Tuesday, October 10

MAT yazindua kampeni ya maadili utoaji huduma


Dar es Salaam. Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kimezindua rasmi kampeni ya kitaifa kuhamasisha wataalamu wa afya kuzingatia maadili katika utoaji huduma.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumanne, Rais wa MAT, Dk Obadia Nyongole amesema kampeni hiyo itakuwa sehemu ya kongamano la afya la 49 kitaifa ikiwa ni agenda kuu ya kukuza maadili ya kitabibu na kitaaluma miongoni mwa wataalamu wa afya.
Amesema kuwa kampeni hiyo itaanzia jijini Mwanza Oktoba 16, ambapo viongozi wa chama na watoa mada watazungumza na madaktari kama sehemu ya kampeni na baadaye wataelekea mikoa mingine.
"Malalamiko yapo kwamba hivi sasa kuna pengo kubwa la mawasiliano kati ya wataalamu wa afya na wagonjwa au ndugu wa wagonjwa. Kuna baadhi ya mifano hai hapa nchini, hususani pale ambapo ndugu wa wagonjwa hujichukulia sheria mikononi na kuwashambulia watoa huduma," amesema Dk Nyongole.
Amesema lengo la kampeni ni kuimarisha mahusiano kati ya wagonjwa na watoa huduma kwa kuwakumbusha wanataaluma juu ya majukumu waliyonayo kwa wagonjwa au wateja wao.  "MAT inachukua jukumu la kusimamia wanataaluma katika kuzingatia viwango vya utoaji huduma za kitabibu nchini Tanzania," amesema.

No comments:

Post a Comment