Kampala, Uganda. Spika wa Bunge la Uganda, Rebecca Kadaga ameahidi kuwa atahakikisha unaongezwa ulinzi kwa ajili ya usalama wa wabunge baada ya hivi karibuni nyumba za wabunge wa upinzani kushambuliwa kwa magruneti.
Wabunge wa upinzani ambao nyumba zao zilishambuliwa kwa magruneti ni Moses Kasibante wa Rubaga Kaskazini, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine wa Kyadondo Mashariki na Allan Ssewanyana wa Makindye Magharibi.
Wabunge hao ndio walikuwa vinara wa kupinga mpango wa kutaka kuondolewa kwenye katiba ibara inayoweka ukomo wa umri wa rais.
Kadaga alitoa kauli hiyo ya kutuliza alipomtembelea Mbunge wa Manispaa ya Mityana, Francis Mutebi Zaake ambaye alijeruhiwa zilipofumuka ngumi ndani ya Bunge. Pia alitembelea nyumbani kwa Kasibante.
“Nitakwenda kuzungumza na polisi ili wahakikishe unakuwepo ulinzi wa ziada. Nitazungumza na Inspekta Jenerali wa Polisi ahakikishe unakuwepo uangalizi katika maeneo ili wasishambuliwe,” alisema.
Zzake ambaye bado anauguza majeraha anadai kwamba alipigwa ngumi na Waziri wa Kazi, Jenerali Katumba Wamala hadi akapoteza fahamu.
Ssewanyana na Bobi Wine walishambuliwa wiki iliyopita na watu wasiojulikana ambao walirusha magruneti kwenye nyumba zao.
Mashambulizi dhidi ya wabunge hao yalifanyika wiki moja baada ya magruneti kurushwa na kulipuka katika nyumba ya Kasibante kulipokuwa kunakaribia kupambazuka.
Wapinzani waliishutumu serikali kuwa nyuma ya mashambulizi hayo kwa lengo la kuwatisha na kuwafanya wananchi wanaopinga mpango wa kuondoa ukomo wa umri wa rais wawe na hofu
Hata hivyo, msemaji wa serikali Ofwono Opondo alielezea matukio hayo kuwa ni mbinu za wapinzani wenyewe kuiingiza serikali.
No comments:
Post a Comment