Saturday, April 11

Polisi Ajiua Kwa Kujipiga Risasi.


Askari wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, H 3416 PC Charles, amejiua kwa kujipiga risasi.

Baadhi ya wananchi wanaoishi jirani na kituo hicho cha polisi, Paulo Lazaro na Furahisha Felix, walisema tukio hilo lilitokea Aprili 4, mwaka huu, saa 1:00 usiku kituoni hapo.

“Suala hili limetushangaza, kwani sisi tulikuwa nyumbani. Ghafla tulisikia mlio wa bunduki katika kituo cha polisi. Tulipofika, tulimkuta askari huyo akiwa amekufa kwa kujipiga risasi,” alisema Lazaro.

Wananchi hao walisema kutokana na hali hiyo, walilazimika kuwauliza baadhi ya askari waliokuwa zamu, ambao walidai hata wao hawajui ni kwanini mwenzao amechukua uamuzi wa kujiua.

Waliomba ufanyike uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha kujiua kwa askari huyo kwani inawezekana kuna kitu ambacho alikuwa amechukizwa nacho.
  
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzana Kaganda, alithibitisha kujiua kwa askari huyo. “Ni kweli askari huyo amejiua kwa kujipiga risasi wakati akiwa kituoni majira ya saa 1:00 usiku,” alisema Kamanda Kaganda.

Hata hivyo, Kamanda Kaganda alisema hakuna ujumbe wowote ulioachwa na askari huyo kuelezea sababu za kujiua. Kutokana na hali hiyo, Kamanda Kaganda aliwataka askari wote kutatua matatizo yao kupitia kwa viongozi wao badala ya kujichukulia sheria mkononi.

Alisema uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha askari huyo kujiua.

No comments:

Post a Comment