Monday, November 13

Tamu na chungu ya bei elekezi mpya ya mbolea


Hivi karibuni, Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) ilitangaza bei elekezi ya mbolea yenye unafuu.
Unafuu huo umekuja huku pia kukiwa na mfumo mpya wa uagizwaji wa mbolea wa pamoja, ambao umesababisha bei kushuka kutokana na udhibiti wake.
Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Kilimo, Charles Tizeba Agosti 15, 2017 inasema bei hiyo ni hadi kwenye duka la muuzaji wa rejareja.
“Kwa utaratibu huu, bei elekezi ya mfuko wa kilo 50 wa mbolea ya kupandia (DAP), itakuwa kati ya Sh50,500 na Sh53,000 kwa mikoa ya Kanda ya Mashariki, Kati na Kaskazini,” inasema taarifa hiyo.
“Kwa mikoa ya Kanda za Magharibi, Ziwa na Nyanda za Juu Kusini, bei elekezi ya mfuko mmoja wa mbolea wa kilo 50 itakuwa kati ya Sh53,500 na Sh56,000. Bei hizi ni pungufu kwa wastani wa asilimia 13 hadi 42 ukilinganisha na bei ya mbolea aina ya DAP iliyokuwa ikiuzwa kati ya Sh60,000 na Sh100,000 kwa mfuko wa kilo 50.
Kwa upande wa mbolea ya kukuzia (Urea), anasema mfuko wa kilo 50 utauzwa kati ya Sh41,000 na Sh43,000 kwa mikoa ya Kanda ya Magharibi, Ziwa na Nyanda za juu Kusini na kwa Kanda ya Mashariki, Kati na Kaskazini, bei itakuwa kati ya Sh38,000 na 43,000.
“Bei hizi ni pungufu kwa wastani wa asilimia 15 ukilinganisha na bei ya mbolea aina ya Urea iliyokuwa ikiuzwa kati ya Sh45,000 na Sh70,000 kwa mfuko wa kilo 50,” anasema Dk Tizeba.
Bei haina faida
Hata hivyo, wakizungumza katika mkutano wa wadau wa mbolea uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, baadhi ya wafanyabiashara walisema bei hizo hazina faida kwao.
Mmoja wa wafanyabiashara mbaye hakutaja jina lake liandikwe gazetini akidai kulinda masilahi yake ya biashara, anasema bei elekezi iliyopangwa na Serikali haina faida kwao.
“Wametumia mfumo wa Sumatra (Wakala wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini) usio na uhalisia. Bei hiyo haijazingatia gharama za kuhifadhi mzigo ukishaununua bandarini, utaweka wapi?
“Bei elekezi ya mbolea hapa Dar es Salaam unanunua Sh48,000 hivi, sasa kama unaipeleka Mbeya ukaiuze Sh53,000 usafiri wa treni ni Sh4,500 kwa mfuko.
“Ukishafika Mbeya kwa mfano kuna gharama za kutoa mzigo stesheni kwenda ghalani tena, inaweza kuwa Sh500 kwa mfuko, kama ni Tukuyu kwa mfano inaweza kuwa Sh1,500, kuna kushusha tena Sh200 hapo bado, wakala hajadai naye faida yake. Mwisho utakuta gharama zimezidi bei elekezi,” anafafanua mfanyabiashara huyo.
Kuhusu elimu, mfanyabiashara huyo alisema bei hiyo haikuzingatia utoaji wa elimu kwa kuwa nao una gharama kubwa.
“Waziri amesema tutoe elimu kwa wakulima, lakini ajue kuwa tunatakiwa kukodi kumbi, kulipa posho za wataalamu na washiriki, kwa bei hiyo hiyo?” anahoji mfanyabiashara huyo.
Naye meneja masoko wa Kampuni ya Yara Tanzania Ltd, William Ngeno anasema japo awali hawakuukubali mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja lakini wameamua kufuata sheria.
“Sheria ikishasema usipite hapa, inabidi usipite kwa hiyo tulikubali. Tunashirikiana na Serikali na wataalamu kutoa elimu kwa wakulima,” anasema Ngeno.
Hata hivyo, anasema Serikali imedhibiti mbolea aina mbili tu za DAP na Urea wakati kampuni hiyo inatengeneza mbolea zaidi ya aina 10.
Akizungumzia changamoto ya usafiri, mfanyabiashara Jaison wa Kampuni ya Staco, anasema wamekwepa kusafirisha mbolea kwa treni kwa sababu ya gharama.
“Sisi tunatumia barabara kwa sababu ukisafirisha kwa treni, utalazimika tena kuihamishia kwenye magari unapofika mikoani. Tunachofanya ni kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha wakulima wadogo wanafaidika,” anasema.
Msimamo wa Serikali
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba anasema bei elekezi imeshapigiwa hesabu za usafirishaji na faida, hivyo wafanyabiashara hawapaswi kuongeza faida zaidi.
“Tumeshachukua uamuzi kwenye biashara ya mbolea aina mbili yaani DAP na Urea, bei isiwaumize wakulima. Tumeondoa tozo mbalimbali ili kila upande ufaidike ikiwezekana mkulima afaidike zaidi,’ anasema na kuongeza:
“Nimesimama kwenye mkutano jimboni kwangu mwezi uliopita, nikauliza wangapi wanatumia mbolea, hakuna aliyenyoosha mkono, nilipouliza wangapi hawatumii, wote wakanyoosha, hii haikubaliki.”
Wakulima watoa ya moyoni
Wakizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, wakulima kutoka vijiji vya Luganga, Utengule na Mtandika wilayani Kilolo Mkoa wa Iringa wanaeleza changamoto za upatikanaji wa mbolea.
Kwa maelezo yao wanaonyesha kutegemea zaidi mbolea ya ruzuku na kutoelewa kinachoendelea kuhusu bei mpya za mbolea.
Immaculate Kagogo ambaye ni mkulima wa Kijiji cha Luganga wilayani Kilolo, anasema mbolea hiyo wanaipata kwa kuchelewa.
“Mara ya mwisho walipoleta walitaka tununue ikiwa kwenye gari lakini mwenyekiti alikataa hadi iliposhushwa na kuwekwa kwenye ghala. Lakini huwa inaletwa kwa kuchelewa sana,” anasema.
Maelezo yake yanafanana na ya Oswald Joseph wa kijiji hicho anayesema:
“Wanaweza kuleta mbolea ya kupandia mwezi wa kwanza au wa 12 mwishoni na mvua zimeanza Novemba kwa hiyo inakuwa shida. Mbolea ya DAP tulikuwa tunanunua hadi Sh70,000 na Urea 50,000 hadi 54,000.”
Anaongeza: “Hiyo ni bei kubwa na ni kwa wakulima waliozoea kilimo cha mbolea, lakini wa wakulima wa kawaida hawatumii kabisa mbolea. Wanachofanya ni kubahatisha kwa kutumia mbolea za kienyeji kama samadi. Unaweza kupanda ekari mbili ukapata magunia mawili ya mahindi.”
Akieleza sababu ya ucheleweshwaji huo wa mbolea, Evans Msofu ambaye ni meneja wa TFC Mkoa wa Iringa anataja mchakato wa utoaji mizigo bandarini kuwa chanzo.
“Sababu zinazochelewesha mbolea hasa vijijini ni mchakato unaofanyika kutoka mbolea zinakotoka, mfano bandarini ambako kuna mchakato wa kushusha na mengineyo sasa mpaka ukasafirishe, ndio unakuta inachelewa,” anasema.
Akifafanua zaidi, Msofu anasema mawakala wa pembejeo ndiyo wanaohusika na usafirishaji wa mbolea kutoka bandarini Dar es Salaam kwenda mikoani na watakaowahi kupata ni walio karibu hasa mijini.
Kauli ya TFRA
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mbolea Tanzania (TFRA), Lazaro Kitandu anasema tayari kumekuwa na mafanikio tangu bei hizo zilipotangazwa sambamba na mfumo wa uagizaji wa pamoja wa mbolea.
“Nchi imefaidika na bei ya chini ya mbolea kupitia ununuzi wa pamoja kutokana na punguzo linalopatikana katika bei kwa sababu ya kiwango kingi kilichonunuliwa na kupungua kwa gharama za uendeshaji,”anasema.
Anatoa mfano wa zabuni iliyofunguliwa Julai 21, 2017 ambapo bei ya ununuzi (FOB) kwa mbolea ya kupandia (DAP) ilipatikana kwa Dola 3047 ambayo ni chini kwa asilimia 15 ya bei iliyokuwa katika soko la dunia ambayo ni Dola 365.
“Mfumo huu umewawezesha wafanyabiashara wadogo kushiriki katika biashara ya mbolea na hivyo kuimarisha mtandao wa usambazaji hadi ngazi ya mkulima,” anasema.
Hata hivyo, anasema kumekuwa na changamoto ya baadhi ya wadau kuuchanganya mfumo huo na ule wa vocha au ruzuku za mbolea, huku baadhi ya kampuni zikijaribu kuuhujumu ili kupunguza ushindani unaotokana na wafanyabiashara wadogo kuingia kwenye soko la mbolea.
Akizungumzia mfumo mpya wa bei elekezi, Kitandu anasema umepokelewa vizuri na wakulima kwa sababu unawafikishia mbolea kwa bei nafuu kulinganisha na hali ilivyokuwa awali.

No comments:

Post a Comment