Kampuni ya Udalali ya Msama Auction Mart ikishirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),sambamba na Wizara ya Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo,wanatarajia kuanzisha msako mkali kwa wale wote wanaofanya biashara ya uharamia wa kazi za Wasanii hapa nchini.
Akizungumza na Waandishi wa habari mapema jana jijini Dar,Mkurugenzi wa Msama Auction Mart,Alex Msama alisema kuwa tayari wameishapata kibali na kupewa baraka zote za kuifanya kazi hiyo,ya kuhakikisha wizi/uharamia wa kazi za Wasanii unapungua ama kufika kikomo kabisa.
“Tayari tumepata kibali,hivyo Sisi kama kampuni tumejipanga vyema kukabiliana na hayo mapambano ya wizi wa kazi za Wasanii,tutakae mkuta anauza nyimbo za CD feki,ama anauza nyimbo za wasanii kwa kuziweka kwenye flash,kwenye simu sambamba na wale wote wanaomiliki kompyuta kwa kufanyia kazi hiyo ya kuuza nyimbo za wasanii kinyume cha sheria, tutawakamata popote pale walipo na kuwafikisha katika vyombo vya sheria”alisema Msama.
Amesema kuwa Wasanii wameibiwa vya kutosha,ifike mahali nao sasa wanufaike na jasho la kazi yao,na si kumnufaisha mtu mwingine,alisema na kuongeza kuwa Wasanii wamekuwa wakilalamika muda mrefu kuhusiana na hili jambo la kuibiwa kazi zao na kusambazwa hovyo hovyo bila utaratibu wa aina yoyote,wao kama kampuni watalibeba jukumu hilo huku wakiamini ushirikiano ndio jambo kubwa la kuifanikisha kazi hiyo yenye changamoto kubwa.
“Tunawaomba wasanii mbalimbali na Wadau wa sanaa ya Muziki,watuunge mkono ikiwemo na kutupa ushirikiano wa taarifa,zikihusu maeneo yoyote ambako uharamia wa kazi zao unafanyika,nasi tutachukua hatua za haraka na kuwakamata wahusika”alisema Msema.
Msama alimaliza kuwa kuwapa tahadhari ya mapema kwa wale wote wanaouza kazi wasanii kinyume cha sheria,hasa katika vituo vya mabasi,nyumbani,kwenye Maduka ya biashara waache mara moja,wakipuuza wajue kabisa kiama chao kimefika.
No comments:
Post a Comment