Hata hivyo, imesisitiza kuwa licha ya deni hilo, ndege hiyo itakuja huku ikiwatuhumu wanasiasa kutengeneza mgogoro huo.
Juzi, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alidai kuwa ndege hiyo imezuiwa nchini Canada na kampuni hiyo ya ujenzi kwa kuwa inaidai Serikali Dola 38.7milioni za Marekani (Sh87 bilioni).
Lissu alisema kampuni hiyo ilipewa kibali cha kukamata mali za Tanzania na Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro katika nchi za Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, Ubelgiji, Uganda na Canada.
Jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Zamaradi Kawawa alithibitisha deni hilo na kusema ndege hiyo itakuja na taarifa za ujio wake zitatolewa kulingana na mwenendo wa kesi hiyo.
“Ndege itakuja na hao wanaokwamisha watapanda na ndugu na wafuasi wao, Serikali haiwabagui Watanzania kwa itikadi za kisiasa, dini, kabila, rangi au utofauti wowote ule,” Zamaradi aliwaambia waandishi wa habari bila kuruhusu swali lolote na alikuwa makini na matumizi ya maneno.
Juzi, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani alisema makubaliano ya Serikali na kampuni ya Bombardier ni kukamilisha matengenezo hayo na kuikabidhi Serikali ndege yake.
“Ninachojua ndege itakuja. Katika makubaliano ilitakiwa ifike Julai, lakini ratiba zao kwa miezi miwili ijayo hadi Oktoba, ndege itakuwa tayari na itakuwa imeshakamilika, ukweli utajulikana baadaye. Wasipoleta watakuwa wame-breach contract (wamekiuka mkataba),” alisema Ngonyani.
Katika madai yake, Lissu alisema kwa sasa kampuni hiyo inataka ipewe Dola 12.5 milioni za Marekani kama malipo ya awali ili isiipige mnada kwa kibali ilichopewa na Mahakama Kuu ya Montreal Juni 30. “Kampuni ya Stirling ilikubali kuweka masharti nafuu ili Serikali isilipe deni kubwa, lakini Serikali yetu ikakataa, ni nani anayetakiwa kuwajibishwa leo hii kwa hasara hii?” alihoji Lissu.
Tuhuma kwa wanasiasa
Licha ya kukiri kuwapo wa mgogoro huo, Zamaradi alidai kuwa umetengenezwa na Watanzania wasio na uzalendo.
Alisema wanasheria waliokwenda kufungua madai ya kuidai Serikali na kutaka ndege ishikiliwe hawana uhalali wa kufanya hivyo na ni matapeli ambao wamesukumwa na baadhi ya wanasiasa wasioitakia mema Tanzania.
Mkurugenzi huyo alisema wapo baadhi ya wanasiasa na Watanzania ambao wameweka masilahi yao mbele kwa kuchochea mgogoro huo ili kukwamisha jitihada za maendeleo zinazofanywa na Rais John Magufuli.
“Serikali ilipata fununu mapema kwamba kuna baadhi ya viongozi wa chama cha siasa walikuwa na mpango huo na sasa wamejidhihirisha wazi kuwa wao ndiyo wapo nyuma ya pazia la kuhujumu jitihada za Serikali kwa masilahi yao,” alisema na kuongeza:
“Awali, Serikali ilikuwa ikiwahisi baadhi ya wanasiasa kuhusika na hujuma hizi, sasa sio hisia tena bali baadhi yao wameshaanza kujitokeza hadharani.”
Hakuishia hapo, kaimu msemaji huyo alisema Serikali inaendelea kuzifanyia uchunguzi fununu kwamba watu hao wanahujumu jitihada za maendeleo na pia usalama wa raia kwenye baadhi ya maeneo nchini.
“Serikali imesikitishwa na hujuma zinazofanywa waziwazi tena kwa ushabiki wa hali ya juu na baadhi ya viongozi wa kisiasa kupingana na mwelekeo mzuri wa Rais. Kwa mtu mwenye uchungu na nchi yake angepambana ili jambo linalohusu masilahi ya Taifa likiwamo la kununua ndege lisikwame,” alisema Zamaradi.
“Hii si mara ya kwanza kwa wanasiasa kutoa maelezo ya kuvuruga na kukejeli jitihada za Serikali, walishawahi kushawishi wafadhili wasilete misaada Tanzania.Walibeza pia jitihada za kunusuru madini yetu na maliasili.”
Kufuatia hali hiyo, Zamaradi alisema kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwamo za kidiplomasia ili kumaliza suala hilo kwa ajili ya kuhakikisha ndege hiyo inakuja nchini.
Majibu ya Lissu, Zitto Kabwe
Alipotafutwa kujibu tuhuma hizo, Lissu alijibu huku akihoji mazingira ya uzalendo kati yake na Serikali.
“Ni nani ambaye ni mzalendo kati yangu na Serikali, sisi tuliosema hadharani Serikali inadaiwa au Serikali ambayo ilivunja mkataba ikalisababishia hasara Taifa? Nani anayeichafua Tanzania kati yangu na Serikali iliyoshindwa kulipa deni hilo linaloongezeka tangu mwaka 2010?” alihoji.
Lissu ambaye ni wakili wa kujitegemea alisema hakuna haja ya kuvutana, badala yake Serikali inatakiwa kulipa deni hilo ili ndege isipigwe mnada kwa kibali ilichopewa kampuni hiyo na Mahakama Kuu ya Montreal.
Akizungumzia tuhuma hizo, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema kama mpinzani wajibu wake ni kuibua hoja na kuuliza maswali na wajibu wa Serikali ni kutoa majibu.
“Wajibu wangu huo nimeutimiza, nilimuuliza waziri (mwenye dhamana, Profesa Makame Mbarawa) kuhusu suala hili kwenye mtandao wa Tweeter, lakini majibu yake yalikuwa finyu. Haya yanayoendelea sasa ni propaganda za kuchafuana na sihitaji kujihusisha nazo,” alisema Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini.
Mtazamo wa kisheria
Lissu alisema Tanzania ni mwanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara (ICSID) hivyo haiwezi kukwepa katika ulipaji wa deni hilo.
Alisema endapo Serikali haitalipa deni hilo, ndege hiyo itapigwa mnada. “Nchi yoyote ambayo ni mwanachama wa mahakama hiyo, ikitolewa hukumu lazima itekelezwe na nchi zote ambazo ni wanachama na ndiyo maana kampuni hiyo imepewa kibali cha kukamata mali za Serikali katika nchi hizo. Kibali walichopewa kwa kawaida kinadumu kwa wiki mbili hadi mwezi mmoja kabla ya kupiga mnada,” alisema.
Wakili wa kujitegemea wa Mahakama Kuu, Onesmo Mpinzile alisema changamoto iliyopo ni uwazi wa mkataba kati ya Serikali na kampuni ya Stirling baada ya Serikali kuvunja makubaliano ya ujenzi wa barabara hiyo.
“Katika makubaliano ya mkataba mnaweza kukubaliana, endapo mgogoro ukitokea katika makubaliano yenu mtamalizaje, mtatumia mahakama za ndani au za kimataifa au mtatumia sheria zipi, sasa makubaliano ya Serikali na kampuni hiyo wakati wa ujenzi wa barabara hatuyafahamu msingi wake katika eneo hilo,” alisema.
Alisema mamlaka ya utatuzi wa mgogoro yaliyotolewa kupitia kifungu cha usuluhishi, hakijalishi kama nchi husika itakuwa mwanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi. “Kwa hiyo inakuwa vigumu kujua mazingira ya mgogoro huo,” alisema.
Sakata la ndege
Uamuzi uliofanywa na Serikali wa kuvunja mkataba na kampuni hiyo ya Canada iliyokuwa ikijenga Barabara ya Tegeta Wazo-Bagamoyo ndiyo uliochelewesha ujio wa ndege hiyo.
Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki, alisema baada ya uamuzi huo, Stirling ilifungua kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi ikidai kukiukwa kwa mkataba na ilipofika Juni 2010, mahakama hiyo ilitoa tuzo ya ushindi kwa kampuni hiyo ikiitaka Serikali ilipe fidia ya Dola25 milioni za Marekani, huku deni hilo likiwekewa riba ya asilimia nane.
Kwa madai ya Lissu, Serikali ilikataa kulipa fidia hiyo hadi Juni 30 wakati mahakama hiyo ilipoipa Stirling kibali cha kukamata mali zote za Tanzania zitakazokuwa katika nchi ilizozitaja.
Akizungumzia suala hilo, Lissu alidai kuwa hata Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga alikuwa Canada Agosti 3 kushughulikia suala hilo.
Hata hivyo, kuhusu madai ya kampuni ya Stirling, Naibu Waziri Ngonyani alisema Serikali kudaiwa si jambo la kushangaza akidai kuwa tangu Serikali ilipoingia madarakani mwaka 2015, wizara hiyo ya ujenzi ilikuwa inadaiwa Sh1.12 trilioni, lakini hadi Julai tayari deni hilo limepungua hadi kubaki Sh900 bilioni.
“Mimi sina taarifa kuhusu deni hilo, ila kikubwa Serikali kudaiwa si big deal (jambo la kushangaza), ila tunafanyaje katika kuyalipa madeni, pengine inawezekana deni hilo likawa ni sehemu ya madeni tunayodaiwa,” alisema.
Kauli ya JPM siku ya uzinduzi
Akizindua ndege mbili mpya aina ya Bombardier Q400 NextGen, Septembea 28 ambazo ziliingia nchini Septemba 20 na 27, Rais Magufuli alibeza kundi la watu wanaozikejeli.
“Watu wanaofanya biashara ndiyo wanaopiga vita, ndiyo maana nikasema anayetaka kasi akapande ndege ya jeshi,” alisema.
Rais Magufuli alisema Serikali iliamua kununua ndege hizo kwa fedha taslimu kwa sababu ilikuwa nazo kwa kuwa ununuzi kwa njia ya mkopo ungeweza kugharimu fedha nyingi zaidi.
Wazo la kununua ndege hizo lilianza Januari 25, 2016 Serikali ilipotoa mapendekezo ya mwelekeo wa mpango wa pili wa miaka mitano wa maendeleo wa Taifa unaolenga zaidi kuinua sekta ya viwanda, ilipotaja vipaumbele 20 ikiwamo cha kununua ndege mbili za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Akiwasilisha mapendekezo hayo, Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk Ashatu Kijaji alitoa ahadi hiyo huku akibainisha pia mpango wa kuboresha wa miundombinu ya usafiri wa anga ili kuongeza ufanisi katika sekta hiyo.
No comments:
Post a Comment