Wednesday, January 11

Lowassa aponda nguvu ya umma

Anthony Kayanda, Kigoma
WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, ameibuka na kukemea matumizi ya nguvu ya umma, yanayoendeshwa na baadhi ya vyama vya siasa nchini kushinikiza mambo mbalimbali, akisema hayalifikishi taifa popote.

Akizungumza katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Sekondari ya Kanisa la FPCT Bigabiro, mkoani Kigoma, Lowassa alisema nguvu wanazotumia wanasiasa kuhamasisha nguvu ya umma, ingefaa kutumika kushiriki kazi za maendeleo ili kuliletea taifa maendeleo endelevu.

Ingawa Lowassa hakutaja chama cha siasa kwa jina, lakini Chadema ndicho ambacho kimekuwa kikitumia kauli mbiu ya Nguvu ya Umma (Peoples Power) kushinikiza mambo mbalimbali.

"Badala ya kuonekana wakihamasika kufanya maandamano ya kupambana na Serikali, jambo ambalo halitasaidia taifa kuondokana na umasikini, nguvu hiyo ingetumika kushiriki kazi za maendeleo," alisema Lowassa.

Alisema miradi mingi ya maendeleo imekuwa ikikwama kutokana na wananchi kukataa kushiriki kujitolea nguvu zao kwa kufanya kazi, badala yake, wanataka kulipwa fedha kutekeleza miradi maeneo yao.

“Nguvu ya umma tunayoshuhudia kwenye maandamano ya baadhi ya vyama vyetu, ingekuwa inatumika kwa kiwango kilekile kufanya kazi za kujitolea kwenye miradi ya maendeleo kama ujenzi wa sekondari zetu, hakika taifa lingepiga hatua kubwa ya maendeleo, lakini linapokuja suala la kufanya kazi nguvu ya umma hutoweka,” alisisitiza Lowassa.


Harambee
Katika harambee hiyo, Lowassa na rafiki zake walichangia Sh60.5milioni taslim na kufanya michango yote kufikia Sh125 zikiwamo ahadi.

Lowassa alisema elimu ikitiliwa umuhimu ni wazi taifa litajikomboa kutoka kwenye hali duni kwa kuwa litakuwa na watu wenye uelewa wa kutosha juu ya mabadiliko na mifumo mbalimbali ya dunia, kiasi kwamba itakuwa rahisi kufundishwa na kuelekezwa mambo muhimu.

“Baada ya kubaini hakuna usawa katika taifa, tulilazimika kutembea nchi nzima kuhamasisha ujenzi wa sekondari za kata ili kila eneo watoto wasome. Watoto wa Kigoma wawe kama wenzao wa Kilimanjaro au mikoa mingine iliyopata mwanga wa elimu mapema, ndiyo maana angalau watoto wengi wanafika kidato cha nne sasa ikilinganishwa na miaka ya nyuma,” alisema Lowassa.

Ajira
Lowassa alitumia harambee hiyo kurejea kauli yake kuhusu tatizo kubwa la ukosefu wa ajira kwa vijana nchini, ambao wamehitimu masomo yao ngazi mbalimbali lakini wanaishia mitaani bila kupata kazi zinazoeleweka.

Alisema tatizo la ajira kwa vijana ni bomu linaloweza kulipuka wakati wowote na kuleta shida kwa taifa, kwa vile ndiyo nguvu kazi inayohitajika zaidi kujenga uchumi imara wa nchi, hivyo kusaidia kuondokana na umaskini, mfumko wa bei na hata kudorora kwa uchumi.

“Nimekuwa nikilisemea sana suala hili la ukosefu wa ajira kwa vijana, kiasi kwamba kuna watu walinibatiza jina la Yohana Mbatizaji, lakini bado natoa mwito kama jamii tutafakari kwa makini jambo hili,” Lowassa alirejea kauli hiyo na kuongeza:

“Kila tunapokutana kwenye semina na makongamano tulijadili kwa kina, vinginevyo tutakuja kujilaumu siku moja kwa sababu hata wanaohitimu vyuo vikuu, wanaopata ajira ni asilimia tano tu kwa mwaka.”

Alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali mstaafu Issa Machibya, kusaidiana na kanisa hilo kuwashawishi watu wanaomiliki eneo inapojengwa sekondari hiyo, wapunguze gharama za fidia ya ardhi na mazao yao ya kudumu, inayofikia Sh75milioni kwa madai kwamba ni nyingi ikilinganishwa na thamani ya mradi unaotekelezwa.

Mchungaji
Awali, katika risala yao iliyosomwa na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo la FPCT Bigabiro, David Nkone, alisema wameamua kujenga sekondari ya kidato cha kwanza hadi sita kutokana na uhaba mkubwa wa sekondari za ngazi hiyo mkoani Kigoma, hususan zenye michepuo ya sayansi.

Mchungaji Nkone aisema Chuo cha Theolojia cha FPCT Bigabiro kinachotoa mafunzo ngazi ya stashahada pia kinakusudiwa kupanuliwa na kufikia kutoa Shahada, hivyo kuongeza fursa za elimu na ajira kwa baadhi ya Watanzania.

Kanisa hilo lilimteua Lowassa kuwa mlezi wa sekondari hiyo aliyowekea jiwe la msingi ambayo kwa sasa ina madarasa matatu yaliyofikia hatua ya rinta, lengo likiwa ni kujenga madarasa ya kidato cha kwanza hadi sita.

Katika hatua nyingine, mjumbe wa Halmashauri Kuu (Nec) ya CCM Mkoa wa Kigoma, Muhsin Abdallah Sheni, aliahidi kuchangia Sh10 milioni na kompyuta mbili, huku Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba akiahidi Sh3 milioni, Mbunge wa Viti Maalumu, Josephine Ngenzabuke aliahidi kutoa Sh2 milioni na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Machibya akiahidi Sh2.5 milioni.

No comments:

Post a Comment