Akiwa mkoani Songwe Waziri Mkuu amesema kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ipo makini na imejipanga vizuri katika kutekeleza ahadi mbalimbali zilizotolewa na Rais Magufuli ikiwamo Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 inavyoelekeza.
Waziri Mkuu amesema hayo baada ya mbunge wa jimbo la Songwe, Philipo Mulugo kumuomba awasaidie kumkumbusha Rais Magufuli kuhusu ahadi yake ya ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita nne wilayani Songwe.
“Ahadi zote zilizotolewa na Rais Magufuli tutazitekeleza, ikiwemo na hii aliyoikumbusha Mulugo ya ujenzi wa kilomita nne za barabara ya lami. Tunawaomba wananchi muendelee kuwa na imani na Serikali yenu.” Amesema.
Waziri Mkuu pia amepiga marufuku wananchi kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka katika vyanzo vya maji na kuwataka washirikiane katika utunzaji wa mazingira ili kuliepusha Taifa kugeuka jangwa.
Amesema ni vema wananchi wakazingatia Sheria ya Mazingira inayozuia kufanya shughuli za kibinadamu zikiwemo za kilimo kwenye maeneo yote ya vyanzo vya maji ndani ya mita 60. Aliwaagiza wakuu wa idara kusimamia jambo hilo.
Waziri Mkuu amesema kwa sasa maeneo mengi yanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji jambo ambalo linachangiwa na vitendo vya uharibifu wa mazingira vinavyofanywa na baadhi ya wananchi, hivyo aliwataka wabadilike.
Hata hivyo, amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa kampeni ya Rais Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, ambapo itahakikisha wananchi wote wanapata huduma ya maji katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
Pia Waziri Mkuu aliwaeleza wananchi hao kwamba, Serikali bado inaendelea kutafuta vyanzo mbalimbali vya maji na kuhakikisha vinabainishwa na kufanyiwa tathmini ili viweze kuendelezwa na kuongeza upatikanaji wa maji nchini.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Gallawa amesema watu wanaopata huduma za maji safi na salama katika maeneo ya mijini ni asilimia 42 na vijijini ni asilimia 41.6.
Amesema katika bajeti ya 2017/2018 halmashauri za mkoa huo zimetengewa jumla ya Sh 7.5 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji ikiwa ni pamoja na ujenzi wa matanki ya kuvunia maji ya mvua katika majengo ya Taasisi za Umma.
Pia mkoa huo unatekeleza mpango kazi wa usambazaji maji katika maeneo ya mijini na vijijini kwa kupanua mifumo ya usambazaji na kuzijengea uwezo mamlaka za maji na ifikapo Desemba mwaka huu wataongeza idadi ya wananchi wanaopata huduma hiyo kutoka asilimia 45.04 hadi asilimia 55.63.
No comments:
Post a Comment