Monday, July 17

Kampuni 100 kushiriki maonyesho ya utalii Arusha



Arusha. Zaidi ya kampuni 100 jijini Arusha na mikoa ya jirani zinatarajiwa kushiriki maonyesho ya utalii na viwanda yatakayofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha AICC jijini hapa kwa mara ya kwanza.
Mkurugenzi Mkuu wa AICC, Elishilia Kaaya, amesema maonyesho hayo yanalenga kukuza sekta ya utalii na viwanda ili kufikia azma ya serikali ya awamu ya tano ya uchumi wa viwanda. 
Akizungumza leo Jumatatu, Julai 17, Kaaya amesema kuwa, ukumbi huo umegharimu Sh 3.2 bilioni, fedha ambazo ni mkopo kutoka Benki ya NBC.
Kaaya ameongeza kuwa, ukumbi huo wa maonyesho na   mikutano utazinduliwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustino Mahiga, Julai 20 mwaka huu .
"Ukumbi huo mpya ambao una uwezo wa kuchukua waonyeshaji wa biashara wa kimataifa 2000 umejengwa kutokana na hitaji la Arusha la kutokuwa na ukumbi wowote maalumu wa maonyesho ya biashara, utaondoa kabisa tatizo la ukosefu wa eneo maalumu la kufanyia shughuli za biashara ya kitaifa na kimataifa mkoani Arusha. "amesema Kaaya. 
Akizungumzia maonyesho hayo Kaaya amesema  yatasaidia kukuza sekta ya viwanda na biashara kwa kuwawezesha wafanyabiashara hao kuonyesha bidhaa zao bure bila gharama yoyote. 
Kaaya, alisema ujenzi wa ukumbi huo ambao umepewa jina la Lake Nyasa, ulianza Aprili 2016 na kukamilika Juni 2017, umejengwa na Kampuni ya Hainan International ya China ambayo ilishinda zabuni.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi na Nyumba wa AICC, Victor Kamagenge, amesema ukumbi huo umejengwa kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi wakiwamo walemavu ambapo kuna miundo mbinu maalumu kwa ajili yao.
Alisema kuwa, kuwepo kwa ukumbi huo kutasaidia kuondoa adha ya wafanyabiashara kushindwa kutangaza bidhaa zao ili waweze kupata masoko kutoka ndani na nje ya nchi. 

No comments:

Post a Comment