Saturday, July 29

DKT. SHEIN AFUNGUA TAWI LA BENKI YA CRDB CHAKE CHAKE, PEMBA, LEO



Na Rajab Mkasaba, IKULU ZNZ
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ameeleza kuwa miongoni mwa changamoto zinazowakabili wateja wa Benki nyingi hapa nchini ni msongamano wa wateja pamoja na ucheleweshaji huduma na kuitaka Benki ya CRDB kuwa na mikakati katika kupambana na kadhia hiyo.

Dk. Shein aliyasema hayo leo huko Chake Chake Pemba, katika sherehe ya ufunguzi wa Tawi jipya la Benki ya CRDB likiwa Tawi la 280 ndani ya mtandao wa benki hiyo kutoka matawi 19 iliyokuwa nayo mara tu baada ya kuanzishwa mnamo mwaka 1996.

Katika hotuba yake, Dk. Shein alisema kuwa wananchi wanaeleza kwamba, miongoni mwa changamoto zinazosababisha msongamano ni kuwa benki za hapa nchini bado haziendani na kasi ya mabadiliko yanayotokea katika sekta ya fedha.

Alieleza kuwa katika Siku ya Sherehe za Maadhimisho ya Mei Mosi, mwaka huu yaliyofanyika katika viwanja vya Mahonda, Unguja, Wafanyakazi walipendekeza kuwa Serikali ikae na uongozi wa benki mbali mbali ili ione namna ya kupunguza kero hii kubwa ya msongamano na kuchelewa kutolewa huduma, hasa ifikapo mwisho wa mwezi.

“Leo nimeona ni busara nikuleteeni mawazo hayo ya wafanyakazi, ambao pia, ni baadhi ya wateja wa benki zenu. Wahenga wanasema ‘Mjumbe hauawi’ ndio maana na mimi nimeufikisha ujumbe kama nilivyoambiwa”, alisema Dk. Shen.

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa ni matumaini yake kuwa CRDB, itakuwa na mikakati imara ambayo itaweza kupunguza msongamano wa ucheweleshaji wa huduma katika matawi yake.

Dk. Shein aliongeza kuwa miongoni mwa sifa za Watanzania ni kuwa wako mstari wa mbele katika kutafuta huduma bora sifa ambayo imethibitika juu ya namna walivyozipokea huduma za uwekaji, upokeaji na utoaji wa fedha kwa njia ya mitandao.

Aliongeza kuwa kwa matumizi ya huduma hizo, Tanzania ni miongoni mwa nchi iliyopiga hatua kubwa na kuwa mfano Barani Afrika, hivyo wananchi Pmba watajitokeza kwa wingi kufungua akauti na kufuata huduma wanazozitoa na kuitaka CRDB kuendelea kutoa huduma bora.

Pia, alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa uongozi wa benki kuendelea kubuni mipango imara ya utoaji wa elimu kwa umma kuhusu umhmu wa kutumia benki na kuitaka CRDB kuwapa wateja wao na wananchi elimu juu ya umhimu wa kuweka akiba, kukopa, kurejesha na kufanya shughuli za malipo kupitia benki.

Dk. Shein alieleza kufurahishwa kwake na Benki ya CRDB kwa kuwa na utaratibu na mfumo wa kutoa huduma zake kupitia simu za mkononi, mfumo ambao unawaondolea wananchi ulazimu wa kwenda kwenye matawi ya benki ili kupata huduma na badala yake hupata huduma zote kupitia simu za mikononi.

Kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi wote wa Unguja na Pemba Dk. Shein alitoa shukurani za dhati kwa Benki ya CRDB kwa kuchangia madawati 150 yenye thamani ya TSZ milioni 20 kwa ajili ya skuli za msingi za Chake Chake pamoja na michango kadhaa waliyowahi kuitoa sambamba na waliyoahidi kuitoa.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa uzinduzi wa Tawi hilo ni kielelezo cha juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibatr katika kushajiisha wawekezaji wa ndani na nje kuja kuwekeza katika sekta ya fedha kwa kutambua kuwa huduma za benki ni msingi muhimu katika mabadiliko ya kweli katika sekta zote za kiuchumi na kijamii.

Alieleza kuwa CRDB ni miongoni mwa Benki kubwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo, kufunguliwa kwa Tawi la Benki hiyo kisiwanai Pemba ni habari njema, Pia ni benki yenye kuaminika yenye ubunifu na kuendesha shughuli zake kwa umakini na umahiri mkubwa tangu ilipoanzishwa mwaka 1996.

Aliongeza kuwa kukua kwa sekta ya Benki kisiwani Pemba kutachochea ari na mwamko wa wananchi wa kuwa na utamaduni wa kuweka fedha na amana zao Benki huku akitoa wito kwa wananchi kujiunga na SACCOS ili wapate kuongeza nguvu za uzalishaji na kuirejesha mikopo kwa wakati ili na wenzao waweze kufaidika.

Dk. Shein alieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya uvuvi sambamba na hata zilizofikiwa ili wavuvi pamoja na sekta hiyo izidi kuimarika na kuleta tija kwa wavuvi pamoja na Taifa kwa jumla.

Mapema Kaimu Waziri wa Fedha na Mipango Salama Aboud Talib ambaye ni Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira alieleza kuwa Serikali ya Mapindzi ya Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano wake na Benki hiyo huku akisisitiza haja kwa benki hiyo kushirikiana na ZSTC katika kuimarisha zao la karafuu.

Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB Ally Hussein Laay, alisema kuwa takwimu zinaonesha kuwa kisiwa  cha Pemba kimeendelea kujenga uchumi imara na hivyo kuongeza umuhimu wa kuwa na mfumo thabiti wa fedha na ndio maana CRDB ikaamua kuanzisha tawi hilo huko Pemba.

Alieleza kuwa katika tawi hilo jipya pamoja na uwepo wa huduma zote za kibenki ikiwemo akauti, mikopo, bima na ushauri wa fedha na uwekezaji, benki hiyo pia, imo mbioni kuazinsha huduma maalum inayozingatia sheria na misingi ya dini ya kiislamu “Islamic Banking”.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dk. Charles Kimei alisema kuwa ukubwa wa amana za benki hiyo tayari umeshafikia TZS trilioni 4.1 hadi mwezi Juni mwaka huu 2017 na tayari imeshafungua matawi katika nchi ya Burundi.

Aidha, alitoa pongezi zake kwa Dk. Shein kwa mashirikano makubwa inayoyapata Benki hiyo kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar huku akieleza kuwa mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka jana benki ya CRDB ilitoa mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 3.3 kwenye sekta za kilimo, usafirishaji, utalii, viwanda na ujenzi wa miundombinu.

Alieleza kuwa baadhi ya miradi mikubwa iliyofaidika na mikopo hiyo ni ujenzi wa uwanja wa ndege wa kisasa wa Dar-es-Salaam (terminal 3), mradi mkubwa wa umeme vijijini (REA), Ujenzi wa Soko kuu la Mwanjelwa-Mbeya na mingineyo mingi ikiwemo ya watu binafsi.

No comments:

Post a Comment