Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuzindua bodi hiyo leo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, amesema Serikali ina matumaini makubwa na bodi hiyo katika kuhakikisha inatimiza wajibu wake.
Amesema wakati sekta ya utalii inaendelea kukua nchini, bodi hiyo inakabiliwa na kazi ya kuhakikisha inashirikiana na menejimenti ya NCAA kukabiliana changamoto ya ongezeko la watu na mifugo ndani ya hifadhi.
Amesema sheria iliyoanzisha mamlaka hiyo, inawatambua wenyewe wa Ngorongoro kuwa ni wakazi halali ambao mwaka 1959 walikuwa 8000 tu lakini sasa wakazi wamefikia zaidi ya 97,000.
"Lazima watu waliohamia ndani ya hifadhi, waondolewe sambamba na mifugo ambayo si ya wenyeji na nitumie fursa hii kuwataka waanze kuhama wenyewe,"amesema.
Profesa Maghembe amesema sensa ambayo inaendelea sasa itabainisha wenyeji halali wa Ngorongoro na idadi ya mifugo ambayo itawekwa alama na wenyeji watapewa vitambulisho.
Amesema changamoto nyingine iliyopo Ngorongoro ni ubovu wa barabara ambayo inalalamikiwa pia na wangoza watalii na akaeleza ukarabati ambao unaendelea sasa utaondoa tatizo la barabara hiyo.
Profesa Maghembe pia amesema kuna mpango wa kuijenga vizuri barabara hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu tofauti na ukarabati unaofanyika kila mwaka.
Kaimu mwenyekiti wa bodi hiyo, Mudhihir Mudhihir amesema bodi yao inatambua majukumu yao makubwa ni kuendeleza utalii, uhifadhi na jamii iliyopo ndani ya Ngorongoro.
Amesema wana uhakika wa kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali katika kwani bodi hiyo, imekamilika kutokana na aina ya wajumbe walioteuliwa.
Awali Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dk Fred Manongi alisema, mamlaka hiyo, imejipanga kuongezea idadi ya watalii lakini pia kuboresha uhifadhi na maendeleo ya wenyeji wa Ngorongoro.
No comments:
Post a Comment