Saturday, November 11

Vyama vinapoendeshwa kwa nidhamu ya kijeshi

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisikiliza risala ya vijana wa kikosi cha ulinzi cha chama hicho katika moja ya matukio ya kisiasa mwaka 2015 
Wiki hii taifa lilishtushwa na kuzizima kwa habari za Lazaro Nyalandu kujiuzulu ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM pamoja na nafasi zake zote ndani ya chama hicho kuanzia Oktoba 30, 2017.
Nyalandu, ambaye alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya Awamu ya Nne, pia ameachia nafasi yake ya ubunge wa Jimbo la Singida Kaskazini. Sambamba na kujivua nyadhifa pia alitangaza kuomba kujiunga na Chadema.
Lazaro kaeleza mengi kuhusu sababu za kujitoa CCM na kujiuzulu nyadhifa zake, lakini tunaweza kueleza kujitoa kwake kwa maneno machache kuwa Nyalandu ametofautiana mawazo na uongozi wa chama chake.
Kitendo cha Nyalandu kujiuzulu kinanipeleka kwenye hoja yangu ya leo: Je, hivi ni lazima kweli watu ndani ya chama kimoja wakitofautiana mawazo na mitazamo, basi kundi moja lijitoe au lifukuzwe? Je, ni wakuu wa vyama vya siasa pekee ndiyo wenye haki ya kufikiri na kutoa maoni yao? Je, hakuna uhuru wa kufikiri vinginevyo kwa wanachama wengine?
Naandika makala haya kwa dhana kuwa Nyalandu aliwekwa katika mazingira magumu ya kiuadui ambayo yalisababisha ajiuzulu. Ingekuwa si hivyo nimehoji pia, kwa nini wanachama wenye mawazo tofauti wasipambane ndani ya chama kusukuma ajenda zao badala ya kujitoa?
Siulizi maswali haya kwa sababu ya suala la Nyalandu pekee, bali ni hoja ninayoiibua ifikiriwe na vyama na wanasiasa wote kwa sababu Nyalandu si mtu wa kwanza kulazimika kuachana na chama chake ama kwa kujitoa au kufukuzwa.
Kabla ya Nyalandu walikuwapo wakina Profesa Abdallah Safari aliyetoa CUF na kujiunga na Chadema, Hamad Rashid (aliyeondoka CUF na wenzake na kujiunga na ADC), na Zitto Kabwe aliyetoka Chadema na wenzake na kujiunga na ACT- Wazalendo.
Hawa nao waliondoka kwa sababu walikuwa na mawazo tofauti na viongozi wao. Walidhani, kama alivyodhani Nyalandu, kuwa vyama vyao vilipoteza dira. Kwa hiyo, kwa kanuni za Tanzania, ukiwa kwenye chama ukawa na mawazo tofauti, ni lazima utoke.
Ndiyo maana, kila palipoibuka tofauti ya mawazo, badala ya tofauti hizo kuchukuliwa kwa mtazamo chanya, kuwa ndiyo afya ya chama; ilikuwa kinyume. Tofauti ya mawazo iligeuzwa kuwa mgogoro ambao ili uishe lazima kundi moja litoke.
Hakuna siasa bila mijadala
Hakuna chama cha siasa kinachostahili kuitwa kwa jina hilo la chama cha siasa kama hakuna tofauti ya mawazo na kuwepo mijadala ya masuala ya kimaendeleo katika kuunda sera mtakazouza kwa wananchi.
Ni kwa sababu hii, inaniwia vigumu kuelewa mantiki ya kuwa na vyama bila uwepo wa uhuru wa fikra kwa wanachama, ikizingatiwa kuwa vyama hivyo vipo katika nchi ambayo inatajwa kufuata siasa za kidemokrasia, tena katika karne ya 21.
Moja kati ya kanuni muhimu za demokrasia ni uwepo wa uhuru wa fikra na uhuru wa kujieleza. Mijadala kuhusu masuala mbalimbali ni muhimu sana sio tu katika siasa bali katika kila sekta ya maendeleo ya nchi kwa jumla.
Ni kwa kutambua umuhimu wa kupata mawazo tofauti ndiyo maana kila Serikali inapotunga sera, sheria au kanuni, wadau mara nyingi hudai nao washirikishwe. Na Serikali hukubali. Ni wazi wadau hushirikishwa kwa lengo la kukusanya maoni tofauti, yanayokinzana, ikitegemewa kuwa kwa nafasi, majukumu na uzoefu wa kila kundi la wadau, watakuwa na uelewa fulani ambao kundi jingine halina.
Mijadala huchochea ushindani wa akili ambazo ndiyo zinazalisha mawazo. Taifa au taasisi isiyo na mijadala ni mfu. Je, vyama vya siasa vinataka kufa kifikra? Au labda viongozi wanataka kuendesha vyama kama jeshi, wakuu wanatoa amri wengine wanatekeleza.
Ukifuatilia baadhi ya migogoro iliyopelekea baadhi ya wanachama kufukuzwa, hususan katika vyama vya upinzani, utagundua kuwa kosa pekee waliofanya ni kuamini kuwa vyama vyao vinahitaji mabadiliko makubwa ya kisera au kiuongozi. Hilo linakuwaje ni kosa katika chama chenye demokrasia?
Mwisho wa siku unagundua kuwa watu wanafukuzwa katika vyama si kwa sababu ya maslahi ya chama bali kulinda viongozi waliopo, wasiopenda kukosolewa. Mara nyingi katika kuhalalisha hatua za kupambana na washindani ndani ya chama hutokea wale viongozi madikteta wa vyama kwa kuhofia kupokwa madaraka, hukimbilia kuwapakazia wakosoaji kuwa ni ‘wasaliti’ na kudai kuwa wana ushahidi wa kiintelijinsia kuwa anashirikiana na chama tawala. jiulize, Profesa Safari alikuwa msaliti CUF aliyekihujumu chama lakini ni huyo huyo ambaye alipokewa Chadema. Kwa kinachoitwa ‘inteligensia’ kali ya Chadema, wameshindwa kujua hilo? Au ndiyo ukitaka kumuua mbwa, mpe jina baya kwanza?
CCM na mwelekeo mpya
Nimekuwa nikiamini kuwa CCM ni chama chenye demokrasia imara, si tu wakati wa uchaguzi hata muda mwingine. Kabla ya uchaguzi wa 2015, tofauti za fikra zilizodhihiri kupitia makundi ziliichangamsha CCM, kiasi kwamba baadhi ya watu walidhani chama kingegawanyika.
Kuelekea uchaguzi, kulikuwa na ukosoaji mkali dhidi ya Rais Jakaya Kikwete. Kikwete aliitwa kila aina ya majina na baadhi ya watu: dhaifu, fisadi, mswahili…. lakini, licha ya tofauti hizo, maamuzi yalifanyika kupitia mifumo, sera, sheria na kanuni za chama, kukawa na washindi na walioshindwa.
Kwa kiasi kikubwa, walioamua kujitoa, haikuwa kwa sababu walitimuliwa bali kwa ni sababu walitaka kwenda kutafuta nafasi ya kugombea katika vyama vingine.
Sasa, hali inaonekana kubadilika. Tayari zipo dalili za CCM kupoteza demokrasia ya ndani ya chama. Yale ambayo tumekuwa tukiyaona wakitendewa wapinzani, yaani kukandamizwa kwa uhuru wa kutoa mawazo, yanajitokeza ndani ya CCM sasa.
Baada ya kuondoka Nyalandu, baadhi ya wana CCM tayari wameanza kutaja majina ya watu wengine ambao wanadhani nao wangepaswa kuondoka kwa sababu tu wana mawazo tofauti, jambo ambalo linatishia kuua demokrasia hususan uhuru wa fikra ndani ya CCM.
Kama hali hii itaendelea, tusishangae CCM ikarudi nyuma hadi enzi zile za ‘Zidumu fikra za Mwenyekiti’.
Kurejea kwa enzi zile ni jambo la kuogopwa kwa sababu tushaipitia na kuona madhara yake. Mwalimu Nyerere, labda kwa nia nzuri tu, alitaka kutekeleza ndoto na mradi wake wa ujamaa kwa Tanzania. Hata hivyo, kwa sababu ndoto zake hazikupitia michakato ya ushindani huru wa mawazo; zilishindwa.
Mwendelezo wa watu kufukuzwa kutoka katika vyama au kushinikizwa mpaka wanajitoa, ni dalili ya kuendelea kuporomoka kwa demokrasia ndani ya vyama vya siasa. Viongozi wanataka wanachosema kiwe ndio ukweli pekee, kusiwe na mawazo mbadala.
Vyama vingi vya siasa Tanzania vinapenda demokrasia tu katika siasa za kitaifa zinazopambanisha vyama, lakini havitaki demokrasia ndani ya vyama vyao. Kwa mfano, katika historia ya vyama vingi tumeona mara nyingi vyama vinalalamikia Serikali kukandamiza uhuru wao wa kisiasa lakini wakati huohuo, vyama hivyo hivyo vinavyolalamika vinakandamiza uhuru wa fikra na mawazo wa wanachama wake.
Ifike wakati tutofautishe muundo wa utendaji wa vyama vya siasa na taasisi nyingine. Kwa ilivyo sasa, vyama vinaendeshwa kama jeshi. Amri moja. Umefika wakati sasa, turudi darasani na kusoma upya ni maana ya chama cha siasa hasa katika muktadha wa mifumo ya siasa za kidemokrasia.

Wasiwasi dhidi ya waangalizi wa uchaguzi barani Afrika

Waangalizi wa uchaguzi nchini Kenya
Waangalizi wa uchaguzi nchini Kenya wakijadiliana jambo jijini Nairobi. Kutoka ushoto ni Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry na Waziri Mkuu mstaafu wa Senegal, Aminata Toure Agosti 9, 2017. Picha ya Reuters 
Katika uchaguzi mkuu wa Kenya wa Agosti 8 mwaka huu na ule wa marudio wa urais wa Septemba 26, nadharia mbili zinazopingana zilichomoza kuhusu matokeo ya chaguzi hizo.
Je, muhimu ni idadi ya kura alizopigiwa mgombea, hivyo akatangazwa kuwa mshindi, au kipaumbele kiwekwe juu ya mwenendo mzima wa uchaguzi - tangu pale wapigaji kura wanapoandikishwa, taratibu na kampeni za uchaguzi, upigaji, ukusanyaji na kuzihesabu kura au namna ya kuyatangaza matokeo.
Katika chaguzi zote hizo mbili Tume Huru ya Kenya ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imedhihirisha haijaimudu hata kidogo kazi iliyopewa ya kuzisimamia chaguzi hizo, licha ya mabilioni ya shilingi zilizotumika.
Baada ya uchaguzi wa marudio wa Septemba 26, mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati alisema asilimia 47 kati ya watu zaidi ya milioni 19 walioandikishwa kupiga kura ndio walishiriki katika zoezi hilo. Baada ya saa chache alidai kwamba asilimia 38 ya watu walio na haki ya kupiga kura ndiyo waliotumbukiza kura zao.
Kila kura kutoka katika wilaya za uchaguzi zilipojumlishwa mwishowe katika makao makuu mjini Nairobi, matokeo yalibadilika.
Huenda hii ilitokana na kuhesabiwa sivyo, kwa makosa, lakini pia isikatalike moja kwa moja kwamba jambo hilo huenda lilifanyika kwa makusudi.
Kilichojidhihirika wazi, hata hivyo, ni kwamba tume hiyo ya IEBC isingeachiliwa hata kidogo kusimamia uchaguzi wa Agosti 8, seuze tena kabisa ule wa marudio wa Septemba 26. Tume hiyo imejifanya kuwa kichekesho kwa Wakenya na kwa walimwengu pia. Lakini kulikuwa hakuna mbadala. IEBC ndiyo inayotakiwa na Katiba ya Kenya isimamie chaguzi za nchi hiyo, tangu za kaunti, bunge, Baraza la senati, magavana hadi ule wa rais wa nchi.
Idadi ya kura zilizopigwa na zile zinazodaiwa amepata Rais mteule, Uhuru Kenyatta zinabishiwa na wapinzani. Katika uchaguzi wa urais wa marudio watu walishuhudia namna vituo kadhaa vya uchaguzi vilivyobakia vitupu au kuwa na milolongo mifupi ya watu waliotaka kupiga kura, wacha kwamba sehemu kadhaa za nchi hakujafanywa uchaguzi kutokana na vurugu na watu walioususia uchaguzi na kuzifunga barabara za kupitia magari ya kusafirisha vifaa vya uchaguzi.
Wiki moja kabla ya kufanywa uchaguzi wa marudio, Chebukati alikiri kwamba asingeweza kuhakikisha kwamba uchaguzi huo ungekuwa wa kuaminika na salama. Lakini siku mbili kabla ya uchaguzi alibadilisha kauli yake na akasema kwamba ana matumaini uchaguzi huo ungekwenda vizuri. Kitu gani kilichomfanya afikie uamuzi huo hajakitaja.
Itakuwa maajabu pindi matokeo ya uchaguzi wa Septemba 26 hayatabishwa na mtu yeyote mbele ya Mahakama Kuu ya Katiba ya Kenya, seuze tena na upinzani.
Mambo yanatazamiwa yatakuwa kama vile baada ya uchaguzi wa Agosti 8, na huenda Mahakama Kuu ya Kikatiba ikaubatilisha tena uchaguzi wa Septemba 26, kwa hoja ya kutoendeshwa kwa mujibu wa katiba na sheria. Dosari ya uchaguzi wa Septemba 26 yanaonekana ni mengi zaidi kuliko yale ya Agosti Nane.
Muda mfupi kabla ya IEBC kutangaza matokeo ya Uchaguzi wa Agosti 8, waangalizi wa kigeni wa uchaguzi huo kwa haraka walianza kutoa taarifa wakidai uchaguzi huo ulikuwa safi kabisa, huru na wa haki, na kwamba ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta aliyekiongoza Chama cha Jubilee ulikuwa wa haki na bila dosari.
Walimtaka kiongozi wa Upinzani wa Muungano wa NASA, Raila Odinga akubali ameshindwa, ama sivyo, walimtuliza aende mahakamani kubisha, lakini si kuwaruhusu wafuasi wake waende kulalamika mabarabarani.
Odinga alihisi ameporwa ushindi alioudai ni wake kama ule wa chaguzi tatu za hapo kabla. Alikwenda mahakamani na akashinda, majaji wakiamuru uchaguzi mpya urudiwe. Hilo lilikuwa kofi kubwa lililopigwa juu ya mashavu ya waangalizi wa uchaguzi kutoka ng’ambo, hasa wale wa nchi za Ulaya Magharibi na wa Marekani (Kutoka Wakfu wa Jimmy Carter waliongozwa na waziri wa zamani wa mambo ya kigeni wa Marekani, John Kerry).
Katika Kenya, kama ilivyo katika nchi nyingi za Afrika, kuna desturi ya mgombea aliyeshindwa katika uchaguzi mara nyingi kulalamika kwamba ameibiwa ushindi, kwamba uchaguzi ulifanyika kwa udanganyifu.
Malalamiko hayo mara nyingi huwa yana sababu za kimsingi. Ndio maana kabla ya uchaguzi wa Agosti 8 huko Nairobi, Serikali ya Marekani na Umoja wa Ulaya ziliamua ziipatie Kenya kompyuta mpya za kuhesabia kura ili angalau kupunguza malalamiko ya udanganyifu katika zoezi la kupiga kura. Mfumo wa kuhesabu kura katika Kenya ni wa kielektroni, kinyume na ule wa kuhesabu kwa mkono tu, na ambao unapunguza wizi wa kura.
Hadi Euro nusu bilioni zilitumika kununulia kompyuta hizo, na sehemu kubwa ya fedha hizo zilirejea Ulaya kwani ni makampuni ya Ulaya yaliyopewa kandarasi za kuiuzia IEBC kompyuta hizo.
Hayo yalifanyika licha ya kwamba Kenya inayo makampuni yanayoanza kufanikiwa katika shughuli hiyo. Siku ya uchaguzi kompyuta hizo mpya zilianza kufanya kazi, bila ya shaka kwa furaha ya pia waangalizi wa nchi za Magharibi. Na haijawa pia mshangao kwa waangalizi hao wa Magharibi kutamka mara baada ya uchaguzi kwamba mambo yote yalienda salama na kwa haki.
Mahakama Kuu ya Katiba ya Kenya iliyamulika zaidi matokeo ya Uchaguzi wa Agosti Nane na ikagundua kwamba kompyuta hizo mpya zilitoa uwezekano wa kuchakachua zaidi matokeo.
Siku chache kabla ya kufanywa uchaguzi, mkuu wa kitengo cha mawasiliano ya kompyuta cha IEBC, Chris Msando aliuawa, hivyo kutumia data zake za siri katika kuchakachua zaidi matokeo ya uchaguzi. Kwanini hayo yote hayajatajwa katika ripoti za waangalizi wa nchi za Magharibi?
Jibu ni kwamba wao walitaka uchaguzi ufanyike kwa vyovyote vile bila ya kujali kasoro mbalimbali zilizochomoza ambazo zingewekea alama kubwa za kuuliza juu ya busara ya kufanyika uchaguzi huo wakati huo. Pale Mahakama Kuu ya Katiba ya Kenya ilipogundua kwamba uchaguzi wa Agosti 8 haujawa chochote kingine bali ni uchafuzi, hivyo inabidi ufanyike mpya mwingine, wakaguzi hao wa Magharibi walishangilia na kusifu kwamba tukio hilo ni la mara ya kwanza katika Afrika - ni ushindi wa demokrasia.
John Kerry alijitoa kimasomaso na kufikia karibu kukiri makosa aliyoyafanya ya harakaharaka kuupa uchaguzi huo hati safi kabisa na kuzikubali mbiombio hesabu zilizotolewa na IEBC kwa msaada wa kompyuta za nchi za Magharibi.
Raila Odinga alizikejeli nchi za Magharibi pale aliposema kwamba “ushindi” wa Uhuru Kenyatta ulikuwa wa “Vifaranga vya Kompyuta.” Waangalizi wa nchi za magharibi walisahau kwamba kompyuta hizo za nchi za Magharibi zilikuwa zinasimamiwa na Wakenya waliokuwamo ndani ya sekretariati ya IEBC.
Swali la msingi ni kwanini nchi za Magharibi zilizotuma waangalizi wao huko Nairobi hazijajiuliza kama lilikuwa wazo zuri kwa IEBC, iliyochafua uchaguzi wa mwanzo wa Agosti 8, iruhusiwe isimamie tena uchaguzi wa marudio, tena bila ya kuyasahihisha makosa yaliofanywa katika uchaguzi wa mwanzo, na bila ya kuwawajibisha maofisa waliosababisha uchafuzi katika uchaguzi wa mwanzo?
Nchi za Magharibi, licha ya kuyaona mbele ya macho yao, maajabu yote hayo, zilinyamaza kimya. Demokrasia inayozungumzwa na kushikiliwa katika nchi hizo za Magharibi, si ile ambayo Wazungu wanaitakia Afrika. La mwanzo kwa Wazungu hao ni kuitakia nchi ya Kiafrika “utulivu” pale utulivu huo utaendeleza pia maslahi yao ya kiuchumi au ya kijeshi. Pia cha mwanzo kwao ni “kuchochea vurugu” pale vurugu hizo zitasaidia pia, kwa muda fulani, kupeleka mbele maslahi yao ya kisiasa, kiuchumi na kijeshi.
Kwa nchi za Magharibi hivi sasa Kenya iliyo “tulivu” ndiyo kipaumbele, na jambo hilo ni zuri, lakini nchi hizo hazijali hata ikiwa demokrasia itapigwa teke, utarejea utawala wa kiimla au udikteta utakaowatenga watu wengi mbali na madaraka ya Serikali.
Uhuru Kenyatta ameshinda, amepata karibu asilimia 100 ya kura zilizopigwa katika uchaguzi wa marudio. Lakini ukweli ni kwamba Wakenya sasa wamegawanyika zaidi kuliko wakati wowote mwingine tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1963.
Raila Odinga aliyeshindwa amesema ataugeuza Umoja wake wa Nasa kuwa vuguvugu la kuukaidi utawala wa Kenyatta. Na magavana wa Mombasa na Kilifi, sehemu ya pwani ya Kenya ambao ni washirika wakubwa wa Raila Odinga, wamezusha suala la uwezekano sehemu yao ya Pwani ya Kenya kujitenge na Kenya kwa vile maslahi yao hayaangaliwi na Serikali kuu ya Jubilee huko Nairobi. Huo si mustakabali mzuri kwa Kenya.
Cha kusikitisha juu ya chaguzi za Kenya ni kwamba uamuzi anakuwa nao mtu anayekamata mwiko jikoni mbele ya sufuria la minofu ya nyama - naye ni rais wa nchi.
Yeye anahakikisha kwamba Tume ya Uchaguzi ina watu wanaomtii au anaoweza kuwatisha pale inapohitajika yeye aendelee kubakia madarakani. Hapo tena haijali nini watakachosema waangalizi wa uchaguzi kama ni wa ndani au wa nje.
Kwa vyovyote waangalizi wa nje hukaa katika nchi inayohusika kwa siku chache. Isitarajiwe kwamba wao ni wajuzi tosha wa siasa na mabishano yalio ndani ya jamii za Kiafrika. Ni makosa kutegemea ripoti zao kuwa ndiyo ukweli wote wa mwisho, asilimia 100, kama uchaguzi uliofanyika ulikuwa wa haki na sawa.
Swali jingine linazuka kwamba inakuwaje chaguzi za Afrika mara nyingi hujiwa na waangalizi wa kutoka Ulaya na Marekani na kinyume na hivyo si sana kusikika?
Karika jibu lake usiusahau ule msemo kwamba anayelipia muziki ndiye mwenye haki ya kuucheza muziki wenyewe. Chaguzi katika nchi nyingi za Afrika hugharimiwa pia na fedha za kutoka nchi wafadhili za Ulaya na Marekani.

Kamatakamata ya wapinzani yageuka mwiba kampeni za uchaguzi wa madiwani

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akitoka nje ya Ofisi za Kitengo cha Uhalifu wa Makosa ya Kifedha kilichopo Kamata jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni mdogo wake Thabitha Kabwe na kulia ni Ofisa Habari wa Chama hicho, Abdallah Khamis. Picha na Ericky Boniphace 
Kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani zinaendelea kushika kasi katika kata 43 nchini. Ni uchaguzi uliosubiriwa kwa hamu kubwa na vyama vya siasa.
Vyama vya siasa, hasa vya upinzani vinataka kutumia miku-tano hiyo kuzungumzia masuala mbalimbali ya kitaifa na kukiko-soa chama tawala na Serikali yake katika masuala mbalimbali baada ya kukosa nafasi hiyo kutokana na marufuku ya mikutano ya hadhara na maandamano.
Vilevile, vinataka kupima kuku-balika kwake kwa wananchi baa-da ya siku nyingi za kutoonana nao mikutanoni kiasi cha kubadili mkakati na kuanza kuwasiliana na wananchi kwa kutumia katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, huku chama tawa-la kikitegemea zaidi mikutano ya mwenyekiti wake, Rais John Magufuli.
Hata hivyo, inaelekea wap-inzani hawataweza kukata kiu yao baada ya Jeshi la Polisi kuanza kuwakamata na kuwahoji vion-gozi na wafuasi wa vyama hivyo kwa tuhuma tofauti zitokanazo na mikutano hiyo.
Jijini Dar es Salaam wiki iliyopita jeshi hilo lilimkamata kiongozi wa chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe kwa madai ya kutoa kauli za uchochezi wakati wa uzinduzi wa kampeni za udiwani katika Kata ya Kijichi.
Kiongozi huyo mpaka sasa anaripoti polisi baada ya jeshi hilo kuchukua maelezo yake na kuendelea na uchunguzi na endapo litajiridhisha kuhusu makosa hayo, kiongozi huyo atafikishwa mahakamani.
Wakati kiongozi huyo akiendelea kuripoti polisi, mwishoni mwa wiki jeshi hilo mkoani Arusha liliwakamata wafuasi 12 wa Chadema kwa madai kuwa walimshambulia mgombea wa CCM wa Kata ya Muriet, Francis Mbise.
Miongoni mwa wanaoshikiliwa ni kaimu katibu wa Chadema wilayani Arusha, Innocent Kisanyage.
Mbali na wafuasi hao, polisi pia wamekamata gari la matangazo la Chadema ambalo inaelezwa lilikuwa linatumika kutangaza mikutano ya chama hicho katika kampeni za uchaguzi mdogo.
Katika taarifa yake, kamanda wa polisi wa Arusha, Charles Mkumbo anasema wafuasi hao walikamatwa kwa kuwavamia wafuasi wa CCM wakati wakitoka kwenye mikutano ya kampeni eneo la Muriet na kuanza kuwashambulia na kwamba Mbise alishambuliwa na kuumizwa sehemu mbalimbali mwilini na kupelekwa hospitalini kwa matibabu.
Taarifa zaidi zinasema pia mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema anatafutwa na jeshi hilo na kwamba wakati wowote atakamatwa kutokana na kauli zake.
Juzi, mbunge huyo alipinga kukamatwa kwa wafuasi hao pamoja na gari la matangazo, akisema kitendo hicho kinalenga kuathiri uzinduzi wa kampeni.
Lema alinukuliwa akisema alikwenda polisi kuwawekea dhamana wafuasi hao, lakini ilishindikana ikielezwa ni kutokana na maelekezo kutoka ngazi za juu.
Si matukio hayo tu, hata Mbunge wa Ndanda ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kusini, Cecil Mwambe amejikuta mikononi mwa polisi baada ya kudaiwa kusema maneno ya uchochezi katika mkutano wa kampeni hizo mjini Mtwara.
Kwa takriban miaka miwili sasa, wanasiasa wa vyama shindani wamekosa jukwaa la kuikosoa Serikali mbele ya wananchi, lakini sasa angalau walitegemea wamepata fursa ya sehemu ya kupumulia kutokana na kuwepo kwa kampeni hizo za uchaguzi mdogo utakaofanyika Novemba 26, mwaka huu baada ya waliokuwa wakishikilia nafasi hizo kujiuzulu au kufariki dunia.
Kamatakamata hiyo inayohusisha wanasiasa wa upande mmoja inaweza kuathiri uchaguzi huo na kutafsiriwa kuwa inalenga kuupendelea upande mmoja.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwahi kunukuliwa na gazeti hili akisema mikutano hiyo ya uchaguzi ina umuhimu mkubwa tofauti na ya hadhara.
Kauli hiyo iliungwa na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliyetuma salamu kutokea Hospitali ya Nairobi ambako anatibiwa baada ya kushambuliwa kwa risasi, akitaka wananchi kutumia nafasi hiyo kutoipigia kura CCM.
Katika salamu hizo alizotuma kwa njia ya sauti iliyorekodiwa akiwa kitandani, Lissu anasema kuendelea kuipa kura CCM ni kuruhusu hali ya kupigana risasi hadharani, ubomoaji nyumba, ukamataji wanasiasa na ukandamizaji kuendelea na hivyo kuwataka wananchi kujitokeza kuipigia kura Chadema.
Wakati Chadema wakijipanga hivyo, Abdul Kambaya, ambaye ni mkurugenzi wa habari wa CUF upande wa Profesa Ibrahim Lipumba anasema chama chake kitatumia kampeni hizo kukata kiu ya siasa waliyonyimwa kwa karibu miaka miwili.
“Kwanza tulikosa nafasi ya kujenga vyama vyetu kwa mujibu wa sheria na Katiba, hivyo hatua ya kamatakamata haitutishi,” anasema Kambaya.
“Tutaitumia fursa hiyo kuzungumza ajenda zetu katika chama. Kwa mfano, suala la maendeleo na utawala wa sheria. Kwa sasa hali inavyokwenda bila kufuata sheria tunaelekea kubaya.”
Lakini, mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Profesa Gaudens Mpangala anasema vyama vya upinzani visiogope na vitumie nafasi hiyo kujipambanua.
Hata hivyo, Profesa Mpangala anaonya tabia hiyo ya Jeshi la Polisi ya kuwakamata wapinzani inaweza kuathiri uchaguzi huo kwa kutotoa fursa sawa kwa washiriki wote.
“Ni fursa nzuri. Watumie nafasi hiyo kupeleka hoja kwa wananchi ili kupinga yale yote yaliyokuwa yakiwaminya ili wananchi waamue,” alisema.
Profesa Mpangala anasema kwa muda wote wa miaka miwili hakukuwa na usawa katika shughuli za kisiasa kutokana na chama tawala kutumia shughuli za kiserikali kufanya siasa, huku upinzani ukikatazwa.
“Mara kadhaa tumeshuhudia Rais akiwa katika ziara za kiserikali akichomekea masuala mbalimbali ya kisiasa. Hakukuwa na usawa hata kidogo,” anasema Profesa Mpangala na kuongeza kuwa hata kinachofanyika sasa kikiendelea hakileti usawa.
Profesa Mpangala alitahadharisha kuwa endapo hali hiyo itaendelea mpaka 2020, Uchaguzi Mkuu utakuwa na kasoro kubwa kutokana na Serikali kushindwa kutoa haki na uhuru sawa kwa vyama vyote.
Anasema kipindi cha kampeni wanasiasa waachiwe wafanye kampeni za kistaarabu ili kuweka usawa badala ya kuwatisha kwa kuwakamata.
Jeshi la Polisi lanena
Wakati hali ikiwa hivyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Barnabas Mwakalukwa anasema Jeshi la polisi linaongozwa kwa mujibu wa sheria na wao kama wasimamizi wa sheria hizo ni lazima wahakikishe hazivunjwi.
Mwakalukwa anasema kuwa Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa kufuata taratibu na sheria na kwamba kila kamanda wa mkoa ana haki ya kukamata watu wote wanaofanya jinai au kuvunja sheria.
“Hata kama ni kipindi cha kampeni ni lazima kila mmoja afuate sheria, huwezi kujificha katika mwamvuli wa kampeni na kufanya jinai tukuangalie. Tutawakamata na tutaendelea kuwakamata mpaka pale watakapoona umuhimu wa kufuata sheria.”
Anasema jeshi la polisi katika kuhakikisha inafanikisha uchaguzi huo wamejipanga kutoa ulinzi katika kipindi chote kuanzia kampeni, wakati wa uchaguzi na siku ya kutangaza matokeo ili watu wapate haki yao ya kidemokrasia.
“Huo ndiyo utawala bora, haiwezekani wewe kwa sababu tu ni kiongozi wa upinzani ufanye mambo yasiyostahili kwa kisingizio cha kampeni, halafu tukuangalie. Hata uwe nani tutakukamata kwani hayupo aliye juu ya sheria,” anasisitiza.
Alipoulizwa kwamba haoni hatua hiyo itaathiri uchaguzi huo kwani hautatoa fursa sawa kwa vyama vyote, Mwakalukwa anasema jeshi hilo haliangalii itikadi ya kwamba yoyote atakayejihusisha na jinai atakamatwa.
“Sisi tunashughulika na waalifu, haijalishi anatoka chama cha upinzani au tawala wote tutawapatia haki yao endapo watajihusisha na jinai, mwisho wa siku tunachotaka ni iwepo nidhamu kipindi chote kwa watu wote kufuata sheria,” anasema.

Kipindupindu,utapiamlo watajwa chanzo cha kufa watoto


Morogoro. Watoto 270 walio chini ya umri wa miaka mitano wanafariki dunia kila siku kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo magonjwa.
Idadi hiyo imepungua ikilinganishwa na takwimu za mwaka 2015 zinazoonyesha kuwa idadi ya watoto waliokuwa wakipoteza maisha yao kila siku ilikuwa 2015.
Akizungumza katika Mafunzo ya namna ya kuandika habari za watoto yanayoendeshwa na Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), Mtaalamu wa masuala ya kuzuia maambukizo ya Vrusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa Mtoto kutoka Shirika la Afya Duniani (Unicef), Hafsa Khalfani amesema malaria  na magonjwa yatokanayo na lishe duni yanachangia vifo hivyo.
Khalfani amesema  asilimia 34 ya watoto nchini wana utapiamlo, 20 hawapati mlo kamili, 40 hawapati haki zao za msingi  wakati asilimia 75 wameshafanyiwa ukatili.
Mtaalamu huyo amesema  huyo changamoto zinazowahusu watoto zinaweza kutatuliwa ikiwa kila  mmoja ikiwamo waandishi wa habari watashiriki kuzitatua.
Mwenyekiti wa TEF, Theophil  Makunga amesema  mafunzo hayo yanafanyika ili kuwanoa waandishi kuhusu habari za watoto kutokana na umuhimu wa kuwapo kwaajili ya  kuandika kiweledi habari za watoto lazima waandishi wa habari wabobee kwenye eneo hilo.
Katika hatua nyingine, Ofisa Habari wa Unicef, Usia Nkoma amesema  wazazi wana jukumu la kuhakikisha watoto wao wanasafiri kwenye shule na kurejea nyumbani kwenye usalama.
Amesema  wazazi na walezi wamekumbushwa wajibu wao wa  kuwalinda watoto baada ya baadhi ya tafiti kuonyesha moja ya maeneo wanayofanyiwa ukatili wa ngono  kwenye mabasi ya shule.
Nkoma amesema mtoto wa kwanza kuingia kwenye gari la shule na wa mwisho kushuka wapo hatarini kufanyiwa ukatili huo, ikiwa usafiri huo utabaki na watumishi bila usimamizi wa walimu au walezi.
“Hata kama mzazi umebanwa na kazi bado jukumu la kuhakikisha mtoto yupo salama, mfano tu kwenye  masuala ya usafiri  mtoto wa kwanza kuingia kwenye basi la shule na wa mwisho, ikiwa basi hilo halina muhudumu mwingine au mwalimu ni hatari kwa hiyo, wanafanyiwa ukatili wa kingono,” amesema ma.
Makunga amesema waandishi wa habari wanalo jukumu la kuandika habari zinazowahusu watoto ili kuendelea kuikumbusha jamii itimize wajibu wao.
Akifundisha masuala ya sheria za watoto, Jesse Kwayu amesema chanzo kikubwa cha uhalifu ni malezi hafifu ya watoto.
“Hivi mmewahi kujiuliza mtoto wa mtaani anapokua mtu mzima anaenda wapi? Jambo hili kila mmoja anapaswa kutafakari kwa sababu vinginevyo kila mmoja ataathirika na hili,” amesema.

Kauli ya Majaliwa kuhusu Katiba yapingwa


Dar es Salaam. Wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisema Serikali kwa sasa haina mpango wa kuendeleza mchakato wa Katiba mpya kwa sababu ya gharama, wanasiasa na wanaharakati wamesema hicho si kigezo.
Akijibu swali la mbunge wa Temeke (CUF), Abdallah Mtolea katika maswali ya papo kwa papo bungeni mjini Dodoma juzi, Majaliwa alisema kipaumbele cha Serikali ni kutoa huduma ya jamii kwa wananchi.
Mtolea alitaka kujua mpango wa Serikali kuhusu Katiba mpya baada ya kukwama miaka mitatu iliyopita.
Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashim Rungwe akizungumzia suala hilo alisema, “Mimi nadhani fedha si kitu, suala ni kwamba Watanzania wanataka Katiba mpya. Ama ianze pale ilipoishia au ianzishwe upya.”
“Hata kama kuna huduma za jamii, hii ni nyeti kuliko kitu chochote. Bila hivyo wananchi wanazidi kuteseka, bila Katiba mtazidi kubanwa. Katiba ndiyo msingi, tupate inayofanana na wakati tulionao, siyo Katiba iliyopita, ile tumetoka nayo kwenye mpito wa chama kimoja kuja vyama vingi,” alisema.
Aliyekuwa mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Deus Kibamba alisema kwa kauli ya waziri mkuu haoni dalili za kupatikana kwa Katiba mpya kabla ya mwaka 2020.
“Kwa kauli ya Majaliwa, ndoto ya Katiba mpya itazimika. Labda itokee Watanzania wakatae jambo hili. Lakini kwa hali ilivyo hakuna Katiba mpya,” alisema Kibamba.
Alisema ni wakati muafaka wa kuitishwa kwa mjadala wa kitaifa kuhusu mustakabali wa Taifa na mambo yatakayojadiliwa yatasaidia kuongoza suala la upatikanaji wa Katiba mpya.
Kibamba alisema hakubaliani na hoja ya waziri mkuu kuwa mchakato wa Katiba mpya unahitaji gharama kubwa na kwamba Serikali sasa imejikita kuboresha huduma za jamii.
“Mchakato kwa Katiba mpya ulipofikia hauhitaji gharama kubwa sikubaliani na waziri mkuu kabisa. Ninachokiona ni kwamba wana hofu ya kisiasa, lakini wakae wakijua kadri siku zinavyozidi kwenda watu wanasahau na siku ya kurudia mchakato huu watalazimika kuanza upya,” alisema Kibamba.
Mbali na hilo, alisema anachokiona sasa ni kama Serikali ya CCM imeshindwa kuwaweka watu pamoja na ndiyo maana ndani ya chama hicho kuna dalili za mgawanyiko, baadhi wanasema Katiba si kipaumbele, wengine wanasema ni kipaumbele na ndiyo wanaokihama chama hicho.
Aliyekuwa mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu alisema Katiba mpya ilishapewa kipaumbele na wananchi ndiyo maana walijitokeza kwa wingi kutoa maoni wakati mchakato huo ulipoanza.
“Kinachotakiwa ni Katiba ya wananchi, halafu mambo mengine baadaye. Huwezi kuwa na maendeleo endelevu kama hauna katiba imara, hata Rais John Magufuli anavyosema ananyoosha nchi, atambue hawezi kufanikiwa bila kuwa na Katiba mpya.
“Serikali itambue kitendo cha kupiga danadana suala la Katiba mpya, kitaleta hali ya sintofahamu siku za mbele kwa sababu iliyopo sasa haina maisha na ukizingatia kuna mfumo wa vyama vingi,” alisema Profesa Baregu ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.
Profesa Baregu alisisitiza kuwa endapo Serikali itaendeleza suala la Katiba itakuwa imewaheshimu Watanzania ambao wana kiu ya kuipata ili kuhakikisha ina kuwa na misingi bora ya maendeleo.
Aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu aliungana na Profesa Baregu akisema hoja yake kutaka kurejea upya mjadala wa Katiba mpya kwa kuzingatia Rasimu ya Katiba ilivyowasilishwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba aliyokusudia kuipeleka bungeni kabla ya kujiuzulu ilikuwa na mashiko.
“Niliona kuna vipengele vimeachwa katika Rasimu ya Katiba hasa vya separation of power (mgawanyo wa madaraka) kati ya Serikali, Bunge na Mahakama na ndiyo maana nilitaka wabunge wenzangu tuvijadili vipengele hivi muhimu ili kuzuia mwingiliano ya mihimili hii,” alisema Nyalandu.
Licha ya kwamba amejiuzulu na kujitoa CCM, Nyalandu katika mahojiano na Mwananchi alisema aliiunga mkono Rasimu ya Warioba na ndiyo maana baada ya kujitoa amehamia upande wa waliokuwa wakiiunga tangu mwanzo.
Hata hivyo, Nyalandu alisema hapingani na dhamira nje ya Serikali ya kuboresha huduma kwa Watanzania, lakini suala la Katiba ni miongoni mwa mambo ambayo wananchi wanahitaji, ndiyo maana kwa kutambua hilo Serikali iliyopita ilianzisha mchakato wake
Alisema sasa yupo huru baada ya kutoka ndani ya CCM na kwamba yupo tayari kuungana na wadau wenye nia ya kutetea Katiba mpya.
Mkurugenzi wa Mtandao wa Watetezi wa Binadamu (THRD), Onesmo ole Ngurumwa alisema ni wakati muafaka kwa wataalamu wa Katibu kutoa elimu kwa Serikali kuhusu Katiba.
“Hata sisi tupo tayari kushirikiana nao endapo watakuwa tayari. Kwa sababu hauwezi kuitenganisha Katiba na huduma za jamii, tunaipigania Katiba mpya ili kuweka mfumo bora hata yule kiongozi atakayekuja aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ya kuongoza nchi hii,” alisema Ole Ngurumwa.
Alisema Katiba inajumuisha masuala mbalimbali ikiwamo huduma za kijamii ambazo zitakuwa katika utaratibu bora unaotakiwa na utakaowanufaisha Watanzania wote.

Wabunge waibana Serikali bungeni


Dodoma. Mijadala mikali jana ilitawala bungeni huku Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye akisema miradi mikubwa itakayotekelezwa na Serikali, itafanya deni la Taifa kufikia dola za Marekani 47 bilioni (Sh. 103.4 trilioni)
Hayo yalijitokeza wakati wabunge wakichangia mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa Taifa na mwongozo wa kuandaa bajeti kwa mwaka wa fedha 2018/2019 uliowasilisha bungeni na Waziri wa Fedha na Mpango, Dk Philip Mpango.
Akichangia taarifa hiyo kwa hisia, Nape alisema hapingi kutekelezwa kwa miradi mikubwa ila anapingana na Serikali jinsi ya kuifadhili na kuiendesha kwa kutumia fedha za Serikali.
“Niliposoma nilishtuka kidogo kuona Serikali inapendekeza kuwekeza pesa za Serikali kwenye miradi ambayo inaweza kuendeshwa kibiashara. Nilitegemea miradi hii tungeruhusu sekta binafsi,” alisema.
Alitaja baadhi ya miradi ya ambayo alisema ingeweza kutekelezwa na sekta binafsi kuwa ni ujenzi wa reli ya kisasa ya kati, mradi wa umeme Rufiji, mradi wa bandari na uboreshaji shirika la ndege.
“Kama mpango huu utatekelezwa kama ulivyo, miradi hii inakwenda kuua uchumi wa nchi yetu. Miradi hii mikubwa inaweza kujiendesha kibiashara na ikajilipa yenyewe,” alisisitiza Nape.
Alisema miradi hiyo ni mikubwa na itagharimu fedha nyingi ambazo zitailazimisha Serikali kukopa fedha nyingi, hali ambayo itaathiri deni la Taifa ambalo kwa sasa ni Dola bilioni 26.115 (Sh57.453 trilioni)
“Serikali ikienda kukopa na kwa sababu miradi hii inachukua muda mrefu, maana yake tutaanza kulipa deni kabla ya miradi hiyo haijaanza kurudisha faida kwa Taifa,” alisema katika mchango wake.
“Kuna madhara makubwa kwa deni la Taifa. Ndio hapa ninapohoji uzalendo wa wachumi wetu katika kuishauri Serikali na Rais Magufuli katika kuchukua pesa za Serikali na kuwekeza katika miradi hii.
“Kwa mujibu wa takwimu, ripoti uliyotupa hapa, deni letu la Taifa limefikia Dola 26 bilioni ambayo ni sawa na asilimia 32 ya ustahimilivu wa deni la Taifa. Ukomo ni asilimia 56.
“Sasa kama Dola bilioni 26 zimetupeleka kwenye asilimia 32 unahitaji Dola bilioni 45 kufikia ukomo wa asilimia 56 ambao ni mwisho wa kukopesheka. Tuchukue mifano ya miradi mitatu tu,” alisema na kuendelea, “Ujenzi wa Reli ya Kati ambayo kwa tathmini yake unaweza kugharimu Dola bilioni 15. Stiegler’s Gorge utagharimu Dola bilioni 5 na uboreshaji wa shirika la ndege karibu Dola bilioni 1”
“Kwa hiyo unazungumzia Dola bilioni 21. Ukijumlisha na deni la Taifa la bilioni 26 unazungumzia Dola bilioni 47. Kwa vyovyote vile hii ime bust. Kama inakwenda ku bust maana yake tunakwenda kutokopesheka. Kwa nini tunataka kung’ang’aniza kuchukua pesa ya Serikali? Hebu tufikirie upya. Dk Mpango rudini mkafikiri upya.”
Nape alisema kuanzia awamu ya pili chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi hadi awamu ya nne, Serikali ilitengeneza mazingira mazuri ya kuishirikisha sekta binafsi katika miradi mbalimbali ya kiuchumi.
“Wakati wa awamu ya nne Rais Magufuli alikuwa Waziri wa Ujenzi. Wakati wake waliruhusu wakandarasi kutoka sekta binafsi. Wakachukua mikopo benki wakaanzisha makampuni. Leo dhamana walizozitumia kukopa fedha zinauzwa kwa sababu ya madeni wanayoidai Serikali lakini Serikali nayo imeanza mkondo wa miradi yake ya ujenzi kutekelezwa na Serikali yenyewe.
“Kwa hiyo hawa tuliowatengeneza kwa miaka yote tumewakosesha pesa. Huu mpango wako mzuri lakini rudini kwenye mawazo ya kutumia sekta binafsi. Tukienda hivi tunaenda kuua uchumi,” alisema.
Katika mchango wake, Mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), Anthony Komu alisema Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kurudi kwenye zama za kufanya biashara badala ya kuiachia sekta binafsi.
“Ukiangalia tunataka kujenga uchumi wa viwanda lakini Serikali inarudi kule nyuma tulikotoka kwa Serikali kufanya biashara. Leo hii inamiliki kwa asilimia 100 TTCL (kampuni ya simu),” alisema.
“Leo hii Serikali inamiliki kiwanda cha General Tyre kwa asilimia 100. Leo Hii TBA (Wakala wa Majengo) inafanya kazi za ujenzi. Wajibu wa Serikali ni kujenga mazingira wezeshi kwa sekta binafsi.”
Mbunge wa Mufindi Kaskazini (CCM), Mahmood Mgimwa alisema Serikali inazungumzia uchumi wa nchi unakua, lakini akashangaa maisha ya Watanzania kuwa magumu.
“Tunazungumzia uchumi unakua lakini maisha ya Watanzania yameendelea kuwa magumu wala hayaendani na taarifa za kukua kwa uchumi,” alisema mbunge huyo na kuongeza:
“Tunazungumza hali ya uchumi unakuwa lakini hali za Watanzania ni mbaya. Inaonekana vigezo ulivyovitumia kupima uchumi unakua ni tofauti na tunavyovifikiria sisi.
“Kwa mfano ukichenji Sh10,000 leo unaweza usijue umeitumia kununua nini. Waziri atuambie tuko kwenye mdororo wa uchumi au ni nini? Unatuambia uchumi unakuwa lakini shilingi inashuka.”
Mbunge wa Konde (CUF), Hatibu Said Haji alisema kuiachia Serikali itekeleze kila kitu kwa pesa yake ni jambo ambalo haliwezekani na kuitaka iruhusu sekta binafsi iingie kutekeleza miradi ya kibiashara.
“Miaka kadhaa sasa tunataka kufufua General Tyre lakini ni zaidi ya miaka saba. Kama tunashindwa kufufua kiwanda kama kile licha ya umuhimu wake kwa nini tusiwape watu binafsi?” alihoji Haji.
Wabunge wa Zanzibar waja juu
Moja kati ya jambo lililoibua hisia za wabunge kutoka Zanzibar ni suala la Zanzibar kutohusishwa katika mpango huo licha ya kuuita ni wa taifa wakisema hakuna Taifa la Tanzania bila Zanzibar.
Mbunge wa Mpendae (CCM), Salim Hassan Turky, naye alilalamikia Zanzibar kutojumuishwa katika mpango huo na kutaka urekebishwe uitwe mpango wa maendeleo Taifa Tanzania bara.
“Katika mpango huu hakuna sehemu hata moja iliyowataja Wazanzibari. Kwa namna moja ama nyingine mpango huu umetudhalilisha Wazanzibari. Hatustahili kupangiwa chochote katika taifa letu”.
Mbali na suala la Muungano, mbunge huyo alilalamikia hatua ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kile alichodai kuwanyanyasa Wazanzibari wanaoingiza bidhaa Tanzania Bara.
“Kuna watendaji wa Serikali hawaitendei haki Zanzibar. Bidhaa zinazotoka Zanzibar zinazokuja Tanzania Bara wakionyesha tu risiti wanatakiwa waonyeshe nyaraka za kuingiza hiyo bidhaa.
“Hili lishughulikiwe Wazanzibari wasinyanyaswe. TRA ilipoanzishwa kulikuwa na kauli mbiu kuwa sisi ni patners (wabia) katika maendeleo. Sasa hivi kauli mbiu inaondoka,” alisema na kuongeza:
“TRA imekuwa ni watu wa mabunduki, watu wa mabavu,” alisema mbunge huyo na kusema bila kufafanua kuwa wafanyabiashara hao wanaadhibiwa kwa sababu ya makosa ya Serikali ya Awamu ya Nne.
Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BWZ), Jaku Hashim Ayoub alisema mtu anayekutwa na bidhaa za Zanzibar katika Bandari ya Dar es Salaam ananyanyaswa, “Leo mali za Zanzibar ukiingia nayo utadhani umeingiza unga (dawa za kulevya). Wazanzibar mnatuonea sana” alisema na kuongeza kusema:
“Leo Mzanzibari anachukua gauni zake tatu anakuja nazo bandarini (Dar es salaam) anaambiwa kaa chini. TV moja tu. Huu muungano wa upande mmoja tu?”
Mjadala huo utaendelea hadi Jumatatu kabla ya Bunge kupokea miswada mbalimbali ukiwamo muswada wa kuanzisha Wakala wa Meli Tanzania wa mwaka 2017.

Rais Magufuli amaliza ziara ya siku 3 Uganda, Rais Museveni atoa tamko dhidi ya ICC

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipita kwenye gwaride la Kimya lililoandaliwa kwa heshma na Jeshi la Uganda mara baada ya kumaliza ziara yake ya siku tatu nchini Uganda na kurejea nchini.



 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mke wake Mama Janeth Magufuli wakifurahia ngoma ya asili iliyokuwa ikipigwa na watoto wa nchini Uganda katika eneo la mpakani la Mutukula kabla ya kurejea nchini.  

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi wa mpakani Mutukula upande wa Tanzania mara baada ya kuwasili akitokea Uganda.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi wa Mpakani mwa Tanzania na Uganda (Mutukula) kuhusu  ujenzi wa barabara ya Kutoka Miziro hadi Mutukula bila kupitia wilayani Misenyi. Pembeni yake ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akisikiliza.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi wa mpakani Mutukula upande wa Tanzania mara baada ya kuwasili akitokea Uganda.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi wa mpakani Mutukula upande wa Tanzania mara baada ya kuwasili akitokea Uganda.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na viongozi wakuu wa Majeshi ya Uganda mara baada ya kumaliza ziara yake nchini Uganda.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwapungia wananchi wa mpakani  Mutukula upande wa Uganda mara baada ya kumaliza ziara yake ya siku tau nchini Uganda. PICHA NA IKULU
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwapungia wananchi wa mpakani  Mutukula upande wa Uganda mara baada ya kumaliza ziara yake ya siku tau nchini Uganda. PICHA NA IKULU

WANAWAKE WATAALAMU WA KILIMO ,UVUVI NA MIFUGO WAZINDUA KITABU CHAO KATIKA MKUTANO WA MWAKA WA 21 WA CHAMA CHAO


Mgeni rasmi Bi. Butano Philipo wakiwa na Mwenyekiti wakizindua vitabu mbalimbali ikiwemo kitabu cha  Ufugaji wa samaki.

Chama cha wanawake  wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo,Mifugo,Uvuvi na Mazingira, Tanzania association of women leaders in agriculture and environment  ( TAWLAE) wamefungua rasimi mkutano wa mwaka  wa 21 na kuhudhuriwa na Naibu katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa raisi bi Butamo Philipo kwa  niaba ya waziri wa  Mazingira  Mhe. January Makamba ambao umefanyika  jana katika viwanja vya wizara ya mifugo na uvuvi.

 Akizungumza katika mkutano huo wenyekiti wa chama cha wanawake kiongozi katika kilimo na mazingira Dkt. Sofia Mlote amesema Lengo kubwa la mkutano huo ni kuunganisha wakulima na tafiti mbalimbali  zilizoandaliwa na wataalamu hao.

 Maadhimisho ambayo yamebeba kaulimbiu isemayo  uchumi wa viwanda Tanzania wanawake tupo tayari,hapa ni kazi tu.

Aidha, Dkt. Sofia Mlote amesema kazi ya TAWLAE ni kuwaunganisha wakulima wadogo au wakubwa na tafiti mbalimbali ambaozo  zimetafitiwa hapa nchini  ili kuongeza uwekezaji na ajira kwa watanzania katika kilimo.

Akizungumza Dkt.Mlote amesema kilimo kilikuwa na faida ndogo kwa sababu utalaam,teknolojia na juhudi zilikuwa bado hazijatumika vizuri katika kilimo
 kuingia na uchumi wa viwanda  ni lazima uzalishaji  wa kilimo uwe na  tija , kuwepo na uboreshaji wa masoko na teknolojia ambapo wataalamu wanawake ndio wanajukumu kubwa katika kuleta mapinduzi ya kilimo alisema Dkt.Mlote
Getrude Mongela mlezi wa Tawlea ambaye ana PHD ya Philosophy alisema wanawake Uchumi wa viwanda Tanzania wanawake tupo tayari , Hapa kazi tu.

Vile vile amefarijika kuona amelea wanawake toka wakiwa wadogo na sasa wamesoma na wengine wana PHD lengo kubwa hasa alisistiza mpaka kufikia 2020 wanawake wawe wamekua kiuchumi na kuendelea kutoa  wasomi wa kutosha na kufikia malengo.
Kiongozi wa Chama cha Wanawake viongozi katika Kilimo na Mazingira Dkt. Sophia Mlote akimkaribisha mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya makamu wa raisi Bi. Butano Philipo katika uzinduzi wa mkutano huo leo.