Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu
na Bunge), William Lukuvi amesema baadhi ya majina ya wabunge yametajwa
miongoni mwa watu wanaoshukiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya
lakini Serikali haiwezi kuwataja hadharani kwa haraka.
Majibu hayo ya Waziri Lukuvi yamekuja baada ya wabunge
kumbana na wengine wakizomea baada ya kueleza ugumu wa kutaja majina ya
washukiwa pasi na ushahidi wa kutosha.
“Serikali haiwezi kutaja majina haraka kiasi hicho kwani
inaogopa kukurupuka na kushindwa mahakamani, hivyo lazima tuwe makini sana na
jambo hilo. Hatuwezi kukurupuka tu eti ni fulani wakati hatuna vithibitisho.
“Kumbukeni wengine mpo humu ndani ya Bunge na tukianza wengi
mtakwisha maana katika orodha hiyo kubwa na ninyi mmo na orodha ni kubwa kweli
ambayo wakati mwingine inatakiwa umakini wa hali ya juu,” alisema Lukuvi
alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Karatu (Chadema), Mchungaji
Israel Natse.
Katika swali lake ambalo lilisababisha kelele za kuzomea,
Natse alitaka majina hayo yatajwe hadharani. Hata hivyo, hali ilitulia baada ya
Spika wa Bunge, Anne Makinda kuingilia kati na kusema: “Hii tabia ya zomeazomea
siitaki humu ndani, acheni tabia hiyo lazima mumsikilize mtu kwa kile
anachokisema kwanza lakini mtindo huu si mzuri...”
Patashika hiyo ilitokana na swali la Mbunge wa Viti Maalumu
(CCM), Catherine Magige aliyetaka kujua iwapo Serikali inaweza kuwaambia
Watanzania ukubwa wa biashara hiyo nchini na kama haioni kama kuna tatizo
katika ukaguzi wa abiria na mizigo katika viwanja vya ndege na juhudi za
Serikali kumaliza tatizo hilo.
Akijibu swali hilo, Lukuvi alisema ukubwa wa biashara hiyo
hapa nchini unadhihirishwa na idadi ya Watanzania 274 waliokamatwa kati ya
mwaka 2008 hadi Julai mwaka huu kwa kosa la kujihusisha na dawa za kulevya
katika nchi mbalimbali za nje.
Alisema Serikali inafahamu ukubwa wa tatizo la matumizi ya
biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya nchini na alitaja takwimu za ukamataji
wa dawa hizo katika kipindi cha kuanzia mwaka 2000 hadi Machi, 2012.
Alisema pamoja na kukamatwa kwa Watanzania hao nje ya nchi,
wageni 31 wanashikiliwa mahabusu katika Magereza ya Keko na Ukonga, Dar es
Salaam ambao ni raia wa Iran, Pakistan, Senegal na Afrika Kusini.
Hata hivyo, katika swali lake la nyongeza, Magige alisema
uteketezaji wa dawa zinazotajwa kukamatwa umekuwa wa siri kiasi cha kutiliwa
shaka kuwa huenda zinachukuliwa na maofisa waliozikamata ndiyo maana hakuna
uwazi.
Kuhusu hilo, Waziri Lukuvi alisema suala la uteketezaji wa
dawa hizo hauko wazi kutokana na sheria zilizopo kutotoa nafasi ya kuteketezwa
mapema kwa kuwa zinatumika kwa ajili ya ushahidi akisema wakati mwingine hukaa
zaidi ya miaka 10.
No comments:
Post a Comment