Saturday, December 24

Serikali yapiga marufuku shule binafsi kufanya mitihani ya kuchuja wanafunzi

Serikali imepiga marufuku utaratibu wa shule binafsi kuendesha mitihani ya mchujo kwa wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya kitaifa ili shule zao ziweze kuongoza kwa kubaki ma wanafunzi wazuri(walio na uwezo mzuri darasani)

Agizo hilo pia linapiga marufuku kuwafukuza shule wanafunzi wanaoshindwa mitihani ya mchujo,kuwasajili kama private candidate wale wanafunzi wanaofeli mitihani hiyo,kuwahamisha shule au kuwakaririsha madarasa.

========

Kibano kipya chaja kwa shule binafsi
Hiyo ni baada ya kutangaza kupiga marufuku utaratibu wa kuwachuja wanafunzi wanaotakiwa kufanya mitihani ya taifa uliokuwa unaofanywa na baadhi yao kwa lengo la kuonekana shule zao zinafaulisha vizuri.

Hivi karibuni, Nipashe iliripoti kuhusu hofu ya baadhi ya shule hizo; za msingi na sekondari ziko hatarini kubadilishwa matumizi kutokana na kukosa wanafunzi wa kutosha baada ya Serikali kuboresha shule zake na kutoa elimu bure, huku hali ya kiuchumi ikiwaumiza wananchi.

Huku udahili kwenye shule za serikali ukiongezeka na kuonekana kuwa tishio kwa ustawi wa shule za watu na taasisi binafsi, imewabana tena wamiliki wa shule binafsi kwa kuwazuia kufanya mchujo wa wanafunzi wanaoingia kwenye madarasa au vidato vyenye mitihani ya taifa.

Mmoja wa wazazi aliliambia Nipashe kuwa mwanawe anayesoma kidato cha tatu katika shule moja ya binafsi jijini Dar es Salaam, amepangiwa kuhamishiwa shule nyingine ya mmiliki huyo huyo kutokana na kufaulu kwa daraja la tatu.

Kwa mujibu wa mzazi huyo, kuna wanafunzi takribani 70 wa kidato cha tatu, wanatarajiwa kuhamishwa katika shule hiyo waliyosajiliwa tangu kidato cha kwanza, watahamishwa shule hiyo na kubaki wale waliofaulu kwa viwango vya madaraja ya kwanza na pili tu.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo, akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam juzi, alisema ni marufuku shule kumkaririsha darasa, kumfukuza, kumhamishia shule nyingine au kumsajili kama mtahiniwa binafsi (PC) mwanafunzi kwa kigezo cha kutofanya vizuri katika mitihani ya shule husika.

"Ni marufuku kabisa kufanya hivyo. Mitihani tulionayo sisi (Wizara ya Elimu) ndiyo mchujo sahihi. Na mtihani ambao unamkaririsha mwanafunzi ni mtihani wa taifa wa kidato cha pili na mtihani wa darasa la nne tu," alisema.

"Wala siyo mtihani wa shule na madarasa mengine hayana mtihani wa kumkaririsha mtoto au kumfanya aondolewe shuleni au ahamishiwe shule nyingine, hatuna utaratibu huo na serikali haiwezi kukubaliana nao," aliongeza Dk. Akwilapo.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (Tamongosco), Benjamin Nkonye, aliiambia Nipashe jana kuwa utaratibu wanaoutumia ni kushauriana na wazazi wa wanafunzi wanaoshindwa kufanya vizuri shuleni ikiwamo kuwapeleka katika vyuo vya ufundi (Veta).

Alisema shule binafsi zinapaswa kupongezwa kwa kudahili hata wanafunzi hasa wa sekondari ambao shule za serikali huwa haziwachukui kutokana na kushindwa kufanya vizuri katika mitihani ya shule za msingi.

“Hakuna shule ambazo zinapaswa kupongezwa kama za binafsi, serikali yenyewe imekuwa ikichagua wanafunzi wote. Inatuachia ‘vilaza’, lakini sisi kwa kujitoa kuwasaidia watoto wa Kitanzania, tunakubali kuwachukua hao hao wanaoonekana wabaya, tunawafundisha na mwisho wa siku wanakuwa wazuri kuliko hata hao wanaokuwa wamethaminiwa na serikali,” alisema Nkonya.

“Na sisi hatuchuji wala kumfukuza mwanafunzi, isipokuwa kinachofanyika kwa kuwa tunapokea wakati mwingine wanafunzi ambao ni ‘vilaza’ kabisa, huwa tunawagawanya katika makundi kulingana na uelewa wao, wenye uelewa wa kwanza, wa kati na wa mwisho. Na mwisho na tunawafundisha kulingana na ‘speed’ (kasi) ya uelewa wao na wanajikuta wanafanya vizuri.

“Lakini kwa sababu sisi tunakuwa na wanafunzi ambao ni wagumu sana, inapoonekana wakatokea wachache hawawezi kabisa huwa tunashauriana na wazazi wao, kuwapeleka Veta ili kule wanapokuwa wanaendelea kujifunza, wengine wanafanya vizuri hadi wanafika vyuo vikuu, hatuwaachi kama ilivyo katika shule za serikali na vyuo vya serikali, haya maneno mengine yanayozungumzwa ni ya kisiasa tu."

HALI ILIVYO

Uchunguzi wa Nipashe uliofanyika hivi karibuni katika baadhi ya mikoa, ulibaini baadhi ya wamiliki wa shule binafsi wamekuwa na utaratibu wa kuchuja wanafunzi kila mwaka kwa lengo la kupata wenye uwezo mkubwa darasani.

Ilibainika kuwa utaratibu huo umekuwa ukifanywa kwa nia ya kuwa na wanafunzi wenye uwezo mkubwa ili shule hizo zifanye vizuri katika mitihani ya taifa, hivyo kuvutia wazazi wengi zaidi kupeleka watoto wao.

Gazeti hili lilibaini kuwa, baadhi ya shule binafsi zimekuwa zikiendesha utaratibu huo kipindi cha mitihani ya mwishoni mwa mwaka kwa kuwafukuza, kuwakaririsha darasa au kuwahamishia shule nyingine wanafunzi wanaoshindwa kufikia kiwango kinachowekwa na shule husika kwenye mitihani ya kufunga mwaka.

Nipashe pia ilibaini baadhi ya shule hizo zimekuwa na utaratibu wa kuwachuja kwa kuwasajili kama watahiniwa binafsi (Private Candidates) kwenye mitihani ya taifa wanafunzi wake wanaoshindwa kiwango kilichowekwa wanapofanya mitihani ya shule husika.

MTOTO WA PROFESA AKACHA KULA

Akizungumzia suala hilo katika mahojiano maalumu na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Masomo ya Shahada ya Kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Allen Mushi, alisema haungi mkono utaratibu wa baadhi ya shule binafsi kuwafukuza wanafunzi wanaoshindwa kufikia kiwango cha alama zilizojiwekea.

Alisema: "Ni makosa kumfukuza shule mwanafunzi aliyekuwa amedahiliwa, anasoma halafu unamsitishia, unamwambia nenda katafute shule nyingine.

"Na ni kweli wana tabia hiyo. “Nina kijana wangu yuko ‘Form One’ (Kidato cha Kwanza) anasoma shule ... (anataja eneo ilipo shule hiyo), yaani anasoma kupindukia. Nilikuwa na wasiwasi hata akija likizo hawezi kula vizuri, anasoma tu."

Alisema kuwa katika shule hiyo ya jijini Dar es Salaam anayosoma mtoto wake, wameambiwa ni lazima awe na wastani wa kuanzia alama 50 katika mitihani ya shule ili aruhusiwe kuingia kidato kinachofuata, vinginevyo wakatafute shule nyingine.

"Katika utaratibu wa elimu, siyo sahihi kufanya hivyo, wewe kama wanafunzi wameshindwa, wewe siyo ndiyo mwalimu, ndiyo kazi yako ya kufanya wanafunzi waelewe," alisema na kufafanua zaidi:

“Sasa ukiwa unafanya hivyo, mwisho wa siku utakuwa unafelisha darasa zima na kujitamba kwamba unafaulisha kwa sababu umefukuza wengi na kubaki na wazuri wachache. Sasa hiyo ni biashara, siyo elimu tena. Wewe kama ni mwalimu, unatakiwa kufundisha wanafunzi wote.

“Kwa hiyo, wanasema shule za ‘private’ (binafsi) zinafaulisha wanafunzi wote, kumbe wengine mliowachuja. Mimi binafsi sikubaliani na hali hiyo kabisa."

Alisema ni muhimu wizara yenye dhamana ya elimu nchini iweke masharti kwamba ukishadahili wanafunzi, wasiondolewe shuleni kwa utaratibu wa viwango vya ufaulu katika mitihani ya shule husika isipokuwa kwa sababu za tabia mbaya na zisizofaa kwa mwanafunzi kwa mujibu wa sheria za nchi.

MAKUNDI YA UELEWA

Msomi huyo alisema wanafunzi wamegawanyika katika madaraja mawili kiuelewa darasani, la kwanza likiwa la wenye uelewa wa haraka (fast learners) na jingine likiwa la wenye uelewa hafifu (‘slow learners).

"Wote hao wanapaswa wazingatiwe katika elimu. Sasa hawa (shule binafsi) wenyewe wanaangalia 'fast learners' tu. Ni vema wote wakachukuliwa katika vigezo sawa, siyo unawachuja wengine halafu unasema unafaulisha wote," alisema Prof. Mushi.

BIASHARA

Aliyekuwa Rais wa Chama cha Walimu (CWT), Gratian Mukoba, akizungumza na Nipashe jana kuhusu changamoto hiyo, alisema si vyema kumfukuza, kumkaririsha darasa au kumhamisha mwanafunzi aliyefanya vibaya katika mitihani ya shule.

"Mtihani wa Kidato cha Pili ni mchujo sahihi tu. Shule binafsi wanakosea. Ufundishaji wa kawaida huwezi kuwa na wanafunzi wanaopata daraja la kwanza na la pili tu," alisema.

"Hao shule binafsi kuna muda wanateleza kidogo, kwa sababu hakuna mwanafunzi asiyefundishika labda kwa sababu wao wanataka suala la biashara. Ni kuonea wanafunzi, bahati mbaya akishaanza shule ya 'private' (binafsi) kidato cha kwanza, hawezi kurudi kwenye mfumo wa serikali, kwa hiyo wanafunzi wanahangaika," alisema zaidi Mukoba.