Friday, June 21

Mbowe, Lema wahojiwa polisi,watoa msimamo

Arusha. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema jana, walijisalimisha Makao Makuu ya Polisi ya Mkoa wa Arusha na kuhojiwa kwa zaidi ya saa nne kabla ya kuachiwa kwa kujidhamini wenyewe huku wakitakiwa kurejea kituoni hapo, Julai 22, mwaka huu.

Pia Mbowe na Lema wamemtaka Rais Jakaya Kikwete kuunda tume huru ya uchunguzi wa kimahakama ili kuchunguza vurugu za Arusha zilizoanza Jumamosi iliyopita baada ya bomu kurushwa kwenye mkutano wa Chadema na kusababisha vifo pamoja na zile zilizofuatia wakati polisi ilipowasambaratisha wafuasi wa chama hicho kwa mabomu walipokusanyika kwenye Viwanja vya Soweto kwa lengo la kutoa heshima za mwisho kwa marehemu.

Wakiongozwa na mawakili watatu, Mbowe na Lema waliwasili polisi saa 3.50 asubuhi na kuhojiwa hadi saa 9.10.

Viongozi hao walipokewa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha, Diwani Nyanda kabla ya kutenganishwa kwenye vyumba viwili tofauti kwa mahojiano.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mbowe, Lema na wakili Albert Msando walitaja mambo mawili ambayo polisi waliwahoji kwanza ikiwa ni ushiriki wao katika mkusanyiko usio halali kwenye Viwanja vya Soweto, Jumanne iliyopita ambao ulisambaratishwa na polisi.

Jambo jingine ambalo polisi iliwahoji ni kauli yao ya kuwa na ushahidi unaohusisha polisi na tukio la bomu lililorushwa kwenye mkutano wa Chadema na kusababisha vifo vya watu wanne huku zaidi ya 60 wakijeruhiwa.

Mbowe alisema kwa pamoja wamewaeleza polisi kuwa hawaamini kama mkusanyiko wa Jumanne iliyopita haukuwa halali kwa sababu waliruhusiwa kuzungumza na wananchi waliokusanyika ili kuwashawishi watawanyike.

“Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) wa Arusha, Gilles Mroto ndiye aliyeturuhusu kuzungumza na wananchi wale kuwataka watawanyike na ndicho tulichofanya, lakini tukashangaa kuanza kupigwa mabomu mara baada ya kuwataka watu wanaotaka kutoa heshima za mwisho kwa marehemu kwenda Hospitali ya Mount Meru,” alisema Mbowe.

Alisema Mkuu wa Operesheni wa Polisi, Kamishna Paul Chagonja kuwa naye aliyewaomba viongozi wa Chadema kuwatawanya wafuasi wa chama hicho baada ya kuzuiwa kutoa heshima za mwisho katika viwanja hivyo vinavyomilikiwa na Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).

Msimamo wa Mbowe

Kuhusu ushahidi anaodai unawahusisha polisi na tukio la bomu, Mbowe alisisitiza kuwa Chadema kina ushahidi wa kutosha kuthibitisha hilo lakini alisema hakitaukabidhi mikononi mwa polisi.

Alisema hakitafanya hivyo kwa kuwa jeshi hilo ni watuhumiwa wakuu hivyo hawawezi kuwa na dhamira na nia njema katika upelelezi wao. Alisema ndiyo maana badala polisi kuwaona ni msaada, kimeanza kutoa vitisho kwa wote wanaosema waliwashuhudia askari wakishambulia watu kwa risasi kabla ya kuondoka na aliyerusha bomu kwenye gari lao.

“Chadema tuko tayari kukabidhi ushahidi huu kwa tume huru ya uchunguzi ya Mahakama. Rais Kikwete atumie mamlaka yake ya kikatiba kuunda tume kuchunguza tukio la bomu Arusha ili ukweli ujulikane. Polisi ni watuhumiwa katika jambo hili, hivyo hawana dhamira safi na ushahidi wetu,” alisema Mbowe.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema polisi inawasiliana na wanasheria kutafuta ushauri wa hatua za kuchukua... “Polisi ndiyo wenye jukumu la kuchunguza na kukusanya ushahidi wote kuhusiana na matukio ya uhalifu. Hili ni jukumu la kisheria la polisi. Chadema wakabidhi ushahidi wao badala ya kupiga danadana ya kutaka tume huru ya uchunguzi ya kimahakama.”

Alisema hata ikiundwa tume, bado jukumu la kuchunguza na kukusanya ushahidi litarejeshwa mikononi mwa polisi, hivyo Chadema wanapaswa kutimiza wajibu wa kusaidia uchunguzi kwa kuwasilisha ushahidi wao wa polisi kuhusika katika tukio la bomu.



Askofu alia na dola

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Jimbo la Arusha Mashariki, Isaac Kisir ameitaka Serikali kuchukua hatua kali kulinda usalama huku akivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kujitathmini kiutendaji.

Akizungumza katika ibada ya mazishi ya aliyekuwa kada wa Chadema, Judith Moshi iliyofanyika katika Usharika wa Sokoni One, Askofu Kisir alisema mlipuko wa bomu haukuwa mapenzi ya Mungu, bali ni ugaidi.

“Tunapomzika mwenzetu lazima tuseme ukweli, tusimung’unye maneno, ukweli utatuweka huru. Nchi yetu sasa haina usalama ule tuliokuwa nao. Kumekuwa na utekaji nyara watu wanaosema ukweli. Kumekuwa na matumizi ya nguvu kupita kiasi kwa vyombo vya usalama, uchomaji wa makanisa na milipuko ya mabomu.

“Tulitegemea Serikali itatoa adhabu kwa wanaohusika lakini tunasikia maneno ya kejeli… mara tuko mbioni, mara tuko imara, huku watu wanauawa na kupata vilema.”

Judith ni mmoja wa watu wanne waliouawa katika shambulio la bomu lililolipuka wakati wa kuhitimisha kampeni za udiwani za Chadema katika Viwanja wa Soweto Juni 15 mwaka huu, huku watu wengine zaidi ya 60 wakijeruhiwa.

No comments:

Post a Comment