Sunday, July 2

Foleni za ulipaji kodi ya majengo TRA zayeyuka Dar

Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zilizopo mtaa wa Samora jijini Dar es Salaam zikiwa zimefungwa jana. Juzi ofisi hizo zilikuwa na foleni kubwa ya wananchi waliokuwa wakihakiki taarifa za kodi ya majengo. Picha na Said Khamis 
Siku moja baada ya Mamlaka ya Mapato (TRA) kuongeza muda wa ulipaji kodi ya majengo, idadi ya watu wanaokwenda kuhakiki taarifa zao za kodi katika ofisi hizo imepungua.
TRA imeongeza muda wa ulipaji kodi juzi hadi Julai 15 badala ya Juni 30 kama ilivyokuwa awali.
Kupungua kwa watu katika ofisi hizo ni tofauti na juzi iliyokuwa siku ya mwisho, ambapo msongamano ulionekana katika ofisi za mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam.
Kutokana na hali ilivyokuwa katika ofisi mbalimbali jijini hapa kwa siku ya juzi, gazeti hili lilitembelea Temeke, Ilala na Kinondoni jana kuangali kama kungekuwa na msongamano au la. Hata hivyo, Mwananchi ilikuta ofisi hizo hazina idadi kubwa ya watu kama ilivyotegemewa licha ya TRA kufanya kazi hadi saa kumi jioni.
Mfanyakazi wa mamlaka hiyo eneo la Mbagala ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa si msemaji alisema wanafanya kazi mpaka saa kumi jioni. “Hapa sisi tunatoa huduma mpaka jioni, Juni 29 na 30 tulikusanya fomu za watu 1,222 ambazo tunazifanyia kazi kwa leo kama hivi ulivyokuta,” alisema huku akionyesha boksi lililojaa fomu hizo.
Alisema kwa kuwa muda umeongezwa wanajitahidi kufanya kazi kwa kasi zaidi ingawa juzi mtandao ulikuwa chini.
Mkazi wa Mbagala aliyekuwa akisubiri kuingia katika ofisi hizo, Ally Mbwela alisema hakuwahi kulipa kodi hadi tarehe ya mwisho ilipotangazwa kuwa ni Juni 30 na baada ya kusikia muda umeongezwa amepata fursa ya kwenda kufanyiwa uhakiki.
Meneja wa TRA Mkoa wa Temeke, Gemalieli Mafie alisema wameongeza kituo eneo la Sabasaba ambapo wananchi wanaweza kufika kuhakiki taarifa zao na kupata fomu za malipo.
Pia, Mafie alisema wananchi wanaweza kupata taarifa za madai yao katika kituo hicho bila kujali walikojengea nyumba zao nchini.

No comments:

Post a Comment