Saturday, November 11

Kauli ya Majaliwa kuhusu Katiba yapingwa


Dar es Salaam. Wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisema Serikali kwa sasa haina mpango wa kuendeleza mchakato wa Katiba mpya kwa sababu ya gharama, wanasiasa na wanaharakati wamesema hicho si kigezo.
Akijibu swali la mbunge wa Temeke (CUF), Abdallah Mtolea katika maswali ya papo kwa papo bungeni mjini Dodoma juzi, Majaliwa alisema kipaumbele cha Serikali ni kutoa huduma ya jamii kwa wananchi.
Mtolea alitaka kujua mpango wa Serikali kuhusu Katiba mpya baada ya kukwama miaka mitatu iliyopita.
Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashim Rungwe akizungumzia suala hilo alisema, “Mimi nadhani fedha si kitu, suala ni kwamba Watanzania wanataka Katiba mpya. Ama ianze pale ilipoishia au ianzishwe upya.”
“Hata kama kuna huduma za jamii, hii ni nyeti kuliko kitu chochote. Bila hivyo wananchi wanazidi kuteseka, bila Katiba mtazidi kubanwa. Katiba ndiyo msingi, tupate inayofanana na wakati tulionao, siyo Katiba iliyopita, ile tumetoka nayo kwenye mpito wa chama kimoja kuja vyama vingi,” alisema.
Aliyekuwa mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Deus Kibamba alisema kwa kauli ya waziri mkuu haoni dalili za kupatikana kwa Katiba mpya kabla ya mwaka 2020.
“Kwa kauli ya Majaliwa, ndoto ya Katiba mpya itazimika. Labda itokee Watanzania wakatae jambo hili. Lakini kwa hali ilivyo hakuna Katiba mpya,” alisema Kibamba.
Alisema ni wakati muafaka wa kuitishwa kwa mjadala wa kitaifa kuhusu mustakabali wa Taifa na mambo yatakayojadiliwa yatasaidia kuongoza suala la upatikanaji wa Katiba mpya.
Kibamba alisema hakubaliani na hoja ya waziri mkuu kuwa mchakato wa Katiba mpya unahitaji gharama kubwa na kwamba Serikali sasa imejikita kuboresha huduma za jamii.
“Mchakato kwa Katiba mpya ulipofikia hauhitaji gharama kubwa sikubaliani na waziri mkuu kabisa. Ninachokiona ni kwamba wana hofu ya kisiasa, lakini wakae wakijua kadri siku zinavyozidi kwenda watu wanasahau na siku ya kurudia mchakato huu watalazimika kuanza upya,” alisema Kibamba.
Mbali na hilo, alisema anachokiona sasa ni kama Serikali ya CCM imeshindwa kuwaweka watu pamoja na ndiyo maana ndani ya chama hicho kuna dalili za mgawanyiko, baadhi wanasema Katiba si kipaumbele, wengine wanasema ni kipaumbele na ndiyo wanaokihama chama hicho.
Aliyekuwa mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu alisema Katiba mpya ilishapewa kipaumbele na wananchi ndiyo maana walijitokeza kwa wingi kutoa maoni wakati mchakato huo ulipoanza.
“Kinachotakiwa ni Katiba ya wananchi, halafu mambo mengine baadaye. Huwezi kuwa na maendeleo endelevu kama hauna katiba imara, hata Rais John Magufuli anavyosema ananyoosha nchi, atambue hawezi kufanikiwa bila kuwa na Katiba mpya.
“Serikali itambue kitendo cha kupiga danadana suala la Katiba mpya, kitaleta hali ya sintofahamu siku za mbele kwa sababu iliyopo sasa haina maisha na ukizingatia kuna mfumo wa vyama vingi,” alisema Profesa Baregu ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.
Profesa Baregu alisisitiza kuwa endapo Serikali itaendeleza suala la Katiba itakuwa imewaheshimu Watanzania ambao wana kiu ya kuipata ili kuhakikisha ina kuwa na misingi bora ya maendeleo.
Aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu aliungana na Profesa Baregu akisema hoja yake kutaka kurejea upya mjadala wa Katiba mpya kwa kuzingatia Rasimu ya Katiba ilivyowasilishwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba aliyokusudia kuipeleka bungeni kabla ya kujiuzulu ilikuwa na mashiko.
“Niliona kuna vipengele vimeachwa katika Rasimu ya Katiba hasa vya separation of power (mgawanyo wa madaraka) kati ya Serikali, Bunge na Mahakama na ndiyo maana nilitaka wabunge wenzangu tuvijadili vipengele hivi muhimu ili kuzuia mwingiliano ya mihimili hii,” alisema Nyalandu.
Licha ya kwamba amejiuzulu na kujitoa CCM, Nyalandu katika mahojiano na Mwananchi alisema aliiunga mkono Rasimu ya Warioba na ndiyo maana baada ya kujitoa amehamia upande wa waliokuwa wakiiunga tangu mwanzo.
Hata hivyo, Nyalandu alisema hapingani na dhamira nje ya Serikali ya kuboresha huduma kwa Watanzania, lakini suala la Katiba ni miongoni mwa mambo ambayo wananchi wanahitaji, ndiyo maana kwa kutambua hilo Serikali iliyopita ilianzisha mchakato wake
Alisema sasa yupo huru baada ya kutoka ndani ya CCM na kwamba yupo tayari kuungana na wadau wenye nia ya kutetea Katiba mpya.
Mkurugenzi wa Mtandao wa Watetezi wa Binadamu (THRD), Onesmo ole Ngurumwa alisema ni wakati muafaka kwa wataalamu wa Katibu kutoa elimu kwa Serikali kuhusu Katiba.
“Hata sisi tupo tayari kushirikiana nao endapo watakuwa tayari. Kwa sababu hauwezi kuitenganisha Katiba na huduma za jamii, tunaipigania Katiba mpya ili kuweka mfumo bora hata yule kiongozi atakayekuja aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ya kuongoza nchi hii,” alisema Ole Ngurumwa.
Alisema Katiba inajumuisha masuala mbalimbali ikiwamo huduma za kijamii ambazo zitakuwa katika utaratibu bora unaotakiwa na utakaowanufaisha Watanzania wote.

No comments:

Post a Comment