Monday, September 8

Sarafu ya Sh. 500 kuanza kutumika mwezi ujao

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kutoa toleo jipya la sarafu ya Sh. 500, inayotarajiwa kuingizwa kwenye mzunguko na kutumika rasmi kama fedha halali nchini, kuanzia mwezi ujao.

Hatua hiyo imechukuliwa na BoT kwa kuzingatia sababu mbalimbali, ikiwamo noti ya Sh. 500 iliyopo sasa kwenye mzunguko kupita kwenye mikono ya watu wengi katika kipindi cha muda mfupi na hivyo, kuchakaa haraka.

Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki wa BoT, Emmanuel Boaz, aliwaambia waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana kuwa sarafu hiyo itakuwa ikitumika sambamba na noti zilizopo za Sh. 500 mpaka hapo noti hizo zitakapokwisha katika mzunguko.

“Hatua hii imezingatia kwamba, noti ya Sh. 500 ndiyo inayotumika zaidi kwenye manunuzi ya kawaida ya kila siku ya wananchi wengi kuliko noti nyingine yoyote. Hivyo, noti hiyo hupita kwenye mikono ya watu wengi katika kipindi cha muda mfupi sana na kuchakaa haraka,” alisema Boaz.

Alitaja sababu nyingine iliyozingatiwa katika kutoa sarafu hiyo kuwa ni noti hizo (za Sh. 500) kukaa katika mzunguko kwa muda mrefu bila kurejeshwa kwenye mabenki kwa wakati muafaka ili zibadilishwe zinapokuwa zimefikia ukomo wake.

Sababu nyingine ni sarafu kuwa na uwezo wa kukaa kwenye mzunguko kwa miaka mingi (zaidi ya miaka 20) zaidi kuliko noti.

Alisema sarafu hiyo ina umbo la duara lenye michirizi pembezoni, kipenyo cha milimita 27.5 na uzito wa gramu 9.5, ina rangi ya fedha na imetengezwa kwa madini aina ya chuma na “Nickel”.

Pia upande wake wa mbele ina sura ya Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Sheikh Abeid Aman Karume, na kwa nyuma ina taswira ya mnyama nyati akiwa mbugani.

Vilevile, ina alama maalumu ya usalama iitwayo “latent image”, iliyopo upande wa nyuma, ambayo ni kivuli kilichojificha, ambacho huonesha thamani ya sarafu “500” au neno BoT inapogeuzwageuzwa.

No comments:

Post a Comment