Thursday, July 20

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI AHIZIMIZA USHIRIKIANO KUKABILI UKATILI DHIDI YA ALIBINO


Mwanasheria Mkuu wa Serikali  Mhe. George  Masaju ametoa wito  kwa Asasi zisizo za kiserikali ( NGO)    kushirikiana na kufanya kazi kwa  karibu na Ofisi ya Mwanasheria  Mkuu wa Serikali    ili  kupitia ushirikiano huo kukomesha   na hatimaye kumaliza kabisa  changamoto zinazowakabili  watanzania wenye albinism.
Mwanasheria Mkuu ametoa  wito huo  leo  ( Jumatano)wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Bi  Ikponwosa Ero,  Mtaalamu Huru wa Baraza la  Haki za Binadamu  la Umoja wa Mataifa kuhusu  watu wenye albinism
“  Ningependa  kutoa shukrani zako kwa kuamua kuja Tanzania  na kukutana na viongozi mbalimbali wa Serikali,  hii ni fursa  muhimu kwako    ya kupata taarifa sahihi na rasmi kuhusu  jitihada , juhudi na mikakati mbalimbali inayofanywa na serikali na taasisi zake katika kukabili  vitendo vya jinai dhidi ya watanzania wenzetu wenye  albinism” akasema Mhe. Mwanasheria Mkuu
Na Kuongeza “ kupitia kwako nikuombe basi  uwahimize   viongozi wa asasi zisizo za kiserikali hususani zile zinazojihusisha na  watanzania wenye  albinism kushirikiana na kufanya kazi kwa karibu na  Ofisi yangu  na Taasisi nyingine za serikali kwa sababu wote tuna nia na lengo moja la  kuwasaidia  watanzania wenzetu”..
Akasema  Serikali  inachukulia kwa uzito wa hali ya juu  makosa  ya kijinai dhidi ya watu wenye albinism na kwamba, watuhumiwa wote ambao wamepatikana na hatia wamefikishwa mbele ya vyombo vya sheria na  sheria kuchukua mkondo wake.
Akasisitiza kwamba  Katiba ya  Jamhuri ya Muungano  imesisitiza sana juu ya haki ya mtu kuishi na kwamba haki hiyo ni kwa watanzania wote bila ya kubagua   wakiwamo  watu wenye  albinism au ulemavu wa aina yoyote.
“ Haki ya mtu kuishi imefafanuliwa na kuelezwa kwa kina kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na haki hiyo  haimbagui mtu mwenye albinisim au  mtanzania yoyote ile na ndio maana  makosa ya jinai  dhidi ya  haki ya mtu kuishi  awaye yeyote yule  yanachukuliwa kwa uzito ule ule”.
Kuhusu takwimu  zinazohusu matukio ya jinadi dhidi ya  watanzania wenye albinism,Mwanasheria Mkuu  wa Serikali  amesema kwamba tangu  mwaka  2006  hadi  mwaka huu kumekuwa na matukizo 66 dhidi ya watu wenye albinisma na   huki  miaka mingine ikiwa na haina tukio  lolote lile na kwamba kutokana na  juhudi zinazofanywa na serikali   matukio hayo yameendelea kupungua kwa kiasi kikubwa sana mwaka  hadi mwaka.
Kuhusu    hukumu dhidi ya  watuhumiwa,  Mwanasheria mkuu amesema utekelezaji wa hukumu dhidi ya  watuhumiwa wa makoja hayo ya jinai umekuwa wa mafanikio makubwa kwa zaidi ya asilimi 90 na kwamba  hukumu   zilizotolewa ni pamoja na vifungo,   huku  ya kifo kwa baadhi ya watuhumiwa. Ingawa pia kuna walioachiwa huru kutoka na  kukosekana kwa ushahidi wa kujitosheleza.
Mwanasheria  Mkuu wa Serikali ametaja baadhi ya mafanikio mengine ni pamoja na Ofisi yake  kuandaa na kutekeleza  uratibu wa uhuishaji wa takwimu  za matukio  ya kijinai dhidi ya  watu wenye albinism.  Uratibu  ambao ulifanyika mwaka 2014 kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu, Wizara ya Sheria na Katiba na  Asasi za Kiraia.
Aidha  ametaja mafanikio mengine  ni  kuanzishwa kwa dawati maalum katika Divisheni ya  Mwendesha Mashtaka  kuhusu watu wenye albinism, kusimamia  upepelezi na kuendesha kesi.
Kwa upande wake Bi. Ikponwosa Ero akielezea madhmuni  ya  ziara yake hiyo hapa nchini  kuwa , pamoja na mambo mengine,  kutathimini hali ya haki za bindamu za watu wenye   albinisma,,  kutathimini hatua na jitihanda zinazofanywa na Serikali  katika kukabiliana na  changamoto zinazowakabili watu wenye albinism,  kubainisa mapungufu  na kuona uwezekano  wa kuziba mapengo ya mapungufu hayo.
Pamoja na kuuliza maswali  mbalimbali kwa Mwanasheria  Mkuu wa Serikali , maswali na hoja  zilizojibiwa na  Mwanasheria  Mwenyewe, pamoja na Mkurugenzi wa Divisheni ya  Katiba na  Haki za Binadamu na Mkurugenzi Msaidizi kutoka Divisheni ya Mashtaka, Mtaalamu huyo amemshukuru Mwanasheria Mkuu   kwa kutenga muda wa kukutana naye na kwa  maelezo na taarifa zikiwamo za kitakwimu ambazo  zimewasilishwa kwake. Pamoja na kutambua juhudi za serikali katika  eneo hilo.
Bi. Ikponosa Ero aliteuliwa na  Baraza la Haki za Binadamu  la Umoja wa Mataifa June 15, 2015 kuwa Mtaalamu  Huru wa haki za bindamu kwa watu wenye albinism. 

Imetolewa na Kitengo cha Mwasiliano
Ofisi ya Mwansheria Mkuu wa  Serikali

No comments:

Post a Comment