Pia, Serikali na mamlaka husika zimetakiwa kufuta vipengele na sheria zinazoelekeza adhabu hiyo.
Kituo hicho kimeshauri mamlaka husika kuweka adhabu mbadala wa kifungo cha maisha ili kuthamini uhai ambao ni haki ya kila binadamu.
Akizungumza leo Jumanne, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Ana Henga amesema adhabu ya kifo inaondoa uwezekano wa mkosaji kujirekebisha na badala yake ni kuendeleza ukatili na kuondoa ubinadamu.
Henga amesema adhabu ya kifo inavunja misingi ya tamko la kimataifa la haki za binadamu la mwaka 1948 ambalo linasema kila mtu ana haki ya kuishi.
Amesema Tanzania inapaswa kujifunza kutoka kwa mataifa mengine duniani ambayo hayatekelezi adhabu ya kifo na badala yake kutoa adhabu mbadala kama vile kifungo cha maisha na kazi ngumu kwa watuhumiwa wa mauaji ili kulinda haki ya msingi ya kuishi.
Henga amesema harakati za kupinga adhabu ya kifo hazimaanishi kuwa ni kutetea uhalifu, hasa mauaji ila ukweli ni kwamba, hakuna ushahidi kuwa uwepo wa adhabu hiyo unaweza kupunguza uhalifu badala yake umekuwa ukiongezeka.
Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani kama vile China, Korea Kaskazini na Marekani ambazo zinaruhusu na kutekeleza adhabu ya kifo katika sheria zake.
Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania, kifungu cha 197 kinaeleza mtu yeyote anayepatikana na hatia ya kuua atahukumiwa adhabu ya kifo.
Henga ameitaka Serikali itekeleze pendekezo la mpango wa kujitathmini wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 2016 kwa kuridhia mkataba wa nyongeza wa haki za kiraia na kisiasa na kutangaza kuwa haitekelezi adhabu hiyo.
Amesema kwa mujibu wa ripoti ya haki za binadamu ya mwaka 2016 takwimu zinaonyesha hadi mwaka 2015 kulikuwa na watu 472 waliohukumiwa kunyongwa kati yao wanaume wakiwa 452 na wanawake 20.
Pia, kati ya hao wanaosubiri kunyongwa ni 228, huku 244 wakisubiri uamuzi wa rufaa zao.
"Hii ni adhabu ya kibaguzi maana mara nyingi wanaopatikana na hatia na kupewa adhabu ni masikini wasioweza kuwa na uwakilishi na ushauri wa kisheria," amesema Henga.
No comments:
Post a Comment