Tuesday, October 10

KDF yauwa wanamgambo 5 wa Al-Shabaab


Wanajeshi wa Kenya jana waliwaua wanamgambo watano wa kundi la Al-Shabaab kwenye oparesheni yao katika msitu wa Boni kaunti ya Lamu. Wanajeshi hao pia walipata bunduki sita aina ya AK-47, risasi-321, guruneti tatu na vilipuzi kadhaa baada ya kuwavizia wanamgambo hao katika eneo la Bodhei. Katika taarifa, afisa wa maswala ya umma katika jeshi la KDF, kanali David Obonyo aliwahakikishia wakenya kuwa msako dhidi ya wanamgambo wa Al-Shabaab utaendelea ili kukomesha visa vyovyote vya mashambulizi ya kigaidi katika eneo hilo. Kanali Obonyo alisema wanamgambo waliouawa ni sehemu ya kundi ambalo limekuwa likitekeleza mashambulizi katika eneo la Pwani. Mnamo Julai mwaka huu, watu tisa waliuawa katika kijiji cha Jima, eneo la Lamu Magharibi ilihali mwezi Agosti watu watatu waliuawa kwenye shambulizi la wanamgambo wa Al-Shabaab dhidi ya basi la abiria katika eneo la Witu, kaunti ya Lamu.

KAULI ZAWAPONZA MWIGULU, IGP SIRRO

Na ASHA BANI
ALIYEKUWA Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi katika utawala  wa Serikali ya Awamu ya Nne, Lawrance Masha, amemshangaa Waziri anayeiongoza wizara hiyo sasa, Mwigulu Nchemba na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro,  kwa kushindwa kuyafanyia kazi matukio ya kutisha yanayoendelea kutokea nchini.
Matukio hayo ni pamoja na mauaji, utekaji na vitisho ambavyo alisema ni mambo mapya kwa Tanzania katika miaka ya hivi karibuni.
Masha aliyasema hayo jana mbele ya vyombo vya habari, katika ofisi za Makao Makuu ya Chadema, akiwa ameongozana na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano Uenezi na Mambo ya Nje  wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mrema na Mkurugenzi wa Mafunzo Oganaizesheni wa chama hicho, Benson Kigaila.
Masha, ambaye alikuwa akizungumzia matukio hayo  akilinganisha na uzoefu wake ndani ya Wizara hiyo,  alisema yeye binafsi tayari angekuwa amekwishayapa uzito wa namba moja  matukio hayo na kuanza kuyashughulikia kikamilifu.
“Mimi nilipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wakati huo kulikuwa na tatizo huko Rorya, watu walikuwa wakipigana na kuuana, lakini niliweka kambi huko kubaini tatizo na likapungua kama si kwisha kabisa.
“Ningekuwa leo Waziri hili ndio lingekuwa namba ‘one’ la kulifanyia kazi, kwani wakati huo sisi tuliacha kazi  ofisini na kwenda kusimamia mambo hayo kule Rorya na tulifanikiwa, sasa sijui yeye kwanini amekuwa na ukimya anashindwa kuchukua hatua,’’ alihoji Masha.
Kwa sababu hiyo, Masha amemwomba Rais  Dk. John Magufuli,  kutosita kuwaelekeza watendaji wake katika Jeshi kuomba msaada  wa kimataifa kuja kuchunguza waliomshambulia kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, kwani kwa kufanya hivyo si dhambi wala fedheha.
Ili kuthibitisha hoja yake hiyo kama kuomba msaada isichukuliwe ni jambo la aibu, Masha ambaye pia ni msomi wa sheria, akiwahi kuiongoza wizara hiyo kati ya mwaka 2008 hadi  2010,  alihoji mbona makamanda wengi nchini wapo Marekani wakisoma, kwanini waogope kupokea msaada wa uchunguzi wakati si dhambi?
“Ningeomba Rais Magufuli kuwaagiza makamanda wake kuomba msaada ili Watanzania wasiendelee kuishi kwa hofu, si kawaida sisi Watanzania kukuta sehemu moja ndani ya wiki mbili au tatu, maiti 17 zinakutwa zikielea katika Bahari ya Coco Beach,” alieleza Masha, huku akionyesha kukerwa.
Masha ambaye katika vuguvugu la uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 alitangaza kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuhamia  Chadema,  alitumia fursa hiyo kumtaka waziri mwenye dhamana kwa sasa, Mwigulu na Jeshi lake kujifunza na kuelewa kwamba ndani ya Jeshi kunatakiwa kufanya kazi kwa weledi na kuweka pembeni masuala ya itikadi za siasa na dini.
Alisema wakati yeye akiwa Waziri katika wizara hiyo,  mambo ya migogoro ya kidini na siasa kwa hayakusumbua nchi kama sasa  na ilikuwa hata nchi nyingine zikiwaonea wivu Watanzania.
Akielezea athari ya matukio hayo kuachwa hivi hivi, Masha alisema hayaathiri  Watanzania  peke yao, bali hata mataifa ya nje kwa kuwa tayari  mataifa mbalimbali wameanza kuulizana kulikoni Tanzania iko hivi kwa sasa?
“Mtaani huko watu wanaogopa  hata kutoka nje, kutembea usiku na hata kuongea, wanajiuliza ule uhuru tuliouzoea kama Watanzania uko wapi, mbona kuna sintofahamu inaendelea nchini na kwanini.’’
Alisema polisi pia wanatakiwa kuelewa kuwa kazi yao kuu ni kulinda raia na mali zao bila kuangalia itikadi.
Akizungumza kabla ya Masha, kwa upande wa Mrema, alisema anashangazwa na hatua za Jeshi la Polisi kushindwa kuyafanyia upelelezi matukio mbalimbali ya mauaji, utekaji yanayoendelea nchini.
Alisema hadi sasa tayari zimepita siku 695 tangu kuuawa kwa kiongozi wao wa Chadema huko Geita, Alphonce Mawazo, siku 329 kupotea kwa mlinzi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Ben Saanane  na siku 30 za kupigwa risasi kwa Lissu na watu wasiojulikana.
Alisema matukio hayo yote hadi sasa  Jeshi la Polisi hawajaeleza chochote zaidi ya kushikiliwa  kwa gari aina ya Nissan nane zikiwa hazina dereva ambazo zimehifadhiwa kusikojulikana  na madereva wake wasiojulikana.
Alisema matukio hayo yakiwa yanaendelea  viongozi na wabunge wa Chadema wameendelea kutishwa na watu wasiojulikana, akiwamo kiongozi wa Kanda ya Ziwa, Ansbert Ngurumo, Mbunge wa Bunda,  Ester Bulaya, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari.
Hivi karibuni, Ngurumo aliandika ujumbe ambao ulisambaa katika mitandao ya kijamii akieleza maisha yake jinsi yalivyo hatarini kutokana  na kazi zake za uandishi wa ukosoaji.
Bulaya inaelezwa alifuatwa nyumbani kwake Bunda na mara kadhaa amelalamika akifuatiliwa na watu ambao hajawafahamu.
“Haya ni matukio ya kuogofya kwa kuwa hata Saanane alitishiwa na kutoa taarifa, Tundu Lissu naye alitoa taarifa kwa zaidi ya wiki tatu pindi akiwa anafuatiliwa na hatimaye akashambuliwa sasa na haya yametolewa taarifa, Jeshi la Polisi kazi yao kufuatilia lakini kimya.
“Aliyekuwa Waziri, Nape Nnauye,  alitishiwa bastola  na baadaye matamko ya Waziri na IGP wanasema ni mtu asiyejulikana wakati alionekana, Lissu risasi hadharani  hakuna kilichofuatiliwa, hivi wako ‘serious’ kweli hawa?” alihoji Mrema.
Kwa upande wake, Kigaila, ambaye alizungumza baada ya Mrema, alilinyooshea kidole Jeshi la Polisi kwa kushindwa kuwakamata watu wanaoandika mitandaoni na kutoa vitisho.
Aliwataja watu hao kuwa ni pamoja na mtu mmoja anayejiita Jerry Muro, aliyekuwa mwandishi wa habari, ambaye ameandika ujumbe kupitia mitandao ya kijamii, ambao katika moja ya vipengele vyake vinasomeka … angekuwa yeye ndio Jeshi la Polisi kwa utoto wanaofanya Lema na Nassari angewapoteza.
Kutokana na hilo, alisema  andiko hilo la Jerry litakuwa ni ushahidi tosha kwao endapo wabunge hao watakuja kudhurika mbele ya safari.
Mbali na Jerry, mwingine waliyemtaja  ni Suleiman Othman,  ambaye naye aliandika  kupitia mitandao ya kijamii akimlenga Lissu  kwamba: “Hiyo ni dawa kwa watu wenye siasa kama zake waache mara moja,” akaandika tena: “Naomba ruhusa ya kumuua Lissu, waliompiga Lissu walikosea kwa kuwa hajafa.”
Kigaila hakuishia hapo, alisema kuwa, mtu huyo ambaye wamekuwa wakifuatilia maandiko yake hivi karibuni ameandika vibaya zaidi kuwa, kwanini aliyempiga Lissu amemuacha hai alitegemea asikie amekufa na kwamba, akifika Tanzania mara hii hatafanya makosa.
Alisema kitendo cha Jeshi la Polisi kuwaacha watu hao pasipo kuwachukulia hatua yoyote kinawatia shaka na kuwafanya wajenge hisia kwamba Serikali huenda ikawa inahusika.
Alisema watu hao wangeandika ujumbe hasi dhidi ya Serikali tayari wangekuwa wameshatiwa hatiani kwa ajili ya kulisaidia Jeshi la Polisi.
“Huyu mtu awe yeye halisi asiwe yeye, lakini tulitegemea kuwa mikononi mwa polisi kwa sasa, ina maana IGP haoni?’’ alihoji.
Alisema kuwa, kuna watu walitupia picha za askari kupigwa risasi Mbagala, lakini waliofanya vile walikuwa Mahenge, hivyo walichukuliwa kutoka Mahenge hadi Dar es Salaam kuisaidia Polisi Makao Makuu.
Pia alishangazwa na tamko la Mwigulu la kusema kuwa gari lililotajwa na Lissu lipo Arusha na wala halijawahi kuletwa Dar es Salaam.
“Jeshi la Polisi halina kifaa cha kugundua magari yanayotembea, hawana kamera za usalama za nchi nzima, sasa Waziri amejuaje au amekuwa wakili wa watuhumiwa?” alihoji.
Kigaila pia alilikumbusha Jeshi la Polisi kuanza upelelezi na walinzi wa wawili wa Kampuni ya Suma JKT waliokuwa wakilinda nyumbani kwa Lissu, kuliko kumtaka dereva ambaye anatibiwa kisaikolojia kwa sasa.
Kwa upande wake,  Lema alimweleza IGP Sirro kuwa nafasi yake haijengwi na kuwa na ghala kubwa la silaha, bali kwa kusema kweli mbele ya bosi wake.
Alisema kutokana na matukio yanayotokea sasa nchini, kama kweli serikali ingekuwa inafuata na kuzingatia utawala wa sheria na Katiba, basi Mwigulu na IGP Sirro wasingekuwa bado wako ofisini.
Alisema juzi walipeleka ushahidi kwa  IGP Sirro wa aliyemtishia bastola  aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye,  lakini wanashangaa Jeshi la Polisi kudai kwamba hajulikani.
Alisema kijana huyo amekuwa akionekana mara kadhaa akimlinda Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, lakini baada ya kumwonyesha bado IGP amekaa kimya pia.
“Sasa  sijui Mwigulu na IGP wanafanya nini ofisini hadi leo, anaulizwa anajibu watu wasiojulikana sasa kama hawajulikani na yeye Waziri hajulikani atoke ofisini,’’ alieleza Lema.
Alisema kwa sasa wanaishi kama wakimbizi katika nchi yao, akitolea mfano wa yeye binafsi kwamba  ametishiwa kuuawa na hivi karibuni saa saba usiku alikimbia na kumwacha mkewe akiwa kwenye gari  baada ya kuona wanafuatiliwa na watu wasiojulikana.
Alisema hayo mambo yana mwisho na kama Jeshi linashindwa kufanya kazi yake, basi jamii mwisho wa siku itafanya yenyewe.
“Sisi tuna mwili na tuna damu na ndugu, kama Rais Magufuli, Serikali yake haijui nani anafanya mambo haya, basi yeye mwenyewe hayuko salama pia na nchi haiko salama.’’

Mugabe amshusha cheo makamu wa rais


Harare, Zimbabwe. Rais Robert Mugabe amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri ambalo amewaondoa baadhi na kuingiza sura mpya lakini habari kubwa ni kushushwa kwa makamu wa rais wake, Emerson Mangagwa.
Katika mabadiliko hayo, Mangagwa sasa atakuwa waziri wa utalii hali ambayo imetafsiriwa kwamba ameshushwa cheo.
Shirika la habari la ZimNews, likinukuu chanzo cha uhakika kutoka ndani ya serikali limesema Mnangagwa alikwishadokezwa kujiandaa kwa makubwa yanayotarajia kumfika na sasa amepokonywa nafasi zote za makamu wa rais na ile ya makamu wa rais katika chama tawala cha Zanu-PF.
Wakati fulani Mnangagwa alikuwa anapewa nafasi ya kumrithi Mugabe ikiwa atafariki dunia au kuamua kung’atuka. Lakini katika siku za hivi karibuni alianza kutopikika na wenzake hususan mke wa Raus Mugabe, Grace Mugabe.
Mnangagwa aliwahi kushutumiwa na mwanamama huyo kwamba anashirikiana na watu waliofukuzwa Zanu PF. Pia,  alishutumiwa na Grace kuwa alikuwa anafanya njama za kutaka kumpindua rais ili arithi nafasi yake. 
Kilichomponza zaidi ni king’ang’anizi chake kwamba alikula sumu iliyokuwemo kwenye Ice Cream kutoka kampuni ya maziwa inayomilikiwa na Grace na akapelekwa Afrika Kusini kwa matibabu. Rais Mugabe alisema aliambiwa na madaktari waliokuwa wanamtibu makamu huyo wa rais kwamba kuugua kwake hakukutokana na sumu, lakini yeye alishikilia kwamba alilishwa sumu hali iliyoonekana ni kumdhalilisha Rais Mugabe.
Haya yakiwa hivyo, ndani ya Zanu PF kuna makundi makubwa mawili yanayonyukana kuwania uteuzi wa kugombea urais; la kwanza linaitwa G40 ambalo kuna makamu wa Rais Phelekezela Mphoko huku likiungwa mkono na Grace, na la pili linaitwa Lacoste ambalo linaongozwa na Mnangagwa. Kwa mabadiliko haya ni kama makamu huyo wa rais amepunguzwa kasi.
Aliyekuwa Waziri wa Fedha Patrick Chinamasa nafasi yake imechukuliwa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Ignatius Chombo, ambaye ni katibu mkuu wa Zanu PF anayehusika na masuala ya utawala. Wadadisi wa masuala ya siasa wameshtushwa na uteuzi huo wakihoji atafanya nini kuhusu sarafu ya Zimbabwe ambayo inaendelea kushuka.
Chinamasa amepewa wizara mpya isiyofahamika ya Usalama wa Mitandao. Muda mfupi baada ya kupewa nafasi hiyo, mwigizaji maarufu Carl Joshua Ncube alitania: "Jamani Patrick Chinamasa anawafuatilia kwenye Twitter ".
Aliyekuwa Waziri wa Utalii, Walter Mzembi sasa ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje.
Mpwa wa Mugabe, Patrick Zhuwao anayeonekana kuwa mfuasi mkuu wa kundi la G40 linalopigiwa upatu na Grace ameteuliwa kuwa Waziri wa Kazi akitokea Wizara ya Vijana na Utamaduni.
Hatua ya kupandikwa kwake ni ushahidi wa kutosha kwamba umelenga kulipa nguvu kundi la G40 dhidi ya lile la Mnangagwa linaloitwa Lacoste.

Walionusurika kifo Ziwa Victoria wamlaumu dereva


Misungwi. Walionusurika ajali ya daladala iliyotumbukia Ziwa Victoria, wamesema iwapo dereva angesikiliza ushauri madhara yasingekuwa makubwa.
Akizungumza katika Hospitali ya Bukumbi Mission wilayani Misungwi alikolazwa, Yohana Ngabula (28) mkazi wa Kijiji cha Buyagu wilayani Sengerema amesema amepoteza mama na dada katika ajali hiyo.
Ngabula amesema walikuwa wakitoka jijini Mwanza kufuatilia mafao ya baba yao katika ofisi za Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).
“Nilimshauri dereva agonge hata gari lililokuwa mbele yake badala ya kulielekeza ziwani lakini hakusikia mwisho wake ndiyo hayo yaliyotokea,” amesema.
Amesema baada ya gari kutumbukia ziwani alipasua kioo na kutoka ndipo walipofika vijana wakamuokoa.
Majeruhi mwingine mkazi wa Ibisabageni, Paulo Lazaro ambaye ni mwalimu wilayani Sengerema amesema, “Tulimshauri dereva agonge vitu nchi kavu kuliko kuipeleka gari majini lakini hakusikiliza ushauri wetu, pengine tungepona wengi zaidi.”
Mwalimu huyo amesema alipita dirishani baada ya gari kutumbukia ziwani na kwamba, ana maumivu mabegani na mgongoni.
Mwingine aliyenusurika katika ajali hiyo, Sophia Biambina (32) amesema amepoteza watoto wawili katika ajali hiyo.
Amesema walikuwa wakitoka kwenye msiba wa baba yake wilayani Magu na alikuwa akielekea nyumbani kwake Nyapande wilayani Sengerema.
“Baada ya ajali nilijikuta nimeshatoka nje sikujua nimetokaje, najihisi maumivu makali kwa sababu nilikunywa maji mengi. Kinachoniuma ni kuwapoteza watoto wangu, tulitoka msibani kumzika baba yangu,” amesema.
Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Bukumbi, Dk Robert Shija amesema walipokea maiti 12 na majeruhi hao watatu.
Amesema walipokea miili ya Joseph Paulo, Rehema Makalanga, Mariamu Kagosha, Pendo Msafiri, Salome Msafiri, Joyce Hamadi, Martha Makenzi, Gwanchele Mswagi na Kazungu Lukuba wote wakazi wa Wilaya ya Sengerema.
Wengine ni Martine Kamlamo mkazi wa Bukumbi, Hamadi Zahalaki wa Bukoba na Ally Abdul wa Kayenze wilayani Ilemela.
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda ameuagiza uongozi wa hospitali kuwa, ndugu watakaoshindwa kusafirisha miili wawasiliane na ofisi ya wilaya kwa ajili ya kupata msaada.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole amesema walipanga kuisafirisha miili hiyo lakini tayari ndugu wameshaichukua.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi amesema hakuna miili mingine ambayo imeopolewa lakini Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kimerudi eneo la tukio.
Msangi alisema jana Jumatatu kuwa hawajapata idadi kamili ya watu waliokuwemo kwenye gari hilo.

TRA yatangaza makusanyo ya miezi mitatu

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi,
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo 
Dar es Salaam. Makusanyo ya kodi kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2017/2018 (Julia, Agosti na Septemba) yamefikia Sh3.65 trilioni ambayo ni ongezeko la asilimia 1.2 ukilinganisha na makusanyo ya kipindi hicho kwa mwaka uliopita.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo amesema makusanyo hayo ni hatua nzuri kuelekea lengo la mwaka ambalo ni Sh17 trilioni.
Ametoa mchanganuo wa makusanyo hayo kwa kila mwezi ambao umeonyesha kuwa wamekusanya zaidi ya Sh1 trilioni.
“Julai tulikusanya Sh1.1 trilioni, Agosti Sh1.2 trilioni na Septemba Sh1.3 trilioni. Watu wamekuwa wakitaka makusanyo hayo yawe yanasomwa kila mwezi lakini tukitoa kila robo ya mwaka tunaonyesha kiasi kwa kila mwezi,” amesema Kayombo.
Ukizidisha makusanyo hayo mara nne ambayo ni tafsiri ya mwaka mzima jumla inakuwa Sh14.6 trilioni lakini Kayombo anasema makusanyo ya robo moja hayawezi kutoa picha ya jumla kwasababu misimu ya biashara inatofautina hivyo ana matumaini lengo litafikiwa.
Amevitaja vyanzo vikuu vya mapatio kuwa ni viwanda, ajira na uingizaji wa bidhaa lakini amesema vyanzo hivyo hutoa kodi zaidi kulingana na wakati.
Kadhalika Kayombo amewakumbusha wamiliki wa majengo nchi kulipa kodi zao mapema badala ya kusubiri mwishoni mwa mwaka na kusababisha misongamano na usumbufu usio wa lazima.
Pia wamewataka wenye michezo ya bahati nasibu wametakiwa kulipa kodi zao kama sheria inavyoelekeza. “Anayepaswa kulipa kodi kwa wiki alipe na anayepaswa kulipa kwa mwezi au mwaka naye afanye hivyo.”
Kayombo amewataka wananchi kutumia na kuziamini takwimu zinazotolewa na mamlaka hiyo kwani takwimu zote nyingine kuhusiana na mapato ambazo hazijatolewa na TRA sio za kuaminika. 

MAT yazindua kampeni ya maadili utoaji huduma


Dar es Salaam. Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kimezindua rasmi kampeni ya kitaifa kuhamasisha wataalamu wa afya kuzingatia maadili katika utoaji huduma.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumanne, Rais wa MAT, Dk Obadia Nyongole amesema kampeni hiyo itakuwa sehemu ya kongamano la afya la 49 kitaifa ikiwa ni agenda kuu ya kukuza maadili ya kitabibu na kitaaluma miongoni mwa wataalamu wa afya.
Amesema kuwa kampeni hiyo itaanzia jijini Mwanza Oktoba 16, ambapo viongozi wa chama na watoa mada watazungumza na madaktari kama sehemu ya kampeni na baadaye wataelekea mikoa mingine.
"Malalamiko yapo kwamba hivi sasa kuna pengo kubwa la mawasiliano kati ya wataalamu wa afya na wagonjwa au ndugu wa wagonjwa. Kuna baadhi ya mifano hai hapa nchini, hususani pale ambapo ndugu wa wagonjwa hujichukulia sheria mikononi na kuwashambulia watoa huduma," amesema Dk Nyongole.
Amesema lengo la kampeni ni kuimarisha mahusiano kati ya wagonjwa na watoa huduma kwa kuwakumbusha wanataaluma juu ya majukumu waliyonayo kwa wagonjwa au wateja wao.  "MAT inachukua jukumu la kusimamia wanataaluma katika kuzingatia viwango vya utoaji huduma za kitabibu nchini Tanzania," amesema.

Wafanyakazi wawili wa chuo wauawa pwani ya Kenya

Ukunda
Wafanyakazi wawili wa chuo kikuu kimoja mjini Mombasa wameuawa baada ya watu wenye silaha kushambulia gari karibu na bewa la chuo katika kaunti ya Kwale, pwani ya Kenya.
Watu kadha wenye silaha walifyatulia magari yaliyokuwa yakisafirisha wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa (TUM) kutoka kwenye vyumba vyao vya malazi hadi kwenye bewa la chuo Ukunda.
Afisa wa polisi aliyezungumza na shirika la habari la Reuters, lakini hakutaka jina lake litajwe, amesema dereva na polisi wawili wamejeruhiwa.
Afisa huyo amenukuliwa na Reuters akisema: "Basi lilikuwa likiwasafirisha wanafunzi wa chuo kutoka vyumba vyao vya malazi hadi kwenye bewa la chuo Ukunda kwa masomo na lilikuwa linasindikizwa na gari ndogo lililokuwa na wafanyakazi wa chuo na polisi wawili wa kuwalinda."
Haijabainika nani alihusika katika shambulio hilo.
Wanamgambo wa kundi la Kiislamu la al-Shabab kutoka Somalia mara kwa mara hutekeleza mashambulio pwani ya Kenya na maeneo ya Kenya yanayopakana na taifa hilo.
Mwaka 2015, walishambulia Chuo Kikuu cha Garissa na kuua wanafunzi 148.
Majeshi ya Kenya yamekuwa yakikabiliana na wapiganaji hao nchini Somalia chini ya kikosi cha Umoja wa Afrika (Amisom).
Nchini Kenya, jeshi la nchi hiyo limekuwa likitekeleza mashambulio katika msitu wa Boni unaopakana na Somalia kuwafurusha wapiganaji ambao wanadaiwa kupanga na kutekeleza mashambulio kutoka katika msitu huo.
Jumatatu usiku, jeshi la Kenya (KDF) lilitangaza kwamba liliwaua wanamgambo watano wa al-Shabab katika msitu huo.
Msemaji wa jeshi David Obonyo alisema wanajeshi hao walipanda bunduki sita aina ya AK-47 na risasi 321 wakati wa operesheni hiyo ya kijeshi Bodhei, Boni.

Kituo cha Sheria chataka adhabu ya kifo ifutwe



.  Spika wa Bunge la Uganda, Rebecca Kadaga
.  Spika wa Bunge la Uganda, Rebecca Kadaga 
Kampala, Uganda.  Spika wa Bunge la Uganda, Rebecca Kadaga ameahidi kuwa atahakikisha unaongezwa ulinzi kwa ajili ya usalama wa wabunge baada ya hivi karibuni nyumba za wabunge wa upinzani kushambuliwa kwa magruneti.
Wabunge wa upinzani ambao nyumba zao zilishambuliwa kwa magruneti ni Moses Kasibante wa Rubaga Kaskazini, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine wa Kyadondo Mashariki na Allan Ssewanyana wa Makindye Magharibi.
Wabunge hao ndio walikuwa vinara wa kupinga mpango wa kutaka kuondolewa kwenye katiba ibara inayoweka ukomo wa umri wa rais.
Kadaga alitoa kauli hiyo ya kutuliza alipomtembelea Mbunge wa Manispaa ya Mityana, Francis Mutebi Zaake ambaye alijeruhiwa zilipofumuka ngumi ndani ya Bunge. Pia alitembelea nyumbani kwa Kasibante.
“Nitakwenda kuzungumza na polisi ili wahakikishe unakuwepo ulinzi wa ziada. Nitazungumza na Inspekta Jenerali wa Polisi ahakikishe unakuwepo uangalizi katika maeneo ili wasishambuliwe,” alisema.
Zzake ambaye bado anauguza majeraha anadai kwamba alipigwa ngumi na Waziri wa Kazi, Jenerali Katumba Wamala hadi akapoteza fahamu.
Ssewanyana na Bobi Wine walishambuliwa wiki iliyopita na watu wasiojulikana ambao walirusha magruneti kwenye nyumba zao.
Mashambulizi dhidi ya wabunge hao yalifanyika wiki moja baada ya magruneti kurushwa na kulipuka katika nyumba ya Kasibante kulipokuwa kunakaribia kupambazuka.
Wapinzani waliishutumu serikali kuwa nyuma ya mashambulizi hayo kwa lengo la kuwatisha na kuwafanya wananchi wanaopinga mpango wa kuondoa ukomo wa umri wa rais wawe na hofu
Hata hivyo, msemaji wa serikali Ofwono Opondo alielezea matukio hayo kuwa ni mbinu za wapinzani wenyewe kuiingiza serikali.

Kituo cha Sheria chataka adhabu ya kifo ifutwe

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Ana Henga akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo ikiwa ni katika maadhimisho ya kupinga adhabu ya kifo duniani. 
Dar es Salaam. Ikiwa dunia leo inaadhimisha siku ya kupinga adhabu ya kifo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeitaka Serikali kuifuta adhabu hiyo.
Pia, Serikali na mamlaka husika zimetakiwa kufuta vipengele na sheria zinazoelekeza adhabu hiyo.
Kituo hicho kimeshauri mamlaka husika kuweka adhabu mbadala wa kifungo cha maisha ili kuthamini uhai ambao ni haki ya kila binadamu.
Akizungumza leo Jumanne, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Ana Henga amesema adhabu ya kifo inaondoa uwezekano wa mkosaji kujirekebisha na badala yake ni kuendeleza ukatili na kuondoa ubinadamu.
Henga amesema adhabu ya kifo inavunja misingi ya tamko la kimataifa la haki za binadamu la mwaka 1948 ambalo linasema kila mtu ana haki ya kuishi.
Amesema Tanzania inapaswa kujifunza kutoka kwa mataifa mengine duniani ambayo hayatekelezi adhabu ya kifo na badala yake kutoa adhabu mbadala kama vile kifungo cha maisha na kazi ngumu kwa watuhumiwa wa mauaji ili kulinda haki ya msingi ya kuishi.
Henga amesema harakati za kupinga adhabu ya kifo hazimaanishi kuwa ni kutetea uhalifu, hasa mauaji ila ukweli ni kwamba, hakuna ushahidi kuwa uwepo wa adhabu hiyo unaweza kupunguza uhalifu badala yake umekuwa ukiongezeka.
Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani kama vile China, Korea Kaskazini na Marekani ambazo zinaruhusu na kutekeleza adhabu ya kifo katika sheria zake.
Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania, kifungu cha 197 kinaeleza mtu yeyote anayepatikana na   hatia ya kuua atahukumiwa adhabu ya kifo.
Henga ameitaka Serikali itekeleze pendekezo la mpango wa kujitathmini wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 2016 kwa kuridhia mkataba wa nyongeza wa haki za kiraia na kisiasa na kutangaza kuwa haitekelezi adhabu hiyo.
Amesema kwa mujibu wa ripoti ya haki za binadamu ya mwaka 2016 takwimu zinaonyesha hadi mwaka 2015 kulikuwa na watu 472 waliohukumiwa kunyongwa kati yao wanaume wakiwa 452 na wanawake 20.
Pia, kati ya hao wanaosubiri kunyongwa ni 228, huku 244 wakisubiri uamuzi wa rufaa zao.
"Hii ni adhabu ya kibaguzi maana mara nyingi wanaopatikana na hatia na kupewa adhabu ni masikini wasioweza kuwa na uwakilishi na ushauri wa kisheria," amesema Henga.

UTPC YAWANOA WAANDISHI WA HABARI DODOMA


Umoja  wa Vilabu vya waandishi wa habari nchini (UTPC) inaeendesha mafunzo ya siku (5) ya waandishi  habari za mazingira (27)mkoani Dodoma, kwa waandishi kutoka mikoa yote nchini ikiwa ni awamu wa kwanza

Afisa program wa (UTPC) anayefanya kazi kitengo cha Mafunzo ,Utafiti na Machapisho Victor Maleko amesema kuwa  lengo kubwa la mafunzo hayo ni  kuwapata waandishi waliobobea katika kuandika habari za mazingira katika maeneo yao.

"Unapowapata wabobezi hawa ni rahisi kwa wadau wa habari kutoka mikoani kufanya kazi na waandishi amabao wapo madhubuti kwenye maeneo yao,wapo waandishi wengi makanjanja hawajui wanachokifanya"alisema Victor.

Mafunzo mengine yanayoendeshwa sambamba na haya ni pamoja na  mkoani Pwani yanaendelea mafunzo ya uandishi wa habari za Jinsia ,mkoani Morogoro yanaendelea mafunzo ya uandishi wa habari za Vijijini na mkoani Dodoma mafunzo ya uandishi wa habari za Mazingira

"tunataka tuwapate machampion watakao simamia habari za mazingira peke yayake,Jinsia  pamoja na  waandishi wa habari za vijijini tu"alisema

Amewaasa waandishi wa habari ambao hawajajiunga katika vilabu vya waandishi  habari vilivyopo kila mkoa wajiunge  kwani zinawasaidia kuwakutanisha pamoja watanufaika na mafunzo mbalimbali yanayotolewa na UTPC ,ambapo amesema  mafunzo kama haya hayawezi kutolewa kwa mwandishi ambaye siyo mwanchama .

Kwa upande wake muwezeshaji wa mafunzo hayo Deodatus Mfugale amesema kuwa lazima mwandishi awe na malengo,waandike habari zinazoleta mabadiliko na zinazogusa hisia za jamii kwa ujumla.''Mwandishi kama unaandika kila kitu muda wako unakaribia kwisha"alisema Mfugale.

Amesema kuwa UTPC itaendelea kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari wa habari chini ufadhili wa Ubalozi wa Sweeden hapa nchini kwa muda wa miaka (5) ambapo huu ni mwaka wa( 2) hadi 2020 wataendelea kubadilisha mafunzo hayo kadri ya  uhitaji wa waandishi .
 Muwezeshaji wa mafunzo Deodatus Mfugale akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mafunzo hayo katika ukumbi wa Centurion Nala Hotel Dodoma
Afisa program wa (UTPC) anayefanya kazi kitengo cha Mafunzo ,Utafiti na Machapisho Victor Maleko akizungumza na waandishi katika Mafunzo hayo mkoani Dodoma.
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika mafunzo hayo

Diego Costa aongezeka kitambi


Madrid, Hispania. Diego Costa ameanza maisha mapya katika klabu yake ya zamani Atletico Madrid inayoshiriki Ligi Kuu Hispania.
Costa alirejea kwa mbinde Atletico Madrid, baada ya kocha wa Chelsea Antonio Costa kumwambia hamtaki katika kikosi chake muda mfupi baada ya kutua Stamford Bridge.
Mchezaji huyo mzaliwa wa Brazil mwenye uraia wa Hispania, aligoma kurejea Chelsea licha ya kukingiwa kifua na vigogo wa klabu hiyo kabla ya kupigwa bei katika usajili wa majira ya kiangazi.
Costa, 29, juzi alikuwa na uso wa tabasamu alipokuwa akijifua katika mazoezi na wachezaji wenzake kwa lengo la kujiweka fiti.
Pia mshambuliaji huyo alipewa mazoezi binafsi ili kurejesha 'shepu' yake ya kawaida baada ya kubainika ana uzito mkubwa.
Baadhi ya wachezaji wa timu hiyo waliokuwa wakipasha moto misuli ni Fernando Torres, Kevin Gameiro na Angel Correa.
Mshambuliaji anataka kujiweka fiti kuendeleza makali katika kikosi hicho kama alivyokuwa Chelsea alipokuwa kinara wa mabao licha ya kutajwa kuwa ni mtukutu.
Baada ya kurejea Atletico kwa 57 pauni milioni, klabu hiyo itasubiri kuanza kupata huduma yake hadi mwakani kwa kuwa imefungiwa kusajili majira ya kiangazi baada ya kukiuka kanuni.

Kocha ashangaa kuonyeshwa kadi nyekundu


Kilimanjaro. Mchezo wa SDL kati ya AFC Arusha na Pepsi zote za Arusha uliochezwa Jumatatu katika Uwanja wa Ushirika na kumalizika kwa sare ya bao 1-1, umeibua malalamiko baada  ya mwamuzi wa kati kudaiwa kuharibu mchezo huo, huku kocha wa AFC akilimwa kadi nyekundu.
Mwamuzi Goodluck Simba kutoka Pwani alilaumiwa na AFC kuwa aliwapa Pepsi bao ambalo sio halali pamoja na kuwanyima penalti, katika mchezo huo kocha mkuu wa timu ya AFC, Gerald Totoo alioneshwa kadi nyekundu kwa kuondoka eneo lake wakati mchezo ukiendelea.
Totoo alisema baada ya kurudi katika eneo lake alishangaa kuoneshwa kadi nyekundu wakati hakufanya jambo lolote baya kwa mwamuzi wala kwa kamisaa wa mchezo huo
“Baada ya kuona mwamuzi anachezesha sivyo nilimfuata kamisaa wa mchezo huo Babtise Mihafu aliyekuwa jukwaani na kumweleza jinsi ataharibu mchezo, kisha nikarejea kwenye benchi langu,” alisema Totoo.
 Kocha huyo aliongeza kuwa, timu zinapaswa kuwa makini kwa kila mchezo hasa za Arusha ambazo zimehamia Moshi kwenye Uwanja wa Ushirika wasipokuwa makini itawagharimu.

Zari apata dili Mercedez Benz


Dar es Salaam. Mwanadada Zarina Hassan maarufu kwa jina la Zari the boss lady amepata dili la kuonyesha magari aina ya Mercedez-Benz ya kampuni ya AMG Performance Centre iliyoko nchini Afrika ya Kusini.
Hayo yameonekana baada ya mwanadada huyo kuweka picha katika ukurasa wake wa Instagram gari nyeupe aina ya Mercedez-Benz huku akiwa amevalia suti yenye rangi ya zambarau.
Katika kurasa huo aliweka picha tofauti tofauti na kuandika maneno yafuatayo ‘amgperformancecentremenlyn is your centre for class & #stateTheArt cars. Thank you for the car’ na nyingine akiweka #closeDealsInHeels.
Baada ya ujumbe huo mashabiki wake wamempongeza kwa hatua hiyo hasa baada ya yote aliyoyapitia katika maisha yake ya mahusiano na msanii Naseeb Abdul maarufu kwa jina la Diamond Platnumz.

Ajirusha akiwa uchi kwenye kundi la simba

Franco Luis akishambuliwa na simba kabla ya
Franco Luis akishambuliwa na simba kabla ya kuokolewa na askari wa bustani ya wanyama.  
Chile. Ukistaajabu ya Mussa utayaona ya Firauni,  kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Franco Luis ameshambuliwa na kundi la simba baada ya kujirusha ndani ya bustani ya wanyama hao akiwa uchi.
Luis  aliwaacha mdomo wazi watu waliofurika kwenye bustani hiyo ya Santiago  mwishoni mwa wiki ambao wengi waliambatana na  familia zao.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Mail la Uingereza, kijana huyo mwenye miaka 20, alikimbizwa hospitali baada ya walinzi wa bustani hiyo kumuokoa kwa  kuwaua simba wawili waliokuwa wanamshambulia.
Uongozi wa bustani hiyo ulithibitisha tukio hilo na kudai kwamba kijana huyo alishambuliwa akiwa uchi wa mnyama baada kuvunja uzio na kuingia kwenye kundi hilo.
Mkurugenzi wa Santiago Alejandra Montalva alisema walijua kijana huyo aliingia  kwenye bustani hiyo kama wateja wa kawaida wanavyolipa tiketi  kwa lengo  la kutembelea hapo.
‘‘Baada ya kufanya malipo kama mteja wa kawaida kijana huyo hakupita kwenye njia inayotumiwa na wateja bali aliezua paa la simba hao na kutumbukia ndani na kuanza kushambuliwa,’’ alisema
Alisema ni kitendo cha kushangaza kwani kila mtu alishikwa na bumbuwazi baada ya kumuona kijana huyo akijirusha kwenye kundi hilo la simba na kuanza kupigana nao.
Alisema askari wa bustani hiyo walitumia nguvu za ziada kuhakikisha wanaokoa maisha ya kijana huyo, ambaye hawajafahamu fika kama alikuwa na akili timamu.
 Atoa sababu
 Kwa upande wake kijana huyo alisema alifanya kitendo hicho cha kustaajabisha kila mtu kutokana na ufunuo alioshushiwa na  Mungu.
Shuhuda
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Cynthia Vasquez alisema  baada ya Luis kujirusha ndani ya bustani hiyo, simba waliokuwa ndani hawakumdhuru kwanza.
“Cha kushangaza simba hao walianza kucheza naye,”alisema Vasquez
 Vasquez ambaye alikuwa miongoni mwa wageni waliotembelea bustani hiyo, alisema baada ya dakika chache   Lius alisikika akipiga kelele. “Walianza kumrarua...alipiga kelele aliita jina la Yesu,”alisema.                       
Alisema kelele hizo ziliwavuta watu wengi ambao walifika kushuhudia tukio hilo.
Vasquez alisema walinzi waliofika kuokoa maisha ya Luis walilazimika kufyatua risasi juu ili kuwatawanya watu. “Waliingia baada ya kuwaua simba hao na kumtoa Luis ambaye alikuwa ameshajeruhiwa vibaya,” alisema.
Baba aongea
Baba mzazi wa Luis alisema  alishaanga kusikia watu wanapiga kelele na alipofika katika eneo la tukio alimkuta kijana wake akiwa amejeruhiwa vibaya na simba.

Rais Museveni amvika nishani ya heshima Aga Khan


Kampala, Uganda.  Rais Yoweri Museveni amemvisha Mtukufu Prince Karim Aga Khan IV nishani ya juu ya heshima barani Afrika (Most Excellent Order of Pearl of Africa, The Grandmaster) ili kutambua miongo kadhaa ya mchango wake katika maendeleo ya Uganda.
Museveni alimvisha nishani hiyo Jumatatu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru yaliyofanyika kwenye viwanja vya Bushenyi-Ishaka katika wilaya ya Bushenyi.
Mtukufu Aga Khan, ambaye ni Imam wa madhehebu ya Ismailia, kupitia taasisi ya Aga Khan ana miradi mingi ya maendeleo katika nyanja za elimu, nishati, afya, hoteli na utalii, vyombo vya habari.
Aga Khan aliwasili nchini Uganda Jumapili kuwahi maadhimisho ya miaka 55 ya uhuru na alikuwa na kikao na Rais Museveni pamoja na maofisa waandamizi wa serikali katika Ikulu ya Entebbe.
Mapema wakati wa utoaji taarifa kwa waandishi wa habari katika Kituo cha Habari Uganda, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Esther Mbayo alidokeza sababu za kumtunukia nishani hiyo ya heshima Aga Khan.
“Atatunukiwa nishani ya heshima ya juu kwa sababu ya mchango wake mkubwa wa kiuchumi alioutoa kwa nchi yetu duniani kwa ujumla,” alisema Mbayo.

Mwakilishi ahoji sababu za wingi wa ajali Z’bar


Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar, Mohamed Ahmada Salum 
Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imesema sababu kuu za ajali za mara kwa mara ni uzembe wa baadhi ya madereva na kutozingatia alama za barabarani.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar, Mohamed Ahmada Salum aliyasema hayo jana katika kikao cha Baraza la Wawakilishi wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Chake Chake, Suleiman Sarahan Said aliyehoji kwanini sheria za usalama barabarani zilizopo hazijasaidia kutatua suala la ajali za barabarani.
Pia mwakilishi huyo alisema sababu anayoiona ni ukosefu wa alama za barabarani na hivyo Serikali kutoa adhabu kwa madereva ni sawa na kuwaonea.
Akijibu swali hilo, Salum alisema pamoja na uwapo wa uhaba wa alama za barabarani, lakini uzembe wa madereva ndilo tatizo kubwa.
“Pamoja na hilo lakini suala la sheria linamwajibikia kila mmoja wetu, hivyo hatutakuwa tayari kuona uzembe unafanyika kisha tusimchukulie hatua za kisheria dereva kwa kosa lake la makusudi,” alisema Salum.
Hata hivyo mwakilishi huyo alisema kuwa licha ya uchache wa alama hizo lakini katika baadhi ya maeneo zipo isipokuwa kinachofanywa na baadhi ya madereva hao ni kuzipuuza na kusababisha ajali. Alisema kuwa pamoja hali hiyo kuna baadhi ya watu wamekuwa wakiharibu miundombuni ya barabara kwa makusudi, hali ambayo nayo huchangia kutokea kwa ajali.
Alisisitiza kwamba si jambo la kufurahisha kuona Serikali inafanya jitihada kubwa kujenga miundombinu kwa manufaa ya wananchi, lakini liwepo kundi ambalo linaiharibu. “Tunashirikiana na polisi kutoa elimu kwa madereva na wananchi juu ya matumizi sahihi ya barabara ili kila mmoja awajibike kwa mujibu wa nafasi yake,” alisema Salum.

Iceland: Taifa la watu 335,000 lafuzu Kombe la Dunia

IcelandHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionIceland waliwashinda Croatia na Uturuki na kufuzu kutoka Kundi I
Iceland imekuwa nchi ndogo zaidi kuwahi kufuzu kwa Kombe la Dunia baada ya kuwalaza Kosovo 2-0 na kumaliza kileleni kundi lao la kufuzu kwa michuano hiyo itakayofanyika Urusi 2018.
Iceland, ambao walifika robofainali Euro 2016, baada ya kuwaondoa England hatua ya 16 bora, ni taifa la raia 335,000 pekee.
Ndiyo nchi ya kwanza kufuzu kwa Kombe la Dunia ikiwa na idadi ya watu ambao ni chini ya milioni moja.
Gylfi Sigurdsson wa Everton na Johann Gudmundsson wa Burnley ndio waliofungia taifa hilo Jumatatu.
Sigurdsson aliwapa matumaini kwa kufunga muda mfupi kabla ya mapumziko na kisa akamsaidia Gudmundsson kufunga bao la kuwahakikishia ushindi.
Iceland sasa wameshinda mechi saba kati ya 10 Kundi I la kufuzu kwa Kombe la Dunia.
World Cup minnows
Image captionMataifa madogo zaidi kuwahi kufuzu kwa Kombe la Dunia

Mkufunzi alihofia sherehe zingewaathiri

Mkufunzi wa Iceland Heimir Hallgrimsson alikuwa na wasiwasi kwamba angetatizika kuwapa motisha wachezaji wake baada ya kufana sana Euro 2016 nchini Ufaransa.
"Bia ya kwanza baada ya sherehe huwa si nzuri. Jambo ngumu zaidi lilikuwa kuendeleza ufanisi baada ya sherehe yetu kubwa kutokana na ufanisi Ufaransa," alisema.
"Na isitoshe, tulikuwa kwenye kundi lenye ushindani mkali lililokuwa na Croatia, Uturuki, Ukraine na Finland, nchi ambazo zinatuzidi kwa viwango vya soka.
"Ufanisi huu si mwisho bali ni safari ndefu ya kuelekea hadi kwenye mwisho wa safari."
Meneja wa Kosovo Albert Bunjaki amesifu sana Iceland kwa ufanisi wao na kusema kuwa hilo litatia moyo mataifa madogo.
"Naipongeza timu yote ya Iceland," amesema Bunjaki, ambaye taifa lake la Kosovo lina watu mara sita zaidi ya Iceland.
"Ni mfano mwema kwa mataifa madogo kama nchi yetu ambao hulenga kuwa na timu nzuri, yenye mpangilio mzuri, siku za usoni."