Thursday, March 21

‘Tunahitaji dunia inayolinda maisha’

Vatican City. Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amesimikwa rasmi, huku akiitaka dunia kuungana kwa ajili ya kuwatetea wanyonge na kulinda mazingira.
Akizungumza wakati wa misa maalumu ya kumsimika katika wadhifa huo mpya iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Peter mjini Vatican, Papa Francis alisema hiyo ndiyo njia pekee ya kuijenga dunia iliyo njema na salama, isiyo na vifo visivyo vya lazima na maangamizi.
Francis akitoa hotuba yake alikuwa akishangiliwa na kufunikwa kila mara kwa sauti ya hadhira iliyokuwa ikimsikiliza, hasa alipozungumzia umuhimu wa kulinda mazingira, kusaidiana, kupendana na kutoruhusu namna yoyote ya maangamizi, chuki, wivu na majivuno yanayoweza ‘kuharibu maisha yetu’.
Alisema kwamba wajibu wake mkuu ni kunyoosha mikono yake na kulinda utu, hasa ‘wa maskini, wasiojiweza, wale wanaodharauliwa hasa ambao Mtakatifu Mathayo aliwataja alipokuwa akihitimisha falsafa ya upendo: wenye njaa, wenye kiu, wageni, wasio na mavazi, wagonjwa na wale waliofungwa magerezani’.
“Leo tunahitaji kuona mwanga wa matumaini katika giza lililopo mbele yetu na kuwa wanaume na wanawake wanaotoa tumaini jipya kwa wengine. Kulinda uumbaji, kulinda wanaume na wanawake, kuwaangalia kwa upendo na kujali, hii ikiwa njia pekee ya kutoa tumaini jipya, ili kutoa mwanga mpya na kuangaza kuliko na wingu nene,” alisema.
Kauli hiyo ilianza kutolewa na kiongozi huyo mkuu wa Kanisa lenye zaidi ya waumini 1.2 bilioni duniani tangu alipotangazwa rasmi kuchaguliwa na jopo la makadinali Jumatano wiki iliyopita, ambapo alianza kutangaza ujumbe wake wa amani wa kuwajali na kuwapenda maskini.
Katika misa hiyo maalumu iliyohudhuriwa na wageni maalumu 132 wakiwamo viongozi wa kidini na wa mataifa mbalimbali akiwamo Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, ujumbe wake kwa wafuasi wa Kanisa hilo na watu wote duniani ulichukua muda mfupi usiofikia saa moja, hivyo kumfanya aonekane mtu mwenye staha na kujali muda.
“Ninawaomba wote wenye wajibu katika kusimamia uchumi, siasa, maisha ya watu kuwajibika.” pamoja na wanaume na wanawake wote wenye nia njema, tuwe walinzi wa uumbaji wa Mungu, tulinde mpango wa Mungu ulio wa asili, tulindane na kupendana na kuyalinda mazingira.”
Papa Francis alijumuika na waumini waliokusanyika katika uwanja huo ambapo alizunguka katika eneo hilo kwa kutumia gari maalumu, akisalimiana na waumini kuwabariki wasiojiweza na kuwabusu watoto wenye matatizo.

No comments:

Post a Comment