Hayo yalijitokeza wakati wabunge wakichangia mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa Taifa na mwongozo wa kuandaa bajeti kwa mwaka wa fedha 2018/2019 uliowasilisha bungeni na Waziri wa Fedha na Mpango, Dk Philip Mpango.
Akichangia taarifa hiyo kwa hisia, Nape alisema hapingi kutekelezwa kwa miradi mikubwa ila anapingana na Serikali jinsi ya kuifadhili na kuiendesha kwa kutumia fedha za Serikali.
“Niliposoma nilishtuka kidogo kuona Serikali inapendekeza kuwekeza pesa za Serikali kwenye miradi ambayo inaweza kuendeshwa kibiashara. Nilitegemea miradi hii tungeruhusu sekta binafsi,” alisema.
Alitaja baadhi ya miradi ya ambayo alisema ingeweza kutekelezwa na sekta binafsi kuwa ni ujenzi wa reli ya kisasa ya kati, mradi wa umeme Rufiji, mradi wa bandari na uboreshaji shirika la ndege.
“Kama mpango huu utatekelezwa kama ulivyo, miradi hii inakwenda kuua uchumi wa nchi yetu. Miradi hii mikubwa inaweza kujiendesha kibiashara na ikajilipa yenyewe,” alisisitiza Nape.
Alisema miradi hiyo ni mikubwa na itagharimu fedha nyingi ambazo zitailazimisha Serikali kukopa fedha nyingi, hali ambayo itaathiri deni la Taifa ambalo kwa sasa ni Dola bilioni 26.115 (Sh57.453 trilioni)
“Serikali ikienda kukopa na kwa sababu miradi hii inachukua muda mrefu, maana yake tutaanza kulipa deni kabla ya miradi hiyo haijaanza kurudisha faida kwa Taifa,” alisema katika mchango wake.
“Kuna madhara makubwa kwa deni la Taifa. Ndio hapa ninapohoji uzalendo wa wachumi wetu katika kuishauri Serikali na Rais Magufuli katika kuchukua pesa za Serikali na kuwekeza katika miradi hii.
“Kwa mujibu wa takwimu, ripoti uliyotupa hapa, deni letu la Taifa limefikia Dola 26 bilioni ambayo ni sawa na asilimia 32 ya ustahimilivu wa deni la Taifa. Ukomo ni asilimia 56.
“Sasa kama Dola bilioni 26 zimetupeleka kwenye asilimia 32 unahitaji Dola bilioni 45 kufikia ukomo wa asilimia 56 ambao ni mwisho wa kukopesheka. Tuchukue mifano ya miradi mitatu tu,” alisema na kuendelea, “Ujenzi wa Reli ya Kati ambayo kwa tathmini yake unaweza kugharimu Dola bilioni 15. Stiegler’s Gorge utagharimu Dola bilioni 5 na uboreshaji wa shirika la ndege karibu Dola bilioni 1”
“Kwa hiyo unazungumzia Dola bilioni 21. Ukijumlisha na deni la Taifa la bilioni 26 unazungumzia Dola bilioni 47. Kwa vyovyote vile hii ime bust. Kama inakwenda ku bust maana yake tunakwenda kutokopesheka. Kwa nini tunataka kung’ang’aniza kuchukua pesa ya Serikali? Hebu tufikirie upya. Dk Mpango rudini mkafikiri upya.”
Nape alisema kuanzia awamu ya pili chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi hadi awamu ya nne, Serikali ilitengeneza mazingira mazuri ya kuishirikisha sekta binafsi katika miradi mbalimbali ya kiuchumi.
“Wakati wa awamu ya nne Rais Magufuli alikuwa Waziri wa Ujenzi. Wakati wake waliruhusu wakandarasi kutoka sekta binafsi. Wakachukua mikopo benki wakaanzisha makampuni. Leo dhamana walizozitumia kukopa fedha zinauzwa kwa sababu ya madeni wanayoidai Serikali lakini Serikali nayo imeanza mkondo wa miradi yake ya ujenzi kutekelezwa na Serikali yenyewe.
“Kwa hiyo hawa tuliowatengeneza kwa miaka yote tumewakosesha pesa. Huu mpango wako mzuri lakini rudini kwenye mawazo ya kutumia sekta binafsi. Tukienda hivi tunaenda kuua uchumi,” alisema.
Katika mchango wake, Mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), Anthony Komu alisema Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kurudi kwenye zama za kufanya biashara badala ya kuiachia sekta binafsi.
“Ukiangalia tunataka kujenga uchumi wa viwanda lakini Serikali inarudi kule nyuma tulikotoka kwa Serikali kufanya biashara. Leo hii inamiliki kwa asilimia 100 TTCL (kampuni ya simu),” alisema.
“Leo hii Serikali inamiliki kiwanda cha General Tyre kwa asilimia 100. Leo Hii TBA (Wakala wa Majengo) inafanya kazi za ujenzi. Wajibu wa Serikali ni kujenga mazingira wezeshi kwa sekta binafsi.”
Mbunge wa Mufindi Kaskazini (CCM), Mahmood Mgimwa alisema Serikali inazungumzia uchumi wa nchi unakua, lakini akashangaa maisha ya Watanzania kuwa magumu.
“Tunazungumzia uchumi unakua lakini maisha ya Watanzania yameendelea kuwa magumu wala hayaendani na taarifa za kukua kwa uchumi,” alisema mbunge huyo na kuongeza:
“Tunazungumza hali ya uchumi unakuwa lakini hali za Watanzania ni mbaya. Inaonekana vigezo ulivyovitumia kupima uchumi unakua ni tofauti na tunavyovifikiria sisi.
“Kwa mfano ukichenji Sh10,000 leo unaweza usijue umeitumia kununua nini. Waziri atuambie tuko kwenye mdororo wa uchumi au ni nini? Unatuambia uchumi unakuwa lakini shilingi inashuka.”
Mbunge wa Konde (CUF), Hatibu Said Haji alisema kuiachia Serikali itekeleze kila kitu kwa pesa yake ni jambo ambalo haliwezekani na kuitaka iruhusu sekta binafsi iingie kutekeleza miradi ya kibiashara.
“Miaka kadhaa sasa tunataka kufufua General Tyre lakini ni zaidi ya miaka saba. Kama tunashindwa kufufua kiwanda kama kile licha ya umuhimu wake kwa nini tusiwape watu binafsi?” alihoji Haji.
Wabunge wa Zanzibar waja juu
Moja kati ya jambo lililoibua hisia za wabunge kutoka Zanzibar ni suala la Zanzibar kutohusishwa katika mpango huo licha ya kuuita ni wa taifa wakisema hakuna Taifa la Tanzania bila Zanzibar.
Mbunge wa Mpendae (CCM), Salim Hassan Turky, naye alilalamikia Zanzibar kutojumuishwa katika mpango huo na kutaka urekebishwe uitwe mpango wa maendeleo Taifa Tanzania bara.
“Katika mpango huu hakuna sehemu hata moja iliyowataja Wazanzibari. Kwa namna moja ama nyingine mpango huu umetudhalilisha Wazanzibari. Hatustahili kupangiwa chochote katika taifa letu”.
Mbali na suala la Muungano, mbunge huyo alilalamikia hatua ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kile alichodai kuwanyanyasa Wazanzibari wanaoingiza bidhaa Tanzania Bara.
“Kuna watendaji wa Serikali hawaitendei haki Zanzibar. Bidhaa zinazotoka Zanzibar zinazokuja Tanzania Bara wakionyesha tu risiti wanatakiwa waonyeshe nyaraka za kuingiza hiyo bidhaa.
“Hili lishughulikiwe Wazanzibari wasinyanyaswe. TRA ilipoanzishwa kulikuwa na kauli mbiu kuwa sisi ni patners (wabia) katika maendeleo. Sasa hivi kauli mbiu inaondoka,” alisema na kuongeza:
“TRA imekuwa ni watu wa mabunduki, watu wa mabavu,” alisema mbunge huyo na kusema bila kufafanua kuwa wafanyabiashara hao wanaadhibiwa kwa sababu ya makosa ya Serikali ya Awamu ya Nne.
Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BWZ), Jaku Hashim Ayoub alisema mtu anayekutwa na bidhaa za Zanzibar katika Bandari ya Dar es Salaam ananyanyaswa, “Leo mali za Zanzibar ukiingia nayo utadhani umeingiza unga (dawa za kulevya). Wazanzibar mnatuonea sana” alisema na kuongeza kusema:
“Leo Mzanzibari anachukua gauni zake tatu anakuja nazo bandarini (Dar es salaam) anaambiwa kaa chini. TV moja tu. Huu muungano wa upande mmoja tu?”
Mjadala huo utaendelea hadi Jumatatu kabla ya Bunge kupokea miswada mbalimbali ukiwamo muswada wa kuanzisha Wakala wa Meli Tanzania wa mwaka 2017.
No comments:
Post a Comment