Rais Nicolas Maduro amedai kupata ushindi mkubwa katika kura ya kumwidhinisha kuchagua wajumbe wa Bunge la kuandika Katiba mpya ya nchi huku jumuiya ya kimataifa ikilaani upigaji kura uliogubikwa na ghasia zilizosababisha watu 10 kuuawa.
Baraza la Taifa la Uchaguzi la Venezuela lilitangaza jana kwamba zaidi ya watu milioni nane walipiga kura kumpa Rais Maduro mamlaka yasiyo na kikomo katika uundwaji wa Bunge la Katiba.
Watu waliojitokea kupiga kura walikuwa mara mbili kinyume cha matarajio ya wapinzani wa Serikali na wachambuzi huru.
"Tumepata Bunge la Katiba,” alisema Maduro katika hotuba yake kwa mamia ya wafuasi wake katikati ya Jiji la Caracas baada ya tume kusema waliojitokeza walikuwa asilimia 41.5.
“Huu ni ushindi mkubwa ambao wanamapinduzi wameupata katika historia ya miaka 18,” alisema.
Takriban watu kumi wameripotiwa kuuawa katika siku inayotajwa kuwa ya umwagikaji damu baada ya miezi minne ya machafuko.
Kumekuwa na mapambano kati ya polisi na waandamanaji ambao wanapinga Bunge hilo la Katiba ambapo wamekuwa wakiweka vizuizi barabarani.
No comments:
Post a Comment