Friday, July 7

Mke, mtoto watuhumiwa kushiriki kumuua baba

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Wilbroad Mtafungwa

Tabora. Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya Mahona Pondamali (50) mkazi wa Wilaya ya Sikonge yanayosadikiwa kufanyika Aprili mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Ijumaa, Julai 7, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Wilbroad Mtafungwa amesema Aprili 4 mwaka huu, mke wa marehemu Pondamali alitoa taarifa Polisi za kupotea kwa mume wake katika mazingira ya kutatanisha na ndipo Jeshi la Polisi lilipoamua kuanza uchunguzi wa tukio hilo na kufanikiwa kubaini kuwa mtu huyo hakupotea bali aliuawa.
RPC Mtafungwa amesema kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa marehemu alikuwa na tabia ya ulevi na baada ya kulewa alikuwa akimpiga mke wake na watoto.
“Inadaiwa wanafamilia hiyo waliandaa mpango wa kumkodi  mtu wa kumpiga kwa ajili ya kumrekebisha tabia hali iliyosababisha mauti yake,” amesema.
Amesema kuwa baada ya wahusika kubaini kuwa amekufa ndipo walipoamua kwenda kumtupa katika shimo la wachanaji mbao.
“Polisi kwa kushirikiana na wananchi waligundua kuwa  kuna mwili katika shimo la wachana mbao  na kuamua kulifukua ndipo ndugu wa marehemu waliposema kuwa  ni ndugu yao aliyedaiwa kupotea,” amesema.
Amewataja wanaotuhumiwa kufanya mauaji hayo kuwa ni  mke wa marehemu Tatu Said (30), mtoto wa marehemu Katambi Mahona (13) na mlinzi jamii wa kukodi, Mwanza Mburuka (31).
Kamanda Mtafungwa amesema Polisi walifanikiwa kukamata ng’ombe mmoja kwa Mburuka ambaye inadaiwa kuwa alikuwa ni ujira kwa muuaji, (Mburuka.)
Watuhumiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

No comments:

Post a Comment