Monday, November 13

CCM, Chadema wanavyotifuana kwenye kampeni za udiwani


Mwenyekiti  Chadema Taifa, Freema Mbowe
Mwenyekiti  Chadema Taifa, Freema Mbowe akizungumza wakati wa Mkutano wa kampeni wa uchanguzi  mgodo wa udiwani  Kata ya Reli uliofanyika katika Uwanja wa Serengeti  Mjini Mtwara jana. Picha na mpigapicha Wetu 
Siku 17 tangu kuanza kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 43 nchini, vyama vya CCM na Chadema vimeendelea kupimana ubavu.
Kampeni za uchaguzi huo zilianza Oktoba 27 na zitahitimishwa Novemba 25. Uchaguzi umepangwa kufanyika Novemba 26.
Akizungumzia mwenendo wa kampeni hizo, katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Elias Mpanda alisema jana kuwa chama hicho hakitumii nguvu kubwa kwa kuwa kina uhakika wa kushinda kata zote nane mkoani humo.
Alisema hilo linatokana na kazi zinazofanywa na Rais John Magufuli ambaye ni mwenyekiti wa CCM kwa kuwa amefungua njia na kila mmoja anaona utendaji kazi wake, hivyo chama hicho kinaaminiwa.
Mgombea udiwani wa Kata ya Muriet (CCM), Francis Mbise aliwaomba wananchi kumchagua ili kuibadili kata hiyo kwa kuhakikisha huduma ya maji inapatikana.
Kwa upande wake, mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amemshauri Rais Magufuli kusikiliza kilio cha wananchi kuhusu Katiba Mpya.
Akizungumza katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za udiwani Kata ya Moita wilayani Monduli, Lowassa alisema nchi inakwenda vizuri kwa katiba iliyo bora na kwamba, nchi inaongozwa kwa umoja na hakuna nchi ambayo inaongozwa na mtu mmoja.
Lowassa alisema haiwezekani katika uchaguzi mgombea mmoja anapata kura milioni sita lakini hapati kitu na mshindi anapata kura milioni nane.
“Mimi walinipa kura milioni sita na Magufuli alipata kura milioni nane na kutangazwa mshindi sasa haiwezekani kura sita milioni kutosikilizwa,” alisema na kuongeza kuwa, katika nchi nyingine aliyepata kura milioni sita anapata nafasi.
Aliwataka wananchi wa Moita kumchagua mgombea wa Chadema, Loburu Lomyaki akisema kata hiyo ni miongoni mwa alizowezesha maendeleo wilayani Monduli alipokuwa mbunge.
“Hapa kuna maji, umeme, shule mbili za kata na maendeleo mengine nawahakikishia sintowasahau,” alisema.
Chadema kamwe haitakufa
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema siku atakayoingia kaburini ndiyo wasaliti watafanikiwa kukivunja chama hicho.
Alisema ametoka mbali akiwa na watu anaowaamini na waliojiita wanamapinduzi ambao baadaye waliteleza.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo katika Kata ya Reli mkoani Mtwara, alisema silaha pekee ya kusonga mbele katika siasa za upinzani ni kuungana.
Alisema mwaka 2015 alijaribu kwa kila hali kufanikisha hilo kwa kuwataka alioamini wana mapinduzi wenzake kuweka masilahi yao pembeni na kuangalia mustakabali wa Taifa.
“Niliwaambia wenzangu Dk Wilbroad Silaa weka masilahi yako pembeni, Profesa Ibrahim Lipumba weka masilahi pembeni na nikajiambia Mbowe weka masilahi pembeni. Cha kushangaza Profesa Lipumba na Dk Slaa wakateleza, mimi nimekomaa na wasaliti waliowarubuni wao wamejaribu kwa kila hali kuivunja Chadema, lakini wamegonga mwamba na ninasema litafanikiwa hilo siku nikiingia kaburini,” alisema Mbowe.
Kuhusu umuhimu wa Katiba Mpya, Mbowe alisema upo palepale na si takwa la watawala bali ni la wananchi.
“Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwa Katiba hii mtu akiamua kuwa dikteta anakuwa kwa sababu inampa mamlaka makubwa Rais,” alisema Mbowe.
Kukosekana Nyalandu
Aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu aliyejiondoa CCM alishindwa kupanda jukwaani mjini Mtwara katika mkutano wa Chadema.
Mbowe akihutubia mkutano wa kampeni ya uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Saranga jijini Dar es Salaam alisema amempokea Nyalandu na jana na angeungana naye kwenye mkutano mjini Mtwara.
Hata hivyo, kukosekana kwa ndege inayofanya safari kati ya Dar es Salaam na Mtwara kumemsababishia Nyalandu kushindwa kuhudhuria mkutano huo.
Mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema alisema Nyalandu aliyekuwa Nairobi nchini Kenya kumjulia hali Tundu Lissu amekosa ndege ya kwenda Mtwara.
Mke wa mgombea jukwaani
Stella Mang’ati, mke wa mgombea udiwani Kata ya Kitwiru, Manispaa ya Iringa kwa tiketi ya CCM, Baraka Kimata alipanda jukwaani kumuombea kura mumewe akitumia fursa hiyo kujibu maswali kadhaa aliyodai yameibuliwa na wapinzani kwamba amekuwa hafuatani na mumewe kwenye kampeni.
“Maswali mengi nimeyapata hata ninyi mmeyasikia, wanasema mnatembea na mgombea hana mke waambieni leo mmeniona,” alisema.
Kimata aliyekuwa diwani wa kata hiyo kupitia Chadema kabla ya kujiuzulu na kuhamia CCM alisema baadhi ya miradi alishindwa kuitekeleza kutokana na kutokuwa na maelewano mazuri na viongozi wake wa juu.

Wanafunzi 400 wanavyopokezana darasa


Mkuu mpya wa mkoa wa Geita, Robert Lughumbi amekutana na jambo jipya katika elimu baada ya kuambiwa madarasa mawili yenye wanafunzi 400 yanachangia chumba kimoja.
Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Nyarubanga wilayani hapa, Boaz Masalu amemwambia Lughumbi kuwa, shule yake yenye wanafunzi 1, 799 ina vyumba sita vya madarasa, hali inayosababisha baadhi ya darasa kukaliwa na wanafunzi zaidi ya 300.
Mwalimu huyo akamweleza mkuu wa mkoa ambaye aliteuliwa hivi karibuni na Rais Magufuli kuwa, wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili wanaofikia 400 wanachangia chumba kimoja kusomea na hupokezana kwa zamu. Shule hiyo pia inakabiliwa na upungufu wa matundu ya vyoo na kwa sasa ina matundu manne yanayotumiwa na wanafunzi 1,799. Kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa 8,000 vinavyoukabili mkoa huo katika shule za msingi, Lughumbi ameanza kampeni ya ujenzi kupitia michango na nguvu ya wananchi pamoja na wadau.
Kwa kuanzia ameanza kuhamasisha ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa kuchimba msingi katika shule hiyo inayokabiliwa na upungufu wa vyumba 34 vya madarasa. “Haiwezekani Geita inayosifika kwa utajiri wa dhahabu karibia kila eneo liendelee kukabiliwa na changamoto ya uduni wa huduma za kijamii na maendeleo ikiwamo upungufu wa vyumba vya madarasa, lazima tufikie lengo na sera ya elimu ya darasa moja kutumiwa na wanafunzi wasiozidi 45,” alisema Lughumbi.
Katika hafla ya kuhamasisha ujenzi wa madarasa shuleni hapo, mifuko 200 ya saruji ilipatikana kupitia michango ya wananchi, viongozi wa halmashauri, ofisi ya mkuu wa wilaya na mbunge wa Geita pamoja na ile ya mkuu wa mkoa.
Akishukuru kwa niaba ya wananchi, diwani wa Luenzera, Jeremia Misango aliwataka wananchi kujitokeza kuchangia miradi ya maendeleo katika maeneo yao badala ya kutegemea Serikali na wafadhili.

Wanaosubiri kuchimbiwa vyoo vya msaada waelezwa wasahau


Mkuu wa wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, Louis Bura ametathmini baadhi ya watu wasivyojituma kisha akawaambia wanaotegemea msaada wa kuchimbiwa vyoo wasahau kwa kuwa haitatokea wakaupata katika kipindi hiki.
Bura hakuishia hapo, bali alikwenda mbali zaidi na kusema hata wale wanaosubiri msaada huo kutoka kwa wafadhili ni wazi wamepitwa na wakati kwa vile mambo hayo hayapo tena.
Kauli hiyo aliitoa jana wakati wa shughuli ya kuweka mazingira safi na afya salama wilayani Kibondo kupitia mradi unaotekelezwa katika vijiji 10 kwa kuhamasisha jamii kuchimba na kutumia vyoo bora ili kutunza vyanzo vya maji.
“Muda wa kusaidiwa na mjomba hata kuchimba choo haupo tena, wananchi tujue kwamba mambo yanayohusu ulinzi wa afya zetu ni lazima tuyagharamie kwani siku tukiugua magonjwa yatokanayo na kutumia maji machafu au ukosefu wa vyoo ndipo tutakapoona umuhimu,” alisema Bura.
Mratibu mradi kutoka shirika la TCRS, Terry Raphael alisema mradi huo unalenga kuielimisha jamii juu ya matumizi ya vyoo bora na usafi wa mazingira.
Ofisa afya, maji na usafi wa mazingira kutoka shirika la misaada la Norway (NCA), Zakayo Makobero aliwataka wakazi wa Kibondo kutumia ujuzi waliopata kuelimisha wengine juu ya umuhimu wa kulinda vyanzo vya maji na kuvitumia kwa usahihi.

Walimu wa hisabati watakiwa kubuni mbinu kuvutia wanafunzi


Katika kukabiliana na ufaulu duni wa somo la hisabati, hususan kwa shule za Serikali, walimu wametakiwa kubuni mbinu rahisi ambazo wanafunzi watazifahamu na kupenda kujifunza na hatimaye kuinua ufaulu wa somo hilo.
Hayo yalisemwa juzi na katibu tawala mkoa wa Geita, Selestine Gesimba wakati wa mahafali ya wahitimu 86 wa kidato cha nne katika Sekondari ya Waja.
Gesimba alisema kushuka kwa kiwango cha ufaulu masomo ya sayansi hasa hisabati inatokana na ufundishaji.
Alisema kwamba ufundishaji ndiyo unaomfanya mwanafunzi toka awali kulipenda somo au kulichukia na kwamba, iwapo walimu watabadilika na kutafuta mbinu rahisi na rafiki ya kufundisha itasaidia wanafunzi kulipenda na kuelewa somo hilo.
Awali, mkurugenzi wa shule za Waja, Chacha Mwita alisema Watanzania wengi wamejijengea akilini kuwa somo la hisabati ni gumu hali inayomfanya mwanafunzi kuliogopa kabla hata ya kufundishwa.
Mwita alisema kwa shule za Waja wameweka mikakati ya kuwasaida wanafunzi ikiwa ni kuwaandaa kisaikolojia kulipenda somo hilo, mitihani ya majaribio kila mwanzo wa wiki na kutoa motisha kwa wanaofanya vizuri ili kuwafanya wanafunzi walipende.
Mwita alisema siri kubwa ya ufaulu katika shule yake ni motisha kwa walimu na wanafunzi, kwa kidato cha nne wanafunzi wanaopata daraja la kwanza hupewa ufadhili wa kusoma kidato cha tano na sita bure na wale wa kidato cha sita huzawadiwa gari isiyopungua Sh10 milioni.
Zawadi kwa wanafunzi
Katika mahafali hayo wanafunzi sita ambao walifanya vizuri katika mitihani 14 ya majaribio waliyopatiwa kwa mwaka huu, wamepewa ufadhili wa kusoma kidato cha tano na sita bure.
Pia, alitoa nafasi kama hiyo kwa wanafunzi wote nchini ambao watapata daraja la kwanza alama saba na nane, kusoma bure katika shule yake. “Tukiwapa watoto motisha watapenda kusoma kwa bidii, naamini motisha kama hii inampunguzia pia mzazi mzigo wa ada na anafurahia kuwa na mtoto ambaye anapenda kusoma na kufaulu,” alisema Mwita.
Mwita alisema katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2016 sekondari kwa upande wa wavulana kidato cha nne ilikuwa ya 24 kati ya shule 1,439 na wasichana ilishika nafasi ya 19 kati ya shule 1,439.

Tamu na chungu ya bei elekezi mpya ya mbolea


Hivi karibuni, Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) ilitangaza bei elekezi ya mbolea yenye unafuu.
Unafuu huo umekuja huku pia kukiwa na mfumo mpya wa uagizwaji wa mbolea wa pamoja, ambao umesababisha bei kushuka kutokana na udhibiti wake.
Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Kilimo, Charles Tizeba Agosti 15, 2017 inasema bei hiyo ni hadi kwenye duka la muuzaji wa rejareja.
“Kwa utaratibu huu, bei elekezi ya mfuko wa kilo 50 wa mbolea ya kupandia (DAP), itakuwa kati ya Sh50,500 na Sh53,000 kwa mikoa ya Kanda ya Mashariki, Kati na Kaskazini,” inasema taarifa hiyo.
“Kwa mikoa ya Kanda za Magharibi, Ziwa na Nyanda za Juu Kusini, bei elekezi ya mfuko mmoja wa mbolea wa kilo 50 itakuwa kati ya Sh53,500 na Sh56,000. Bei hizi ni pungufu kwa wastani wa asilimia 13 hadi 42 ukilinganisha na bei ya mbolea aina ya DAP iliyokuwa ikiuzwa kati ya Sh60,000 na Sh100,000 kwa mfuko wa kilo 50.
Kwa upande wa mbolea ya kukuzia (Urea), anasema mfuko wa kilo 50 utauzwa kati ya Sh41,000 na Sh43,000 kwa mikoa ya Kanda ya Magharibi, Ziwa na Nyanda za juu Kusini na kwa Kanda ya Mashariki, Kati na Kaskazini, bei itakuwa kati ya Sh38,000 na 43,000.
“Bei hizi ni pungufu kwa wastani wa asilimia 15 ukilinganisha na bei ya mbolea aina ya Urea iliyokuwa ikiuzwa kati ya Sh45,000 na Sh70,000 kwa mfuko wa kilo 50,” anasema Dk Tizeba.
Bei haina faida
Hata hivyo, wakizungumza katika mkutano wa wadau wa mbolea uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, baadhi ya wafanyabiashara walisema bei hizo hazina faida kwao.
Mmoja wa wafanyabiashara mbaye hakutaja jina lake liandikwe gazetini akidai kulinda masilahi yake ya biashara, anasema bei elekezi iliyopangwa na Serikali haina faida kwao.
“Wametumia mfumo wa Sumatra (Wakala wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini) usio na uhalisia. Bei hiyo haijazingatia gharama za kuhifadhi mzigo ukishaununua bandarini, utaweka wapi?
“Bei elekezi ya mbolea hapa Dar es Salaam unanunua Sh48,000 hivi, sasa kama unaipeleka Mbeya ukaiuze Sh53,000 usafiri wa treni ni Sh4,500 kwa mfuko.
“Ukishafika Mbeya kwa mfano kuna gharama za kutoa mzigo stesheni kwenda ghalani tena, inaweza kuwa Sh500 kwa mfuko, kama ni Tukuyu kwa mfano inaweza kuwa Sh1,500, kuna kushusha tena Sh200 hapo bado, wakala hajadai naye faida yake. Mwisho utakuta gharama zimezidi bei elekezi,” anafafanua mfanyabiashara huyo.
Kuhusu elimu, mfanyabiashara huyo alisema bei hiyo haikuzingatia utoaji wa elimu kwa kuwa nao una gharama kubwa.
“Waziri amesema tutoe elimu kwa wakulima, lakini ajue kuwa tunatakiwa kukodi kumbi, kulipa posho za wataalamu na washiriki, kwa bei hiyo hiyo?” anahoji mfanyabiashara huyo.
Naye meneja masoko wa Kampuni ya Yara Tanzania Ltd, William Ngeno anasema japo awali hawakuukubali mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja lakini wameamua kufuata sheria.
“Sheria ikishasema usipite hapa, inabidi usipite kwa hiyo tulikubali. Tunashirikiana na Serikali na wataalamu kutoa elimu kwa wakulima,” anasema Ngeno.
Hata hivyo, anasema Serikali imedhibiti mbolea aina mbili tu za DAP na Urea wakati kampuni hiyo inatengeneza mbolea zaidi ya aina 10.
Akizungumzia changamoto ya usafiri, mfanyabiashara Jaison wa Kampuni ya Staco, anasema wamekwepa kusafirisha mbolea kwa treni kwa sababu ya gharama.
“Sisi tunatumia barabara kwa sababu ukisafirisha kwa treni, utalazimika tena kuihamishia kwenye magari unapofika mikoani. Tunachofanya ni kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha wakulima wadogo wanafaidika,” anasema.
Msimamo wa Serikali
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba anasema bei elekezi imeshapigiwa hesabu za usafirishaji na faida, hivyo wafanyabiashara hawapaswi kuongeza faida zaidi.
“Tumeshachukua uamuzi kwenye biashara ya mbolea aina mbili yaani DAP na Urea, bei isiwaumize wakulima. Tumeondoa tozo mbalimbali ili kila upande ufaidike ikiwezekana mkulima afaidike zaidi,’ anasema na kuongeza:
“Nimesimama kwenye mkutano jimboni kwangu mwezi uliopita, nikauliza wangapi wanatumia mbolea, hakuna aliyenyoosha mkono, nilipouliza wangapi hawatumii, wote wakanyoosha, hii haikubaliki.”
Wakulima watoa ya moyoni
Wakizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, wakulima kutoka vijiji vya Luganga, Utengule na Mtandika wilayani Kilolo Mkoa wa Iringa wanaeleza changamoto za upatikanaji wa mbolea.
Kwa maelezo yao wanaonyesha kutegemea zaidi mbolea ya ruzuku na kutoelewa kinachoendelea kuhusu bei mpya za mbolea.
Immaculate Kagogo ambaye ni mkulima wa Kijiji cha Luganga wilayani Kilolo, anasema mbolea hiyo wanaipata kwa kuchelewa.
“Mara ya mwisho walipoleta walitaka tununue ikiwa kwenye gari lakini mwenyekiti alikataa hadi iliposhushwa na kuwekwa kwenye ghala. Lakini huwa inaletwa kwa kuchelewa sana,” anasema.
Maelezo yake yanafanana na ya Oswald Joseph wa kijiji hicho anayesema:
“Wanaweza kuleta mbolea ya kupandia mwezi wa kwanza au wa 12 mwishoni na mvua zimeanza Novemba kwa hiyo inakuwa shida. Mbolea ya DAP tulikuwa tunanunua hadi Sh70,000 na Urea 50,000 hadi 54,000.”
Anaongeza: “Hiyo ni bei kubwa na ni kwa wakulima waliozoea kilimo cha mbolea, lakini wa wakulima wa kawaida hawatumii kabisa mbolea. Wanachofanya ni kubahatisha kwa kutumia mbolea za kienyeji kama samadi. Unaweza kupanda ekari mbili ukapata magunia mawili ya mahindi.”
Akieleza sababu ya ucheleweshwaji huo wa mbolea, Evans Msofu ambaye ni meneja wa TFC Mkoa wa Iringa anataja mchakato wa utoaji mizigo bandarini kuwa chanzo.
“Sababu zinazochelewesha mbolea hasa vijijini ni mchakato unaofanyika kutoka mbolea zinakotoka, mfano bandarini ambako kuna mchakato wa kushusha na mengineyo sasa mpaka ukasafirishe, ndio unakuta inachelewa,” anasema.
Akifafanua zaidi, Msofu anasema mawakala wa pembejeo ndiyo wanaohusika na usafirishaji wa mbolea kutoka bandarini Dar es Salaam kwenda mikoani na watakaowahi kupata ni walio karibu hasa mijini.
Kauli ya TFRA
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mbolea Tanzania (TFRA), Lazaro Kitandu anasema tayari kumekuwa na mafanikio tangu bei hizo zilipotangazwa sambamba na mfumo wa uagizaji wa pamoja wa mbolea.
“Nchi imefaidika na bei ya chini ya mbolea kupitia ununuzi wa pamoja kutokana na punguzo linalopatikana katika bei kwa sababu ya kiwango kingi kilichonunuliwa na kupungua kwa gharama za uendeshaji,”anasema.
Anatoa mfano wa zabuni iliyofunguliwa Julai 21, 2017 ambapo bei ya ununuzi (FOB) kwa mbolea ya kupandia (DAP) ilipatikana kwa Dola 3047 ambayo ni chini kwa asilimia 15 ya bei iliyokuwa katika soko la dunia ambayo ni Dola 365.
“Mfumo huu umewawezesha wafanyabiashara wadogo kushiriki katika biashara ya mbolea na hivyo kuimarisha mtandao wa usambazaji hadi ngazi ya mkulima,” anasema.
Hata hivyo, anasema kumekuwa na changamoto ya baadhi ya wadau kuuchanganya mfumo huo na ule wa vocha au ruzuku za mbolea, huku baadhi ya kampuni zikijaribu kuuhujumu ili kupunguza ushindani unaotokana na wafanyabiashara wadogo kuingia kwenye soko la mbolea.
Akizungumzia mfumo mpya wa bei elekezi, Kitandu anasema umepokelewa vizuri na wakulima kwa sababu unawafikishia mbolea kwa bei nafuu kulinganisha na hali ilivyokuwa awali.

Mmiliki wa shamba lililofutwa asema JPM amedanganywa



Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela 
Tanga. Shamba la mkonge la Mnazi wilayani Lushoto lililotangazwa leo Jumatatu na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela kuwa limefutwa na Rais John Magufuli  kutokana na kutoendelezwa limezua utata baada ya aliyekuwa  akilimiki kudai kwamba hajawahi kulitelekeza.
Mkurugenzi wa kampuni ya Le-Marsh Enterprises Ltd iliyokuwa
ikiendesha shamba hilo, Lawarence Macharia amedai kuwa Rais Magufuli amedanganywa kwa sababu hadi mwaka jana kati ya hekta 1,460 zilizopo hekta 900 alishakuwa amepanda mkonge.
Ametoa takwimu hizo alipokuwa akizungumza na Mwananchi mara baada ya Shigela kutangaza rasmi kwamba Rais amefuta umiliki wa kampuni ya Le-Mash Enterprises katika shamba la mkonge la Mnazi wilayani Lushoto.
Shigela ambaye alikuwa akifungua mkutano wa “Mkonge Day” uliohudhuriwa na wadau kutoka mikoa mbalimbali nchini amesema kuwa Rais amelirejesha serikalini shamba la Mnazi na kuelekeza kuwa maombi yafanyike upya na kwamba lisibadilishwe matumizi bali watakaochukua wahakikishe
wanazalisha zao la mkonge.
“Kwa taarifa hii nakaribisha rasmi maombi kwa watakaokuwa na uwezo wa kuzalisha mkonge katika shamba la Mnazi, nitatoa maelekezo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ya namna ya kuendesha mchakato kwa watakaokuwa na uwezo wa kulichukua shamba hilo,” amesema Shigela katika
mkutano huo.
Baada ya tangazo hilo, Mwananchi ilizungumza na Macharia ambaye alikuwepo kwenye mkutano huo na kueleza kushangazwa kwake kusikia taarifa hizo na kubainisha kuwa Rais amedanganywa kuhusiana na shamba la Mnazi huku akisisitiza amenyang’anywa kwa sababu za kisiasa.
“Wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2015, mbunge aliwaambia wapigakura akishida atahakikisha kuwa shamba hilo linanyang’anywa na watagawiwa mashamba ya kulima mahindi na mazao mengine,” amesema
Macharia.

Amesema  Oktoba 27 mwaka jana aliandikiwa barua na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mnazi akiambiwa kuwa kampuni yake imeshafutiwa usajili wa shamba hilo na kwamba asikanyage shambani hapo.

Amesema hadi sasa ameshapanda hekta 537 za mkonge mpya, hekta 147 zikiwa na mkonge wa zamani na hekta 216 zililimwa upya kwa ajili ya kupanda mkonge mwingine na kwamba kampuni yake ilitarajia kuuza nje ya nchi tani 425 za singa.
“Hata hivyo, nimefurahishwa na taarifa kwamba Rais ameelekeza lisibadilishwe matumizi kwa sababu mkonge una faida kubwa katika uchumi wa viwanda,” amesema Macharia na kusisitiza kuwa atafuataili ili aweze kurejeshewa shamba hilo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Mkonge(SAT), Deogratius Ruhinda amesema wadau wameonyesha kuridhishwa baada ya kusikia kuwa Rais ameamuru shamba la Mnazi lisibadilishwe matumizi ya kilimo cha Mkonge.

Museveni: Kufanya masihara ni kosa kubwa


Hoima, Uganda. Rais Yoweri Museveni amesema kuwa watu wanaomchukulia kimasihara wanatenda “kosa kubwa” akitolea mfano namna alivyotendewa na chama tawala wa cha Uganda People’s Congress (UPC) miaka ya 1980.
Rais Museveni alitoa mfano wa mambo yaliyo nyuma ya pazia alivyopambana na watu wa nje kuhusu nini cha kufanya kibiashara na hazina kubwa ya mafuta itakapogundulika wazi.
Alisema muda mfupi baada ya kushika madaraka mwaka 1986, baadhi ya wazurungu kutoka Ulaya walimfuata ili awaidhinishe kufanya kazi ya utafutaji na uchimbaji mafuta nchini Uganda.
Museveni alisema, hata hivyo, aliwakatalia na badala yake aliamua kuwapeleka Waganda kusomea uchumi wa mafuta na gesi ili kujenga uwezo wa ndani kabla ya kuanza kazi ya uchimbaji.
“Mimi sitaniwi,” alisema Rais. “Hata UPC walifanya kosa hilo.”
Mwaka 1980, Museveni ambaye aligombea urais kwa tiketi ya Uganda Patriotic Movement (UPM) alionya kwamba atakwenda msituni ikiwa uchaguzi utavurugwa. Milton Obote alishinda hivyo akarudi kuiongoza Uganda kwa mara ya pili baada ya kupinduliwa na Idi Amin mwaka 1971.
Museveni alianzisha vita vya msituni dhidi ya serikali ya Obote iliyopinduliwa na Tito Okello Lutwa ambayo pia ilipinduliwa na Museveni Januari 1986.
Rais akizungumza Jumamosi iliyopita wakati wa sherehe fupi za uzinduzi wa ujenzi wa bomba la mafuta katika Mradi wa Bomba la Mafuta Afrika Mashariki, alitaja umuhimu wa kubuni vyanzo vya uchumi na akasema wanaofanya masihara naye wanatenda kosa kubwa.

Wachina, Watanzania wavizia fursa vifaa vya upimaji ardhi

Meneja Mkuu wa Kampuni ya China TopRS
Meneja Mkuu wa Kampuni ya China TopRS Technology Co. Ltd, kutoka nchini China, Profesa Li Yingcheng akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Ndege za upimji Ardhi zisizokuwa na rubani (drones). Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya  Suryeying Eguipment Service Centre (EA) Ltd  (Sesc ) ya nchini inayomiliki ndege hizo, Haji Mchatta na kushoto ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Dk Elifuraha Saria . Mpigapicha wetu 
Kampuni ya uzalishaji vifaa vya upimaji ardhi na ramani ya China, imekubali kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha upatikanaji wa vifaa vyake ili kupunguza gharama, kwa nchi za Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla.
Katika kutimiza azma hiyo, kampuni hiyo ya South Surveying and Mapping Company imeingia makubaliano ya uuzaji vifaa hivyo nchini na kampuni ya Suryeying Eguipment Service Centre (EA) Ltd (Sesc ).
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ndege za upimaji ardhi zisizokuwa na rubani (drones), mkurugenzi mkuu wa Sesc, Haji Mchatta alisema kuwa makubaliano hayo yamefikiwa wiki iliyopita walipofanya ziara nchini China.
Mbali na South, kampuni nyingine ya China iitwayo China Toprh Technology Ltd, nayo imeonyesha nia ya kushirikiana na Sesc katika eneo hilo ili kukabiliana na changamoto za upimaji ardhi zinazotokana na tatizo la vifaa.
Meneja mkuu wa kampuni hiyo, Profesa Li Yingcheng aliyeshiriki katika uzinduzi wa drones hizo, alisema licha ya kushirikiana na Sesc eneo hilo pia wanaangalia uwezekano wa kutumia Satelite.
Mchatta ambaye pia ni mtaalamu wa vifaa vya upimaji, alisema kwamba zaidi ya asilimia 80 ya ardhi ya Tanzania haijapimwa.
“Upatikanaji wa vifaa ni wa gharama za juu, hivyo bei ya upimaji inakuwa kubwa,” alisema Mchatta.
Mchatta na kuongeza:
“Lakini tatizo lingine hapa nchi hakuna mahali penye huduma ya matengenezo ya vifaa hivyo, na hivyo kufanya muda wa kufanya kazi kwa vifaa hivyo kuwa mfupi sana..”,
Alibainisha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya vifaa vya upimaji ardhi hapa nchini havifanyi kazi na hii si kwa sababu kwamba vimekufa bali ni kwa sababu ya ukosefu wa huduma ya matenengezo na vipuli.
Hivyo alisema kuwa Sesc imekusudia kukabiliana na tatizo hilo kwa kuhakikisha kuwa vifaa vya upimaji vya kisasa vinapatikana kwa gharama nafuu na huduma za matengenezo ili kuongeza tija katika sekta hiyo.
Mtaalam huyo alibainisha kuwa ili kutimiza lengo hilo Sesc baada ya kutafakari kwa mambo mengi iliichagua kampuni ya South kufanya nayo kazi na kwamba kwa ushirikiano tayari wameweza kuanzisha karakana ya kisasa kuhakikisha kuwa aina zote za huduma/ukarabati wa vifaa zinafanyika nchini.
“Wanatoa vipuli, wakati wowote vinapohitajika na pia wanatoa mafunzo.”, alifafanua Mchatta.
Alisema kuwa kampuni hiyo ambayo ni ya nne kwa ukubwa na ubora wa teknolojia duniani inakidhi viwango vya kimataifa vya uzalishaji wa vifaa vya upimaji ardhi na ramani ambavyo vinauzwa duniani kote na zaidi sana bei zao ni nafuu sana.

Serikali yatishia kulivunja Baraza la Madiwani Kigoma Ujiji


Dodoma. Serikali imeionya Manispaa ya Mji wa Kigoma Ujiji kuacha kuendelea kuwasiliana na Mpango wa Kuendesha Shughuli za Serikali kwa Uwazi (OGP) na kama ikiendelea itachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kuvunja Baraza la Madiwani.
Hatua hiyo imekuja baada ya Serikali kujiondoa katika mpango huo mapema mwaka huu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi Umma na Utawala Bora, George Mkuchika amesema bungeni leo Jumatatu wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe ambaye chama chake kinaongoza manispaa hiyo.
Zitto katika swali lake la nyongeza amesema kuwa nchi za Hungary na Urusi ambazo Serikali inasema nazo  zimejitoa katika mpango wa OGP ni miongoni mwa nchi zinazoendeshwa kidikteta kwa kutofuata utawala bora.
"Nchi za Hungary na Urusi zinaendeshwa bila kufuata demokrasia zinaendeshwa kidikteta ni aibu sana kwa Serikali kusema inaiga nchi ambazo zinaenda kinyume na demokrasia," amesema.
Amesema majukwaa hayo ya kimataifa yanatengeneza mahusiano na kwamba Canada ni mwenyekiti wa mpango huo.
Hata hivyo, amesema juzi ameona Rais John Magufuli amemwandikia Waziri Mkuu wa Canada kuhusu suala la Bombardier.
"Serikali haioni kwamba ingeendelea kuwa mwanachama wa OGP na mwenyekiti ni Canada hili ombi lingeshughulikiwa kwa uzito zaidi," amehoji Zitto.
Zitto amesema Manispaa ya Kigoma Ujiji ni miongoni mwa miji 15 duniani ambayo ipo katika mpango huo na kwamba Serikali inatoa kauli gani juu ya ushiriki wa mji huo  katika OGP ambayo imekuwa ikifaidika na mpango huo na miji mingine inayotaka kuingia katika mpango huo.
Akijibu hayo Mkuchika amesema Tanzania imejitia katika mpango kwa hiari yake  yenyewe na kwamba hawajaiga nchi yoyote.
"Sisi ni Taifa huru linalojitawala linalofanya matumizi yake yenyewe, bila kushurutishwa na Taifa lolote liwe dogo ama kubwa duniani," amesema.
Amesema Canada na Tanzania ni wanachama wa Jumuiya ya Madola na pia Tanzania ina ubalozi wake na hivyo kuwa mwanachama wa OGP na kutokuwa mawasiliano na nchi hiyo haiwezi kuwa tatizo.
Amesema andiko la mpango huo linasema nchi ikijiondoa uanachama na washirika wake wote shughuli na uanachama unakoma.
Hata hivyo, amesema kuwa Serikali ina taarifa kuwa Manispaa ya Kigoma Ujiji bado inaendelea na mpango huo na OGP walimwandikia waziri wa mambo ya nje kuwa bado wana nia ya kuendelea na halmashauri hiyo.
"Sasa nataka kupitia Bunge lako tukufu kuionya Manispaa ya Ujiji kutoendelea. Nchi inayozingatia utawala bora haiwezi Serikali kuu ikafanya maamuzi lakini baraza la madiwani likasema haliwezi kutekeleza. Nataka nionye Halmashauri ya Kigoma Ujiji iache mara moja. Yale ni maamuzi ya Serikali na wakiendelea kufanya mawasiliano kama wanavyofanya sasa Serikali itachukua  hatua kali za kisheria na nyinyi mnajua kwenye baraza la madiwani hatua kali za kisheria ni kulivunja baraza na kuunda Tume ya Manispaa," amesema.
Mkuchika ameomba madiwani na Zitto kutoifikisha Serikali huko.
Katika swali lake la msingi Zitto amehoji kwanini Serikali imeamua kujiondoa kwenye mpango huo.
Akijibu Mkuchika amesema Serikali imejiunga na mipango ya kikanda na kimataifa mbalimbali hivyo ni maoni yake kuwa shughuli zinazotekelezwa kupitia mipango hiyo mingine kupitia vyombo mbalimbali inatosha kwa nchi kujijengea misingi imara ya uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa uwazi kuongeza uwajibikaji na mapambano dhidi ya rushwa.
Mkuchika amesema kujitoa katika mpango huo hakuna madhara yoyote.

Msanii Lulu atupwa jela miaka miwili


Dar es Salaam. Mwigizaji wa filamu nchini, Elizabeth Michaeli maarufu kama Lulu amehukumiwa kwenda jela miaka miwili kwa kosa la kuua bila kukusudia.
Hukumu hiyo imetolewa muda mfupi uliopita leo Jumatatu katika kesi iliyokuwa ikimkabili ya kuua bila kukusudia msanii mwenzake Steven Kanumba.
Watu mbalimbali wamejitokeza kufuatilia huku hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Maelezo ya Jaji Rumanyika: Ushahidi umejikita kwenye ushahidi wa mazingira hata mtuhumiwa alikubali.
"Mtuhumiwa alikubali marehemu alikuwa mpenzi wake na alikuwa naye siku ya tukio,"
"Walevi wanapolewa mambo mojawapo yanayoweza kutokea ni pamoja na kuanguka,"
"Mshtakiwa alijichanganya kama marehemu alikuwa kalewa hakusema kama wakati anamkimbiza aliwahi kuanguka."
"Wakati tunaambiwa kuwa daktari Parpas ni daktari wa familia hatukuwahi kuelezwa kuwa Josephine Mshumbusi kuwa ni daktari wa familia,"
"Mshtakiwa huyu akiwa ni mtu wa mwisho na marehemu ni nini hasa kilitokea. Mshtakiwa kipindi kile alikuwa mtoto wa miaka 16 ina maana alikuwa hajui jema na baya, lakini alikuwa ana uwezo wa kuitwa mke na kujua wapi pakwenda na muda gani wa kurudi."
"Kama mtoto ana uwezo wa kufanya mambo ya kiutu uzima akafanikiwa basi tutegemee iko siku Mahakama hii  atafanya mambo ya kitoto na kuombwa alindwe."
"Sheria yakuua bila kukusudia inaleta udhibiti kuwa watu wanatakiwa wafanye mambo kwa tahadhari, wivu wa maendeleo huleta maendeleo wivu wa mapenzi huleta maangamizi."

Polisi yaendelea kumhoji Dk Shika


Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Benedict Kitalika amesema jeshi la polisi bado linamshikilia Dk Louis Shika na kwamba linaendelea na uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili.
Kitalika amesema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani muda wowote baada ya uchunguzi kukamilika. Amesema mpaka sasa hakuna ndugu yeyote wa mtuhumiwa huyo aliyejitokeza kushirikiana na jeshi la polisi katika uchunguzi unaoendelea.
Kabla ya kumfikisha mahakamani, Kitalika amesema jeshi la polisi linawasiliana na mamlaka nyingine za Serikali kuangalia kama kuna uwezekano wa kumpima Dk Shika kama ana matatizo ya akili.
“Bado tunamshikilia huyu mtu (Dk Shika) wakati tunaendelea na uchunguzi. Tunashauriana na taasisi nyingine za Serikali kuona kama tunaweza kumpima akili,” amesema Kitalika na kusisitiza kwamba hana uhakika ni lini mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani.
Dk Shika anatuhumiwa kwa kuvuruga mnada wa nyumba za bilionea Said Lugumi ulioendeshwa na kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart baada ya kushindwa kulipa asilimia 25 ya malipo ya awali ya gharama za nyumba hizo.

Serikali kupiga mnada ng’ombe 10,000


Dodoma. Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ametangaza kupiga mnada ng'ombe zaidi ya 10,000 wa nchi za Uganda na Rwanda waliokamatwa katika operesheni inayoendelea nchini.
Mpina alitangaza hayo leo Jumatatu bungeni mjini Dodoma wakati akichangia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa 2018/2019.
Waziri huyo ambaye alikuwa akijibu hoja zilizoibuliwa na baadhi ya wabunge amesema ng'ombe hao watapigwa mnada wakati wowote kama ilivyofanya kwa ng'ombe 1,325 wa Kenya.
Amesema uhusiano wa Tanzania nchi nyingine washirika wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni mzuri na akisisitiza hakuna ushirikano wa kihalifu.
Mpina amesema walioingiza ng'ombe hao ni wahalifu na wamevunja sheria za nchi na kutahadharisha wafugaji wa nchi jirani kufuata sheria wanapotaka kuingiza mifugo nchini.

Waziri Kigwangala amshukia Nyalandu


Dodoma. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangala amemlipua waziri wa zamani wa wizara hiyo, Lazaro Nyalandu akimtuhumu kwa matumizi mabaya ya madaraka.
Akichangia Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 207/2018, Dk Kigwangalla ameiagiza Takukuru na polisi kumchunguza Nyalandu.
Dk Kigwangala amesema Nyalandu aliikosesha Serikali mapato ya Sh32 bilioni kwa miaka miwili aliyohudumu katika wizara hiyo kwa kushindwa kusaini sheria ya tozo kwa hoteli za kitalii.
Mbali na tuhuma hiyo, pia alimtuhumu kutumia helkopta ya mwekezaji mmoja raia wa kigeni, kipindi cha kampeni zake  za kugombea urais 2015, wakati kampuni ya raia huyo ilikuwa ikituhumiwa kwa ujangili.
Hata hivyo wakati Kigwangala akitoa tuhuma hizo tayari Nyalandu alishasema kuwa tuhuma ambazo zimeanza kuibuliwa mitandao dhidi yake si za kweli bali zinalenga tu kumchafua.
Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni alishangaa iweje ziibuliwe sasa zaidi ya miaka miwili tangu aachie uwaziri.

Diamond, Wema wamlilia Lulu


Dar es Salaam. Mwanamuziki Diamond Platnumz amesema hukumu ya miaka miwili aliyopewa mwigizaji Elizabeth  Michael maarufu Lulu siyo adhabu bali ni mtihani ambao unalenga kumfanya kuwa imara zaidi.
Amesema mwigizaji huyo ambaye leo Jumatatu Mahakama Kuu imemhukumu kifungo cha miaka miwili jela, amechaguliwa na Mungu kwa kuwa anaamini anao uwezo wa kuhimili mikikimikiki.
Katika mtandao wa Instagram, Diamond anayetamba na wimbo Halleluyah, ameandika:  "Mwenyezi Mungu ameamua kukupa mtihani huu wewe kwa sababu anaamini wewe ni shujaa na imara...pia anaamini wewe ndio msichana pekee unayeweza kuuhimili mtihani huu... hivyo usisononeke, Make him Proud.”
Mbali na Diamond, wasanii wengine wametuma salamu za pole kwa Lulu akiwamo Wema Sepetu, Mboni Masimba, Snura, Dj Choka, Dk Cheni na wengine wengi.
Dk Cheni ambaye amekuwa karibu na Lulu kwa muda mrefu amesema huu ni wakati wa kumuombea Lulu kwa kuwa hakuna anayejua kesho atapata mkasa gani.
Katika mtandao wa Instagram aliweka picha ya Lulu na kuandika: "Tumuombee mtoto huyu kwa kuwa hakuna anayeijua kesho yake,".

Mnyika asema bomoabomoa iliyofanyika barabara ya Morogoro ni haramu


Dodoma. Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika amesema bomoabomoa iliyofanyika katika barabara ya Morogoro ni haramu kwa sababu sheria ya barabara iliyotumika ilitungwa mwaka 1932 na ilishafutwa.
Akiuliza swali bungeni leo Jumatatu Mnyika amesema Rais John Magufuli akiwa katika ziara Mwanza alitoa kauli ya kibaguzi na kwamba kama si ya kibaguzi basi Serikali itoe kauli ya kuwalipa fidia wakazi hao waliobomolewa nyumba zao.
"Kwa sababu Serikali ilisingizia sheria mimi kama mbunge nilichukua hatua nilileta marekebisho bungeni ili barabara yote iwe mita 60 lakini Serikali ikafanya njama na Katibu wa Bunge aliyeondoka(Thomas Kashililah) kuzuia huo muswada ni lini hasa ikaachana na hizi njama ikakubaliana na Rais na muswada ukaletwa hapa bungeni ili barabara hii iwe na upana wa mita 60? Amehoji.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukizi na Mawasiliano, Elias Kuandikwa amesema sheria mbalimbali za barabara zilipokuwa zikitungwa zilikuwa zikizingatia maendeleo na kwamba Sheria ya Barabara ya Mwaka 1932 ilianisha ukubwa wa barabara katika maeneo yote inapojengwa.
Alimtaka mbunge huyo kuwasiliana na mamlaka za halmashauri za serikali za mitaa ambazo ndio wasimamizi kuona kama kuna mahitaji ya baadhi ya maeneo kufanyiwa marekebisho kwenye sheria hiyo.
"Hakuna njama yoyote na suala la fidia litakwenda kwa mujibu wa sheria," amesema.
Waziri wa Nchi katika ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema Kanuni za Bunge sehemu ya nne inaonyesha jinsi shughuli za Bunge zinavyopangwa na sehemu ya tano inaonyesha namna majadiliano yatakavyofanywa ndani ya Bunge.
"Si kweli kwamba Serikali ilipanga njama na Bunge kuzuia muswada wowote uliokuwa uletwe ndani ya Bunge, suala liloelezwa na Mnyika katika swali la nyongeza si kweli ni suala lililojitokeza katika muswada wake," amesema.
Mhagama amesema Serikali haina utaratibu wowote wa kula njama na Bunge.
Katika swali la msingi Mnyika alitaka kujua ni lini Serikali itawasilisha muswada wa marekebisho ya sheria ya barabara ili eneo la hifadhi ya barabara iwiane na barabara nyingine.
Akijibu swali hilo Kuandikwa amesema Serikali haina mpango wa kufanya marekebisho sheria ili kufanya barabara ya Morogoro kuwiana na barabara kuu nyingine kwa kuwa eneo la hifadhi la barabara hiyo lilotengwa linahitahika kwa ajili ya upanuzi wa barabara ili kuwiana na mahitaji ya sasa na ya miaka ijayo.