SERIKALI imesema kuwa inatumia mikopo inayoipata kutoka kwa wadau wa maendeleo kwenye miradi ya uzalishaji na miundombinu ili iweze kuwa na tija kwa jamii.
Hayo yamesemwa jana Dar es Salaam na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Sweden nchini, Katarina Rangnitt.
Alisema Serikali imejipanga kulipa madeni kwa wadau mbalimbali baada ya kuhakikiwa.
Hata hivyo, alisema kuwa hatua za kukopa zitaangaliwa kwa umakini mkubwa ili kuzuia kuwa na madeni ambayo hayana tija kwa wananchi na Serikali.
“Katika kuhakikisha Serikali inaendelea kuwahudumia wananchi ipasavyo, kumekuwa na mikakati ya kuwaongezea watumishi ujuzi ili kuendana na kasi ya maendeleo, kuelekea uchumi wa kati kwa kuwa tuna uhaba wa watu wenye ujuzi wa kutosha, hivyo ni vyema wadau wa maendeleo wakalitazama hilo ili kusaidia katika kuharakisha ukuaji wa uchumi.
“Siwezi kuwa Waziri wa Fedha ikiwa sitakuwa na wafanyabiashara, kwa kuwa wao ndio wanaolipa kodi zinazosaidia kuendesha nchi,” alisema Dk. Mpango.
Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa demokrasia na haki za binadamu, alisema kuwa mambo hayo yapo katika katiba, hivyo Serikali inaifuata na kuiheshimu, na kwamba haki za binadamu zinafuatwa kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, alieleza kuwa ni vema tamaduni za Mtanzania zikaendelea kuheshimiwa wakati wa utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano wa maendeleo.
Alitoa wito kwa jamii kuendelea kutangaza mazuri yanayojitokeza nchini, yakiwamo ya kukua kwa uchumi kwa kuwa Tanzania itajengwa na Watanzania.
“Inashangaza kuona baadhi ya watu wakieleza mabaya tu ilihali kuna mafanikio mengi yaliyopatikana, tunakaribisha ukosoaji, lakini wenye tija,” alisema Dk. Mpango.
Alisema Serikali inafanya jitihada za dhati kuhakikisha kuna mazingira bora ya biashara na ili kufikia huko, kumekuwa na majadiliano ya mara kwa mara na wafanyabiashara nchini na kwamba kero zao nyingi zimetatuliwa ikiwamo kupungua kwa wingi wa kodi.
Kwa upande wake Balozi Rangnitt alisema kuwa nchi yake ina nia ya kusaidia kukuza sekta ya nishati na tayari mazungumzo na wizara husika yameanza.
Alisema kuna umuhimu wa sekta binafsi katika kukuza uchumi wa nchi.
Balozi huyo alisema nchini mwake wafanyabiashara wanachangia pato la ndani kwa asilimia 50 kwa kuwa kuna biashara huria.