Thursday, August 29

Dk Ndalichako: Siasa zisipewe nafasi kwenye mitihani yetu


Swali: Unazungumziaje alama za upimaji wa mwanafunzi (continuous assessment) zinazotoka shuleni na nafasi yake katika matokeo ya mwisho?

Jibu: Ni vigumu kujua uhalisia wa alama zinazoletwa kutoka shuleni, wengine wanasema Necta tufuatilie huko shuleni ili kujua uhalisia wake, tutafanya vipi hilo wakati wafanyakazi wote wa Necta ukijumlisha na walinzi tupo 297 na shule za sekondari pekee zipo 430?

Mwaka 2011 wale wanafunzi walioandika vitu visivyoeleweka kwenye mitihani ya mwisho, kwenye alama zao za maendeleo zilizoletwa walikuwa mpaka na 75. Wengine walishindwa kuandika chochote kwenye mtihani wa mwisho lakini kwenye alama zao za maendeleo walikuwa na alama nzuri tu.

Ukiwauliza walimu wengine wanasema hawakuwa na walimu, wanasema walikuwa wanatumia waliomaliza kidato cha sita na hawajui kujaza vizuri hizo alama.

Wengine walisema mitihani ya ndani watoto wanatazamiana majibu na sababu nyingi kama hizo.

Kwa sasa kuna kamati imepewa jukumu la kuangalia hizo alama za maendeleo, kwa hiyo hilo ni eneo ambalo lazima tuliangalie.

Pia nafikiri kwa sababu ya mazingira ya shule zetu, tufike mahali tuwe na uwazi zaidi.

Nafikiri tufike mahali kwenye cheti tuweke alama za mtihani wa Necta na zile zilizotoka shuleni.

Tuseme mathalan huyo mtoto amepata A, lakini kwenye mtihani wa Necta alipata alama hii na ile ya shuleni alipata hivi. Baada ya hapo tukifika kwenye soko la ajira mwajiri achague kama ataangalia alama za shule au za Necta.

Swali: Tangu uanze kuiongoza Necta mpaka sasa unajivunia nini?

Jibu: Nimekaa Necta tangu mwaka 2005, yapo mengi naweza kujivunia, kwanza wakati naingia kila kitu kilikuwa manual (hatukutumia mashine), lakini hivi sasa kila kitu kuhusu mtihani kuanzia usajili tunatumia kompyuta.

Hili limesaidia kupunguza makosa, hasa kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea kwa sababu zamani watu walikuwa wanafanya udanganyifu sana.

Sasa hivi haiwezekani kutumia namba ya mtu mwingine. Usahihishaji kwa darasa la saba sasa hivi pia tunatumia mfumo wa OMR, zamani tulikuwa tunatumia watu 480 kusahihisha mitihani kwa siku 30.

Baada ya kufanya tathimini ya mfumo huu kwa mwaka jana, tumebaini kuwa mashine haikufanya kosa hata moja, baadhi yaliyotokea yalisababishwa na watu na mashine iliwaumbua.

Kwa kidato cha nne na kuendelea, hatujaanza kutumia kompyuta lakini kuna mengi tumefanya, sasa hivi tumeweka mfumo kuweka alama, zikishaingizwa kwenye mfumo kutoka kwenye kituo cha usahihishaji hakuna mtu anayeweza kuzigusa na akigusa anaonekana.

Hata msahihishaji akishaziweka mara moja hawezi kuzigusa tena na akigusa anaonekana. Kwa hiyo kwa mfumo huu, huwezi kumwongezea mwanafunzi alama. Kwa hiyo alama za wanafunzi zinakuwa katika mazingira salama sana.

Databank (benki ya mitihani) tumeiimarisha, maswali ni mengi tofauti na zamani ulikuwa unakuta kwa somo husika kuna mitihani miwili tu.

Kwa sasa maswali ni mengi, ndiyo maana hata kuvuja kwa mitihani hakuna. Kwa mfano, somo kama hisabati kuna maswali kama milioni moja, hata ukimpa mwanafunzi hawezi kuyafanya yote na ajue kwenye mtihani ni lipi litatoka.

Sasa hivi kweli mitihani ni salama sana, lengo letu ni kupunguza mikono kwenye mitihani. Naamini zaidi mifumo kuliko mtu na kwenye mitihani tukileta kuaminiana tunaweza kuwa pabaya.

Swali: Nini ambacho bado unatamani kukifanya ndani ya Necta?

Jibu: Ninachotamani kwa sasa ni kufika mahali tuwe na mashine zinazochapisha mitihani, kuhesabu na kuweka zenyewe kwenye bahasha.

Kwa sasa tunatumia kama siku 40 kuweka mitihani ya shule za msingi kwenye bahasha tu, hii ni kwa sababu lazima watu wanaofanya hii kazi wawe ni wachache na wenye weledi mkubwa. Hawa watu wangetumia hizi siku kufikiri namna ya kuwa na mitihani bora zaidi ingesaidia.

Suala jingine ni kuwajengea uwezo wa wafanyakazi wetu, haswa wa kuandaa maswali. Nina bahati nimesoma nje ya nchi nikasoma kwa undani juu ya mitihani.

Nataka tuwe tunawepeleka watu nje kusomea zaidi juu ya kazi zao, utunzi wa mitihani na masuala mengine, wawe na taaluma nzuri mtu awe na shahada au shahada ya uzamili kwenye eneo la utungaji wa mitihani tu.

Natamani pia jamii ijue majukumu yetu sisi kama baraza, baraza ni kama daktari tu, ukija unapimwa na kuambiwa una vijidudu 10 vya malaria. Daktari akishakupa hayo majibu ni jukumu lako kuangalia kama unatumia neti au mazingira yako vipi na ufanye nini ili usipate tena malaria. Kwa sasa watu wanakuwa na mtizamo hasi sana.

Nimekaa miaka minane baraza, wakati naingia watoto walikuwa hawaandiki madudu lakini sasa hali ni ngumu, wanachora vitu vya ajabu wanaandika matusi, wengine wanaonyesha kabisa hawajui kitu walichokuwa wanafanya.Baada ya hali hiyo, watu wengine wanasema kwa nini mnapeleka mitihani shuleni na hakuna vifaa, wengine wanasema kwa nini mtihani mmoja wakati shule hazifanani, mimi nauliza kwa nini shule isiwe na vitabu.

Wanasema mitihani ilingane na mazingira, Watanzania wote tuko sawa, kama hakuna vifaa shuleni hiyi siyo kazi ya baraza, umma unabidi uelewe hilo. Kwa sasa kitu ambacho naona ni tishio kwa baraza na mitihani ni mitizamo watu. Wengi wanaukataa ukweli, muda wote anatumia nguvu nyingi kuukataa ukweli.

Suala ni la kweli kabisa lakini mtu anakataa mimi naona hiyo ni hatari sana, huwezi kutibu tatizo bila kujua na kuukubali ukweli, ili tuweze kuboresha elimu lazima tukubali ukweli na kukubali kurekebisha, hali ikiendelea ilivyo sasa huko mbele tutakuwa kwenye hali mbaya sana


No comments:

Post a Comment