Saturday, November 11

Nyalandu, Mbowe kumnadi mgombea wa Chadema


Dar es Salaam. Aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini Lazaro Nyalandu kesho ataungana na viongozi wa Chadema kwenye kampeni za  uchaguzi mdogo wa udiwani utakaofanyika katika kata 43 nchi.
 Akizungumza leo Novemba 11, kwenye ufunguzi wa kampeni hizo Kimara Suka jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chadema Freeman  Mbowe amesema  amempokea Nyalandu na ataungana naye kwenye mkutano mwingine kama huo utakaofanyika Mtwara mjini hapo kesho.
‘’Kila anayeondoka chama tawala anaitwa fisadi, potelea mbali wamempokea na wengine wengi watahamia kuleta mabadiliko’’ amesema na kuongeza
"Mabadiliko hayaji  ghafla  yanakuja taratibu na ujio wao ndiyo mwanzo wa mabadiliko  tulipoanza na tulipo sasa kuna tofauti kubwa" amesema  Mbowe.
Amefafanua  kwamba haungi mkono nchi kuwa na wezi, lakini anashauri sheria iachwe iamue haki badala ya kuingiliwa kama inavyofanyika kwa mahakama.Huku akidai kwamba watawala wana hofu ndiyo maana hawataki ushauri.
Amesema wataendelea kupigania haki ya kupigania haki ya kufanya mikutano ya kisiasa na ipo siku wataingia mtaani kuidai bila kuogopa vifaru.
Amesema huu siyo wakati wa kuogopa na kukaa kimya ni wakati wa kusimama na kutetea haki ya kufanya siasa.
Kuhusu uchumi kusinyaa amesema ni kweli umesinyaa na inaonekana wazi jinsi maisha yalivyo  wananchi, wafanyabiashara, watawala wote wanalia njaa hakuna mwenye nafuu.
Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob amesema anahitaji kuongeza nguvu ya kuleta maendeleo katika manispaa hiyo, hivyo  mgombea udiwani  kata ya Saranga Ephram Kinyafu anatosha.
Naye Mjumbe wa Kamati Kuu na Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani Frederick Sumaye amehoji kuhusu hali za wananchi kuendelea kuwa mbaya.
"Tumeamua na tunamaanisha wakati huu ushindi ni lazima, na mtakaotupa ushindi ni nyie wananchi" amesema Sumaye.

Rais Magufuli aagiza barabara ya Mutukula-Minziro ijengwe


Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutafuta fedha na kujenga barabara ya Mutukula – Minziro yenye urefu wa kilomita sita ili kurahisisha usafiri wa abiria na mizigo.
Agizo hilo amelitoa leo Jumamosi Novemba 11,2017 katika mji wa Mutukula mpakani mwa Tanzania na Uganda baada ya kupokea kero za wananchi waliokusanyika jirani na geti la kuvuka mpaka huo.
Taarifa ya Ikulu imesema wananchi hao wamedai kukosekana kwa barabara hiyo kunawalazimu kuzunguka kwa kutumia barabara ya Kyaka.
Rais Magufuli pia amewataka viongozi wa Mkoa wa Kagera kufanyia kazi madai ya wananchi waliolalamikia kupata usumbufu katika kizuizi cha Kyaka jirani na Mto Kagera.
Hata hivyo, Rais amewataka wananchi wa Mutukula kutambua kazi ya ulinzi na usalama inayofanywa na vyombo vya dola. Pia, amewataka kutoa ushirikiano kwa viongozi na Serikali katika kuhakikisha mpaka huo unakuwa salama.
Amewataka wananchi kuongeza juhudi katika shughuli za maendeleo, zikiwemo za kilimo na biashara akirejea agizo lake la kuutaka Mkoa wa Kagera kujenga soko la kimataifa katika maeneo ya jirani na mpaka ili wananchi wapate mahali pa kuuzia bidhaa zao kwa njia halali.

Dereva asinzia akiendesha gari


Moshi,Ikungi.Watu saba wamefariki dunia papo hapo baada ya magari kugongana uso kwa uso huku jingine likiingia chini ya uvungu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 11, Kaimu Kamanda Jeshi la Polisi ,Mkoa wa Singida,Isaya Mbughi, amesema ajali ambayo imetokea Ikungi mkoani humo imesababisha vifo vya watu wawili.
Kamanda Mbughi amesema miili ya abiria hao wa ambao majina yao wala makazi yao bado hayajulikana, imehifadhiwa katika hospitali ya misioni Puma.
 Kamanda Mbughi amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa kuna kila  dalili dereva  wa gari ndogo alikuwa amelala na  gari lilihama kutoka upande wa kushoto,na kwenda kulia.
 “Dereva wa basi amejitahidi mno kukwepa gari hilo ndogo,lakini ilishindikana na hivyo kuingia uvunguni mwa basi.Kwa wakati huo,basi lilihama upande wake wa kulia na kwenda nje ya barabara,lakini alilifuata huko huko”,amesema 
Wilayani Hai ,mkoani Kilimanjaro watu watano wamepoteza maisha na wengine wanne wakijeruhiwa baada ya lori kugongana uso kwa uso na Noah  maeneo ya kikavu kwa Sadala.
Daktari wa zamu  hospital ya wilaya ya Hai,Agness Temba amesema amepokea miili ya watu wa tano.
Amesema miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Hai, na majeruhi  wamekimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya KCMC Moshi.

Dk Shika awa gumzo mtandaoni


Dar es Salaam. Wakati Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ikiendelea kumshikilia Dk Louis Shika kwa tuhuma za kuharibu mnada wa nyumba za mfanyabiashara maarufu Said Lugumi, mijadala kuhusu mteja huyo imeendelea kwenye mitandao ya kijamii.
Novemba 9,2017 kampuni ya udalali ya Yono kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliendesha mnada wa nyumba za Lugumi mbili za Mbweni JKT na moja Upanga jijini Dar es Salaam ambazo zote Dk Shika alifikia bei ya kuzinunua kwa Sh3.2 bilioni.
Hata hivyo, Dk Shika amejikuta akiishia mikononi mwa vyombo vya dola baada ya kushindwa kulipa asilimia 25 ya fedha hizo. Nyumba za Mbweni JKT alifika bei kwa Sh900 milioni na nyingine Sh1.1 bilioni, huku ya Upanga alifika bei ya Sh1.2 bilioni.
Akizungumza na Mwananchi, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema, ‘’Tunaendelea kumshikilia na Jumatatu –Novemba 13,2017 kama jalada litakuwa limerudi kutoka kwa mwanasheria wa Serikali tutamfikisha mahakamani.”
Mwonekano wa mavazi, mazungumzo yake na jinsi alivyofika Mbweni JKT uliwatia shaka baadhi ya watu kama kweli Dk Shika amedhamiria kununua nyumba hizo au katumwa na mtu kufanya hizo.
Dk Shika alifika Mbweni kulikofanyika mnada wa nyumba mbili akitumia pikipiki ‘bodaboda’ na alipoulizwa na Mwananchi ametokea wapi na kama ana gari, alisema hana gari kwa kuwa ameingia nchini hivi karibuni akitokea ughaibuni kwa shughuli hiyo ya mnada na anaishi Kigamboni na Tabata Mawenzi.
Katika mitandao ya kijamii tangu Novemba 9,2017 Dk Shika anaendelea kujadiliwa, huku wengine wakitumia picha zake kumjadili wakiziambatanisha na ujumbe mbalimbali.
Ujumbe mwingine unaosambaa ni ule unaoonyesha jinsi alivyokuwa akipandisha bei kushindana na wenzake baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Yono, Scholastica Kevela kutangaza kufungua mnada.
“Mteja atakayefika bei, atatakiwa kulipa leoleo asilimia 25 ya gharama itakayofikia,” alisema Scholastica akifungua mnada na kutaka mwenye ofa kuanza.
Mmoja wa wateja alijitokeza akisema atatoa Sh300 milioni lakini Dk Shika alisema mia tatu hamsini, mwingine akasema mia nne, Dk Shika akasema mia tano lakini baada ya kufikia mia 700, Dk Shika alisema, “Mia tisa itapendekeza sana.’’
Bei hiyo haikufikiwa na mwingine, hivyo alitangazwa mshindi.

Korea Kaskazini: Trump anachafua amani duniani

Rais wa Korea Kaskazini Kim Jong Un
Image captionRais wa Korea Kaskazini Kim Jong Un
Korea Kaskazini imemuelezea Rais Trump kuwa mchafuzi wa amani na utulivu wa dunia, ambaye anatamani vita vya nuklia vitokee.
Wizara ya mashauri ya nchi za nje ya Korea Kaskazini, imekariri nia ya taifa hilo kubaki na silaha zake za nuklia, ikisema silaha hizo zinalinda heshima na uhuru wa nchi.
Matamshi hayo yanasadifiana na mazoezi makubwa ya manuwari za majeshi ya wanamaji, baina ya Marekani na Korea Kusini.
Hii ni mara ya kwanza katika mwongo mzima, ambapo manuwari tatu za Marekani zinazobeba ndege, kuhusika katika mazoezi hayo.
Akiendelea na ziara yake katika bara la Asia, Rais Trump mara kadha, ameionya Korea Kaskazini, kwamba mradi wake wa silaha za nuklia, ni tishio ambalo halitovumiliwa.

Waandamana kupinga ibada ya Waislamu barabarani Paris

Waislamu mjini Paris wakifanya ibada barabaraniHaki miliki ya pichaAFP
Image captionWaislamu mjini Paris wakifanya ibada barabarani
Takriban wanasiasa 100 wa Ufaransa wameandamana katika barabara za makaazi ya Paris kupinga hatua ya Waislamu kufanya ibada ya maombi hadharani.
Wanasiasa hao waliokuwa wakiimba nyimbo ya taifa hilo waliwaondoa takriban wafuasi 200 wa dini ya Kiislamu waliokuwa wakiomba barabarani katika eneo la Clichy.
Maafisa wa polisi hatahivyo walifanikiwa kuyatawanya makundi hayo mawili.
Wakosoaji wanasema ni makosa kwa wafuasa hao wa dini kutumia eneo la umma ambalo linatumika na watu wa dini tofauti.
Waislamu hao hatahivyo wanasema hawana eneo jingine lolote la kutekeleza ibada yao kwa kuwa baraza la mji huo lilichukua chumba kimoja ambacho walikuwa wakitumia kufanyia ibada mnamo mwezi Machi.
Wanasiasa waliokuwa wakiandamana
Image captionWanasiasa waliokuwa wakiandamana
Ufaransa ina takriban Waislamu milioni tano ,huku wengi wakiwa magharibi mwa Ulaya.
''Maeneo ya umma hayawezi kuchukuliwa kwa njia hii'' , alisemaValérie Pécresse, rais wa baraza la kijimbo la Paris, ambaye aliongoza maandamano ya siku ya Ijumaa yaliofanywa na madiwani na wabunge kutoka chama cha mrengo wa katikati cha Republicans pamoja na vyama vya UDI.

Sanamu ya Adolf Hitler yaondolewa katika jumba la makumbusho

Sanamu moja ya Adolf Hitler inayotumika sana kwa picha za ''Selfie'' na wageni katika makavazi ya Indonesia imeondolewa.Haki miliki ya pichaAFP
Image captionSanamu moja ya Adolf Hitler inayotumika sana kwa picha za ''Selfie'' na wageni katika makavazi ya Indonesia imeondolewa.
Sanamu moja ya Adolf Hitler inayotumika sana kwa picha za ''Selfie'' na wageni katika makavazi ya Indonesia imeondolewa.
Picha zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii zinaonyesha watu wakitabasamu huku wakijipiga picha na sanamu hiyo katika lango la kambi ya Auschwitz.
Ni wakati jamii ya kimataifa ilipotoa hisia kali kuhusu sanamu hiyo ndiposa makavazi hayo ya De ARCA yalipogundua kwamba yamefanya makosa.
Makavazi hayo yalipo Jogjakarta, Java yalisema kuwa yalitaka kuwaelimisha watu.
''Hatutaki kuvutia hisia mbaya'', meneja wa operesheni za makavazi hayo Jamie Misbah, aliambia AFP.
Picha katika mitandao ya kijamii zinaonyesha watu kadhaa wakipiga picha na sanamu hiyo ikiwemo vijana wadogo waliovaa nguo za rangi ya machungwa wakipiga saluti ya Nazi.
Imewacha idadi kubwa ya watu duniani kuhisi vibaya licha ya makavazi hayo kusema kuwa hakuna mgeni aliyelalamika.

Raia wa Korea Kaskazini aiomba China kutorudisha nyumbani familia yake

Mke wa Lee na mwanawao walipanga kukutana na mumewe nchini Korea Kusini
Image captionMke wa Lee na mwanawao walipanga kukutana na mumewe nchini Korea Kusini
Raia mmoja wa Korea Kaskazini amemuomba rais wa China Xi Jinping kutomrudisha nyumbani mkewe na mwanawe wa kiume akisema kuwa watakabiliwa na kifungo jela au kifo iwapo watarudishwa Korea Kaskazini.
Mwanamke na mvulana wa miaka minne wanaeleweka kuwa miongoni mwa kundi la watu 10 wa Korea Kaskazini waliozuiliwa nchini China wiki iliopita baada ya kuvuka na kuingia nchini humo kisiri.
Mtu huyo ambaye alitaka kutambulika kwa jina la Lee pekee , alitorokea Korea Kusini 2015.
Alirekodi ombi lake katika mkanda wa video ambao uliwasilishwa kwa BBC.
Alisema kuwa mkewe na mwanawe watakabiliwa na hatia ya kifo ama kufungwa jela iwapo watarudishwa nyumbani Korea Kaskazini.
''Ningependa rais Xi Jinping na rais Donald Trump kumfikiria mwanangu kama kilembwekeza wao na kumleta mwanangu katika taifa huru la Korea Kusini '', alisema.tafadhali tusaidie.
''Okoa familia yangu kutorudishwa Korea Kaskazini. Mimi kama baba nawaomba viongozi hawa wawili kuisaidia familia yangu. Tafadhalini tusaidieni.Anasema kuwa anafuatwa na kiwiliwili cha mwanaye katika jela''.
''Nasikia sauti ya mwanangu ikiniita'', alisema.
''Namuona mwanangu katika jela ile baridi akimlilia babake, alisema.
''siwezi kusimama na kutochukua hatua yoyote''.

Kinara wa darasa la saba akumbukwa


Tanga. Mwanafunzi  aliyeongoza mtihani wa darasa la saba Hadija Aziz amefunguliwa akaunti na benki ya NMB ikiwa ni sehemu ya pongezi kwake.
Benki ya NMB imetoa Sh 500,00 na kumfungulia akaunti mwanafunzi huyo wa shule ya Sir John ikiwa ni kumpongeza kwa kuwa wa kwanza katika matokeo ya mtihani wa kitaifa wa darasa la saba nchini mwaka huu
Akizungumza leo Novemba 11 ,Meneja wa NMB Tawi la Madaraka, Victor Msofe amesema kuwa akaunti aliyofunguliwa mwanafunzi huyo ni aina ya Chipukizi ambayo itamsaidia katika kununua mahitaji yake muhimu awapo shule ya Sekondari.
“NMB Tawi la Madaraka tumefurahishwa sana kusikia taarifa kuwa mwanafunzi wa kwanza kitaifa ametoka Jijini Tanga, ni faraja kwa mkoa na wateja wetu kwa ujumla hivyo tukaona tumuunge mkono kwa kumfungulia akaunti” amesema  Msofe.
Meneja huyo amesema  hatua hiyo ya NMB ina lengo la kuwahamasisha wanafunzi wengine iwe wa shule za msingi au Sekondari kufanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa na kuwataka wadau wengine kumchangia kwa kutumia akaunti hiyo .
Hadija ameishukuru  NMB kwa kumfungulia akaunti na kubainisha kuwa imempa nguvu na ari ya kufanya vizuri zaidi kwenye masomo ya Sekondari.
“Akili na mawazo yangu yote hivi sasa yapo kwenye masomo, nafikiria nitakwenda kusoma shule gani, na huko lengo langu ni kuhakikisha naongoza mitihani yote ili nifikie lengo langu la kuwa daktari baadaye” amesema  Hadija.
Mama wa mwanafunzi huyo, Jane Kihiyo ameshukuru NMB kwa kumpa nguvu mtoto wake  huyo na kusisitiza kwamba tukio la kumfungulia akaunti limewafurahisha.
Mtaalamu wa masuala ya bima jijini Tanga, Ramadhani Manyeko amewashauri wadau wa elimu kuangalia uwezekano wa kumtafutia shule itakayoweza kuendeleza kipaji chake cha akili darasani bila kujali ni ya Serikali au binafsi.
“Kwa nchi za wenzetu Hadija  na  wenzake walioshika nafasi ya pili hadi tano wangekuwa ni lulu kubwa, wangetafutiwa shule zenye uwezo wa kuwaendeleza vipaji vyao bila kujali ni ya Serikali au binafsi kwani ni faida kubwa kwa Taifa na wangelipiwa gharama zote ili wasome bila usumbufu” amesema Manyeko.

Trump na Putin 'waafikiana kuwashinda Islamic State nchini Syria'

Russian President Vladimir Putin (R) and US President Donald Trump (L) talk at the Apec summit on 11 NovemberHaki miliki ya pichaEPA
Image captionVladimir Putin na Donald Trump wakati wa mkutano wa Apec mnamo tarehe 11 Novemba
Rais wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin wamekubaliana kuhakikisha kundi la wapiganaji wanaojiita Islamic State (IS) wanashindwa nchini Syria, maafisa wa rais wa Urusi wamesema.
Ikulu ya Urusi imesema taarifa imeandaliwa na wataalamu baada ya viongozi hao wawili kukutana kwa muda mfupi pambizoni mwa mkutano wa viongozi wa nchi za Asia na Pasific nchini Vietnam Jumamosi.
Kwa jumla, viongozi hao wawili walikutana mara tatu katika kipindi cha saa 24 katika mji wa Da Nang.
Hakujakuwa na thibitisho lolote rasmi kutoka kwa Marekani kuhusu tamko hilo la Urusi.
Mkutano kati ya Rais Trump na Vladimir Putin ulitarajiwa kufanyika wakati wa mkutano huo wa Apec, lakini ni maelezo machache sana ambayo yametolewa.
Wawili hao walikutana kwa mara ya kwanza Julai katika mkutano wa G20 katika mji wa Hamburg nchini Ujerumani.
Donald Trump na Vladimir Putin wakiwa Danang, Vietnam, 10 Novemba 2017Haki miliki ya pichaREUTERS
Image captionWawili hao walisimama pamoja wakiwa wamevalia shati zilizofanana wakati wa picha ya pamoja Ijumaa
Maswali kuhusu uhusiano wa Donald Trump na Urusi yamekuwa yakiulizwa mara kwa mara.
Wasaidizi wake wakuu wa zamani wanachunguzwa kwa tuhuma za kushirikiana na Urusi kuingilia uchaguzi wa urais wa Marekani wa mwaka 2016.
Urusi imekanusha tuhuma hizo.
Ingawa White House haijasema chochote kuhusu mkutano wa wawili hao, taarifa ya Kremlin iliyotolewa Jumamosi imesema viongozi hao "waliafikiana kwamba mzozo wa Syria hauwezi kutatuliwa kwa njia ya kijeshi".
Kadhalika, walikariri "kujitolea kwao kuwashinda Isis [jina jingine la IS]" na kuzitaka pande zote kushiriki mazungumzo ya amani ya Geneva.
Vladimir Putin na Donald Trump wakiwa Apec 11 NovembaHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionWawili hao walionekana wakizungumza wakati wa kupigwa picha ya pamoja
Kwa mujibu wa shirika la habari la Interfax la Urusi, wameahidi kuendelea kudumisha njia za mawasiliano za kijeshi kati ya majeshi ya Urusi na Marekani kuzuia uwezekano wa kushambuliana wakati wakishambulia IS>
Urusi imekuwa ikiunga mkono serikali ya Bashar al-Assad katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu miaka sita sasa.
Marekani nayo huwasaidia waasi wa makundi ya Waarabu wa Syria na Wakurdi.
Tangu 2014, Marekani imeongoza muungano ambao umekuwa ukitekeleza mashambulio ya kutoka angani dhidi ya IS nchini Syria.

Maswali kibao mteja nyumba za Lugumi



Dk Louis Shika
Dk Louis Shika 

Dar es Salaam. Dk Louis Shika, mteja aliyejitokeza kununua nyumba za mfanyabiashara mashuhuri nchini, Said Lugumi, amejikuta akitupwa rumande baada ya kuzua utata wa malipo ya awali na kutoa majibu yanayojikanganya.
Mnada huo ambao ulifanyika jana katika nyumba za Lugumi zilizopo Mbweni JKT na Upanda uliendeshwa na kampuni ya Udalali ya Yono kwa amri ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kufidia Sh14 bilioni za kodi ambazo Lugumi anadaiwa. Dk Shika akifikia bei ya kuzinunua zote kwa Sh3.2 bilioni.
Utata uliibua pale alipotakiwa kulipa asilimia 25 ya gharama ya kila nyumba kama sheria ya mnada inavyotaka. Nyumba ya kwanza alifika bei ya Sh900 milioni ya pili Sh1.1 bilioni zote za Mbweni JKT huku ile ya Upanga akifikia bei ya Sh1.2 bilioni. Baada ya kushindwa kulipa, alipelekwa Kituo cha Polisi Selander ambako aliomba kompyuta mpakato ili afanye muamala kutoka nje ya nchi kwenda akaunti ya TRA, ambao alisema ungechukua dakika tano. Hata hivyo, ilishindikana na kusema inahitaji saa 48.
Hatua hiyo iliwafanya Yono na mmoja wa maofisa wa TRA kujadiliana na ofisa wa TRA alisikika akisema “Haiwezekani, huyu anahitaji kupelekwa Central (Kituo Kikuu cha Polisi cha Kanda ya Dar es Salaam) na Kamishna amesema huyu asiachiwe.”
Kabla ya safari ya kwenda Central, Dk Shika alimweleza mwandishi wetu ambaye alikuwapo eneo hilo kwamba, “Watu wanasemasema huko mitandaoni, nitawazima midomo nikilipa, subirini mtaona labda hawa wakatae kwani ndani ya saa 48 zitakuwa zimewasili, fedha kidogo sana hizo bilioni tatu kidogo sana.”
Utata wa suala hilo ulianza baada ya mnada kumalizika na maofisa wa TRA kumchukua kwenda benki kwa kufanya malipo ya asilimia 25 ya Sh3.2 bilioni ambazo ni Sh700 milioni ndipo alipowaeleza kuwa hana fedha mkononi au benki hadi afanye muamala kutoka nje ya nchi.
“Sheria ya mnada ni lazima alipe asilimia 25 siku hiyohiyo na sisi tulitangaza matangazo, sasa anaposema hana fedha na anajua kabisa anatakiwa kulipa asilimia 25 hatumwelewi, katuharibia mnada wetu na itabidi urudiwe kwa nyumba mbili,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yono, Scholastika Kevela baada ya kuelezwa Dk Shika ameshindwa kulipa.
Kevela alisema nyumba ya Mbweni JKT ambayo Dk Shika alifikia bei ya Sh1.1 bilioni ilichukuliwa na Justo Malika kwa Sh.1 bilioni na nyumba zingine mbili mnada utarudiwa huku Malika akisema, “Nashukuru nimeinunua nyumba hii, kwani naitaka sana kwa makazi ya familia yangu.’’
Dk Shika alianza kuzua minong’ono mara baada ya kuibuka mshindi kwa nyumba ya kwanza ya Sh900 milioni hasa kutokana na usafiri alioutumia kufika pale, mwonekano wake kimavazi na kushindwa kujibu maswali ya msingi aliyoulizwa na mwandishi wetu.
Miongoni mwa maswali hayo ni umri wake. Awali alisema haujui na alipoonyeshwa pasi yake ya kusafiria ambayo inaonyesha kuwa alizaliwa Desemba 31, 1969 huko Nyegezi, Mwanza alijibu, “Huo ni umri tu ambao niliutumia kupata pasipoti, umri wangu siukumbuki nilizaliwa zamani.’’ Alipoulizwa makazi yake alisema anaishi Tabata Mawenzi na Kigamboni lakini katika mahojiano aliyofanyiwa katika Kituo cha Selander alisema anakaa Tabata Mawenzi na hakuitaja Kigamboni.
Awali, mwandishi wetu alimuuliza ana watoto wangapi na familia yake ipo wapi na alijibu, “Iko Marekani na watoto mimi sijui. Unajua anayejua una watoto wangapi ni mama yao, hata wewe (mwandishi) unaweza kukuta baba yako si yeye, lakini Marekani ninao wawili na nchini Urusi ninao wawili.”
Alipoulizwa alikopata fedha za kununua nyumba hizo alisema, ‘‘Mimi ni daktari bingwa wa magonjwa ya binadamu, Rais wa kampuni ya kimataifa ya Ralcefort ya nchini Urusi, inayojishughulisha kemikali za viwandani na pia ni Balozi wa UNHCR. Hivi vyote ni vyanzo vyangu vya mapato hasa hii kampuni.”
Lakini licha ya kudai kwamba ina matawi Ujerumani, Kenya na Hispania, mwandishi wetu hakufanikiwa kuiona kampuni hiyo kwenye mitandao.

Magufuli aainisha namna vikwazo vya biashara mipakani vinavyoshughulikiwa


Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema nchi za Afrika Mashariki zinashirikiana kwa karibu kuondoa vikwazo vya biashara mipakani kwa kuanzisha vituo vya pamoja vya huduma.
Alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa kituo cha pamoja cha huduma Mutukula mpakani mwa Tanzania na Uganda. Alifanya uzinduzi huo pamoja na Rais Yoweri Museveni wa Uganda na baadaye wawili hao walizindua ujenzi wa bomba la mafuta kwa upande wa Uganda.
Rais Magufuli alisema mwaka jana alizindua vituo kama hicho katika mpaka wa Rusumo akiwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame na kingine cha Holili/Taveta akiwa na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.
Alisema ataendelea kushirikiana na Uganda na nchi nyingine za Afrika Mashariki ili kuhakikisha wanaondoa vikwazo vyote vya biashara na wananchi wanafanya biashara bila shida.
Rais Magufuli alisema biashara ndani ya Afrika imebaki kuwa chini kwa sababu ya matatizo mipakani.
“Ili kuondokana na hilo, nchi za Afrika Mashariki zimeanza kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuanzisha vituo vya pamoja vya huduma,” alisema Rais Magufuli.
Pia, alisema mizigo na abiria sasa wanachukua muda mfupi zaidi kusafiri tofauti za zamani kutokana na ukaguzi kuchukua muda mfupi.
Alisema ukaguzi wa mizigo ya abiria unachukua nusu saa mpaka saa moja ikilinganishwa na zamani ilipokuwa inachukua kati ya saa nne hadi tano.
“Zamani malori yanayobeba makontena yalikuwa yanatumia siku nzima kufanya ukaguzi na utaratibu mwingine wa uhamiaji lakini sasa wanatumia nusu saa mpaka saa moja kukamilisha utaratibu huo,” alisema Rais Magufuli.
Kwa upande wake, Rais Museveni alibainisha sekta nne alizosema ndizo zinazoleta utajiri na ajira kwa wananchi. Alizitaja kuwa ni kilimo cha kisasa, viwanda, huduma na teknolojia, habari na mawasiliano (Tehama).
Alisema sekta hizo zinaweza kuleta mapinduzi ya kiuchumi kwa nchi za Kiafrika.
Pia, aliwataka Watanzania na Waganda wanaoishi mpakani kutowekewa vikwazo vya kuvuka mpaka kwa sababu si dhana halisi ya kuwa na mipaka.
Rais Museveni alisema mpaka hautakiwi kuingilia maisha ya watu ambao wanaishi mpakani bali uwe ni kwa ajili ya watu wengine ambao wanatoka mbali na mizigo yao.
Wakati huohuo, viongozi hao wawili walizindua ujenzi wa bomba la mafuta lenye urefu wa kilomita 1,445 litakalotoka Hoima, Uganda mpaka Tanga, Tanzania uliofanyika katika kijiji cha Luzinga kilichopo Uganda.
Rais Magufuli ametaka kuharakishwa kwa ujenzi wa mradi huo ili wananchi wa nchi hizo mbili waanze kunufaika na matunda ya mradi huo ifikapo mwaka 2019.
Mradi huo wa miaka mitatu utaanza kujengwa Januari 2018 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2020. Alisema hilo litawezekana kwa kuweka makandarasi wengi.
Pia, alimshauri Rais Museveni kuwapa tuzo vijana waliogundua mafuta nchini humo kwa sababu wamefanya kazi kubwa ya kihistoria ambayo itakuwa na manufaa kwa wananchi wa nchi hiyo na Afrika Mashariki kwa jumla.

Serikali yatuma madaktari bingwa kuokoa maisha ya waliojeruhiwa kwa bomu


Ngara. Serikali imepeleka madaktari bingwa katika Hospitali ya Misheni ya Rulenge wilayani Ngara watakaoshiriki kuwatibu majeruhi 43 wa mlipuko wa bomu ulitokea katika Shule ya Msingi Kihinga.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Dk Revocatus Ndyekobora akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo jana asubuhi, alisema timu ya madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera imewasili Ngara kusaidiana na wenzao kuwafanyia uchunguzi na kuwatibu majeruhi hao.
“Watakaobainika kuhitaji huduma maalumu watahamishiwa hospitali zingine kulingana na taarifa ya madaktari,” alisema Dk Ndyekobora.
Alisema majeruhi hao pia wanahitaji uniti 50 za damu ili kuokoa maisha yao na kwamba, baadhi wamebainika kuwa na vipande vya vyuma vilivyotokana na mlipuko wa bomu.
“Tayari wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Alfred Rulenge inayomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge wamechangia uniti 46 za damu kusaidia wenzao,” alisema.
Mbali ya damu, majeruhi pia wanahitaji mashuka na mablanketi zaidi ya 50 kutokana na yaliyopo kutotosheleza mahitaji. Alisema baadhi wamelazimika kulala sakafuni kutokana na vitanda kujaa.
“Msaada wa chakula pia unahitajika kwa ajili ya majeruhi hawa ambao wametoka maeneo ya mbali kiasi cha kutowezesha wazazi, ndugu, jamaa na marafiki kuwaletea chakula,” alisema Dk Ndyekobora.
Usafiri kwa ajili ya kuwahamishia hospitali zingine pia ni miongoni mwa mahitaji ya dharura yanayohitajika kuokoa maisha ya majeruhi hao.
Katika hatua nyingine, mwanafunzi aliyeokota bomu la kutupa kwa mkono akidhani ni chuma chakavu kwa lengo la kwenda kuuza imebainika ni miongoni mwa watano waliokufa baada ya kulipuka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Agustino Ollomi amemtaja mwanafunzi huyo kuwa ni Juliana Tarasisi (13).
Alisema jana kuwa, mwanafunzi huyo alilitunza bomu hilo kwenye begi lake la madaftari ili kwenda kuliuza kwa mnunuzi wa chuma chakavu wakati wa mapumziko.
Wanafunzi wengine waliopoteza maisha katika tukio hilo lililotokea jana ni Evart Theonas (12) Edson Bigilimana (12), Miburo Gabriel (12) na Tumsifu Ruvugo (8).
Wanafunzi 42 wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Kihinga na mwalimu wao wa darasa, Policalipo Clemency aliyekuwa darasani wakati wa tukio wamelazwa kwa matibabu katika Hospitali ya Misheni ya Rulenge.
Wakati huohuo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Aidan Bahama amepiga marufuku biashara ya vyuma chakavu katika maeneo ya shule akionya kuchukua hatua dhidi ya mwalimu mkuu na wakuu wa shule watakaobainika kuruhusu biashara hiyo.
Amri ya Bahama imetokana na uchunguzi wa awali wa polisi kubaini mwanafunzi mmoja aliokota bomu na kulihifadhi kwenye begi lake kwa lengo la kuliuza kama chuma chakavu.
Halmashauri kugharamia mazishi
Bahama alisema halmashauri imechukua dhamana ya kugharimia majeneza na shughuli za mazishi ya watoto watano waliokufa katika tukio hilo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Erick Nkilamachumu na mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Ngara, George Lubagola wameiomba Serikali kuimarisha ulinzi na ukaguzi kwa watu wanaingia nchini kutoka Burundi ili kudhibiti uingiaji holela wa silaha na mabomu ya kutupa kwa mkono.
Kijiji cha Kihinga ni miongoni mwa maeneo yanayopakana na nchi jirani za Burundi na Rwanda na kuna mwingiliano wa watu katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

kushindwa kumeza chakula kuna watesa watu wengi


Tatizo la mtu kushindwa kumeza chakula au kinywaji, huwakumba watu wengi.
Na hali hii mara zote huambatana na maumivu makali kiasi cha kumfanya mtu ashindwe kabisa.
Wapo watu ambao hudai kuwa hali hiyo ya kushindwa kumeza chakula inaweza kuwakumba wale wenye tabia ya kushindwa kukitafuna kiasi cha kutosha au wanokula haraka haraka, la hasha.
Hilo siyo tatizo kubwa kwani mara tu mtu anapobadilisha utaratibu mzima wa kula chakula, hali hii huisha.
Lakini kushindwa kumeza chakula ama kumeza chakula ukiwa na maumivu, inaweza kuwa ni ishara ya tatizo fulani ambalo linahitaji ufumbuzi wa kitaalamu.
Hali hii inaweza kumtokea mtu akiwa na umri wowote. Lakini mara nyingi huwatokea watu wazima (wazee).
Kuna sababu mbalimbali zinazochangia kutokea, lakini na matibabu yake pia hutegemeana na sababu zilizofanya hali hiyo itokee.
Dalili zake
Mtu anaweza kutambua kuwa tayari analo tatizo hilo kama atakuwa anapata maumivu wakati wa kumeza chakula, kuwa na hisia kama chakula kimekwama kooni, kutoa udenda, kushindwa kutoa sauti au inyokwaruza.
Dalili nyingine ni pamoja na kurudisha chakula kinywani toka kooni, kupatwa na kiungulia cha mara kwa mara, kikohozi au kupaliwa wakati wa kumeza kinywaji au chakula.
Mtu akibaini hali hiyo, ni vema akawahi kwenda kumuona mtaalamu wa afya au daktari mapema kabla tatizo halijawa kubwa.
Kwani bila kufanya hivyo, hali hiyo inaweza kuendelea kujitokeza mara kwa mara na mgonjwa akajikuta anapungua uzito pia kwa sababu ya tatizo la kushindwa kumeza chakula kunakoambatana na kutapika.
Sababu ya kutokea kwa hali hiyo
Kumeza chakula ama kinywaji ni tukio ambalo kiutendaji ni rahisi kama msomaji unavyoweza kufanya kila siku, lakini kiutekelezaji linafanyika likihusisha vitu vingi na vinavyoweza kuingilia kati ili lisifanyike kwa ufanisi.
Kwa ujumla, hali hiyo ya mtu kushindwa kumeza chakula au kinywaji inasababishwa na mambo kadhaa.
Miongoni mwa hayo ni pamoja na uvimbe kwenye Koo ambao husababisha kipenyo cha koo kupungua.
Pia, kuwapo kwa kitu kigeni kooni. Wakati mwingine chakula au kitu chochote kinaweza kuziba koromeo. Hali hii mara nyingi huwakumba watu wazima wanaotumia meno ya bandia na watu ambao hawatafuni chakula chao vizuri.
Sababu nyingine ni kucheua mara kwa mara, kwani husababisha kuharibu koromeo kwa kuwa tindikali iliyoko tumboni huja na chakula mpaka kinywani.
Na tindikali hii huweza kuleta madhara ya vidonda kooni na kwenye koromeo na kusababisha mtu kushindwa kumeza chakula.
Saratani inavyoathiri umezaji wa chakula
Ugonjwa wa saratani ambao hutokea kwenye maeneo ya kichwani na shingoni, matibabu yake mara nyingi huathiri koo na kumfanya mgonjwa kumeza chakula.
Magonjwa ya mishipa ya fahamu
Haya husababisha mishipa ya fahamu husababisha pia mgonjwa kushindwa kumeza chakula kama itakuwa imeathirika.
Hata hivyo, licha ya mgonjwa kuweza kupatiwa matibabu, lakini anapaswa kujihadhari na sababu hatarishi zinazoweza kuchangia kutokea kwa tatizo hilo la kumeza chakula.
Sababu hizo ni pamoja na umri mkubwa. Kutokana na kukua na kuongezeka kwa umri, kawaida koo huweza kuwa kwenye hali hatarishi ya kupata magonjwa ya aina kama ya kiharusi au ujulikanao kama Parkinson.
Ndiyo maana hali hiyo ya matatizo ya umezaji wa chakula huweza kuwatokea watu wazima zaidi kuliko watu wa umri wa kati na mdogo.
Baadhi ya magonjwa yanayosababisha mtu kushindwa kumeza chakula.
Kwa watu ambao wana magonjwa yanayoshambulia mfumo wa fahamu, kadiri ugonjwa huo unavyozidi kukua hufikia hatua ya kuathiri koo na hivyo kuleta shida kwenye umezaji wa chakula.
Madhara ya tatizo hilo
Tatizo la umezaji wa chakula huweza kusababisha ukosefu wa lishe, kupungua uzito na kupungukiwa maji mwilini kwa mgonjwa na kumfanya ashindwe kupata virutubisho muhimu.
Matatizo ya mfumo wa hewa na upumuaji. Chakula ama maji yanaweza kuingia kwenye mfumo wa hewa, hivyo kuleta maambukizi kwenye mapafu au mfumo mzima wa hewa.
Matibabu
Matibabu yake huwa magumu lakini hutegemeana na ushirikiana baina ya mgonjwa na wataalamu wa afya.
Kwani mgonjwa hutakiwa kufanya mazoezi maalumu ya kumuwezesha kuifanya misuli yote inayohusika na umezaji wa chakula pamoja na mishipa yake ya fahamu kufanya kazi kwa ufanisi.
Kama mgonjwa atabainika kuwa koromeo lake lina kipenyo kidogo, daktari atalazimika kulitanua kitaalamu na vifaa ili kuondoa tatizo hilo. Tiba ya upasuaji hufanyika pale tu itabainika kuna ulazima wa kufanya hivyo ili kusafisha njia ya koromeo.