Sunday, August 20

Ukusanyaji michango ya harusi sasa kwa mbinde


Moshi. Wakati kiwango cha michango ya harusi inayochangwa na marafiki kikiporomoka kwa kasi nchini, washereheshaji (Ma-MC) wameanza kutumia mashine za kielektroniki za EFD ili kutoa stakabadhi.
Baadhi ya washereheshaji (ma-MC), wameenda mbali na kuwataka wenye kumbi zinazotumika kwa sherehe hizo kutowaruhusu washereheshaji ambao hawatawaonyesha kuwa wanatumia EFD.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa ile ari ya uchangiaji harusi iliyokuwapo miaka ya nyuma imeporomoka kwa kasi kubwa sasa.
Kulingana na uchunguzi huo, katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, harusi za kifahari zilizokuwa zikifungwa ni nyingi kulinganisha na miaka miwili iliyopita kutokana na ugumu wa maisha.
Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, bajeti ya chini ya harusi au kumuaga bibi harusi (send off), ilikuwa kati ya Sh5 milioni na Sh7 milioni wakati kiwango cha juu kilikuwa zaidi ya Sh60 milioni.
Hata hivyo, sasa mambo yamekuwa tofauti kwani bajeti za harusi zinazopangwa na wanakamati zinakusanya kati ya asilimia 50 na 75 tena ni kwa wale wenye ndugu wenye uwezo.
Ugumu kukusanya michango
Uchunguzi huo umebaini kati ya kazi ngumu kwa sasa ni ukusanyaji wa ahadi za michango ya harusi, send off au kitchen party kutokana na kile kinachoelezwa kuwa watu ni wagumu kutimiza ahadi zao.
Chanzo kimoja kimedai kuwa kila mtu analia mambo yamebadilika na kwamba unapoonekana unafuatilia sana michango wapo watu ambao hufikia hatua ya kuzuia mawasiliano ya simu.
“Huu usawa wa sasa si kabisa. Kila mtu analia hana hela sasa hizo za kuchangia harusi anazitoa wapi? Ukiona mtu anakuchangia harusi zama hizi mshike sana huyo,” alidokeza mshereheshaji mmoja.
Mkazi wa Pumuwani mjini Moshi, Ewald John alisema anazo kadi tatu za harusi za marafiki wa karibu, lakini ameshindwa kuwachangia kwa sababu hali ya kifedha imekuwa ngumu. “Mimi nina kadi tatu, lakini mbili zimeshapita. Sio kwamba nilikuwa sijui lakini kiukweli sina pesa nafanyaje? Nafikiri Watanzania sasa tubadili aina ya maisha, hii michango haitawezekana,” alisema.
Mshereheshaji mashuhuri nchini, Sijabu Kiata alisema kiujumla hali ya maisha imebadilika na hata harusi zinazofanyika sasa si za gharama kubwa kulinganisha na miaka mitano au 10 iliyopita.
“Watu hawana pesa wala hilo sio suala la kuuliza. Kuna harusi unaenda unakuta inapita round (mzunguko) moja tu ya vinywaji kabla ya chakula na nyingine wakati wa chakula, basi,” alisema.
Wakili wa kujitegemea wa jijini Arusha ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alisema kama michango ya harusi ingekuwa ya lazima, basi ingebidi watumike madalali kuikusanya.
“Katika kazi mojawapo ngumu kwa sasa ni kukusanya michango ya harusi. Unaweza hata mkapishana kauli na mtu unayeheshimiana naye pale anapokwambia hali ni ngumu. Hali imebadilika,” alisema na kuongeza:
“Huko tunapoelekea itabidi mtu anayetaka kuoa ajiandae mwenyewe na marafiki zake wa karibu, tena unaalika watu wasiozidi 20 mkitoka kanisani mnaenda hotelini mnakula mnarudi nyumbani”.
Mkurugenzi wa Mfinanga Block Supply ya Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, Hussein Mfinanga alisema kutokana na mabadiliko ya maisha hivi sasa anafikiria kusitisha uchangiaji wa harusi.
“Huko nyuma mtu anakupa kadi na anakwambia kama humchangii kuanzia Sh100,000 basi usimchangie. Sasa hivi peleka kadi na masharti hayo uone kama utachangiwa,” alisema.
Mfinanga alisema siku za nyuma kuna harusi ilikuwa mtu akichanga Sh20,000 anapewa kadi ya mtu mmoja (single) na wale wanaochangia zaidi ya Sh50,000 ndio wanapewa kadi ya watu wawili, akisema hilo litafutika.
Ma-MC, TRA nao watoa neno
Baadhi ya washereheshaji waliozungumza na Mwananchi jana walipongeza hatua ya Serikali kuwataka waanze kutumia mashine za EFD, lakini wakataka kuwapo mfumo wa kuwabana ma-MC wote.
Kiata alisema japokuwa ni mpango wa Serikali wa kuwataka washereheshaji wote kulipa kodi na kutumia mashine za EFD, utekelezaji wake ni wa kusuasua.
“Mimi nina mashine ya EFD tangu mwaka jana lakini wengi hawana na hii maana yake hawalipi kodi. Hii si sahihi. Ni lazima TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) ije na mfumo unaoeleweka,”alisema.
“Maisha yamebadilika hakuna pesa kabisa unaweza kukaa mwezi mmoja hujapata kazi na bahati mbaya hii kazi imeingiliwa, watu wanashusha bei hawana EFD mashine, ni vurugu tu.”
“TRA waziamuru hizi kumbi zinazotumika kwa hizi sherehe kuhakikisha kuwa kila MC anayeingia katika ukumbi aonyeshe risiti ya EFD aliyomkatia mwenye harusi. Lazima kuwe na usawa.”
Mshereheshaji mwingine, Ntoly Mayombola alisema hakuna MC anayepinga kutumia mashine hizo, lakini tatizo ni ughali wake kulinganisha na vipato vya washereheshaji.
“Tatizo unainunuaje? Unalipwa Sh100,000 au 150,000 au 200,000 lakini tunaambiwa mashine ni zaidi ya Sh700,000. Bado huu mfumo Serikali inatakiwa itoe bure hizo mashine,” alisema Mayombola.
Msimamo wa TRA
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Walipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alipongeza hatua ya baadhi ya washereheshaji kuanza kutumia mashine hizo.
“Tunataka (washereheshaji) wote waingie kwenye kutoa risiti za EFD na mwaka jana tulikaa nao na wako willing (tayari) kutumia hizo mashine. Tunaendelea kuwahamasisha wafanye hivyo mapema,” Kayombo.
Kayombo alisema matumizi ya EFD yatawasaidia Ma-MC kupata kazi kwa vile wananchi hivi sasa wana mwamko wa kudai risiti za kielektroniki na kwamba, wasio nazo inawanyima kazi kubwa hasa za Serikali.   

No comments:

Post a Comment