RAIS Jakaya Kikwete, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiq, kuomboleza vifo vya watu 13 ambao wamepoteza maisha katika mafuriko makubwa yaliyotokana na mvua ambazo zinaendelea kunyesha jijini Dar es Salaam.
Aidha, Rais Kikwete amempa pole mkuu huyo wa mkoa kutokana na uharibifu mkubwa wa nyumba, makazi na mali nyingine za wananchi uliosababishwa na mvua hizo ambazo pia zimesababisha uharibifu wa miundombinu.
Rais Kikwete pia ameuelekeza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kusaidiana na taasisi na vyombo vyenye uzoefu wa maafa kushirikiana katika kuendelea kuokoa maisha ya watu, kusaidia waliozingirwa na mafuriko na kuwahifadhi na kuwasaidia wale wote waliopoteza nyumba na makazi kutokana na mafuriko hayo.
Katika salamu zake, Rais Kikwete amemwambia mkuu wa mko kuwa: “Nimepokea kwa masikitiko habari za vifo vya wenzetu 13 vilivyotokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa ambayo sote tumeishuhudia katika Mkoa wa Dar es Salaam tokea jana (juzi).
“Nakutumia wewe rambirambi zangu kutokana na vifo hivyo, na kupitia kwako kwa familia, ndugu na jamaa waliopoteza wapendwa wao katika balaa hili la mafuriko. Wajulishe kuwa msiba wao ni msiba wangu, naelewa machungu yao na niko nao katika hali ya sasa ya maombolezo. Mungu aziweke pema peponi roho za marehemu wote,” alisema.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jana, imesema kuwa Rais Kikwete alisema kuwa kupitia kwa mkuu wa mkoa anatoa pole zake nyingi kwa wote walioumia ama kupoteza mali zao katika mafuriko hayo.
“Chini ya usimamizi wako, ningependa kuona uongozi wa Mkoa kwa kushirikiana na taasisi na vyombo vyenye ujuzi na uzoefu wa kupambana na majanga na dharura za namna hii, kuhakikisha kuwa tunaendelea kuokoa watu ambao bado wamezingirwa na mafuriko, tunawapa matibabu wale walioumia katika mafuriko hayo, na tunawahifadhi na kuwapa huduma za kibinadamu wote waliopoteza nyumba na makazi yao katika mafurikio hayo,” alisema Rais Kikwete.
No comments:
Post a Comment