka zuio la kuagiza makaa ya mawe kutoka nchi za nje; wakati nchi ikiwa na makaa mengi ya mawe ardhini.

Amesema STAMICO kupitia mradi huo, itaendelea kuimarisha viwango vya uzalishaji wa makaa ya mawe ili kuwafikia wateja wote kulingana na mahitaji yao

“Uwezo wetu na utaalam katika uchimbaji makaa ya mawe ni wa kimkakati ili kuweza kukidhi soko la ndani na nje ya nchi. Lengo kuu la mradi huu ni kutosheleza mahitaji ya kuzalisha umeme wa viwango mbalimbali katika Mradi wa Umeme wa Kiwira na pia kutosheleza mahitaji ya Viwanda nchini vikiwemo vya saruji.”

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala wa STAMICO, Bwana Deusdedith Magala amewasihi watumishi na wataalam wa Shirika hilo, kuendelea kujifunga mkanda na kufanya kazi kwa bidii ili kuivusha salama STAMICO katika kipindi hiki cha mpito, ambapo Shirika linafufua miradi yake ya uchimbaji madini; itakayoleta mafanikio makubwa na yenye maslahi mapana kwa Taifa.

Bwana Magala amesema STAMICO imeweza kuanza uzalishaji wa makaa ya mawe katika Mgodi wa Kabulo kwa kutumia mtaji mdogo na kubana matumizi; hatua ambayo imedhihirisha kwamba STAMICO tumethubutu na tunaweza kutekeleza miradi yetu kwa wakati, pamoja na hali ngumu ya kifedha inayolikabili Shirika kwa sasa.

“ni matumaini kuwa katika kipindi cha muda mfupi ujao, watumishi wote STAMICO tutafurahi, kwani tutaweza kupanua uzalishaji wa makaa ya mawe huku tukileta matokeo makubwa ya uzalishaji yenye maslahi makubwa kwa Shirika” Alifafanua Bwana Magala.

Awamu ya kwanza ya Mradi wa uchimbaji makaa ya mawe wa Kabulo inatekelezwa kupitia leseni zake mbili za uchimbaji mdogo wa madini Primary Mining Licences (PMLs) zilizopo ndani ya leseni ya utafiti ya Kabulo zenye ukubwa wa Hecta 16.52. 

Leseni hizo mbili za Uchimbaji wa Awali wa Madini katika eneo hilo la Kabulo, zina zaidi ya tani milioni 35 zilizothibitishwa za mashapo ya makaa ya mawe, yaliyoko karibu na uso wa ardhi, katika mgodi huo wa Kabulo. 

Kamishna wa Madini Tanzania Mhandisi Benjamin Mchwampaka akiwa katika picha ya pamoja na timu wa wataalam wa STAMICO (wanaotekeleza Mradi wa Uchimbaji Makaa ya Mawe-Kabulo) alipotembelea Mgodi huo hivi karibuni kukagua maendeleo ya mradi huo ambao ulianza rasmi uzalishaji makaa yam awe tarehe 30 Aprili, 2017 na kufanikiwa kuzalisha tani 6197 mpaka sasa. Soko la ndani la makaa hayo linawalenga wazalishaji viwandani hususani wale wa viwanda vya Saruji (Cement) na watengenezaji wa nguo, pamoja na magereza na watumiaji wengine wa majumbani.

Shughuli za Uchimbaji Makaa ya Mawe zikiendelea katika mgodi wa Kabulo Kiwira, uliopo katika Kijiji cha Kapeta, wilaya ya Ileje, Mkoa wa Songwe. Leseni za Uchimbaji wa Awali wa Madini katika eneo hilo la Kabulo, zina zaidi ya tani milioni 35 zilizothibitishwa za mashapo ya makaa ya mawe, yaliyoko karibu na uso wa ardhi, katika mgodi huo wa Kabulo. Mashapo hayo yanaweza kuchimbwa kwa mfululizo kwa miaka mia moja ijayo.

Mratibu wa Mradi wa Uzalishaji Mkaa ya Mawe wa Kabulo-Kiwira Bwana Alex Rutagwelela ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Uchorongaji wa STAMICO akielekeza kuhusu zoezi zima la upakiaji makaa ya mawe katika Malori tayari kwa ajili ya kupeleka katika eneo la mauzo lililopo katika kijiji cha Kasumulu, Wilaya ya Kyela, mkoa wa Mbeya. Mgodi huo wa Kabulo-Kiwira uliopo katika kijiji cha Kapeta, Wilaya ya Ileje mkoa wa Songwe unamilikiwa na kuendeshwa na STAMICO kwa niaba ya Serikali.
Malori ya Kampuni ya Lake Cement yakipakia Makaa ya Mawe katika eneo la mauzo ya makaa hayo, lililopo umbali wa kilometa mbili kutoka katika barabara kuu ya Mbeya, iendayo nchini Malawi. Eneo hilo la mauzo lipo katika kijiji cha Kasumulu, Wilaya ya Kyela, mkoa wa Mbeya. Makaa hayo ya Mawe yanazalishwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), katika mgodi wake wa Makaa ya Mawe wa Kabulo, ulipo katika kijiji cha Kapeta, Wilaya ya Ileje mkoa wa Songwe.

No comments:

Post a Comment