Sunday, August 20

MWANAMKE MTANZANIA ASHINDA TUZO YA MHASIBU KIONGOZI




Maelfu ya Watanzania wanaishi Uingereza. Wapo wanaoonekana kwenye mitandao jamii na wanaoendelea na shughuli zao bila kusikika. Joyce Materego ni mfano huo. Baada ya kumaliza masomo 2004 alianza kazi ya uhasibu. Anasema mhasibu ni mtu anayeelewa na kutathmini vyema hesabu.
“Kazi yangu ni kuhakikisha fedha zinazoingia ni nyingi kuliko zinazotoka,”anasema. Materego anafafanua kuwa uhasibu ulihitaji kutimiza mitihani 14 kipindi cha miaka 10. Hati inayotolewa ya ACCA (Jumuiya ya Wahasibu Duniani – Association of Chartered Accounts) hutambuliwa popote pale kama walivyo walimu, madaktari na kadhalika. Mafunzo je? Huhusu sheria, kodi, uchumi na kadhalika.
“Unajengwa kisaikolojia kuwa wewe ni mlinzi. Kama daktari anavyoaminiwa na maisha ya watu, wewe unafadhiwa na fedha za watu na makampuni,” anasema.
Badala ya kuchukua miaka 10, Mtanzania huyo alimaliza mafunzo miaka minne tu. Ana bidii sana.
Karibuni aliteuliwa kati ya wafanyakazi wanaowatia wenzao changamoto. Picha iliyotolewa na jarida la kisekta la Focus, kibaruani inaonyesha kasimama na wanaume wawili wa Kizungu na zawadi zao. Nywele sio za bandia, zimesukwa butu kubwa linalotukuza Uafrika. Ni naadra siku hizi kuona mwanamke akisuka namna hiyo. Kila analofanya Materego lina maana na uzito fulani. Mbali ya kulea wanawe wanaosoma sekondari, huenda kazini alfajiri - siku tano kwa wiki na kurejea kuwapikia na kuwahudumia kila siku.
Ingekuwa Tanzania angeajiri mtu wa kufanya kazi nyumbani. Ulaya hilo halipo.
Mbali na kulea, Materego ni mjuzi sana wa lugha na mara kwa mara huajiriwa kama mkalimani wa Kiswahili na Kiingereza fasaha..
Anafanya wapi kazi?
Kaajiriwa na shirika la fadhila linalohudumia watoto maskini la Child Poverty Action Group (CPAG). Mwaka 2015, CPAG ilidai asilimia 28 ya watoto wa Uingereza ni hohehahe. “Ulimwengu mzima” anatathmini. “Tunatakiwa tujue kuna watu wanaoishi maisha ya fahari na duni. Hata Uingereza tuna tatizo hilo. Kampuni yangu inachojaribu ni kuongea na Serikali kuhakikisha wanasiasa wanabadilisha mwongozo wa jinsi fedha za Serikali zinavyotumika kuinua hali ya watoto katika uduni, wawe sawa na wengine.
Unaweza kukuta mtoto anayekulia hali duni kiasi hali nzuri, akienda shule hasikilizi vizuri na hivyo vyote afya kwa mtoto vinachangia mtoto kufanya kazi vizuri.”
Kwanini akapewa tuzo?
Tuzo ilihusiana na namna anavyowasiliana vizuri na wafanyakazi wenzake na wateja wa shirika. Huo ni mfano mzuri wa baadhi ya Watanzania (tusiowajua) wanaolea, huku wakichapa kazi na kutoiaibisha nchi yetu ugenini. Ni siri pia ya undani wa Watanzania. Sisi ni watu waungwana sana kwa ujumla, wageni husema. Tuzo si fedha, bali cheti cha uongozi katika masuala ya fedha. Alisisitiza kuwa usimamiaji wa fedha ni suala muhimu katika sekta na vitengo vyote vinavyotawala dunia zikiwamo kampuni za kibiashara, taasisi za wilaya na mikoa, kiserikali, huduma katika jamii, sanaa na hata uchumi wa nyumbani.
Tumpe hongera mama huyo wa watoto. Kama walivyosema Mwalimu Julius Nyerere na mpigania haki za watu weusi nchini Marekani, Malcolm X ukimuelimisha mwanamke unaelemisha Taifa zima.

No comments:

Post a Comment