Sunday, August 20

Bombardier yashikiliwa

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Zamaradi Kawawa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Saalaam jana. Picha na Said Khamis. 
Dar es Salaam. Serikali imekiri kudaiwa na kampuni ya Stirling Civil Engineering Ltd iliyozuia ndege aina ya bombardier Q400-Dash 8 iliyonunuliwa nchini Canada.
Hata hivyo, imesisitiza kuwa licha ya deni hilo, ndege hiyo itakuja huku ikiwatuhumu wanasiasa kutengeneza mgogoro huo.
Juzi, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alidai kuwa ndege hiyo imezuiwa nchini Canada na kampuni hiyo ya ujenzi kwa kuwa inaidai Serikali Dola 38.7milioni za Marekani (Sh87 bilioni).
Lissu alisema kampuni hiyo ilipewa kibali cha kukamata mali za Tanzania na Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro katika nchi za Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, Ubelgiji, Uganda na Canada.
Jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Zamaradi Kawawa alithibitisha deni hilo na kusema ndege hiyo itakuja na taarifa za ujio wake zitatolewa kulingana na mwenendo wa kesi hiyo.
“Ndege itakuja na hao wanaokwamisha watapanda na ndugu na wafuasi wao, Serikali haiwabagui Watanzania kwa itikadi za kisiasa, dini, kabila, rangi au utofauti wowote ule,” Zamaradi aliwaambia waandishi wa habari bila kuruhusu swali lolote na alikuwa makini na matumizi ya maneno.
Juzi, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani alisema makubaliano ya Serikali na kampuni ya Bombardier ni kukamilisha matengenezo hayo na kuikabidhi Serikali ndege yake.
“Ninachojua ndege itakuja. Katika makubaliano ilitakiwa ifike Julai, lakini ratiba zao kwa miezi miwili ijayo hadi Oktoba, ndege itakuwa tayari na itakuwa imeshakamilika, ukweli utajulikana baadaye. Wasipoleta watakuwa wame-breach contract (wamekiuka mkataba),” alisema Ngonyani.
Katika madai yake, Lissu alisema kwa sasa kampuni hiyo inataka ipewe Dola 12.5 milioni za Marekani kama malipo ya awali ili isiipige mnada kwa kibali ilichopewa na Mahakama Kuu ya Montreal Juni 30. “Kampuni ya Stirling ilikubali kuweka masharti nafuu ili Serikali isilipe deni kubwa, lakini Serikali yetu ikakataa, ni nani anayetakiwa kuwajibishwa leo hii kwa hasara hii?” alihoji Lissu.
Tuhuma kwa wanasiasa
Licha ya kukiri kuwapo wa mgogoro huo, Zamaradi alidai kuwa umetengenezwa na Watanzania wasio na uzalendo.
Alisema wanasheria waliokwenda kufungua madai ya kuidai Serikali na kutaka ndege ishikiliwe hawana uhalali wa kufanya hivyo na ni matapeli ambao wamesukumwa na baadhi ya wanasiasa wasioitakia mema Tanzania.
Mkurugenzi huyo alisema wapo baadhi ya wanasiasa na Watanzania ambao wameweka masilahi yao mbele kwa kuchochea mgogoro huo ili kukwamisha jitihada za maendeleo zinazofanywa na Rais John Magufuli.
“Serikali ilipata fununu mapema kwamba kuna baadhi ya viongozi wa chama cha siasa walikuwa na mpango huo na sasa wamejidhihirisha wazi kuwa wao ndiyo wapo nyuma ya pazia la kuhujumu jitihada za Serikali kwa masilahi yao,” alisema na kuongeza:
“Awali, Serikali ilikuwa ikiwahisi baadhi ya wanasiasa kuhusika na hujuma hizi, sasa sio hisia tena bali baadhi yao wameshaanza kujitokeza hadharani.”
Hakuishia hapo, kaimu msemaji huyo alisema Serikali inaendelea kuzifanyia uchunguzi fununu kwamba watu hao wanahujumu jitihada za maendeleo na pia usalama wa raia kwenye baadhi ya maeneo nchini.
“Serikali imesikitishwa na hujuma zinazofanywa waziwazi tena kwa ushabiki wa hali ya juu na baadhi ya viongozi wa kisiasa kupingana na mwelekeo mzuri wa Rais. Kwa mtu mwenye uchungu na nchi yake angepambana ili jambo linalohusu masilahi ya Taifa likiwamo la kununua ndege lisikwame,” alisema Zamaradi.
“Hii si mara ya kwanza kwa wanasiasa kutoa maelezo ya kuvuruga na kukejeli jitihada za Serikali, walishawahi kushawishi wafadhili wasilete misaada Tanzania.Walibeza pia jitihada za kunusuru madini yetu na maliasili.”
Kufuatia hali hiyo, Zamaradi alisema kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwamo za kidiplomasia ili kumaliza suala hilo kwa ajili ya kuhakikisha ndege hiyo inakuja nchini.
Majibu ya Lissu, Zitto Kabwe
Alipotafutwa kujibu tuhuma hizo, Lissu alijibu huku akihoji mazingira ya uzalendo kati yake na Serikali.
“Ni nani ambaye ni mzalendo kati yangu na Serikali, sisi tuliosema hadharani Serikali inadaiwa au Serikali ambayo ilivunja mkataba ikalisababishia hasara Taifa? Nani anayeichafua Tanzania kati yangu na Serikali iliyoshindwa kulipa deni hilo linaloongezeka tangu mwaka 2010?” alihoji.
Lissu ambaye ni wakili wa kujitegemea alisema hakuna haja ya kuvutana, badala yake Serikali inatakiwa kulipa deni hilo ili ndege isipigwe mnada kwa kibali ilichopewa kampuni hiyo na Mahakama Kuu ya Montreal.
Akizungumzia tuhuma hizo, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema kama mpinzani wajibu wake ni kuibua hoja na kuuliza maswali na wajibu wa Serikali ni kutoa majibu.
“Wajibu wangu huo nimeutimiza, nilimuuliza waziri (mwenye dhamana, Profesa Makame Mbarawa) kuhusu suala hili kwenye mtandao wa Tweeter, lakini majibu yake yalikuwa finyu. Haya yanayoendelea sasa ni propaganda za kuchafuana na sihitaji kujihusisha nazo,” alisema Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini.
Mtazamo wa kisheria
Lissu alisema Tanzania ni mwanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara (ICSID) hivyo haiwezi kukwepa katika ulipaji wa deni hilo.
Alisema endapo Serikali haitalipa deni hilo, ndege hiyo itapigwa mnada. “Nchi yoyote ambayo ni mwanachama wa mahakama hiyo, ikitolewa hukumu lazima itekelezwe na nchi zote ambazo ni wanachama na ndiyo maana kampuni hiyo imepewa kibali cha kukamata mali za Serikali katika nchi hizo. Kibali walichopewa kwa kawaida kinadumu kwa wiki mbili hadi mwezi mmoja kabla ya kupiga mnada,” alisema.
Wakili wa kujitegemea wa Mahakama Kuu, Onesmo Mpinzile alisema changamoto iliyopo ni uwazi wa mkataba kati ya Serikali na kampuni ya Stirling baada ya Serikali kuvunja makubaliano ya ujenzi wa barabara hiyo.
“Katika makubaliano ya mkataba mnaweza kukubaliana, endapo mgogoro ukitokea katika makubaliano yenu mtamalizaje, mtatumia mahakama za ndani au za kimataifa au mtatumia sheria zipi, sasa makubaliano ya Serikali na kampuni hiyo wakati wa ujenzi wa barabara hatuyafahamu msingi wake katika eneo hilo,” alisema.
Alisema mamlaka ya utatuzi wa mgogoro yaliyotolewa kupitia kifungu cha usuluhishi, hakijalishi kama nchi husika itakuwa mwanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi. “Kwa hiyo inakuwa vigumu kujua mazingira ya mgogoro huo,” alisema.
Sakata la ndege
Uamuzi uliofanywa na Serikali wa kuvunja mkataba na kampuni hiyo ya Canada iliyokuwa ikijenga Barabara ya Tegeta Wazo-Bagamoyo ndiyo uliochelewesha ujio wa ndege hiyo.
Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki, alisema baada ya uamuzi huo, Stirling ilifungua kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi ikidai kukiukwa kwa mkataba na ilipofika Juni 2010, mahakama hiyo ilitoa tuzo ya ushindi kwa kampuni hiyo ikiitaka Serikali ilipe fidia ya Dola25 milioni za Marekani, huku deni hilo likiwekewa riba ya asilimia nane.
Kwa madai ya Lissu, Serikali ilikataa kulipa fidia hiyo hadi Juni 30 wakati mahakama hiyo ilipoipa Stirling kibali cha kukamata mali zote za Tanzania zitakazokuwa katika nchi ilizozitaja.
Akizungumzia suala hilo, Lissu alidai kuwa hata Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga alikuwa Canada Agosti 3 kushughulikia suala hilo.
Hata hivyo, kuhusu madai ya kampuni ya Stirling, Naibu Waziri Ngonyani alisema Serikali kudaiwa si jambo la kushangaza akidai kuwa tangu Serikali ilipoingia madarakani mwaka 2015, wizara hiyo ya ujenzi ilikuwa inadaiwa Sh1.12 trilioni, lakini hadi Julai tayari deni hilo limepungua hadi kubaki Sh900 bilioni.
“Mimi sina taarifa kuhusu deni hilo, ila kikubwa Serikali kudaiwa si big deal (jambo la kushangaza), ila tunafanyaje katika kuyalipa madeni, pengine inawezekana deni hilo likawa ni sehemu ya madeni tunayodaiwa,” alisema.
Kauli ya JPM siku ya uzinduzi
Akizindua ndege mbili mpya aina ya Bombardier Q400 NextGen, Septembea 28 ambazo ziliingia nchini Septemba 20 na 27, Rais Magufuli alibeza kundi la watu wanaozikejeli.
“Watu wanaofanya biashara ndiyo wanaopiga vita, ndiyo maana nikasema anayetaka kasi akapande ndege ya jeshi,” alisema.
Rais Magufuli alisema Serikali iliamua kununua ndege hizo kwa fedha taslimu kwa sababu ilikuwa nazo kwa kuwa ununuzi kwa njia ya mkopo ungeweza kugharimu fedha nyingi zaidi.
Wazo la kununua ndege hizo lilianza Januari 25, 2016 Serikali ilipotoa mapendekezo ya mwelekeo wa mpango wa pili wa miaka mitano wa maendeleo wa Taifa unaolenga zaidi kuinua sekta ya viwanda, ilipotaja vipaumbele 20 ikiwamo cha kununua ndege mbili za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Akiwasilisha mapendekezo hayo, Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk Ashatu Kijaji alitoa ahadi hiyo huku akibainisha pia mpango wa kuboresha wa miundombinu ya usafiri wa anga ili kuongeza ufanisi katika sekta hiyo.   

Dereva aliyewagonga na kuwaua watu 13 Barcelona asakwa na polisi

Younes AbouyaaqoubHaki miliki ya pichaAFP/GETTY
Image captionAbouyaaqoub, 22, anaaminika kuwa mafichoni
Dereva ambaye alishambulia watu kwa kuwagonga kwa gari na kuwaua watu 13 mjini Barcelona, huenda bado yuko hai, na mafichoni kwa mujibu wa polisi wa Uhispania.
Polisi wanamtafuta Younes Abouyaaqoub raia wa Morocco, ambaye anatajwa na vyombo vya habari kuwa mshukiwa.
Mwanamume mmoja ambaye alitajwa kuwa mshukiwa mkuu Moussa Oukabir 17, ni mmoja kati ya wanaume watano waliouawa na polisi baada ya shambulizi huko Cambrils magharibi mwa Barcelona.
Ian Moore Wilson and his wife ValerieHaki miliki ya pichaVANCOUVER POLICE
Image captionIan Moore Wilson na mkewe Valerie waliuawa huko Las Ramblas
Polisi wanasema kuwa washukiwa walikuwa wakipanga mashambulizi mengine.
Walisema milipuko ya siku ya Jumatano kwenye nyumba katika mji wa Alcanar, uliwapokonya wapanga mashambulizi vifaa vya kutengeneza milipuko, kwa hivyo waliamua kufanya mashambulizi madogo wakitumia magari.
map
Image captionRamani
Abouyaaqoub, 22, aliishi mji wa Ripoll kaskazini mwa Barcelona. Watu watatu wamekamatwa mji wa Ripoll na mwingine huko Alcanar.
Oukabir awali alionekana kama mshukiwa mkuu lakini baadaye siku ya Ijumaa, mkuu wa polisi alikiambia kituo kimoja cha televiseni kuwa uwezekano kuwa alikuwa ndiye dereva ulikuwa mdogo.
(L-R) Moussa Oukabir, Said Aallaa, Mohamed Hychami and Younes AbouyaaqoubHaki miliki ya pichaAFP
Image caption(kushoto kwenda kulia) Moussa Oukabir, Said Aallaa, Mohamed Hychami na Younes Abouyaaqoub
Oukabir anashukiwa kwa kutumia stakabadjhi za nduguye kukodi gari lililotumiwa kufanya shambulizi la Barcelona na lingine ambalo lilitumika katika mji wa Vic kaskazini mwa Barcelona.
Mapema siku ya Ijumaa polisi waliwaua kwa kuwapiga risasi washambuliaji watano akiwemo Oukabir huko Cambrilis, baada ya wanaume hao kuendesha gari kwenda kwa wapita njia, na kumua mwanamke mmoja na kuwajeruhi watu wengine 6.
Map
Image captionBarcelona

Geita yaanza ujenzi wa machinjio ya kisasa


Halmashauri ya Mji wa Geita imeanza kujenga mradi wa machinjio ya kisasa utakayokuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 100 kwa siku.
Mradi huo unajengwa kwenye Mtaa wa Samina Kata ya Mtakuja na una ukubwa wa eneo la eka 26 na utagharimu Sh2.7 bilioni.
Akizungumza katika eneo la mradi huo hivi karibuni, msanifu majengo idara ya ujenzi katika halmashauri hiyo, Boniface Victor alisema mradi huo umeanza kutekelezwa Juni mwaka huu na unatarijiwa kukamilika Juni, 2018.
“Eneo hili lina jumla ya eka zaidi ya 26, eka sita kati ya hizo ndizo zitakazotumika kutengeneza machinjio zinazobaki zitatumika kwa ajili ya shughuli nyingine kama kujenga viwanda vidogo, sehemu ya kunenepesha mifugo na mnada,” alisema Victor.
Alisema kutokana na mahitaji ya nyama kuwa makubwa katika mkoa huo na kuwapo mgodi mkubwa wa dhahadu wa GGM ambao hupata huduma hiyo nje ya nchi hivyo wanaimani watapata soko la bidhaa hiyo.
Katika hatua nyingine halmshauri hiyo imetenga eneo lenye ukubwa wa eka 586 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vidogo.
Mthamini wa halmashauri ya mji huo, Godliver Kipande alisema tayari eneo hilo limeshafanyiwa uthamini wa watu 71 ambao watalipwa kiasi cha Sh818 milioni kwa ajili ya fidia itakayolipwa kwa awamu mbili.
Kwa mujibu wa mthamini huyo awamu ya kwanza watalipa watu 31 kiasi cha Sh310 milioni sawa na eka 273 ambazo zitakuwa tayari kwa uwekezaji mwaka huu.
Msanifu wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Boniface Victor kutoka idara ya ujenzi alisema mradi wa machinjio una uwezo wa kuchinja ngombe 100 kwa siku.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Modesta Apolinary alisema tayari halmashauri imekwisha saini malipo ya fidia kiasi cha Sh310 milioni kwa ajili ya wananchi hao.

Katibu Soko la Sido ashikiliwa kwa uchochezi

Mfanyabiashara wa Soko la Sido mjini Mbeya

Mfanyabiashara wa Soko la Sido mjini Mbeya akilalamikia kitendo cha Serikali kuwazuia kujenga vibanda vya kudumu ndani ya soko hilo lililoteketea kwa moto.Picha na Godfrey Kahango 


Wakati hali ya amani na utulivu ikiwa imerejea katikati ya Jiji la Mbeya baada ya kutokea vurugu juzi mchana, jeshi la polisi limesema linawashikilia watu 18 akiwamo Katibu wa Wafanyabiashara wa Soko la Sido, Alanus Ngogo kwa tuhuma za kuchochea vurugu hizo.
Juzi mchana, polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi, maji ya kuwasha na upupu kuwatawanya wanafabiashara wa soko hilo waliokuwa wamegoma kutekeleza agizo la Serikali la kuwataka kutoendelea na ujenzi wa vibanda vya kudumu ndani ya soko hilo ambalo liliteketea kwa moto na kuunguza mali zote usiku wa kuamkia Agosti 15 mwaka huu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga aliliambia gazeti hili jana kwamba baada ya kutokea kwa vurugu kuna watu waliokuwa katika soko hilo la Sido waliingia na kufunga barabara kuu ya Tanzania-Zambia kwa mawe na magogo huku wakipiga mawe magari yaliyokuwa yakipita.
“Katika tukio la juzi tuliwakata watu 18 hawa kosa lao ni kuingia barabarani na kuanza kupanga mawe na magogo na kuzuia magari yasipite barabara kuu ya Tanzania-Zambia kuanzia Kabwe hadi Mafiati.
“Lakini yule katibu wa soko (Alanus Ngogo) yeye anatuhumiwa kwa kosa la uchochezi kwani juzi ile mimi nilipopanda jukwaani na kuwataka watu wote waende nyumbani kwao kwa usalama wao yeye alichukua kipaza sauti na kuanza kuwahamasisha watu wasiondoke eneo lile akitamka ‘tutakesha hapa hapa’ na maneno mengine ya kukashifu,” alisema Kamanda Mpinga.
Alisema watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na baada ya kumalizika kwa mahojiano watapandishwa kizimbani kujibu tuhuma zao.
Kuhusu hali ya usalama, Kamanda Mpinga alisema ulinzi katika jiji hilo umeimarishwa na polisi wapo doria muda wote na watu waliamka alfajiri kuendelea na shughuli zao maeneo mengi hususan Soweto, Kabwe, Manjelwa hadi Mafiati ambako juzi biashara zilifungwa kutokana na usalama kuwa mdogo.
Hata hivyo, Serikali ya Mkoa wa Mbeya kupitia kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika ilisisitiza kusimamia msimamo wake wa kutowaruhusu wafanyabiashara hao kuendelea na ujenzi wa vibanda vyao tofauti na ombi lao kutaka kuruhusiwa.
Ntinika aliwataka wafanyabiashara hao kuwa na hali ya utulivu na uvumilivu kwa kusubiri siku tano zilizotengwa na Serikali ili kupisha kamati maalumu iliyoundwa kufanya tathmini ya hasara iliyojitokeza kutokana na janga hilo pamoja na kuchunguza kiini cha moto huo.

MWANAMKE MTANZANIA ASHINDA TUZO YA MHASIBU KIONGOZI




Maelfu ya Watanzania wanaishi Uingereza. Wapo wanaoonekana kwenye mitandao jamii na wanaoendelea na shughuli zao bila kusikika. Joyce Materego ni mfano huo. Baada ya kumaliza masomo 2004 alianza kazi ya uhasibu. Anasema mhasibu ni mtu anayeelewa na kutathmini vyema hesabu.
“Kazi yangu ni kuhakikisha fedha zinazoingia ni nyingi kuliko zinazotoka,”anasema. Materego anafafanua kuwa uhasibu ulihitaji kutimiza mitihani 14 kipindi cha miaka 10. Hati inayotolewa ya ACCA (Jumuiya ya Wahasibu Duniani – Association of Chartered Accounts) hutambuliwa popote pale kama walivyo walimu, madaktari na kadhalika. Mafunzo je? Huhusu sheria, kodi, uchumi na kadhalika.
“Unajengwa kisaikolojia kuwa wewe ni mlinzi. Kama daktari anavyoaminiwa na maisha ya watu, wewe unafadhiwa na fedha za watu na makampuni,” anasema.
Badala ya kuchukua miaka 10, Mtanzania huyo alimaliza mafunzo miaka minne tu. Ana bidii sana.
Karibuni aliteuliwa kati ya wafanyakazi wanaowatia wenzao changamoto. Picha iliyotolewa na jarida la kisekta la Focus, kibaruani inaonyesha kasimama na wanaume wawili wa Kizungu na zawadi zao. Nywele sio za bandia, zimesukwa butu kubwa linalotukuza Uafrika. Ni naadra siku hizi kuona mwanamke akisuka namna hiyo. Kila analofanya Materego lina maana na uzito fulani. Mbali ya kulea wanawe wanaosoma sekondari, huenda kazini alfajiri - siku tano kwa wiki na kurejea kuwapikia na kuwahudumia kila siku.
Ingekuwa Tanzania angeajiri mtu wa kufanya kazi nyumbani. Ulaya hilo halipo.
Mbali na kulea, Materego ni mjuzi sana wa lugha na mara kwa mara huajiriwa kama mkalimani wa Kiswahili na Kiingereza fasaha..
Anafanya wapi kazi?
Kaajiriwa na shirika la fadhila linalohudumia watoto maskini la Child Poverty Action Group (CPAG). Mwaka 2015, CPAG ilidai asilimia 28 ya watoto wa Uingereza ni hohehahe. “Ulimwengu mzima” anatathmini. “Tunatakiwa tujue kuna watu wanaoishi maisha ya fahari na duni. Hata Uingereza tuna tatizo hilo. Kampuni yangu inachojaribu ni kuongea na Serikali kuhakikisha wanasiasa wanabadilisha mwongozo wa jinsi fedha za Serikali zinavyotumika kuinua hali ya watoto katika uduni, wawe sawa na wengine.
Unaweza kukuta mtoto anayekulia hali duni kiasi hali nzuri, akienda shule hasikilizi vizuri na hivyo vyote afya kwa mtoto vinachangia mtoto kufanya kazi vizuri.”
Kwanini akapewa tuzo?
Tuzo ilihusiana na namna anavyowasiliana vizuri na wafanyakazi wenzake na wateja wa shirika. Huo ni mfano mzuri wa baadhi ya Watanzania (tusiowajua) wanaolea, huku wakichapa kazi na kutoiaibisha nchi yetu ugenini. Ni siri pia ya undani wa Watanzania. Sisi ni watu waungwana sana kwa ujumla, wageni husema. Tuzo si fedha, bali cheti cha uongozi katika masuala ya fedha. Alisisitiza kuwa usimamiaji wa fedha ni suala muhimu katika sekta na vitengo vyote vinavyotawala dunia zikiwamo kampuni za kibiashara, taasisi za wilaya na mikoa, kiserikali, huduma katika jamii, sanaa na hata uchumi wa nyumbani.
Tumpe hongera mama huyo wa watoto. Kama walivyosema Mwalimu Julius Nyerere na mpigania haki za watu weusi nchini Marekani, Malcolm X ukimuelimisha mwanamke unaelemisha Taifa zima.

Mahakama yazuia bomoabomoa kwa nyumba 286 Dar


Dar es Salaam. Wakati operesheni ya ubomoaji wa nyumba zilizoko ndani ya umbali wa mita 121.5 kutoka katikati ya Barabara ya Morogoro ikiendelea maeneo ya Kimara mpaka Kiluvya jijini Dar es Salaam, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi imeziwekea kinga ya muda nyumba 286 zinazohusika.
Uamuzi huo wa Mahakama ulitolewa juzi na Jaji Leila Mgonya kutokana na maombi ya zuio yaliyowasilishwa mahakamani hapo na wakazi hao 286 wa maeneo ya Ubungo- Maji hadi Kiluvya wakiomba itoe zuio la muda hadi kesi yao ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Maombi hayo ya zuio la muda kusubiri uamuzi wa kesi ya msingi yamepangwa kusikilizwa Agosti 30 baada ya upande wa wajibu maombi (Serikali) kuwasilisha hati ya kiapo kinzani.
Hata hivyo, wakati wakisubiri usikilizwaji wa maombi ya zuio la muda, wananchi hao kupitia kwa wakili wao, Benito Mandele waliwasilisha maombi ya dharura wakioomba mahakama hiyo iamuru hali iendelee kuwa kama ilivyo kwa sasa hadi maombi hayo yatakaposikilizwa.
Jaji Mgonya anayesikiliza shauri hilo alikubaliana na maombi hayo na kuamuru hali iendelee kuwa kama ilivyo kwa sasa hadi tarehe hiyo ya maombi hayo yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Akizungumza na Mwananchi baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, wakili Mandele alisema kuwa waliamua kupeleka maombi hayo ya kudumisha hali iliyopo kwa sasa baada ya kuona Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) wameanza kutekeleza operesheni hiyo wakati maombi yao ya zuio yakiwa bado hayajasikilizwa.
Kwa uamuzi huo, Tanroads ambayo ndiyo mtekelezaji wa operesheni hiyo haitaweza kuzigusa nyumba hizo hadi hapo mahakama itakavyoelekeza vinginevyo baada ya usikilizwaji wa maombi hayo ya zuio la muda kusubiri kesi ya msingi kumalizika.
Wakili Mandele alisema kuwa watakachofanya baada ya kupata hati ya amri hiyo ya mahakama wataitoa nakala nyingine na kuwagawia kila mdaiwa kwa ajili ya kuiweka kwenye nyumba yake.
Katika kesi ya msingi namba 284 ya mwaka 2017, wananchi hao wanaiomba mahakama itamke kuwa wao ni wamiliki halali wa maeneo hayo yenye mgogoro na kwamba hawapo katika hifadhi ya barabara.
Pia, wanaiomba mahakama hiyo iamuru kuwa kama Serikali inata kuwahamisha na kuyachukua maeneo yao, basi iwalipe fidia stahiki kwa mujibu wa sheria.
Tanroads imetoa notisi kwa wakazi wote walipo katika umbali wa mita 121.5 kutoka katikati ya barabara ya Morogoro kila upande, kuanzia Ubungo - Maji hadi mpakani mwa Dar es Salaam na Pwani kuvunja nyumba zao kwa madai kuwa wapo kwenye hifadhi ya barabara.
Hivyo, Tanroads waliwataka wananchi hao kuondoka katika maeneo hayo ili kupisha upanuzi wa barabara hiyo.
Wananchi hao wanapinga amri hiyo wakidai kuwa wanaishi katika maeneo hayo kihalali kwa kuwa wana hatimiliki halali na hawapo kwenye hifadhi ya barabara, huku wakihoji sheria iliyotumika kuidhinisha umbali huo wa mita 121.5.
Kutokana na hali hiyo, wananchi hao wameamua kwenda mahakamani katika makundi tofauti na kufungua kesi tofautitofauti kupinga operesheni hiyo wakidai kulipwa fidia kama Serikali itawahamisha.
Mbali na kesi hiyo iliyotolewa amri hiyo, pia kuna kesi nyingine mbalimbali ambazo ziko katika hatua mbalimbali.
Kesi hizo nyingine ni ile iliyofunguliwa na Abdallah Maliki kwa niaba ya wenzake 570 ambao ni wakazi wa maeneo ya Kimara, Mbezi na Kiluvya dhidi ya Tanroads na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kwa upande mwingine.
Shauri jingine ni maombi ya kibali cha kufungua kesi ya uwakilishi kupinga operesheni hiyo lililofunguliwa na Ephrahim Kavishe na wenzake wanne ili wawe wawakilishi wa wenzao zaidi ya 198 ambao ni wakazi wa Kimara Stop Over na Mbezi.
Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ni mmoja wa wajibu maombi hayo amewawekea pingamizi akiiomba mahakama hiyo iyatupile mbali maombi hayo huku akiainisha kasoro mbalimbali za kisheria.
Maombi hayo yanasikilizwa na Jaji Crencecia Makuru na amepanga kutoa uamuzi kuhusu pingamizi hilo Agosti 30, uamuzi ambao ndio utakaotoa hatima ya maombi hayo kama yataendelea kusikilizwa au yatatupiliwa mbali.     

Ukusanyaji michango ya harusi sasa kwa mbinde


Moshi. Wakati kiwango cha michango ya harusi inayochangwa na marafiki kikiporomoka kwa kasi nchini, washereheshaji (Ma-MC) wameanza kutumia mashine za kielektroniki za EFD ili kutoa stakabadhi.
Baadhi ya washereheshaji (ma-MC), wameenda mbali na kuwataka wenye kumbi zinazotumika kwa sherehe hizo kutowaruhusu washereheshaji ambao hawatawaonyesha kuwa wanatumia EFD.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa ile ari ya uchangiaji harusi iliyokuwapo miaka ya nyuma imeporomoka kwa kasi kubwa sasa.
Kulingana na uchunguzi huo, katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, harusi za kifahari zilizokuwa zikifungwa ni nyingi kulinganisha na miaka miwili iliyopita kutokana na ugumu wa maisha.
Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, bajeti ya chini ya harusi au kumuaga bibi harusi (send off), ilikuwa kati ya Sh5 milioni na Sh7 milioni wakati kiwango cha juu kilikuwa zaidi ya Sh60 milioni.
Hata hivyo, sasa mambo yamekuwa tofauti kwani bajeti za harusi zinazopangwa na wanakamati zinakusanya kati ya asilimia 50 na 75 tena ni kwa wale wenye ndugu wenye uwezo.
Ugumu kukusanya michango
Uchunguzi huo umebaini kati ya kazi ngumu kwa sasa ni ukusanyaji wa ahadi za michango ya harusi, send off au kitchen party kutokana na kile kinachoelezwa kuwa watu ni wagumu kutimiza ahadi zao.
Chanzo kimoja kimedai kuwa kila mtu analia mambo yamebadilika na kwamba unapoonekana unafuatilia sana michango wapo watu ambao hufikia hatua ya kuzuia mawasiliano ya simu.
“Huu usawa wa sasa si kabisa. Kila mtu analia hana hela sasa hizo za kuchangia harusi anazitoa wapi? Ukiona mtu anakuchangia harusi zama hizi mshike sana huyo,” alidokeza mshereheshaji mmoja.
Mkazi wa Pumuwani mjini Moshi, Ewald John alisema anazo kadi tatu za harusi za marafiki wa karibu, lakini ameshindwa kuwachangia kwa sababu hali ya kifedha imekuwa ngumu. “Mimi nina kadi tatu, lakini mbili zimeshapita. Sio kwamba nilikuwa sijui lakini kiukweli sina pesa nafanyaje? Nafikiri Watanzania sasa tubadili aina ya maisha, hii michango haitawezekana,” alisema.
Mshereheshaji mashuhuri nchini, Sijabu Kiata alisema kiujumla hali ya maisha imebadilika na hata harusi zinazofanyika sasa si za gharama kubwa kulinganisha na miaka mitano au 10 iliyopita.
“Watu hawana pesa wala hilo sio suala la kuuliza. Kuna harusi unaenda unakuta inapita round (mzunguko) moja tu ya vinywaji kabla ya chakula na nyingine wakati wa chakula, basi,” alisema.
Wakili wa kujitegemea wa jijini Arusha ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alisema kama michango ya harusi ingekuwa ya lazima, basi ingebidi watumike madalali kuikusanya.
“Katika kazi mojawapo ngumu kwa sasa ni kukusanya michango ya harusi. Unaweza hata mkapishana kauli na mtu unayeheshimiana naye pale anapokwambia hali ni ngumu. Hali imebadilika,” alisema na kuongeza:
“Huko tunapoelekea itabidi mtu anayetaka kuoa ajiandae mwenyewe na marafiki zake wa karibu, tena unaalika watu wasiozidi 20 mkitoka kanisani mnaenda hotelini mnakula mnarudi nyumbani”.
Mkurugenzi wa Mfinanga Block Supply ya Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, Hussein Mfinanga alisema kutokana na mabadiliko ya maisha hivi sasa anafikiria kusitisha uchangiaji wa harusi.
“Huko nyuma mtu anakupa kadi na anakwambia kama humchangii kuanzia Sh100,000 basi usimchangie. Sasa hivi peleka kadi na masharti hayo uone kama utachangiwa,” alisema.
Mfinanga alisema siku za nyuma kuna harusi ilikuwa mtu akichanga Sh20,000 anapewa kadi ya mtu mmoja (single) na wale wanaochangia zaidi ya Sh50,000 ndio wanapewa kadi ya watu wawili, akisema hilo litafutika.
Ma-MC, TRA nao watoa neno
Baadhi ya washereheshaji waliozungumza na Mwananchi jana walipongeza hatua ya Serikali kuwataka waanze kutumia mashine za EFD, lakini wakataka kuwapo mfumo wa kuwabana ma-MC wote.
Kiata alisema japokuwa ni mpango wa Serikali wa kuwataka washereheshaji wote kulipa kodi na kutumia mashine za EFD, utekelezaji wake ni wa kusuasua.
“Mimi nina mashine ya EFD tangu mwaka jana lakini wengi hawana na hii maana yake hawalipi kodi. Hii si sahihi. Ni lazima TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) ije na mfumo unaoeleweka,”alisema.
“Maisha yamebadilika hakuna pesa kabisa unaweza kukaa mwezi mmoja hujapata kazi na bahati mbaya hii kazi imeingiliwa, watu wanashusha bei hawana EFD mashine, ni vurugu tu.”
“TRA waziamuru hizi kumbi zinazotumika kwa hizi sherehe kuhakikisha kuwa kila MC anayeingia katika ukumbi aonyeshe risiti ya EFD aliyomkatia mwenye harusi. Lazima kuwe na usawa.”
Mshereheshaji mwingine, Ntoly Mayombola alisema hakuna MC anayepinga kutumia mashine hizo, lakini tatizo ni ughali wake kulinganisha na vipato vya washereheshaji.
“Tatizo unainunuaje? Unalipwa Sh100,000 au 150,000 au 200,000 lakini tunaambiwa mashine ni zaidi ya Sh700,000. Bado huu mfumo Serikali inatakiwa itoe bure hizo mashine,” alisema Mayombola.
Msimamo wa TRA
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Walipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alipongeza hatua ya baadhi ya washereheshaji kuanza kutumia mashine hizo.
“Tunataka (washereheshaji) wote waingie kwenye kutoa risiti za EFD na mwaka jana tulikaa nao na wako willing (tayari) kutumia hizo mashine. Tunaendelea kuwahamasisha wafanye hivyo mapema,” Kayombo.
Kayombo alisema matumizi ya EFD yatawasaidia Ma-MC kupata kazi kwa vile wananchi hivi sasa wana mwamko wa kudai risiti za kielektroniki na kwamba, wasio nazo inawanyima kazi kubwa hasa za Serikali.   

Askari wadaiwa kuruhusu magari mabovu barabarani

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Fortonatus Musilimu (kulia) na askari wa kikosi chake kikagua moja ya mabasi ya abiria jana alfajiri  katika Kituo Kikuu cha Mabasi jijini Mbeya katika ukaguzi wa kushitukiza, ambapo mabasi kadhaa yalikuwa na ubovu katika mfumo wake wa usukani, tairi vipara na matatizo mengineyo na kuyazuia.  Picha na Godfrey Kahango 
Mbeya. Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Fortunatus Musilimu ameagiza askari saba wa kikosi hicho katika Kituo Kikuu cha Mabasi Mbeya waondolewe kituoni hapo kwa madai ya kuruhusu mabasi mabovu kubeba abiria.
Kamanda Musilimu alimuagiza Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya (RTO) Butusyo Mwambelo kutekeleza amri hiyo jana baada ya kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika mabasi na madereva eneo hilo.
“Hawafanyi kazi ipasavyo na hii inatokana na kukaa kituo kimoja zaidi ya miaka mitano,” alisema Kamanda Musilimu.
Pia, alisitisha mabasi matano kutoendelea na safari baada ya kubaini hitilafu kwenye mfumo wa usukani na magurudumu.
Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) Mkoa wa Mbeya, Denis Daud alisema chombo cha moto lazima kifanyiwe ukaguzi na maofisa wa polisi kama kina sifa ya kuingia barabarani.
Mdau wa usafiri, Mohamed Abdalah alisema ukaguzi uliofanywa na kamanda unaisadia kubaini mabasi ambayo hayaruhusiwi kuwapo barabarani. 

Maalim Seif aendelea kulia na hujuma akimlima barua msajili


Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ameendelea kulia na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kutokana na kile alichodai ni hujuma anazozifanya dhidi ya chama hicho akishirikiana na Profesa Ibrahim Lipumba.
Maalim Seif alieleza hayo juzi katika barua yake ya kumjibu Jaji Mutungi kuhusu hatua yake ya kuwatambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti halali wa CUF na Magdalena Sakaya kama kaimu katibu mkuu wakati viongozi hao walisimamishwa uanachama kwa tuhuma mbalimbali.
Katibu mkuu huyo alifikia uamuzi wa kumjibu Jaji Mutungi baada ya ombi lake la kuwafukuza uanachama wabunge wawili; Sakaya (Kaliua) na Maftaha Nachuma (Mtwara Mjini) kugonga mwamba kutokana na msajili kumtambua Sakaya kama kaimu katibu mkuu kufutia maelezo aliyopewa na Profesa Lipumba.
Profesa Lipumba alimweleza Msajili kuwa Maalim Seif ameshindwa kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kutofika ofisi ya chama hicho zilizopo Buguruni, hivyo akamteua Sakaya ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Bara kukaimu ukatibu mkuu.
“Kwa mujibu wa katiba ya CUF mimi, Maalim Seif bado ni katibu mkuu wa chama hiki na nipo hapa nchini, ni mzima na nina akili timamu. Na nafasi yangu haiwezi kukaimiwa na Sakaya ambaye tulishamsimamisha uanachama,” inaeleza barua hiyo.
“Mheshimiwa msajili, nashangaa kwa maelezo yako. Mimi ninavyojua ni kuwa kiongozi anakaimiwa ikiwa hayupo nchini au hawezi kutekeleza majukumu yake. Hivyo ndivyo katiba ya CUF ya 1992 (toleo la 2014) kifungu cha 105 (1) kinavyoeleza.”
Aliongeza kuwa Jaji Mutungi alipokea barua ya Profesa Lipumba Machi 16, 2017 huku yeye akiwa hapa nchini akiendelea na shughuli za chama hasa katika ofisi ya makao makuu ya chama hicho iliyopo Zanzibar kwa mujibu wa katiba ya CUF.
Maalim Seif alisema cha kushangaza Msajili wa Vyama vya Siasa alitoa uamuzi kutokana na maelezo ya mwenyekiti anayetambuliwa na ofisi yake. Kutokana na hilo, mwanasiasa huyo alimtaka Jaji Mutungi kuangalia katiba ya CUF ya mwaka 1992 (toleo la 2014) kifungu Na. 1 (2) vinavyoeleza kwamba makao makuu ya chama hicho yatakuwa katika Mji Mkuu wa Zanzibar na anuani yake itakuwa kama itakavyoamuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.
Alisema kifungu cha 1 (3) kinaeleza kwamba kutakuwa na Ofisi Kuu ya Makao Makuu ya Chama Dar es Salaam na anuani yake itakuwa kama itakavyoamuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.
“Kwa mantiki hii, Mheshimiwa Jaji Mutungi wewe mwenyewe umeshawahi kuyatembelea makao makuu hayo au bado ofisi iliyopo Buguruni, Dar es Salaam ndiyo Ofisi Kuu ya Makao Makuu?” inahoji barua ya hiyo. Maalim Seif ambaye pia aliwahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, alisema kesi mbalimbali zinazohusu mgogoro wa CUF zimefunguliwa Mahakama Kuu na kwamba, ni vyema Jaji Mutungi angetumia busara kumweleza Profesa Lipumba asubiri hukumu ya mahakama na endapo angekataa msajili na ofisi yake ingejitenga naye.
Mbali na hilo, Maalim Seif alidai kwamba msajili katika barua yake alieleza kwamba amejiridhisha na maelezo ya Profesa Lipumba kuwa yeye hafiki Buguruni na ameshindwa kufanya kazi, lakini hakumtafuta au kumuita ama kumuuliza ili kupata maelezo yake kujua ukweli wa kilichoandikwa na mwenyekiti anayemtambua.