Monday, July 17

Hamad Rashid Awaponda Tena Chadema na CUF, Adai Wanaweweseka tu Hakuna ‘Ukawa Wala Upawa’


Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Zanzibar Hamad Rashid ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) ameirudia kauli yake aliyoitoa kipindi cha Bunge la Katiba mwaka 2014 kuwa Hakuna “UKAWA wala UPAWA”


Akizungumza Jumapili hii Jijini Dar Salaam Katika kuelekea kuadhimisha miaka mitano ya chama hicho AgostI 22 mwaka huu, Waziri Hamad Rashidi ameeleza kuwa kipindi cha Bunge la Katiba aliposema kuwa Hakuna UKAWA wala UPAWA baadhi ya watu walimcheka lakini kwasasa matokeo yake yanaonekana kwa kile kinachoendelea ndani ya vyama vya siasa ikiwemo mgogoro wa CUF ambao imefikia hatua unaingiliwa na chama kingine cha upinzani ikiwemo CHADEMA.

Waziri Hamad Rashidi amefafanua kuwa “Jambo lolote ambalo halipo katika misingi ya kikatiba na kisheria haliwezi kupiga hatua” jambo ambalo limetokea kwa UKAWA kwasababu haikuwa kikatiba wala kisheria jambo lililopelekea migogoro katika uchaguzi wa mwaka 2015 ambapo baadhi ya maeneo walishundwa kuelewana na kusimamisha wagombea wao kwa kila chama kinyume na matakwa ya kuungana kwao.

Katika hatua nyingine ADC ameviomba vyama vya siasa vyenye migogoro kuiga mfano wa chama hicho kwa kutatua migogoro yao kwa amani na kuwataka wafuate misingi ya Mwenyezi Mungu ambaye ameamrisha kusamehana pindi inapotokea tofauti miongoni mwa watu.

“Namshangaa binadamu ambaye anakataa suluhu maana hata siku ya mwisho mlango wa TOBA ndiyo utakao kuwa wa mwisho kufungwa hivyo kiushi bila kusamehana ni kumkosea Mwenyezi Mungu” Alisema Waziri Hamad Rashid

Katika hatua nyingine Waziri Hamad Rashid ameeleza kuwa ADC imeendelea kufanya kazi kwa ukaribu na jamii kwa kuanzisha vikundi mbalimbali vya VICOBA bila riba na kutoa mafunzo mbalimbali ambayo yamewasaidia watanzania wengi ambao walikuwa wamepoteza matumaini.

No comments:

Post a Comment