Tuesday, October 10

Wafanyakazi wawili wa chuo wauawa pwani ya Kenya

Ukunda
Wafanyakazi wawili wa chuo kikuu kimoja mjini Mombasa wameuawa baada ya watu wenye silaha kushambulia gari karibu na bewa la chuo katika kaunti ya Kwale, pwani ya Kenya.
Watu kadha wenye silaha walifyatulia magari yaliyokuwa yakisafirisha wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa (TUM) kutoka kwenye vyumba vyao vya malazi hadi kwenye bewa la chuo Ukunda.
Afisa wa polisi aliyezungumza na shirika la habari la Reuters, lakini hakutaka jina lake litajwe, amesema dereva na polisi wawili wamejeruhiwa.
Afisa huyo amenukuliwa na Reuters akisema: "Basi lilikuwa likiwasafirisha wanafunzi wa chuo kutoka vyumba vyao vya malazi hadi kwenye bewa la chuo Ukunda kwa masomo na lilikuwa linasindikizwa na gari ndogo lililokuwa na wafanyakazi wa chuo na polisi wawili wa kuwalinda."
Haijabainika nani alihusika katika shambulio hilo.
Wanamgambo wa kundi la Kiislamu la al-Shabab kutoka Somalia mara kwa mara hutekeleza mashambulio pwani ya Kenya na maeneo ya Kenya yanayopakana na taifa hilo.
Mwaka 2015, walishambulia Chuo Kikuu cha Garissa na kuua wanafunzi 148.
Majeshi ya Kenya yamekuwa yakikabiliana na wapiganaji hao nchini Somalia chini ya kikosi cha Umoja wa Afrika (Amisom).
Nchini Kenya, jeshi la nchi hiyo limekuwa likitekeleza mashambulio katika msitu wa Boni unaopakana na Somalia kuwafurusha wapiganaji ambao wanadaiwa kupanga na kutekeleza mashambulio kutoka katika msitu huo.
Jumatatu usiku, jeshi la Kenya (KDF) lilitangaza kwamba liliwaua wanamgambo watano wa al-Shabab katika msitu huo.
Msemaji wa jeshi David Obonyo alisema wanajeshi hao walipanda bunduki sita aina ya AK-47 na risasi 321 wakati wa operesheni hiyo ya kijeshi Bodhei, Boni.

No comments:

Post a Comment