Saturday, November 11

Kamatakamata ya wapinzani yageuka mwiba kampeni za uchaguzi wa madiwani

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akitoka nje ya Ofisi za Kitengo cha Uhalifu wa Makosa ya Kifedha kilichopo Kamata jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni mdogo wake Thabitha Kabwe na kulia ni Ofisa Habari wa Chama hicho, Abdallah Khamis. Picha na Ericky Boniphace 
Kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani zinaendelea kushika kasi katika kata 43 nchini. Ni uchaguzi uliosubiriwa kwa hamu kubwa na vyama vya siasa.
Vyama vya siasa, hasa vya upinzani vinataka kutumia miku-tano hiyo kuzungumzia masuala mbalimbali ya kitaifa na kukiko-soa chama tawala na Serikali yake katika masuala mbalimbali baada ya kukosa nafasi hiyo kutokana na marufuku ya mikutano ya hadhara na maandamano.
Vilevile, vinataka kupima kuku-balika kwake kwa wananchi baa-da ya siku nyingi za kutoonana nao mikutanoni kiasi cha kubadili mkakati na kuanza kuwasiliana na wananchi kwa kutumia katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, huku chama tawa-la kikitegemea zaidi mikutano ya mwenyekiti wake, Rais John Magufuli.
Hata hivyo, inaelekea wap-inzani hawataweza kukata kiu yao baada ya Jeshi la Polisi kuanza kuwakamata na kuwahoji vion-gozi na wafuasi wa vyama hivyo kwa tuhuma tofauti zitokanazo na mikutano hiyo.
Jijini Dar es Salaam wiki iliyopita jeshi hilo lilimkamata kiongozi wa chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe kwa madai ya kutoa kauli za uchochezi wakati wa uzinduzi wa kampeni za udiwani katika Kata ya Kijichi.
Kiongozi huyo mpaka sasa anaripoti polisi baada ya jeshi hilo kuchukua maelezo yake na kuendelea na uchunguzi na endapo litajiridhisha kuhusu makosa hayo, kiongozi huyo atafikishwa mahakamani.
Wakati kiongozi huyo akiendelea kuripoti polisi, mwishoni mwa wiki jeshi hilo mkoani Arusha liliwakamata wafuasi 12 wa Chadema kwa madai kuwa walimshambulia mgombea wa CCM wa Kata ya Muriet, Francis Mbise.
Miongoni mwa wanaoshikiliwa ni kaimu katibu wa Chadema wilayani Arusha, Innocent Kisanyage.
Mbali na wafuasi hao, polisi pia wamekamata gari la matangazo la Chadema ambalo inaelezwa lilikuwa linatumika kutangaza mikutano ya chama hicho katika kampeni za uchaguzi mdogo.
Katika taarifa yake, kamanda wa polisi wa Arusha, Charles Mkumbo anasema wafuasi hao walikamatwa kwa kuwavamia wafuasi wa CCM wakati wakitoka kwenye mikutano ya kampeni eneo la Muriet na kuanza kuwashambulia na kwamba Mbise alishambuliwa na kuumizwa sehemu mbalimbali mwilini na kupelekwa hospitalini kwa matibabu.
Taarifa zaidi zinasema pia mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema anatafutwa na jeshi hilo na kwamba wakati wowote atakamatwa kutokana na kauli zake.
Juzi, mbunge huyo alipinga kukamatwa kwa wafuasi hao pamoja na gari la matangazo, akisema kitendo hicho kinalenga kuathiri uzinduzi wa kampeni.
Lema alinukuliwa akisema alikwenda polisi kuwawekea dhamana wafuasi hao, lakini ilishindikana ikielezwa ni kutokana na maelekezo kutoka ngazi za juu.
Si matukio hayo tu, hata Mbunge wa Ndanda ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kusini, Cecil Mwambe amejikuta mikononi mwa polisi baada ya kudaiwa kusema maneno ya uchochezi katika mkutano wa kampeni hizo mjini Mtwara.
Kwa takriban miaka miwili sasa, wanasiasa wa vyama shindani wamekosa jukwaa la kuikosoa Serikali mbele ya wananchi, lakini sasa angalau walitegemea wamepata fursa ya sehemu ya kupumulia kutokana na kuwepo kwa kampeni hizo za uchaguzi mdogo utakaofanyika Novemba 26, mwaka huu baada ya waliokuwa wakishikilia nafasi hizo kujiuzulu au kufariki dunia.
Kamatakamata hiyo inayohusisha wanasiasa wa upande mmoja inaweza kuathiri uchaguzi huo na kutafsiriwa kuwa inalenga kuupendelea upande mmoja.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwahi kunukuliwa na gazeti hili akisema mikutano hiyo ya uchaguzi ina umuhimu mkubwa tofauti na ya hadhara.
Kauli hiyo iliungwa na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliyetuma salamu kutokea Hospitali ya Nairobi ambako anatibiwa baada ya kushambuliwa kwa risasi, akitaka wananchi kutumia nafasi hiyo kutoipigia kura CCM.
Katika salamu hizo alizotuma kwa njia ya sauti iliyorekodiwa akiwa kitandani, Lissu anasema kuendelea kuipa kura CCM ni kuruhusu hali ya kupigana risasi hadharani, ubomoaji nyumba, ukamataji wanasiasa na ukandamizaji kuendelea na hivyo kuwataka wananchi kujitokeza kuipigia kura Chadema.
Wakati Chadema wakijipanga hivyo, Abdul Kambaya, ambaye ni mkurugenzi wa habari wa CUF upande wa Profesa Ibrahim Lipumba anasema chama chake kitatumia kampeni hizo kukata kiu ya siasa waliyonyimwa kwa karibu miaka miwili.
“Kwanza tulikosa nafasi ya kujenga vyama vyetu kwa mujibu wa sheria na Katiba, hivyo hatua ya kamatakamata haitutishi,” anasema Kambaya.
“Tutaitumia fursa hiyo kuzungumza ajenda zetu katika chama. Kwa mfano, suala la maendeleo na utawala wa sheria. Kwa sasa hali inavyokwenda bila kufuata sheria tunaelekea kubaya.”
Lakini, mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Profesa Gaudens Mpangala anasema vyama vya upinzani visiogope na vitumie nafasi hiyo kujipambanua.
Hata hivyo, Profesa Mpangala anaonya tabia hiyo ya Jeshi la Polisi ya kuwakamata wapinzani inaweza kuathiri uchaguzi huo kwa kutotoa fursa sawa kwa washiriki wote.
“Ni fursa nzuri. Watumie nafasi hiyo kupeleka hoja kwa wananchi ili kupinga yale yote yaliyokuwa yakiwaminya ili wananchi waamue,” alisema.
Profesa Mpangala anasema kwa muda wote wa miaka miwili hakukuwa na usawa katika shughuli za kisiasa kutokana na chama tawala kutumia shughuli za kiserikali kufanya siasa, huku upinzani ukikatazwa.
“Mara kadhaa tumeshuhudia Rais akiwa katika ziara za kiserikali akichomekea masuala mbalimbali ya kisiasa. Hakukuwa na usawa hata kidogo,” anasema Profesa Mpangala na kuongeza kuwa hata kinachofanyika sasa kikiendelea hakileti usawa.
Profesa Mpangala alitahadharisha kuwa endapo hali hiyo itaendelea mpaka 2020, Uchaguzi Mkuu utakuwa na kasoro kubwa kutokana na Serikali kushindwa kutoa haki na uhuru sawa kwa vyama vyote.
Anasema kipindi cha kampeni wanasiasa waachiwe wafanye kampeni za kistaarabu ili kuweka usawa badala ya kuwatisha kwa kuwakamata.
Jeshi la Polisi lanena
Wakati hali ikiwa hivyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Barnabas Mwakalukwa anasema Jeshi la polisi linaongozwa kwa mujibu wa sheria na wao kama wasimamizi wa sheria hizo ni lazima wahakikishe hazivunjwi.
Mwakalukwa anasema kuwa Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa kufuata taratibu na sheria na kwamba kila kamanda wa mkoa ana haki ya kukamata watu wote wanaofanya jinai au kuvunja sheria.
“Hata kama ni kipindi cha kampeni ni lazima kila mmoja afuate sheria, huwezi kujificha katika mwamvuli wa kampeni na kufanya jinai tukuangalie. Tutawakamata na tutaendelea kuwakamata mpaka pale watakapoona umuhimu wa kufuata sheria.”
Anasema jeshi la polisi katika kuhakikisha inafanikisha uchaguzi huo wamejipanga kutoa ulinzi katika kipindi chote kuanzia kampeni, wakati wa uchaguzi na siku ya kutangaza matokeo ili watu wapate haki yao ya kidemokrasia.
“Huo ndiyo utawala bora, haiwezekani wewe kwa sababu tu ni kiongozi wa upinzani ufanye mambo yasiyostahili kwa kisingizio cha kampeni, halafu tukuangalie. Hata uwe nani tutakukamata kwani hayupo aliye juu ya sheria,” anasisitiza.
Alipoulizwa kwamba haoni hatua hiyo itaathiri uchaguzi huo kwani hautatoa fursa sawa kwa vyama vyote, Mwakalukwa anasema jeshi hilo haliangalii itikadi ya kwamba yoyote atakayejihusisha na jinai atakamatwa.
“Sisi tunashughulika na waalifu, haijalishi anatoka chama cha upinzani au tawala wote tutawapatia haki yao endapo watajihusisha na jinai, mwisho wa siku tunachotaka ni iwepo nidhamu kipindi chote kwa watu wote kufuata sheria,” anasema.

No comments:

Post a Comment