Sunday, January 13
Uswisi imeiumbua serikali, sasa fedha zirejeshwe
NILIMSIKILIZA kwa makini Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Frederick Werema, alipokuwa akijibu bungeni hoja ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe aliyoiwasilisha bungeni Novemba mwaka jana kuhusu mabilioni ya fedha yaliyotoroshewa katika mabenki mbalimbali nchini Uswisi.
Werema alisema kuwa Serikali imeanza kuzifanyia uchunguzi tuhuma hizo na kwamba Serikali haijalala bali inaendelea na uchunguzi.
Alisema vyombo vya usalama ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), wanalifanyia kazi suala hilo. Akatoa wito kwa Zitto na wananchi wengine kama wana ushahidi zaidi wauwasilishe katika vyombo hivyo ili fedha hizo ziweze kurejeshwa.
Wakati akiwasilisha hoja hizo Zitto alikwenda mbali zaidi ya kuwaelezea watu walioficha fedha hizo nje ya nchi na miaka ambayo walifanya hivyo.
Bila ya kuwataja kwa majina, Zitto aliwataja watu hao kwa nyadhifa kuwa ni watu wote walioshika nyadhifa za uwaziri mkuu katika kipindi cha 2003 hadi 2010, walioshika nyadhifa za uwaziri wa nishati na madini katika kipindi hicho na waliokuwa makatibu wakuu Wizara ya Nishati na Madini.
Wengine ni mawaziri na makatibu wakuu wa Wizara ya Ulinzi, wakuu wa majeshi, wanasheria wa Serikali, makamishna wa nishati, walioshika wadhifa wa Ukurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Uenyekiti na Ujumbe wa Bodi wa TPDC katika kipindi cha mwaka 2003 hadi 2010.
Pia Zitto alitaka Serikali kuwasiliana na Benki ya Dunia kupitia kitengo cha ‘Assets Recovery Unit’ ili mabilioni ya fedha na mali ambazo zimetoroshwa nje ya nchi kwenda Uswisi, Dubai, Mauritus na maeneo mengine ziweze kurejeshwa.
Hoja hiyo ya Zitto iliungwa mkono na Wabunge mbalimbali wakiwamo wa CCM ambao walitaka serikali kuchukua hatua za haraka kurejesha fedha hizo na wahusika wachukuliwe hatua.
Wapo wabunge ambao walikwenda mbali zaidi ya kutaka watu hao waliotorosha fedha hizo wakipatikana wanyongwe kwa sababu hao ni wasaliti wan chi yetu.
Mwisho wa mjadala bunge likaazimio kuipa serikali muda hadi bunge lijalo kutoa taarifa ya utekelezaji wa azimio hilo la kurejesha fedha hizo nyumbani.
Baada ya hapo kila mmoja tukajua kweli sasa serikali huenda ikalifanyia kazi azimio la bunge la kuzirejesha fedha hizo, kwa sababu siku zote serikali imeonyesha kuwa nzito katika kuzirejesha fedha hizo.
Kauli ya serikali ya Uswisi kuwa Serikali Tanzania haijaonyesha nia ya dhati kutaka kuchunguza na kupata mabilioni ya fedha yaliyofichwa na Watanzania katika benki mbalimbali nchini humo, inashtua sana.
Balozi wa Uswisi nchini, Olivier Chave alisema Ijumaa ya wiki hii kuwa mpaka sasa hakuna jitihada zozote zilizofanywa na Serikali ya Tanzania kutaka ufumbuzi wa tuhuma hizo.
Chave alisema Uswisi iko tayari kushirikiana na Tanzania kujua uhalali wa fedha hizo na endapo zikigundulika ni fedha chafu basi tutazirejesha nchini.
Alisema Serikali yao haina tatizo, kwani wameshafanya hivyo kwa nchi za Ufilipino na Nigeria hivyo watafurahi na Tanzania kama watamaliza suala hilo.
Alisema habari zinazoandikwa kuhusu mabilioni hayo kuhifadhiwa katika Benki za Uswisi, yanaharibu picha ya nchi hiyo mbele ya mataifa mengine, hivyo angependa suala hilo kumalizwa na kwamba wao wako tayari.
Kwa hakika, kauli ya balozi huyu imeimbua serikali ambayo imekuwa ikitoa visingizio vya vingi kwamba inashindwa kuzirejesha fedha hizo kutokana na kukosa ushirikiano.
Naamini kama alivyosema Zitto na watu wengine nchini kwamba fedha hizo zinamilikiwa na vigogo ndani ya serikali au waliowahi kushika nyadhifa za juu serikalini ndiyo maana inakuwa vigumu kuchukua hatua.
Kama serikali ya Uswisi inasema iko tayari kutoa ushirikiano wa kurejeshwa kwa fedha hizo nyumbani, serikali inataka msaada gani tena zaidi ya huo?
Ni kitu cha kushangaza tunapomuona Werema na mawaziri wengine wa serikali Rais Jakaya Kikwete wakisimama kuwapaka mafuta Watanzania kwa maneno matamu kwamba wameanza uchunguzi kuhusu suala hilo, wakati hata hawajawasiliana na serikali ya Uswisi.
Kuonyesha kuwa hawana nia ya dhati hata Zitto mwenyewe hadi sasa anasema Serikali haijamfuata kutaka kutoa ushirikiano wa aina yeyote kuhusu tuhuma hizo.
Zitto alikaririwa Ijumaa ya wiki hii akisema kuwa ingawa Serikali ilitaka iachiwe tuhuma hizo ili iweze kuzifanyia kazi, lakini hadi sasa ukimya umetawala.
Sasa tunaitaka serikali kuacha kutumia visingizio ili kuwazunga Watanzania, tunahitaji fedha hizo zirejeshwe na wahusika wachukuliwe hatua.
0754 304336
juliusmagodi@yahoo.com
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment